Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rufiji
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nitambue dhana iliyoibuliwa yenye dhamira ya kuchangamsha fikra za maamuzi mbalimbali katika Taifa letu na nikushukuru kwa kuridhi dhana hii kujadiliwa. Kama ambavyo kaka yangu aliyekaa muda huu amezungumza hapa. Nchi hii ni ya wananchi, msingi wa Serikali katika kuamua mambo yoyote ni lazima yaamuliwe na wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Simbachawene amezungumzia Ibara ya 8 lakini ukienda Ibara ya 21 inazungumza misingi ya maamuzi mbalimbali ambayo inawashirikisha wananchi kupitia wawakilishi wa wananchi, Wabunge na Madiwani.
Mheshimiwa Spika, swali la kujiuliza hapa ni utekelezaji wa wajibu wa kila mmoja wetu. Hata ukiwasikiliza Waheshimiwa Wabunge, malalamiko ya Waheshimiwa Wabunge ni namna gani wale walioko kule chini wanashindwa kutekeleza wajibu wao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, dhana ya ugatuzi wa madaraka huu ni msingi ambao wa Baba wa Taifa ameturithisha kabla ya kuondoka kwake. Imeingizwa kwenye Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 145 ambayo Mheshimiwa Sendeka ameizungumza hapa. Huko tunakoelekea leo pengine tuna miezi 11 twende kwenye chaguzi na pengine baada ya mwaka mmoja tuna Uchaguzi Mkuu.
Mheshimiwa Spika, swali la kujiuliza hivi leo, maeneo mengi ambayo yameondolewa kutoka TAMISEMI, kutoka kwenye Serikali kule chini yanatuletea matatizo makubwa sana. Hasa ukiangalia kwa mfano tuna migogoro mingi sana ya ardhi eneo hili. Tumekwisha kaa tumezungumza na Waziri wa Ardhi tumekubaliana kwamba hili pia tulipitie na tuone uwezekano wa kuirudisha TAMISEMI. Leo hii… (Makofi)
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, taarifa.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, leo hii…
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Waziri, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Godwin Kunambi.
TAARIFA
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante namuunga mkono Mheshimiwa Waziri Mchengerwa. Kimsingi sio tu kupoka madaraka kwa wananchi kinachokwenda kutokea ni failure ya hawa wanaopelekwa kwenye Wizara ya Kisekta, mfano mzuri Wizara ya Ardhi leo hii hatutatatua migogoro ya ardhi kamwe nchi hii kama hatujarejesha watumishi wa ardhi TAMISEMI, ahsante.
SPIKA: Sina uhakika nimesikia vizuri, umesema nchi hii hatutatatua?
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, nasema hivi, naomba kurejea; nchi hii kama kuna kosa tulifanya ni kutwaa watumishi wa ardhi kutoka TAMISEMI kwenda Wizara ya Ardhi ambayo ni ya Kisekta.
SPIKA: Haya ahsante sana. Mheshimiwa Mchengerwa unaipokea taarifa hiyo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nimeipokea taarifa hii kwa mikono miwili, ni makosa makubwa yalifanyika katika eneo hili na tumekubaliana na Waziri wa Ardhi kwamba suala hili tunakwenda kulifanyia kazi ili hawa watu waje kwangu niwashughulikie vizuri. (Makofi)
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika…
SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kunti Majala.
TAARIFA
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nataka nimpe mzungumzaji anyezungumza kwamba hawa maafisa ardhi walikuwa TAMISEMI tangu enzi hizo na migogoro ilikuwa imekithiri. Wakati huo kumbuka wewe ndiyo ulikuwa Wizara ni hiyo hiyo moja. Vijiji na vitongoji mnapanga ninyi lakini mkitoka hapo suala la ardhi wako kwako mkienda mnawaambia wananchi wamevamia na ninyi ndiyo mlikuwa mnapima mipaka. Kwa hiyo, hiyo haiwezekani kwamba hao watu kutolewa kupelekwa kwenye Wizara ya Kisekta eti mmepunguza migogoro. Hamjapunguza wala hamja… nakushukuru.
SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa unapokea taarifa hiyo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nakuomba unilindie muda, ni vema…
SPIKA: Mheshimiwa ngoja, muda wa taarifa ni sehemu ya muda wako kwa sababu anaboresha mchango wako.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni vema Waheshimiwa Wabunge wakatofautisha masuala ya kiutawala na masuala ya kisera lazima tutofautishe. Lakini… (Makofi)
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, taarifa niko hapa.
SPIKA: SPIKA: Hii ni taarifa ya mwisho kwa Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Miraji Mtaturu.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba siku zote chakula ili kinoge ni lazima kiwe na chumvi. Kilimo kiko kwa wananchi wa chini kabisa kwenye kitongoji utakapokiondoa kilimo kwa maana ya afisa ushirika ukamtoa pale kijijini kilimo kitakufa. Kwa hiyo, naomba nimpe taarifa mtoa taarifa kwamba maafisa ushirika wabaki katika eneo la halmashauri ili wasimamie vizuri kilimo chetu. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Mchengerwa Sekunde 30 kengele ya pili imeshagongwa, samahani kengele imeshagongwa.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nimepokea taarifa lakini jambo hili ni kubwa na niwaombe pamoja na dhana njema ya kulileta hapa Bungeni watuachie Serikali tukalijadili kwa kina na tutaangalia sehemu yenye mapungufu tutakwenda kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, juzi tulichukua maamuzi ya kuwaondoa baadhi ya watendaji kule Mbeya Mjini walioshiriki kwenye ubadhilifu fulani baada ya maamuzi kutolewa na madiwani lakini kama hao pia wangeenda kwenye sekta husika.
SPIKA: Hapo nakuongezea sekunde 30, Waheshimiwa Wabunge humu ndani si huwa tunazungumzia watu wanaofanya kazi vibaya na vizuri? Sasa kama Mkurugenzi wangu wa jiji anafanya kazi vizuri msifie kidogo Mheshimiwa Waziri. (Kicheko/Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge pamoja na nia njema ya kuleta jambo hili. Tukumbuke kwamba tuna changuzi mbele yetu, siku chache tuna chaguzi mbele yetu. Nawaomba sana mridhie jambo hili mliache kama lilivyo ili tuweze kufanya kazi nzuri ya kuhakikisha kwamba tunawasimamia hawa vema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, inawezekana kabisa kwamba jambo la usimamizi lakini nichukue fursa hii kumpongeza mkurugenzi wa Jiji la Mbeya kwa kazi kubwa na kazi nzuri na niwaombe wakurugenzi wengine kwenye maeneo mbalimbali wachukue maamuzi kama haya itatusaidia sana Waheshimiwa Wabunge kuhakikisha kwamba miradi yetu inatekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumuomba mtoa hoja aridhie jambo hili linbaki ndani ya Serikali na sisi tutakaa na Wizara ya Kilimo tuone ni namna gani tunaweza ku…
Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Muda wake umekwisha, Mheshimiwa Waziri weka nukta hapo. Muda umekwisha Mheshimiwa.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru ahsante.