Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudia Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudia Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kwa kukushukuru wewe na wasaidizi wako kwa maana ya Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mussa Zungu, Mheshimiwa Najma Murtaza Giga Mwenyekiti wa Bunge na Mheshimiwa Daniel Baran Sillo Mwenyekiti wa Bunge, kwa jinsi mlivyoendesha mjadala huu kwa umakini na uwazi wa hali ya juu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena kuwashukuru Kamati ya Kuumu ya Bunge ya Bajeti, kwa uchambuzi wao makini na jinsi walivyoibua maeneo mapya katika mapendekezo ya Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote na hususani Wabunge takribani 116 waliopata nafasi ya kuchangia kwa kuongea ndani ya ukumbi huu, kwa maandishi na wale ambao walitoa taarifa. Nilikuwa nahesabu katika mjadala huu kulikuwa na Taarifa 29 na yenyewe ni michango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli binafsi hizi siku tano nilikuwa darasani. Nimejifunza mengi na kubainisha vema zaidi kuhusu kile ambacho watanzania kupitia Waheshimiwa Wabunge, wanataka kutoka kwa Rais wao, Serikali yao na nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unafahamu mimi ni mwalimu. Lazima nikiri kwamba, kupitia mjadala huu nillikuwa nafahamu lakini nimefahamu zaidi kwamba, una Wabunge makini sana. Una wabunge mahiri sana na humu ndani kumesheheni kila aina ya utaalamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana haujawahi kutoa takwimu, jana nilikuwa nafanya uchambuzi kidogo. Nadhani sasa Watanzania wajue kuwa Bunge hili ni tofauti sana. Limejaa watu wenye weledi tofauti na elimu zao ni elimu nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikusudii kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge katika hatua hii. Kwa sababu kwa kweli kazi yetu leo kama Serikali ilikuwa ni kusikiliza na kupokea ushauri na maoni ya Waheshimiwa Wabunge ambayo tumefanya. Kwa hiyo, sikusudii kujibu hoja moja moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli katika mjadala huu sisi kama Serikali tumeweza kubaini vipaumbele vya nchi yetu. tulikuja navyo lakini kupitia michango ya Waheshimiwa Wabunge unaweza ukaona kabisa watanzania wanataka vipaumbele gani. Naomba nikupe takwimu zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uchangiaji huu mpaka jana, Waheshimiwa Wabunge wameongelea mambo 307. Katika mambo haya mgawanyiko wake ni kama ifuatavyo: -

(i) Miundombinu ya usafirishaji ndiyo inayoongoza. Imeongelewa mara 68 kama asilimia 22.

(ii) Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Sekta hii imeongelewa mara 65.

(iii) Nishati imeongelewa mara 36.

(iv) Utalii na Hifadhi mara 38.

(v) Viwanda, Mara 33.

(vi) Biashara na Uwekezaji, mara 25.

(vii) Sekta binafsi, mara 12.

(viii) Afya, Elimu na mengine, mara 30. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, unaweza ukaelewa kwamba, kimsingi katika mipango yetu kwa vyovyote vile lazima tuzingatie maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mjadala wetu tumeendelea pia kubaini baadhi ya kero za wananchi. Tumezipokea na tutazizingatia. Kwa kipekee naomba niwambie wananchi wa Mbalali kwamba, kupitia Mbunge wao makini Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo, tumewasikia. Aidha, tumewasikia wananchi wote wanaoishi karibu na hifadhi mbalimbali nchini. Kwa niaba ya Mheshimiwa Rais na viongozi wetu wengine wakuu na kwa niaba ya Waheshimiwa Mawaziri wenzangu, niwaeleze wananchi kwamba, Rais wetu anathamini maendeleo ya watu kuliko chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila kitu tunachokifanya nia na lengo letu ni hatimaye mwananchi mmoja mmoja, Jamii na nchi yetu kwa ujumla inufaike. Hii ni Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pamoja na sifa nyingine, Rais wetu ni muungwana na mpenda haki. Rais wetu ni Mama mwenye huruma na mapenzi kwa watu wake. Rais wetu ni mwadilifu na mzalendo. Maelekezo yake kwetu ni kwamba, tuwatumikie wananchi na siyo kuwaumiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya yote, hii ni Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. Kwa asili yake, panapotokea mgongano kati ya maendeleo ya Vitu, utu na maisha ya watu, CCM siku zote hukaa upande wa utu na Maisha ya watu. Naomba nirudie, zaidi ya yote hii ni Serikali ya CCM, kwa asili yake, panapotokea mgongano kati ya maendeleo ya vitu, utu na maisha ya watu, siku zote CCM hukaa upande wa utu na maisha ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunao mwongozo, na katika jambo hili tutakaa na kujipanga ili kuona kwamba Hifadhi zetu haziwi kikwazo au kugeuka mateso kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi zetu lazima zithamini maisha ya wananchi ili wananchi wazithamini. Tutajipanga na tutakuja na jibu endelevu katika suala hili. Hata hivyo, lazima pia tuombe Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwamba, nchi yetu tayari tumekwishaamua kwamba, ni nchi itakayoongozwa kwa mujibu wa utawala wa Sheria. Tuombe sote tuzingatie Sheria, kama kuna Sheria zina shida ndiyo maana Bunge linakaa kila siku, tuje tubadilishe ili Sheria zitutumikie na siyo sisi kuzitumikia Sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mjadala huu Waheshimiwa Wabunge wamebainisha na kusisitiza baadhi ya maeneo mapya ya kipaumbele ambayo kwa kweli katika mpango ama hayakuweko ama hatukuyapatia uzito wa kutosha, tutayazingatia. Mambo haya ni pamoja na yafuatayo: -

(i) Artificial intelligence, naomba nitamke hivyo kwa sababu wataalamu wa Kiswahili bado hawajawa na jibu sahihi la what is artificial intelligence in Kiswahili?

