Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali yake ya Awamu ya Sita kwa jinsi ambavyo inaendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Nitahitaji karibu siku nzima kutaja miradi ambayo iko katika jimbo langu, kwa hiyo itoshe kusema tunamshukuru sana na tunaendelea kushukuru kwa niaba ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuzungumzia miundombinu ya barabara na nimwombe Mheshimiwa Waziri kwamba wakati wa kusoma bajeti alitaja barabara kadhaa. Nitamweleza hii barabara na anahitaji tu kuiongeza, haiongezi fedha kwenye bajeti yake tayari ipo. Barabara ya kutoka Iringa kwenda Kilolo ambayo itajengwa kwa kupitia fedha za Rais. Nimejiridhisha na TANROADS kwamba ipo kwenye taratibu za kuandaliwa tenda, lakini wananchi wa Kilolo waliniuliza kwamba kwa nini Waziri hakuitaja. Basi kwenye hitimisho Mheshimiwa Waziri aitaje tu kwa sababu tayari iko kwenye mipango ili wananchi waweze kuelewa kwamba ni mojawapo ya barabara zitakazotengenezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kiutaratibu magari yetu huwa yanakuwa na spare tyre kwa maana kwamba kukitokea dharura basi ile tairi inasaidia kufunga na kuondoka. Barabara ya kutoka Dar es Salaam hadi Mbeya, Tunduma na inayoenda Kyela ipo sehemu moja yenye shida kubwa ambayo huwezi kuchepuka kwa namna yoyote ile na hii ni ile sehemu ya Mlima Kitonga na nimeitaja mara nyingi hapa. Naomba nisikilizwe kwa sababu ni kwa maslahi ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukifika pale kama kukitokea gari ikaharibika kwa sababu zile kona ni nyingi na mara nyingine magari kupinduka na hayo ni matukio ya mara kwa mara, hakuna njia nyingine, kwa maana nyingine barabara ile inakuwa imefungwa na hakuna pakupita. Maana yake ni kwamba lazima kutafuta mbadala ili magari yaweze kuzunguka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni kulitokea tukio kama hilo na wakati napita pale Ilula kulikuwa na ambulance tatu kutoka Mbeya na kutoka Iringa ambazo zilikuwa zinaelekea Dar es Salaam zina wagonjwa ndani. Kama hiyo haitoshi hivi karibuni kutoka Ruaha Mbuyuni kwenye Kituo cha Afya kuna mama mmoja ambaye alikuwa wa kujifungua, alifia pale kwa sababu tayari kulikuwa kumezibwa ile njia pale. Hayo ni matukio ya kiafya, lakini bado hatujazungumzia madhara ya kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkuu wa Mkoa alishawahi kukwama pale, wako Mawaziri walishawahi kukwama pale na Mheshimiwa Waziri wa Fedha asisubiri aje akwame pale ndipo aseme, alichokuwa anasema Mheshimiwa Mbunge kilikuwa cha muhimu. Niombe barabara ya mchepuko ambayo nimesema kwamba tumeshaanza kuitengeneza kwa kupitia fedha za UVIKO kutoka Mahenge kwenda Udekwa, inapita inatoka pale Ilula ni kilomita chache sana na ikitengenezwa itakuwa ukombozi kunapotokea tatizo pale. Niombe sana hilo liangaliwe ili liweze kufanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo napenda kuzungumzia ni suala la lumbesa. Nalo nimeshalipigia kelele sana hapa. Mheshimiwa Waziri inabidi aelewe kwamba waitazame kwa lenzi ya kimapato. Sisi mapato ya halmashauri tunakusanya kwa kuhesabu magunia. Magunia mawili yanazalisha gunia lingine moja, maana yake ni kwamba wanapofika kule ukiwa na gunia, ukiwa unakusanya shilingi bilioni tatu maana yake ni kwamba umepoteza shilingi bilioni moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kila halmashauri kama tukihesabia magunia kwa vipimo vinavyotakiwa, halmashauri zingepata mapato moja ya tatu zaidi wanayopata sasa hivi, lakini tukizungumza kwa lenzi ya hasara wanayopata wakulima, nimeshalisema sana kwa sababu hamna kipimo kinachotumika. Tuangalie kwa lenzi ya kimapato, tunaweza tukaelewa ni mapato kiasi gani halmashauri zinapoteza kwa sababu tu suala la lumbesa linaonekana limeshindikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, siamini kwamba Serikali imeshindwa kufanya udhibiti wa suala la lumbesa. Tungependa sisi wakulima wa kutoka Kilolo, Makete na mikoa mingine ambayo tunazalisha viazi, njegere na hivyo vyote visivyokuwa na vipimo, tunapenda kujua Serikali ina mikakati gani ya kukomesha tatizo la lumbesa ambalo linawaumiza sana wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kuzungumzia suala la ada. Elimu yetu inaenda kama pyramid, huku chini wanafunzi wengi wanakuwa shule ya msingi baadaye wanaenda sekondari, baadaye chuo. Wanapofika Chuo Kikuu wanakuwa ni wachache sana, sasa mtu ameshindwa kulipa 20,000 tumesema elimu bure, mtu ameshindwa kulipa 70,000 tumesema elimu bure, huyu mtu anamfikisha mtoto wake Chuo Kikuu tunasema alipe shilingi laki saba anatoa wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo langu pamoja na kuweka dirisha maalum la kusaidia watu, iangaliwe namna ya watu ambao hawawezi kulipa ada za Vyuo Vikuu. Nimekusanya takwimu kwa mwaka mmoja kwenye Jimbo langu, wanafunzi walionijulisha kwamba wanaahirisha masomo ninao wanafunzi 14 kutoka vyuo mbalimbali walioahirisha masomo kutoka vyuo vya Serikali, kwa sababu hawakuweza kumudu kulipa ada kwenye vyuo vikuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia vyuo vya Kati imesemwa sana niombe kwa sababu tangu nimeingia Bunge hili tunazungumzia vyuo vya kati, watoto wale nao ni wa Watanzania, hatuwezi kuwa na watu wenye digrii watupu, nao waingizwe kwenye elimu bure kwa sababu wana haki kama wanaoenda vyuo vikuu. Nina uhakika na wewe mwenyewe Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Spika na wengine wote tukipata shida za mifumo ya maji kwenye nyumba zetu hata leo, tunawaita hawa hawa ambao tunawakandamiza kwamba walipe ada na tunajua wametoka kwenye familia maskini, hili halikubaliki.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalize kwa kuzungumzia mikopo ya vifaa vya usafiri na kukumbusha tu, kwamba uendeshaji wa Serikali pia unaanzia kwenye ngazi za chini hasa kwa mfano ngazi ya Kata, ambapo tunao Watendaji wa Kata. Ukiangalia sekta nyingine kama kilimo, mifugo na idara nyingine zimeanza kuangalia sekta ya Kata, lakini ujumla wake wale Watendaji wa Kata wenyewe hawana vitendea kazi, hawana pikipiki. Sasa mtakapoanza kutoa vifaa hivi kwa utaratibu wowote mtakaoweka, kumbukeni kwamba ile miradi tunayoipelekea fedha nyingi, wanaoisimamia katika ngazi ya kwanza ni Watendaji wa Kata. Hivyo wakumbukwe ili waweze pia na wao kupatiwa vifaa vya usafiri weweze kuhudumia jamiii yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkona hoja. (Makofi)