Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bahi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa dhati kabisa kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Mpango huu wa Maendeleo. Awali ya yote nimpongeze Waziri wa Mipango pamoja na Waziri wa Fedha kwa kutuletea Mpango huu ambao kwa kiasi kikubwa inaonyesha namna gani ya kutekeleza na kuleta maendeleo katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja katika watu ambao nilichangia katika Bunge lililopita mwaka jana ilikuwa ni kwamba tuwe na Tume ya Mipango. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kuamua kwa dhati kabisa tuwe na Tume ya Mipango, lakini dhana na dhima ya Tume ya Mipango ni kuwa na dira kubwa na kuangalia namna gani Taifa tunalotaka kwenda katika vipaumbele vyetu na katika kujiimarisha zaidi kiuchumi. Nataka nimshauri Waziri wa Mipango, kwamba sera zetu zijielekeze katika kutatua matatizo na kuyamaliza badala ya kuwa na sera za jumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwa Mkoa wa Dodoma, tunaishukuru Serikali sasa ni Makao Makuu ya Nchi, kazi tuliyonayo ni kwamba tunajenga Mji huu, lakini ukiangalia kwa sasa Dodoma haina viwanda umebaki Mji wa Kiserikali, umebaki mji ambapo mzunguko wake wa fedha sio mkubwa kwa sababu hatuna viwanda, Umebaki ni mji wa mwisho wa mwezi, ikifika mwisho wa mwezi mzunguko wa fedha unakuwa mkubwa na tarehe zinavyoisha, unaona kabisa uchumi na watu hawajachangamka. Kwa hiyo, ni lazima tuwe na viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiwa Dodoma huoni bidhaa zinazotoka Dodoma ziende Iringa, Arusha, Kanda ya Ziwa, bado tuna shida ya viwanda. Kwa hiyo, Dodoma inahitaji sera madhubuti kwa namna gani iwe hub…
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana ya kuwa na uchumi wa kuweza kuzalisha katika ili kuhudumia mikoa mingine …
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Ni wapi inatajwa taarifa?
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi hapa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kenneth Nollo, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Hamisi Taletale.
TAARIFA
MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji, hapa Dodoma mnacho Kiwanda cha Wine au hicho sio Kiwanda? Ni hayo tu.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kenneth Nollo, unaipokea taarifa hiyo.
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa kutoka kwa Ustadhi, kwa kujua hili suala la wine, naipokea taarifa ni kweli kiwanda tunacho na kwenye hili bado tuna changamoto, lakini tunaendelea kuweka jitihada zaidi kukuza zao la zabibu. Nakushukuru sana Ndugu yangu Mheshimiwa Taletale. Nilichotaka kusema ni kwamba mji huu unahitaji uwe na viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka niliseme hususani kwa Mkoa wa Dodoma, Waziri amesema habari ya kwamba umaskini unaenda kupungua, lakini kwa Mkoa wa Dodoma, bado kuna shida. Nature yetu ni kwamba Mkoa wetu una ukame, hilo wote tukubaliane, kwamba Mkoa wetu na maeneo yetu ya Kanda ya Kati, ni maeneo kame na umaskini bado ni mkubwa kwa sababu moja, wananchi wengi wanategemea kilimo, lakini jitihada za kuondoa umaskini kwenye suala zima la kilimo na kama nilivyosema namna ya kuweka viwanda, bado hatujakaa sawasawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwa na Sera za Kitaifa, Mipango ya Kitaifa, wenzetu kwa mfano Nchi ya Nigeria walikuwa na sera kwa ajili ya maeneo kame, mipango kwa ajili ya maeneo kame. Naishauri Serikali na namshauri Waziri wa Mipango, tuwe na sera mahsusi katika kuinua na kuleta uchumi kwenye maeneo kame ikiwemo Dodoma. Sawa tunapokea skills za umwagiliaji, lakini bado haitoshi, wananchi wengi wa maeneo yetu kwanza idadi ya watu inaongezeka, ardhi ya kulima inapungua ni lazima Serikali iangalie uchumi wa maeneo haya kame tunafanya nini, hili nataka niliongeze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuhusu wanafunzi wanaosoma Vyuo Vikuu na Vyuo vya Juu. Kutokana na umaskini tulionao kwenye maeneo yetu hasa Kanda ya Kati, watoto wengi hawawezi kwenda kwenye vyuo wakalipiwa ada kwa sababu uwezo wa wazazi wao haukidhi. Nalisema hili kama Mbunge, changamoto ninazozipata kwa sasa, kila mtoto ameshindwa kwenda shule na wanasema Mbunge tusaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kama inaweza kwa nini tusiondoe ada kwenye Vyuo Vikuu tukopeshe watoto kwa ajili ya chakula, fedha ya chakula. Serikali itoe ada kwenye Vyuo Vikuu kwa watoto wa Kitanzania ila kama ni foreign students hao ndiyo walipe ada. Nataka niulize Serikali inapata faida gani kulipisha watu wake kwenye ada za Chuo Kikuu? Naomba sana jambo hili tulitafakari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umaskini ni mkubwa, watoto wetu hawawezi kwenda vyuo na wengi wanaacha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)