Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kawe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2024/2025 ulioletwa mbele yetu na Wizara ya Uwekezaji na Mipango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni muumini wa mipango. Tangu niingie katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nimeongea sana kwa habari ya mipango ya muda mrefu kama njia pekee ya kulipeleka Taifa mahali ambapo linapotakiwa kuwa. Naomba kuzungumza mambo machache ambayo hasa yamekaa kiushauri hasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, ili useme mipango mahali popote katika nchi, data ya kwanza au takwimu ya kwanza ya muhimu ni takwimu ya population. Takwimu ya idadi ya watu ndiyo inaongoza mipango yoyote katika nchi. Idadi ya watu, siyo tu kujua idadi ya watu, ni kuwa na uwezo wa kufanya simulation kwamba kufikia 2050 kwa tunavyoongezeka kwa kuzaana sasa hivi, tutakuwa watu wangapi? Kutokea kwenye simulation hiyo, ndiyo tuweze kupanga mipango ya tunakoelekea baadaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongee hasa kwa habari ya muundo (structure) wa hii Wizara ya Uwekezaji na Mipango. Nafikiri hii Wizara ni ya muhimu sasa kuliko Wizara zote kwa maana hii; kwenye utangulizi wao wameongea kwa habari ya maandlizi ya dira mpya ya Taifa ya 2050. Ina maana tunataka kutengeneza vision au maono ya nchi ya kufikia 2050, lakini ili watengeneze maono haya kwanza kama nilivyosema ni lazima wafanye simulation. Wawe na uwezo wa ku-imagine, for the rate of population, idadi ya watu inavyoongezeka wawe na uwezo wa ku-foresee au kufanya simulation 2050 Tanzania itakuwa imefikia idadi ya watu wangapi ili vision wanayoiweka kwa ajili ya nchi waiweke kwa kuangalia idadi ya watu itakuwa imefikia kiasi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, pia wawe na uwezo wa kufanya simulation ya technology. Maisha tuliyonayo leo ni tofauti na maisha tutakayokuwa nayo 2050. Technology iliyopo leo, ni tofauti kabisa na teknolojia itakayokuwepo 2050. Kwa hiyo, wanapopanga mipango, ni lazima wawe na uwezo wa ku-foresee kwamba ile vision ya 2050 tunayotaka kuiweka katika nchi ita-match na kiwango cha teknolojia na maisha watakayokuwanayo wakati ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, nigusie kidogo tu kuhusu artificial intelligence au ufahamu bandia. Mwaka jana 2022 nilikuwa Uholanzi. Kule kuna gari zisizo na dereva, kuna ma-lawyer robot lakini ni lawyer. Nilikuwa Japan, ma-waiters wengi kwenye hoteli wanawekwa kuwa robot, marubani sasa hivi kwa sababu ya kuepuka ajali, wanaweka robot, wanasheria wanaweka robot, walimu wanaweka robot. Sasa kwenye kupanga mipango ya Taifa, nasi tuweze ku-foresee kwamba tunapopanga mipango ya Taifa tuweze kuona ulimwengu huo tunaouendea wa artificial intelligence (robot): Je, kwa mipango hii tunayopanga leo, itatosha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nikafikiri muundo wa Wizara hii ya Mipango, unatakiwa kuwa tofauti kabisa na muundo wa Wizara nyingine. Kwa mfano, ndugu yangu Kunambi amezungumza hapa akasema kwamba, watu wa madini wamekuja na mpango wao wa 2030, wameutoa wapi? Kwa mfano, ili Wizara ya Mipango ipate mipango yake haitakiwi mtu mmoja au watu wawili au watatu au wataalam wa Wizara hiyo kujifungia ndani na kuanza kupanga mipango ya Taifa ya miaka 2050 ijayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotakiwa kufanyika, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wataalam wake inaandaa mpango wake wa miaka 50; Wizara ya Ardhi Nyumba na Makazi, inaandaa mpango wake wa miaka 50; Wizara ya Kilimo inaandaa mpango wake wa miaka 50; Wizara ya Maji, Wizara ya Mifugo na Wizara ya Uchukuzi wanaandaa mipango yao ya miaka 50 na Mipango hiyo inapelekwa kwenye Wizara ya Mipango. Halafu Wizara ya Mipango inakuwa inagema kwenye hiyo mipango, inatupa mpango wa mwaka mmoja kama mpango iliyoleta, ili kwamba siku zijazo nchi nzima tuwe na mipango inayofanana na mipango isigongane. Leo tunayoita mipango, siyo mipango bali ni mtiririko wa matukio yanayotokea kwa mpangilio. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano kwamba mimi niko Wizara ya Ardhi Maliasili na Utalii. Tunahangaika na Wanyama, wanatoka nje ya hifadhi kwa sababu wanasema maeneo mengi ambayo wanyama wanapita, shoroba zimejengwa. Kwa sababu hiyo, shida ya wanyama kutoka nje ya hifadhi inakuwa kubwa sana kwa sababu shoroba zimejengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shoroba zimejengwa na nani? Ukienda Mvomero pale, Halmashauri ya Mvomero imejenga kwenye ushoroba. UDOM hapo imejengwa kwenye ushoroba, KIA Airport imejengwa kwenye ushoroba na hizi ni taasisi za Serikali zilijenga kwenye ushoroba zikiwa ziomepata building permit. Hii ni kwa sababu ya kukosa maono ya pamoja, kwa hiyo, kama tukipanga maono ya pamoja, tutaondoa contradiction kati ya Wizara hii na Wizara ile na tutaifanya nchi ianze kwenda kwa pamoja kama nchi moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri sana Wizara ya Ardhi inapeleka maono yake ya miaka 50 Mipango, Wizara ya Fedha inapeleka maono yake ya miaka 50 Mipango, Wizara ya kilimo pia. Halafu Wizara ya Mipango inatoka na vision ya miaka 50 ya nchi yote, inakaribisha na stakeholders wengine ambao ni wataalam wa mipango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nadikiri kuwa Wizara ya Mipango inatakiwa kuwa na muundo wa tofauti kabisa na Wizara nyingine ili iweze ku-accommodate maono na vision ya nchi kwa pamoja ili tuweze kwenda tunakoelekea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tabu ya nchi yetu ni kila mtu ana speed kwa mwelekeo tofauti. Narudia tena, tabu ya nchi yetu ni kila mtu ana speed kwa mwelekeo tofauti. Shakespeare aliwahi kusema, una-speed kubwa sawa sawa lakini je, mwelekeo wako ni sawa? Una Speed kubwa lakini una uhakika wa kufika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shida yetu ni hiyo kwamba, tuna speed kali sana lakini kila mtu kwa mwelekeo tofauti. Kwa mfano, ukiangalia Ripoti ya CAG ina leakage kubwa sana ya fedha za Serikali ambazo kama zingelindwa ingekuwa ni rahisi sana kwenda kule ambako tunataka kwenda sawa sawa na ambavyo tumepanga kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nidokeze kidogo halafu nimalize…
MWENYEKITI: Dakika moja malizia, kengele ya pili imekwishagonga.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna idadi ya Wizara 26, kila wizara ikipeleka mipango yake kwenye Wizara ya Mipango, tutakuwa na mipango 26 ya mpaka 2050 iliyoletwa kwa pamoja na hiyo ndiyo itazaa mpango mmoja mmoja wa mwaka ili tuelekee tunakokwenda. Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)