Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Madaba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. DKT. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge waliochangia jana kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Rais pamoja na mawaziri wote wawili ambao wamewasilisha mpango wao. Lakini pia nitumie fursa hii kukupongeza wewe na Kamati yako ya Bajeti kwa kazi nzuri ya uchambuzi ambayo mmeifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maslahi ya muda sitaweka utangulizi mrefu, lakini nitajikita kwenye hoja moja ambayo ninadhani ni muhimu sana kwa maslahi mapana ya Taifa letu, ili tuweze kupata ile picha kubwa ya Tanzania tunayoitaka katika kipindi cha miaka mitano, miaka 15, miaka 25, miaka 50, kadiri ya malengo makubwa ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Muda Mrefu. Miongoni mwa vitu ambavyo vimejitokeza kwenye tathmini ya mwenendo wa uchumi wa Taifa letu ni ukubwa wa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa na huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto hii umeionesha kwanza kwenye ripoti yako, ukurasa wa sita, umeichambua vizuri sana, ninakupongeza. Lakini pia Mheshimiwa Waziri ameichambua na kuieleza vizuri sana kwenye hotuba yake, ukurasa wa 20. Kwamba, moja katika changamoto ambazo zinatukwamisha sana ni hii nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa na huduma ambayo kwa sehemu kubwa ndio imechangia hata kuadimika kwa dola, lakini pia imekwamisha ufanyaji biashara. Wafanyabiashara wengi wakubwa leo wanashindwa kuagiza bidhaa nje ya nchi kwa sababu hawana Dola. Na hili ni tatizo kubwa sana kiuchumi na hatuwezi kulichukulia katika uzito mwepesi, ni lazima tulichukulie katika uzito wake mkubwa. Ninakushukuru Mheshimiwa Waziri, Profesa wangu, Mheshimiwa Profesa Mkumbo, umelifafanua kwenye ukurasa wa 20 wa hotuba yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa sita wa kamati unaeleza namna ukubwa wa tatizo hili; inaeleza kwamba, kati ya mwaka 2021 na 2022 nakisi imeongezeka kwa asilimia 54.8; hili ni ongezeko kubwa sana. Kamati kwenye taarifa yake inaeleza sababu, Mheshimiwa Waziri hajazisema, lakini Kamati imeeleza sababu za ukubwa wa nakisi hiyo ambayo ina madhara makubwa sana kiuchumi. Nitazitaja zile sababu ambazo ziko ndani ya uwezo wetu kwa sababu, nyingine ziko nje ya uwezo wetu na mimi sipendi kushughulika na mambo ambayo hatuna uwezonayo. Masuala ya vita ya Urusi na Ukraine hayatuhusu, hatuna uwezo nayo, nitazungumza sababu ambazo Kamati imezieleza zile ambazo tuna uwezonazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni uagizaji wa bidhaa nyingi za ujenzi kutoka nje ya nchi. Hilo tunalijua, tunajenga SGR, tunajenga miradi mikubwa ya umeme, Bwawa la Mwalimu Nyerere, hayo yamechangia kwa asilimia kubwa sana kuongeza ukubwa wa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa na huduma katika uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiachana na hayo ambayo hatuna uwezo wa kuya-control, kwa sababu tuna miradi hii mikubwa tunaijenga, tunazo bidhaa nyingi ambazo tunaziagiza kutoka nje ambazo zimechangia pia ukubwa wa nakisi hiyo. Moja wamesema mbolea, mbili wamesema mafuta ya kula, tatu wamesema ngano, nne wamesema mazao ya petroli. Kwa hiyo, hayo kwa sehemu kubwa yamechangia ukubwa wa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yaliyotolewa; mapendekezo haya yapo kwenye ukurasa huohuo wa 20 wa Serikali. Wamesema suluhisho ambalo limependekezwa ni kwamba, kupunguza nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa kwa kuongeza mauzo ya nje ya nchi. Yaani tumalize hilo tatizo kwa kuongeza mauzo nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, it is very logical, ni sahihi kabisa, tuongeze mauzo ya bidhaa nje ya nchi ili tuka-attract dola ije, ili tupunguze hiyo nakisi, na ikiwezekana kuiondoa kabisa. Hata hivyo, changamoto yangu ni mapendekezo ya aina ya bidhaa ambazo tunataka tuzipeleke nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo matatu ninakubaliananayo vizuri kabisa. Mheshimiwa Waziri ameeleza kuhusu madini, tunaweza kufanya vizuri tukauza madini sana nje ya nchi. Ameongea kuhusu mazao ya misitu, excellent, tuna uwezo nayo hayo mazao ya misitu, tukayauza nje, tumefanya vizuri. Lakini pia kwenye eneo la huduma ameeleza umuhimu w kupanua huduma ya utalii. Excellent, tutafaulu sana kwenye eneo hilo na tayari tupo vizuri tunaongeza nguvu tu hapo, tuna-concentrate efforts zetu kwenye maeneo hayo matatu tayari tupo vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna eneo moja ambalo tunalisahau sana; tunalisahau lakini lina manufaa makubwa sana katika uchumi wa Taifa letu. leo walaji wakubwa wa nyama wako Middle East, wapo Mashariki ya Kati, na sisi tupo katikati ya Mashariki ya Kati na nchi ya Brazil. Ni kichekesho sana kuliona Taifa letu katika mwaka 2022 limesafirisha nyama tani elfu 10 pekee ilhali Brazil wamesafirisha tani za nyama milioni 2.9, ilhali tupo karibu zaidi na soko kuliko Brazil. