Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kawe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia huu Muswada wa Bima ya Afya kwa Watu Wote. Wewe kama Mwalimu wangu wa mambo ya siasa na kiongozi wangu, naomba nikubaliane na maneno uliyoyasema kwamba kwa habari ya Muswada wa Bima ya Afya kwa Watanzania wote, Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi apewe maua yake. Asiyempa maua yake basi ana fitina binafsi, lakini kwa habari ya Muswada huu nasema tena Mama Samia Suluhu Hassan apewe maua yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikubali kwamba upatikanaji wa dawa nchini umekuwa sana kutoka asilimia 62 mwezi Agosti, 2022 mpaka asilimia 72 mwezi Agosti, 2023. Kwa hiyo, upatikanaji wa dawa umekua sana katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikubali jambo moja kwamba tumeongeza pia uhaba wa watumishi wa Wizara ya Afya, mpaka sasa hivi tumefikia almost asilimia 50.4, hii ndiyo sababu ninaendelea kusema katika suala hili la afya Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan na Waheshimiwa Mawaziri wake wapewe maua yao.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nisema jambo moja, asilimia 26.4 ya Watanzania ambao ni kama Watanzania milioni 15.8 wako kwenye umaskini wa kutupwa na hii ni sawa na kaya milioni tatu na laki sita. Hawa wote kwa namna ya kawaida, hawana uwezo kabisa wa kugharamia huduma za afya mahala wanapokaribia kwenda katika vituo vya afya au zahanati.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia asilimia nane ya Watanzania ambao ni almost milioni 4 ya watanzania wote ni watu walio kwenye ule umaskini uliokithiri. Almost kaya milioni moja na laki moja ni Watanzania ambao wako kwenye umaskini uliokithiri, hawana uwezo kabisa wa kulipa, kugharamia huduma za afya wao wenyewe. Kwa hiyo, naweza kusema asilimia 85 ya Watanzania hawawezi kupata huduma ya afya inavyotakiwa kwa sababu ya vikwazo vya kifedha walivyonavyo. Naomba ku-declare interest, mimi ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020, Ibara ya 83(e) inazungumza kuisimamia Serikali ili kuwapa Watanzania wote Bima ya Afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna hiyo, nataka kuishukuru sana Serikali ya Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan na Waheshimiwa Mawaziri wake, Mheshimiwa Waziri Ummy na Msaidizi wake Mheshimiwa Godwin Mollel kwa kuleta Muswada huu Bungeni ili tuupitishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, Shakespeare aliwahi kusema; ”mto hauwezi kunywa maji yake wenyewe wala mti hauwezi kukaa chini ya kivuli chake wenyewe.” Ndivyo walivyo Watanzania walio maskini wasioweza kumudu afya, wanahitaji kusemewa na sisi, hawawezi wakajisemea wao wenyewe. Nataka kusema kwa uwazi kabisa hatuwezi kuchelewa hata kwa dakika moja kujadili na kupitisha huu Muswada wa Afya ili Watanzania wote, wanawake kwa wanaume, vijana kwa watoto wapate Bima ya Afya na wao waweze kutibiwa.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wetu ni maskini sana. Wananchi wetu wengi wanapoteza maisha kwa magonjwa ambayo yanaweza kutibika. Unakuta mtu anaumwa ugonjwa wa kawaida lakini hawezi kumudu matibabu na matokeo yake anapoteza maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ukifungua simu za Waheshimiwa Wabunge, Mbunge yeyote hapa lazima kwenye simu yake utakuta ujumbe au meseji anaambiwa na wapiga kura wa Jimboni kwake nisaidie fedha nikalipe dawa au nisaidie fedha nikalipe hospitali au nina maiti hospitalini nimeshindwa kuitoa kwa sababu za huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu leo bila kufumba macho, bila kupoteza muda tupitishe na tuujadili huu Muswada wa Bima ya Afya ili akina Mama wa Tanzania watibiwe, vijana watibiwe, wazee watibiwe na Watanzania wote kutoka Mashariki, Magharibi, Kaskazini wapate Muswada wa Bima ya Afya na Tanzania iendelee sawasawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimehudhuria misiba minne tofauti iliyobadili mtazamo wangu juu ya Bima ya Afya. Msiba wa kwanza nilihudhuria mahala fulani kule Bunju, nilikuta Balozi mmoja amefariki, Balozi wetu wa Shina, Mwenyekiti wa Shina. Nilipouliza kwa nini alifariki, wanasema alikuwa hana uwezo akaenda kwenye maabara kupima akaonekana ana malaria, lakini akakosa shilingi elfu tatu ya kununua dawa ya malaria. Alikuwa ana shilingi elfu moja ya kupima kuona ana malaria, hakuwa na shilingi elfu tatu ya kununua dawa ya malaria, akarudi nyumbani. Akakaa baada ya muda akazidiwa akapoteza maisha yake. Ni watu wengi wa namna hii nchi yetu ya Tanzania kutoka mashariki mwa Tanzania mpaka magharibi mwa Tanzania, kusini mpaka kaskazini, wanaopoteza maisha kwa magonjwa ambayo yanaweza yakatibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni saa ya wakati wetu, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tupitishe Muswada wa Bima kwa Watanzania Wote, ndugu zetu watibiwe na Tanzania yetu isonge mbele. Falsafa ya bima ni watu wachache wenye uwezo wa kulipa bima walipe bima na hao wachache wanaolipa bima wawafanye watu wengi wasio na uwezo wa kulipa bima wapate faida.
Mheshimiwa Naibu Spika, inapotokea wagonjwa wote wanakwenda kukata bima, hiyo siyo bima tena. Ninawaomba Watanzania wenye uwezo wa kulipa bima tulipe bima kwa uaminifu kwa ajili ya ndugu zetu wengine ambao wao hawana uwezo wa kulipa bima ili tuwabebe na kwa pamoja mfuko wetu uwe imara na tusonge mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri nilionao, kwa sababu kuna baadhi ya vijiji havina zahanati kabisa, ukienda kule vijijini kuna baadhi ya vijiji havina zahanati kabisa. Hao wananchi na wenyewe ili waweze kutibiwa watalazimika kulipa Bima ya Taifa, Bima ya Afya wakati huohuo hawana mahala pa kutibiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali sana ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Waheshimiwa Mawaziri wake, wajitahidi sana maeneo ya vijiji ambavyo hakuna zahanati, wapeleke zahanati ili ile maana ya hawa wananchi na wao kulipa bima walipe bima na wapate mahala pa kutibiwa kuliko walipe bima halafu hawana mahala pa kutibiwa.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Rwanda ni nchi ndogo sana, hawana rasilimali kama zetu, hawana madini kama yetu lakini wana Bima ya Afya. Hawana milima kama yetu lakini wana Bima ya Afya, hawana mito kama yetu lakini wana Bima ya Afya kwa watu wao. Hawana maziwa kama yetu lakini wanatibu watu wao, hawana bahari kama yetu lakini wanatibu watu wao. Hawana watu wengi kama sisi lakini wanatibu watu wao, hawana ardhi kama ya kwetu lakini wanatibu watu wao, hawana dhahabu, almasi na madini kama ya kwetu lakini wanatibu watu wao. Sisi sasa ni wakati muafaka wa Taifa letu la Tanzania tuwatibu watu wetu wawe na afya njema na naam! Tanzania mpya inakuja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, ninaunga mkono hoja na ninawaomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuupitishe Muswada huu wa Sheria ya Bima ya Taifa kwa Watu Wote kwa kishindo na nguvu ili ndugu zetu wote watibiwe. Nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)