Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa na mimi fursa na mimi nitoe mchango wangu katika mapendekezo haya ya mwongozo wa maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali yetu kwa mwaka unaokuja wa Serikali wa 2024/2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikupongeze wewe Mheshimiwa Rais wa Mabunge yote ya dunia hii, hongera sana tunayo imani kubwa sana na wewe na dunia imeona. Ushindi huo umeonesha kwamba Bunge hili ni Bunge bora kabisa katika Mabunge ya Dunia, kwa hiyo nakupongeza na nakutia moyo tuko pamoja na wewe.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza pia Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambae ameona umuhimu wa hii mipango kuwa na Wizara, leo tuna Wizara ya Mipango ambayo inaongozwa na Profesa mbobezi kabisa Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo damu ya Singida hiyo, hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wanavyosema wenzangu hapa ninyi hapo mapacha wawili mmekabidhiwa eneo nyeti sana, mmekabidhiwa uchumi wa nchi ili mtuokoe, mtuvushe mtutoe hapa tulipo tusonge mbele kiuchumi, nchi yetu isonge kiuchumi. Ninayo imani kubwa na ninyi na ninao uhakika mtatusaidia na mtahakikisha nchi yetu inabadilika kiuchumi. Nimpopngeze pia Rais wetu tena kwa miradi mingi ambayo ametuletea kwenye maeneo yetu, katika tangazo ulilotoa la yale magari na mimi Jimbo langu tumepata gari la kubebeba wagonjwa ambalo nimekuwa nikiliimba sana hapa Bungeni mara kadhaa, leo namshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu ametusikia hivyo wananchi wetu wanaenda kupata nafuu. Ninampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu na hii isiishie hapo, tuendelee kufanya hivyo ili kuendelea kuokoa maisha ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, agenda yangu kubwa hapa ni sekta ya mifugo ambayo imekuwa ni agenda hot sana hapa Bungeni na kwenye nchi yetu kwa ujumla. Kimsingi bado hatujawa na mpango mkakati kwa ajili ya kuepusha wafugaji nchini kuwa digidigi katika nchi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamekuwa ni watu wa kukimbia kimbia, kufukuzwa fukuzwa isivyo halali. Sasa mimi hapa nilikuwa najaribu kutazama, hivi hatujaona bado athari zinazotokana na migogoro kati ya wafugaji na wakulima hadi tunapoteza maisha ya wananchi wetu. Hatujaona athari kwenye jamii zetu kati ya wafugaji na hifadhi, bado hatujaona athari iliyopo kati ya wafugaji wakati mwingine na Kambi za Jeshi. Hawa watu bado hatujaweka mkakati ipasavyo, mkakati madhubuti wa kuhakikisha nao wanafanya kazi zao vizuri na kwa uaminifu. Naomba kwa Mpango huu tulionao sasa wa mwaka huu tunaokwenda wa fedha 2024/2025, niombe sana Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo atuletee mkakati wa kuhakikisha wale wazazi wake waliomsomesha kwa kuku, kwa ng’ombe waache kukimbia kimbia.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu wengi tuliopo hapa Bungeni tumetoka vijijini na wengi tumetokana na mifugo kama siyo mifugo basi ni kilimo, tuwatazame hawa watu. Wale mshahara wao ni ng’ombe, mshahara wao ni mbuzi, tunapokosa mipango mikakati ya kuwawekea mazingira mazuri tunawaumiza wanateseka, mwisho wa siku wanakuwa ni maskini wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana eneo hili liletewe mikakati endelevu ya kudumu ili watu hawa wafanye kazi zao kwa staha, wafanye kazi zao ipasavyo ili waingize katika Pato la Taifa inavyosapwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa ufupi sana kwenye eneo la viwanda ni muhimu sana tuje na mkakati wa kuongeza thamani kwenye mazao yetu kwa kupitia viwanda. Tuje na viwanda ambavyo vinakwenda kule kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi nchi hii haina vijiji tena umeme unapatikana kila kijiji cha nchi hii bado maeneo machache tu, ninaomba sana umeme huu usitumike kuwasha tu nyumbani, utumike kwa ajili ya viwanda, hili litawezekana endapo sisi tutaacha kusafirisha malighafi zetu kuzipeleka nje. Tuhakikishe tunakuwa na processed goods ambazo tutazipeleka nje, tupeleke bidhaa nje badala ya kupeleka raw material nje ya nchi, hii itaongeza kwanza fursa za uwekezaji na itaongeza hata ajira kwa vijana wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatakiwa tutoke hapa tusiwe kila siku tunaongea hayo hayo tunayarudia, Waziri afanye research, Wizara hii ya Mipango ifanye research, waajiri watu wazuri kwa ajili ya kufanya tafiti kwenye maeneo haya ya uwekezaji, viwanda, ili tuondokane na masuala haya ya kila siku tunakuja hapa tunalalamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tuna mifuko, tunasema tunayo mifuko kila mahali lakini ngozi zinatupwa, ngozi zinaharibika, ngozi hazina thamani ni kwa sababu tumeacha viwanda vyetu vya bidhaa za mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kuna mkakati muhimu sana ambao tunatakiwa tuuzingatie na tuurudie, mkakati wa kuhakikisha yale maeneo ya uzalishaji. Leo tunasema hapa tuna kiwanda, maeneo kama ya central zone tuna mazao tunayoyazalisha, tuhakikishe tuna viwanda vyake, ametoka kusema hapa Mheshimiwa Keneth Nollo wa Bahi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanda ya Magharibi wanayo mazao wanayoyazalisha tuweke viwanda vinavyofanana na mazao wanayoyazalisha hii itarurahisishia sisi kuhakikisha mazao yetu tunaya-process kwenye maeneo husika na tunatoa tunapeleka nje ya nchi bidhaa badala ya kupeleka raw materials.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine la muhimu ni kuendelea kuimarisha na kuboresha miundombinu ya usafirishaji. Bado tunayo changamoto kubwa sana ya miundombinu ya usafirishaji, barabara zetu hasa zile za vijijini ambapo ndiko tunapotoa kule raw materials, tunapotoa bidhaa bado hatujaweza kuziboresha ipasavyo, ninashauri tuendelee kuziboresha barabara zetu za vijijini, SGR yetu pia tuendelee kuhakikisha inakamilika kwa wakati.
MWENYEKITI: Haya asante sana, kengele ya pili imeshagonga.
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru naunga mkono hoja. (Makofi)