Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Bahati Keneth Ndingo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mbarali

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. BAHATI K. NDINGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kupata fursa nami nianze kwa kuipongeza sana Serikali inayoongozwa na Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kufanya. Niungane na Waheshimiwa Wabunge kuipongeza sana Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri mnayoifanya kwa bajeti nzuri ambayo mmeileta Bungeni, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri bajeti hii kama ikitekelezwa kwa ufanisi walau hata kwa asilimia 50, kwa ufasaha, nina uhakikia uhakika kabisa tutapiga hatua kama Taifa. Leo hii mchango wangu niuelekeze kwenye Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, tumekuwa mashuhuda humu ndani na ripoti ambazo zimekuwa zikitolewa na Mdhibiti wa Hesabu. Ripoti zile zinakuwa na upotevu mkubwa sana wa fedha. Laiti kama tungeweza kuwekeza nguvu kubwa kwa huyu Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kumtengenezea miundombinu rafiki ya ufanyaji kazi wake, ninaamini kabisa tungeweza kuokoa fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sio mwanasheria, lakini nimejaribu kupitia na kusoma, nimeenda kwenye Katiba yetu ya mwaka 1977 na marekebisho yake, Ibara ile ya 143 imemtaja Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali na imeainisha pale majukumu makubwa matatu. Jukumu la kwanza; ni kudhibiti fedha zote zitakazotoka kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, lakini jukumu la pili alilopewa mdhibiti huyu ni kuhakikisha matumizi yote ya kwenye mfuko huo wa Serikali yamepitishwa na Sheria ya Bunge. Kazi yake ya tatu, ni kufanya ukaguzi walau mara moja kwa mwaka na kutoa ripoti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napata shida kidogo nikija kwenye Sheria ya Ukaguzi wa Umma. Sheria yenyewe inaitwa Public Audit Act, ile Sura ya 418. Sasa sheria hii ambayo ndiyo inaanzisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, imeshaondoa neno “mdhibiti”; pale ni ku-audit. Nikisoma hiyo sheria hiyo, nimejaribu kusoma, kwa uelewa wangu, sijaona muundo wala uongozaji wowote wa mdhibiti huyo anafanyaje udhibiti wa hesabu. Nilichokiona hapa kwenye sheria hii, ni namna gani atakagua; kwa hiyo, nimeona muundo na utendaji kazi wake katika kukagua peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali anatembelea mguu mmoja wa auditing peke yake, lakini udhibiti sheria hii hatujaweza kuitafsiri vizuri Katiba inavyotaka. Ndivyo nilivyoona mimi kwamba sheria hii imetufanya tusiitafsiri vizuri Katiba, hivyo tumeelekeza majukumu yote ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali katika ku-audit lakini kwenye ku-control hatujaweza kulifanya hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine, kwa mfano kwenye ripoti ya ukaguzi, hii ya 2020/2021 CAG anahoji kuwepo kwa Halmashauri 19 ambazo zilipokea shilingi bilioni 47.19 za miradi ya maendeleo zaidi ya bajeti iliyopangwa. Sasa kama huyu ndio controller, ame- control vipi? Kama huyu controller naye anahoji kuzidisha na kuweka matumizi nje ya bajeti, kwa hiyo, tunaona kabisa suala la udhibiti kwa huyu Mkaguzi na Mdhibiti, bado suala la udhibiti hatujalipa nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba nishauri mambo mawili tu kwa Serikali kwenye suala hili. Kwanza, Serikali iangalie uwezekano wa kutenganisha hizi nafasi mbili; ukaguzi na udhibiti; nasi tutakuwa siyo nchi ya kwanza kufanya hivyo. Nchi nyingi tayari zimeshaondoka huko, hata majirani zetu hapo Kenya. Ukishasema kwamba mdhibiti huyo huyo asaini fedha zitoke, huyo huyo akajikague, ufanisi hautakuwa vile kama ulivyo. Kwa hiyo, nilikuwa nashauri tuone uwezekano wa kutenganisha kazi hizi mbili kuleta ufanisi na kupunguza na kutokomeza kabisa upotevu wa mali za umma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, naiomba Serikali ili tuweze kudhibiti mali za umma, waje na miongozo iletwe Bungeni Sheria ya udhibiti ili tumwelekeze huyu atadhibiti vipi na atafanyaje kazi za udhibiti na ripoti zake zitakuwa zinaletwa vipi? Kuliko kusoma tu ripoti za ukaguzi wakati udhibiti tumeuacha pembeni. Kwa hiyo, naomba haya yazingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu, hii nchi ni kubwa, lakini nchi yote hii kila Halmashauri inategemea Mfuko Mkuu wa Serikali. Tumeshauri hapa, tunaomba Wizara ya Fedha shirikianeni na TAMISEMI, wekeni mkazo kwenye hati fungani za Serikali za Mitaa. Serikali za Mitaa zianze sasa utaratibu wa kufanya miradi yao kibiashara, watu wanunue hisa zao watengeneze miradi. Hii ya kusema kila Halmashauri kutegemea Serikali Kuu, tunajichelewesha, kwa sababu hatuwezi kama Taifa kila Halmashauri kuitimizia mambo yake. Hatuwezi!

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana mjitahidi, msisitize uwazishwaji wa hizi hati fungani, ukamilike ili Halmashauri zetu ziweze kujiendesha kibiashara. Kwanza kwa kufanya hivyo, mtaweza kusaidia Halmashauri hizi, watu wawe wamiliki wa miradi ile, lakini vile vile watakuwa wanapata fedha kwa riba ndogo. Maana yake ni tofauti na kukopa fedha kwenye benki. Hati fungani zina riba ndogo. Kwa hiyo, mhakikishe hizi Halmashauri zinaweza kujifanyia miradi ya maendeleo na ikabuni miradi mikubwa ambayo baadaye itakuwa ndiyo vitega uchumi vya Halmashauri zetu kuliko Halmashauri zote kutegemea Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru, na ninaunga mkono hoja. (Makofi)