Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Janeth Elias Mahawanga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Nami pia niungane na wenzangu kumpongeza sana Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii na Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu na Utamaduni. Nawapongeza Mawaziri wa Wizara husika na pia naipongeza na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Wizara hii inafanya kazi kubwa sana na ina program nyingi sana kwenye jamii yetu, lakini tatizo kubwa wanalo-face ni ufinyu wa bajeti. Ukiangalia kwenye hii program yao ya hawa Machinga, fedha walizotakiwa kupewa, ni miaka miwili sasa hawajapewa fedha yoyote. Masoko, miundombinu ya Machinga imeandaliwa lakini fedha bado hazijatoka. Hii inakwamisha juhudi kubwa za Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naiomba Wizara hii ijaribu kuangalia hizi fedha zitakapotoka, wasiangalie tu kundi moja la Machinga; tuna vijana wengi mtaani ambao wanatafuta hizi fursa. Kuna kundi kubwa la vijana wa boda boda ambao ni wengi sana, inawezekana ni wengi kuliko hata Machinga. Kuna program ya kuwaandalia Machinga vitambulisho. Vitambulisho hivyo vitakuja kuwasaidia kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha, lakini bado kuna hata hawa vijana wa boda boda, nao wakiandaliwa hivi vitambulisho wanaweza kusaidiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na mifuko mingi sana ya uwezeshaji katika sekta mbalimbali ambayo haishabihiani jambo linalosababisha fursa hizi kutoleta tija kwenye jamii yetu. Wizara hii pia inamfuko wa maendeleo ya wanawake katika kutoa mikopo kwenye vikundi, na mikopo hii imepitia halmashauri, lakini ukienda huko mtaani wanawake wengi bado wanalia hawajapata hizi fedha. Halmashauri zote 184 za Tanzania zilipewa hizi fedha kwa ajili ya kukopesha akina mama. Ni halmashauri chache sana zimeweza kurudisha lakini nyingi hazijarudisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuiombe Serikali kupitia Wizara waangalie utaratibu wa fedha hizi kuwafikia walengwa, lakini kwa njia tofauti na kupitia halmashauri. Tumeona mikopo ya 10% iliyopo kupitia halmashauri imefeli. Fedha zinakopeshwa hazirudi. Sasa tunajiuliza, fedha hizi ni kweli wanakopeshwa wahusika sahihi? Fedha hizi zinakwenda wapi? Ni kundi gani linalokopeshwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye vikundi vya akina mama mtaani wanalia, hakuna fedha, hakuna mikopo waliyopata, lakini pia mikopo maarufu huko mitaani ni mikopo ya 10%. Sasa kama Wizara ina fursa kama hii kwa akina mama na fursa hii inapitia huko huko halmashauri, mbona bado haitangazwi? Akina mama wengi wajasiriamali hawaijui hii mikopo kama ipo huko halmashauri, lakini ukija kuangalia unaambiwa mabilioni ya hela yameshakopeshwa. Anakopeshwa nani? Hakuna vikundi vinavyofanya biashara kubwa au shughuli kubwa za ujasiriamali kupitia manufaa ya mfuko huu, lakini huku Wizarani ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba fursa kama hizi zitangazwe, akina mama wafahamu kwamba kuna mikopo halmashauri, lakini Wizara ya Wanawake, Jinsia na Maendeleo ya Jamii kuna mikopo mingine fursa zinazotakiwa kwa ajili ya akina mama. Tunaomba Wizara ijitahidi kutangaza fursa hizi ziwafikie walengwa. Pia waangalie namna ya kuwafikishia akina mama hawa hizi fedha tofauti na mfumo wa halmashauri, kwa sababu halmashauri zetu kiukweli zimefeli katika sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunaomba Serikali isaidie kuongeza bajeti ya mashirika yasiyo ya kiserikali katika Wizara hii. Sasa hivi mpaka Augosti, 2023 kuna mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyosajiliwa zaidi ya 9,600. Mashirika haya tunafahamu yapo mengine yanayojihusisha na mmomonyoko wa maadili ambayo ni kinyume na utamaduni wa nchi yetu, pia yapo mashirika mengine yanafanya shughuli za utakatishaji fedha, vile vile yapo mashirika mengine yanajihusisha na siasa wakati wa uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Wizara ili ishuke chini vizuri na kuyabaini, inahitaji bajeti na fungu la kutosha. Tunaomba Serikali iwaongezee nguvu Wizara hii ili wakafanye hii kazi vizuri. Tukienda kwenye mmomonyoko wa maadili, tunaona kabisa mimba za utotoni zinaendelea kuongezeka siku hadi siku, ubakaji na ulawiti umeendelea kuongezeka, pia kampeni ya kuzuia ukeketaji bado tunajiuliza imefikia wapi? Au bado Serikali sasa imeona hiki ni kitu cha kawaida? Tunaomba Wizara hii ijitahidi kujikita zaidi kwenye haya masuala. Ina kampeni nyingi sana. Mheshimiwa Waziri na timu yake wanajitahidi kweli kweli lakini wanashindwa kushuka zaidi huko chini kwa sababu ya ufinyu wa bajeti wanayopewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatamani kuona kwenye kila kata kuna madawati ya jinsia, tunatamani kuona kwenye mashule, tunatamani kuona program mbalimbali kwenye redio, na TV zikihamasisha kutokomeza haya mambo ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia. Pia tunaomba Wizara wadau wajitokeze tuhakikishe adhabu kubwa zinatolewa. Walete hapa Muswada kuwe na adhabu kubwa ya kukomesha hivi vitendo. Inaonekana hii ya kuwapeleka tu jela, bado haikomeshi suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu kuna Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao ulianzishwa mwaka 1993. Mfuko huu mpaka Agosti, 2023 ni kama miaka 30, umeweza kutoa mikopo kwa vijana kiasi cha shilingi bilioni 8.9. Kwa ukubwa na umri wa mfuko huu na hii fedha, bado. Uhitaji kwenye jamii ni mkubwa sana kwa vijana, lakini bado hili fungu ni dogo sana kwa sababu limeenda kwa vijana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)