Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wake na Watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa bajeti nzuri yenye kutatua changamoto mbalimbali za wananchi wa Tanzania ikiwemo wakulima, wafugaji na wavuvi na wafanyabiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa pia ndiye Mwenyekiti wetu wa Chama cha Mapinduzi kwa kuiongoza nchi yetu kwa kutumia busara na weledi wa kuhakikisha nchi yetu inavuka salama katika matukio mbalimbali yaliyotukumba ya kidunia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na sekta ya kilimo. Naipongeza Serikali kwa kuweka bajeti kubwa kwenye Wizara ya Kilimo ambapo sasa kilimo chetu kitakwenda kuwa kilimo chenye tija lakini kilimo kitachomkomboa mkulima mdogomdogo na mkubwa pia kuongeza uchumi wa nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na bajeti kubwa hiyo ya kilimo ambapo nitakwenda kujikita kwenye kilimo cha umwagiliaji, mambo ya viuatilifu, Maafisa Ugani, tunayo mazao ya biashara ambayo wakulima wetu wanapata tija kupitia biashara na Serikali inapata mapato. Naomba kuishauri Serikali pamoja na mazao yetu ya biashara nashauri kwamba kutokana na changamoto zetu za ndani ya nchi tuchague mazao fulani ya kimkakati kwa maana ya kwamba tujikite kwa kipindi cha miaka miwili au mitatu Tanzania tunakwenda kuondokana na tatizo ama la mafuta ya kupikia, sukari au jambo jingine ili tukifika hatua hiyo tukaweza kujitosheleza na tukaweza kuuza baadae tunajiwekea kipindi kingine kutatua changamoto nyingine ambayo inatukabili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu sekta ya uvuvi, naipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali za kuinua uvuvi hapa nchini, kwa kununua vifaa mbalimbali vya uvuvi na kuwasaidia wavuvi wetu. Katika kuimarisha uvuvi wa Bahari Kuu lazima taasisi mbili ziimarishwe ambayo ni TAFICO na ZAFICO. Kwa upande wa TAFICO bado miundombinu yake haijawa kamilifu na kwa bajeti hii itachukua muda kukamilika pamoja na bajeti iliyotengwa nashauri Serikali itafute fedha zaidi ili kuhakikisha TAFICO inafufuka na inafanya kazi zake. Kwa sababu kwenye TAFICO kuna miundombinu ambayo inagharimu fedha nyingi ikiwemo vyumba vya kuhifadhia samaki, vyumba vya kuweka majokofu ya baridi, inatakiwa kutengenezwa gati, inatakiwa kujenga majengo. Majengo ambayo sasa yapo kwenye fukwe ambazo fukwe zinaliwa na bahari, kwa hivyo, panahitajika fedha za kutosha ili kulifufua hili Shirika la TAFICO liweze kujikimu na kujikita katika uzalishaji utakapofika huu uvuvi wa Bahari Kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza Serikali pia kwa kuwekeza kwenye sekta ya maji kwa kununua mitambo na vitendea kazi vya kuchimba visima na mabwawa na hili ndiyo hasa dhamira ya Serikali kwamba kumtua ndoo mwanamke kichwani pia kuhamasisha kilimo, ufugaji na uvuvi. Kwa hivyo, vitu vitatu hivi vimeenda sambamba naipongeza sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kwenye sekta ya mazingira tumeona kwenye bajeti yetu ya Serikali kuna mambo ya mazingira yanakwenda kutekelezwa, lakini mazingira tuyatazame kwa ukubwa na upana wake kulingana na mabadiliko ya tabianchi. Mabadiliko ya tabianchi yanaharibu sana mazingira yetu, kwa hivyo ni vizuri kuwekeza zaidi kwenye kuhifadhi mazingira yetu ili tubaki na nchi ikiwa salama na ubora wake kama ulivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha katika bajeti hii kutambua mchango wa asasi zisizo za Kiserikali katika kuinua uchumi wa Taifa, kuinua uchumi wa wananchi na kuleta maendeleo katika jamii yetu, nampongeza sana kwa kutambua mchango wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naongozea pale katika kuwekeza sekta ya kilimo tumeona kuna fedha hapa zimetengwa Bilioni 6.1 kwa