(ii) Uchumi wa gesi.

(iii) Fursa za kijiografia kwenye kutafuta maendeleo.

(iv) Fursa za mabadiliko ya Tabia ya nchi hasa suala la hewa ya ukaa.

(v) Haja ya kuanzisha mamlaka ya ufugaji na uvuvi, hili limejitokeza. Pia, kwa kweli katika nchi yetu karibu kila sekta ina chombo kinachoisimamia. Hata hivyo, suala la ufugaji na uvuvi nadhani ni eneo la kuliangalia kwa umakini sana.

(vi) Imejitokeza haja ya kuanzisha mamlaka ya maendeleo vijijini. Haya ni mambo ambayo tutayaangalia na kuyazingatia katika kuandaa Mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kusisitiza na kutolea ufafanuzi kidogo kwenye maeneo mawili anbayo yamesisitizwa sana na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni maendeleo vijijini na nashukuru na kufurahi kuona kwamba Waheshimiwa Wabunge wameunga mkono na kuweka uzito mkubwa katika eneo hili. Kimsingi tayari tunao msingi wa maendeleo vijijini yanaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia TARURA mtandao wa barabara vijijini umongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni; kupitia REA vijiji vingi sana vina umeme, kupitia RUWASA huduma ya maji imeendelea kusambazwa. Aidha, huduma za Afya na Elimu zinazidi kusambaa katika vijiji vyote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, watu wetu wakishakuwa na afya, wakapatiwa elimu, wakapata maji na umeme na wakaunganishwa katika mtandano wa barabara, tunahitaji kutumia yote haya kama nyenzo ya kuchochea uzalishaji ili hatimaye wananchi wetu huko vijijini wapate fursa za kiuchumi na kutengeneza vipato. Ndiyo nia yetu ya kusisitiza umuhimu wa kuvutia uwekezaji wa viwanda vidogo vidogo vijijini kwa ajili ya kufanya primary processing. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, umuhimu wa kujenga muafaka wa kitaifa. Wataalamu wa maendeleo wanakubaliana kwamba, moja ya kikwazo cha maendeleo katika nchi yoyote ile, ni pale ambapo panakuwa hakuna muafaka kuhusu Mpango na vipaumbele vya maendeleo miongoni mwa wananchi na hususani watu wenye sauti katika jamii, wakiwemo viongozi wa makundi mbalimbali, wasomi, wafanyabiashara, wanasiasa nakadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana ni muhimu sana kushirikishana ili tukubaliane sote. Tukubaliane tunakwenda wapi? Kama ni kubishana tubishane njia ya kwenda, kama safari yetu ni Mwanza wote tuelekee Mwanza. Mwingine aseme nakwenda kwa gari, ndege, helikopta nakadhalika lakini tunakwenda wapi? Tuwe na mwelekeo mmoja ni jambo la msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihitimishe kwa kujibu swali moja ambalo Waheshimiwa Wabunge wameliuliza na lenyewe je, nilipozungumizia kwenye hotuba yangu nilizungumzia umuhimu wa kuwa na watu wazuri kwenye Serikali. Pia, Waheshimiwa Wabunge wameuliza, je, tuna watu wazuri katika utumishi wetu wa umma? Jibu langu ni ndiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaposema ndiyo, narejea na ninaangalia walimu zaidi ya 250,000 ambao wanafundisha na kulea watoto wetu sisi tukiwa hapa. Ninapozungumzia watu wazuri, ninazungumzia zaidi ya madakatari na manesi zaidi ya 48,000 wanaotibu watu wetu katika zahanati na vituo vyetu vya afya kwa kiwango ambacho leo Tanzania ndiyo nchi yenye vifo vichache vya wakinamama kusini mwa jangwa la Sahara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazungumzia zaidi ya mafundi 9,000 ambao wanasambaza maji vijijini. Ninazingatia uadilifu, uzalendo na umakini wa Rais wangu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Baraza lake la Mawaziri. Ninazungumzia umakini wa viongozi wangu wakuu, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na kwingine. Of course, ninapouzungumzia kwamba tunao, ninazungumzia umakini, uzalendo na umahiri wa Spika wangu Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, wote hawani watu wema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachopaswa kufanya ni kuimarisha mifumo yetu ya uwajibikaji na kuendelea kujenga uwezo wa watu wetu kwenye utumishi wa umma. Hatuwezi kukata mwembe wote kwa sababu ya kuoza kwa maembe mawili. Tuyaondoe maembe mawili yaliooza lakini lazima mwembe ubaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamalizia kwa kusema, ninakubaliana na Waheshimiwa Wabunge kuhusu umuhimu wa kuzingatia maadili kwa watoto wetu. Hata hivyo, tunapoendelea kuelimisha vijana wetu kuhusu maadili, tusije tukawaondolea haki yao ya kuwa watoto. Ni muhimu watoto wakabaki kuwa watoto, kwa sababu bila hivyo watakuja kufanya utoto wakiwa watu wazima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuzingatie kuwa utoto wa watoto wetu hauwezi kuwa utoto ulivyokuwa utoto wetu sisi. Utoto wa watoto wetu mazingira ni tofauti na tukitaka wawe kama tulivyokuwa sisi, tutakuwa tunawakosea. Tuache watoto wawe watoto, tuwape maadili lakini ni muhimu wawe watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo niseme tena kuwa, sisi kama Serikali tumepokea maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge na tutayazingatia katika kuandaa Mpango wa Maendeleo ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsanteni sana kwa fursa hii. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika. Ahsante sana. (Makofi)