Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami nitoe mchango wangu kwenye hoja iliyoko mbele yetu. La kwanza, naomba kuunga mkono hoja iliyoletwa Mezani. Kwa nini naunga mkono hoja hii? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la ugatuaji wa madaraka, suala la uwajibikaji haujaanza leo wala jana. Suala la watu wa TARURA au RUWASA tumekuwa humu ndani, tulianza kupiga kelele. Wakati wakiwa wanasimamiwa na halmashauri, halmashauri zetu zilikuwa haziwapi nafasi watumishi wetu wa kwenye hizi idara ili ziweze kutekeleza wajibu na majukumu yao. ndiyo maana Bunge likafikia maamuzi ya kuwatoa RUWASA pamoja na TARURA wawe taasisi wanaojitegemea waweze kupata fedha lakini pili waweze kutekeleza wajibu na majukumu yao.
Mheshimiwa Spika…
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
TAARIFA
SPIKA: Mheshimiwa Kunti Majala kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Londo.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, wahandisi wa TARURA ama RUWASA walikuwa wameishia kwenye ngazi ya wilaya. Kuna wilaya ambazo walikuwa wana mmoja, wawili na halmashauri nyingine hazikuwa hata na mmoja. Unapozungumzia Maafisa Ugani unawazungumzia wataalamu ambao wako kwenye ngazi ya kijiji. (Makofi)
SPIKA: Haya. Mheshimiwa Kunti Majala unaipokea taarifa hiyo?
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, suala la wahandisi na suala la watu wa maji kuishia wilayani, hilo siyo suala la Bunge wala halmashauri, ni suala la Mpango ambao mmepanga ninyi wenyewe Serikali. Mlikuwa na sababu ya kuwapeleka mpaka mikoani. Tunachoangalia hapa, ni namna gani Maafisa Ushirika na Maafisa Ugani wanatekeleza majukumu yao kwenye halmashauri zao? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikupe mfano.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, taarifa.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, leo tumegawa pikipiki kwa Maafisa Ugani kwenye halmashauri zetu. Uliza zile pikipiki leo zinafanya nini kwenye halmashauri zetu? Wabunge mko humu ndani. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Kunti, kuna taarifa nyingine kutoka kwa Mheshimiwa Jumanne Sagini.
TAARIFA
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ninaheshimu sana mchango wa Mheshimiwa Mbunge anayezungumza, na nimeridhia alivyosema kwamba masuala ya ugatuaji hayajaanza leo. Tulivyoanza uhuru Serikali yetu ilikuwa highly centralized, mwaka 1972 tukafanya deconcentration kwa madaraka mikoani.
SPIKA: Sawa, mpe taarifa nitakupa muda wako wa kuchangia. Mpe taarifa Mbunge.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kama nitapata muda, lakini taarifa ninayotaka kumpa ni kwamba mwaka 1982 Mwalimu Nyerere aliulizwa, katika vitu anavyoumia ambavyo amekosea akiwa madarakani ni yapi? Alitaja mambo mawili. Moja ilikuwa ni kuua ushirika; na la pili kuua Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimpe taarifa kama ataipokea. Ndiyo maana mwaka 1984 ikarudishwa kwenye Katiba, nashukuru. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Kunti unaipokea taarifa hiyo?
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, siipokei. Laiti kungekuwa na uwezekano wa Hayati Baba wa Taifa kufufuka, akaja akasimama hapa mbele, akaona ubadhirifu unaofanywa na Maafisa Ushirika pamoja na ushirika kwa ujumla wake, tungelaaniwa sisi Wabunge humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo…
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, taarifa. (Kicheko)
TAARIFA
SPIKA: Mheshimiwa Kunti kuna taarifa nyingine kutoka kwa Mheshimiwa Ole-Sendeka. (Kicheko)
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, sisi wote tumekula kiapo cha kulinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Ibara ya 146 inasema, “Madhumuni ya kuwapo kwa Serikali za Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi na vyombo vya Serikali za Mitaa vitakuwa na haki na mamlaka ya kushiriki, kuwashirikisha wananchi katika mipango na shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika sehemu zao na nchini kote kwa ujumla.” (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapeleka madaraka karibu na wananchi. Kimsingi, natoa ushauri kwamba pendekezo lako la jambo hili kwenda kwenye Kamati na baadaye lirudi kwenye Bunge zima itakuwa jambo la maana ili tuje tushauriane, turudishe shughuli zote zilizoondoka kwenye Serikali za Mitaa.
SPIKA: Mheshimiwa Ole-Sendeka.
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Naam Mheshimiwa Spika. (Kicheko/Makofi)
SPIKA: Waheshimiwa tusikilizane. Spika akishafanya maamuzi huwezi kuyahoji hapa ndani. Unaruhusiwa kuyahoji kwa kutumia Kanuni ya tano kwa kuandika kwa Katibu wa Bunge. Mimi nimefanya maamuzi ya kuileta hapa ndani, hoja itaamuliwa hapa ndani, haitaenda kwenye Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Kunti unaipokea taarifa hiyo?
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, siipokei kwa sababu hata TARURA leo wanafanya kazi chini kule kwa wananchi wetu wakishirikiana na halmashauri hizo hizo. Kwa hiyo, ninachokisema hapa, hawa Maafisa Ugani na Maafisa Ushirika warudi kwenye Wizara ili tuipe fursa Wizara kufanya maamuzi ya kiuwajibikaji wanapokosea Maafisa Ushirika wetu kule chini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo Maafisa Ushirika na Maafisa Ugani wakifanya makosa…
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, taarifa.
MBUNGE FULANI: Nyie tulieni jamani. (Kicheko)
TAARIFA
SPIKA: Sawa. Sasa nimempa sekunde 30, halafu inatakiwa kutoka taarifa hapo. Basi sekunde 15 kwa 15. Haya Mheshimiwa Kunti kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Prof. Ndakidemi.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mchangiaji kwamba yale maeneo yote muhimu kwa mfano utafiti, masuala ya mbegu, masuala ya umwagiliaji ambayo Waziri wa Kilimo anasimamia, mambo yanakwenda vizuri.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nampa taarifa kwamba anachokisema ni sawa. Tukifanya hivyo mambo yatakwenda vizuri zaidi kama ilivyo kwenye hizo sehemu nilizochangia. (Makofi/Kicheko)
SPIKA: Haya. Sasa inaonekana jamani macho yangu yaliona wapinga hoja, halafu wakubali hoja wote inaonekana sikuwaona. (Kicheko)
Haya Mheshimiwa Kunti unaipokea taarifa hiyo?
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa unyenyekevu mkubwa kwa maslahi mapana ya Taifa letu na wakulima wetu nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nihitimishe hivi. Tunachohitaji hapa siyo nani anawahudumia akina nani? Sote sisi watumishi, sote sisi wawakilishi tunawatumikia Watanzania wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kujali utakuwa Wizarani ama bila kujali utakuwa wapi? Tunachotaka ni uwajibikaji na utumishi uliotukuka kwa Watanzania wenzetu.
SPIKA: Haya, ahsante sana.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hoja iliyoko Mezani mimi naiunga mkono, watumishi hawa; Maafisa Ugani na Maafisa Ushirika warudi Wizarani ili Wizara iweze kuwasimamia watu wake vizuri na iweze kuleta tija, nakushukuru. (Makofi)