ajili ya kumalizia kiwanda cha mbolea. Bado naendelea kusisitiza mbolea ni silaha, tunahitaji mbolea ya kutosha kwa ajili ya kilimo chetu hapa nchini, mbolea za aina mbalimbali kutokana na udongo wetu na mazingira yetu. Kwa hivyo, kuna haja Serikali kuwekeza zaidi kwenye viwanda vya mbolea ili tuweze kujitosheleza hapa nchini kwa mbolea na tuache kuagiza nje mbolea. Kwa sababu ardhi tunayo, malighafi tunayo na fedha tunaweza tukapata katika maeneo mbalimbali kama hizi tulizozitafuta na tutafute kuhamasisha wananchi wa humu ndani ya nchi kuwekeza katika sekta ya viwanda vya mbolea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi kumpongeza Mheshimiwa Waziri katika bajeti yake katika ukurasa wa 74 ameeleza kwa hisia jinsi ya kukitumia Kiswahili na kukienzi Kiswahili. Kiswahili ni fursa, Kiswahili ni ajira, Kiswahili ni bidhaa, pindi tukikitumia vizuri Kiswahili nchi yetu tutazidi kuitangaza na hapa tuunganishe na tuongeze na utalii wa lugha, utalii wa lugha utatuongezea mapato katika nchi na kuitangaza nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utalii si kwa watu wa rangi ya aina Fulani, sasa hivi tunapata watalii wa Afrika wenzetu wanaokuja Tanzania kwa sababu tu ya lugha ya Kiswahili na wakifika hapa Tanzania wanapata fursa ya kuona hivyo vivutio vingine vya utalii kwa maana walikuja tu kwa sababu ya kuona hiyo Tanzania inayosifika na lugha ya Kiswahili inayokua duniani wanataka kuja kuona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosisitiza hapa tuwekeze kwenye watalaam, tuwape motisha wataalam wetu wa lugha ya Kiswahili pia tuweke motisha kwa wanafunzi waweze kujikita katika kusoma Kiswahili na kukisomea na kuwa watalaam, kwa maana ya kuwapatia mikopo na motisha mbalimbali ili tukipende Kiswahili kama tunavyopenda masomo ya sayansi na Kiswahili nacho tukipe kipaumbele. Hayo ni mawazo yangu kwamba wasomi wa Kiswahili tuwaongezee weledi kwa maana ya kwamba tuwekeze wajifunze lugha zaidi ya mbili ndiyo soko linapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiswahili chetu tusiruhusu kikatekwa, ninachotaka kusema sasa hivi kuna lugha zinazungumzwa kwamba Kiswahili kimeanzia nchi fulani kimekuja Tanzania kimefia mahali fulani. Kiswahili ni mali yetu Watanzania tusikubali kikaporwa ikawa kama Mlima Kilimanjaro, sasa hivi Kiswahili ni rasilimali ya nchi tukienzi, tukitunze, tuhakikishe kinakua na kitambulisha nchi yetu, wajanja wasije wakatupora lugha yetu na ndiyo maana nasisitiza tuwekeze kwenye lugha ya Kiswahili kwa kuhamasisha vijana wetu wasome lugha zaidi ya moja au mbili ili tupate soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kiswahili tunapokwenda kupeleka watalaam katika nchi fulani ambayo hawazungumzi kiingereza sisi tunapata nini? Tuhakikishe na zile nchi wanafundishwa wanafunzi wetu lugha nyingi kama Kifaransa, Kibelgiji, Kireno, kwa sababu sisi tunawapa lakini baada ya muda Walimu wetu watakua hawana tena kazi, watafundishana wenyewe kwa wenyewe hilo tuweke angalizo. Watafundishana wenyewe kwa wenyewe ndani ya nchi kutokana na zile lugha zao za ndani wanazozitumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano kuna nchi inaongea Kifaransa baada ya muda hawa watu wetu wakifika huko Wafaransa watachukuana na nchi nyingine za Kifaransa watakwenda huko watasomeshana, ndiyo maana nasema tuwape na sisi tuchukue kwa maana na sisi tupate zile lugha zingine za Kifaransa, Kireno, Kigiriki tuzipate Watanzania, tusibaki tu na Kiswahili na Kiingereza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho namalizia kwa kuipongeza sana Serikali, tumuunge mkono Rais wetu katika kuwaletea wananchi maendeleo tupo nae bega bega. Ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)