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri wa Mipango, kwenye vipaumbele na mwenyewe umetwambia kupanga ni kuchagua. Hatuwezi kufanya kila kitu, hatuwezi kuwa junk of all trades, lazima tuchague, umechagua utalii, umechagua misitu, umechagua madini, ninaomba uongeze nyama kwenye sekta hiyo. Na sababu, zipo wazi, kwanza, critical mass ambayo itapata faida kutokana na biashara hiyo; tunao wafugaji wengi tunachohitaji ku-coordinate ufugaji tupate nyama tukatumie hilo soko. Kwa hiyo, sehemu hiyo naomba iwe mchango wangu; kwamba, kwenye kupunguza nakisi ya urari wa biashara kwa kuongeza mauzo ya nje tuongeze na biashara hiyo, tuwe na vitu walau vinne, vinne vitoshe, kwa sababu tumevifanyia study kwamba vinaweza kuchangia uchumi mkubwa wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sehemu ya pili. Mheshimiwa Waziri hajasema, naomba nimuongezee kwenye mkakati wa kupunguza hiyo nakisi. Ameongelea zaidi kwenye kuongeza mauzo ya nje. Na nimesema kwenye hoja ya Kamati, imeeleza vizuri sana, changamoto ni mauzo yetu ya nje madogo, lakini pia tunaagiza bidhaa nyingi sana toka nje ya nchi unnecessarily. Tunalazimika tutoe dola yetu ya ndani tuipeleke nje tukanunue vitu ambavyo tuna uwezonavyo, tuna uwezo wa kuzalisha mafuta ya kula Watanzania, leo tuna…
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mhagama kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kingu.
TAARIFA
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa kaka yangu anayechangia hoja very scientific, Mheshimiwa Dkt. Mhagama, kwamba, nakisi iliyotajwa katika ripoti hii kwa Mkoa wa Singida peke yake kwa juhudi zilizofanywa na Serikali ya Rais huyu huyu chini ya Wizara ya Kilimo inayoongozwa na Mheshimiwa Bashe, uzalishaji wa mafuta, mbegu za mafuta na ukamuaji wa mafuta umepanda kwa kiwango ambacho kimesababisha sasa hivi bei ya mafuta imeshuka sana. Kwa hiyo, ninampa taarifa msemaji kwamba, moja ya bidhaa zilizotajwa zinazotoa fedha nyingi za kigeni ni uagizaji wa mafuta, na nchi mwaka huu imejitosheleza sana na uzalishaji wa mafuta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa msemaji kwamba, achukue na hilo kuiambia Serikali hii sikivu kwamba habari ya kuagiza mafuta tunaweza tuka-adjust policy zetu katikati kulingana na uzalishaji mkubwa uliofanikiwa kutokana na juhudi kubwa za Wizara ya Kilimo. Ahsante. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa. Mheshimiwa Dkt. Mhagama, taarifa hiyo unaipokea?
MHE. DKT. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nipokee kwa mikono miwili taarifa ya comred Kingu, mwamba na main campaigner wa ushindi wa Mheshimiwa Spika. Ninampongeza na ninamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ndio hoja yangu. Kwa sababu ya muda nimuombe Mheshimiwa Waziri, kwenye hoja namba sita, kwenye ukurasa ule wa 20 ameweka hoja namba sita ambayo inahusu kuongeza mauzo ya nje. Naomba aongeze hoja namba saba, kupunguza ununuaji wa bidhaa ambazo tunaweza kuzizalisha ndani ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na nina takwimu, lakini kwa sababu ya muda naomba nizitaje tu; mbolea mpaka mwaka jana, Mheshimiwa Bashe nampongeza sana, asilimia 12 ya mbolea tuliyotumia nchini tumezalisha ndani ya nchi hii. Asilimia inayobaki kama tani 617,000 bado zinaagizwa nje. Mheshimiwa Bashe umeshaweza kwa asilimia 15, unaweza kwa asilimia 80, we can make it. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini eneo la pili, petroli. Wizara ya Nishati mmepambana sana mna masuala ya gesi, n.k. Tupunguze uagizaji wa petroli, tutumie bidhaa zetu za ndani zinazoweza ku-solve, hizo ni alternative products. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye mafuta ya kula inatudhalilisha Watanzania kuona kwamba mpaka leo asilimia 60 ya mafuta tunayokula nchini tunaagiza kutoka nje, what a shame? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kwa Tanzania hatustahili hilo. Mheshimiwa Bashe umepambana kwenye eneo hilo. Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Mheshimiwa Waziri wa Fedha ongezeni nguvu kwenye sekta hiyo tuimalize na tuweze kutatua tatizo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna eneo la ngano limefafanuliwa vizuri. Hayo ni mazo ambayo unapozidi kuyaagiza nje unawanyima Watanzania fursa ya masoko, unawanyima Watanzania fursa ya kukua, halafu unaendelea kuendeleza uchumi wan je wakati tuna nakisi kubwa ya fedha za kigeni kwa hiyo, tuna eneo la sukari na mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, sehemu ya mchango wangu nitaiandika na nitaiwasilisha Serikalini. Ahsante sana. (Makofi)