Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambae ameniwezesha mchana wa leo kuwa ndani ya Bunge lako hili Tukufu na kuwa mchangiaji wa kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuwatumikia nchi hii. Tatu sina budi kuwashukuru Mawaziri wote wawili kwa uwasilishaji wao mzuri Profesa Kitila Mkumbo kwa uwasilishaji wake mzuri wa Mapendekezo wa Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2024/2025. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze katika yale maeneo ambayo yana lengo la kuisaidia Serikali kupunguza nakisi ya urari wa biashara ya nje, hivyo nitajielekeza katika maeneo ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ule uwasilishaji wa Mwenyekiti wa Bajeti ambae aliwasilisha Makamu Mwenyekiti walieleza kwa kina kwamba kilimo cha umwagiliaji ndicho ambacho kinaweza kikaitoa nchi yetu kutoka sehemu tuliyonayo na kwenda sehemu nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika takwimu ambazo amezieleza, wameeleza kwamba nchi yetu ina eneo la hekta 29.8 za kilimo kwa ajili ya umwagiliaji. Hadi Juni, 2023 ni hekta 822 tu ambazo zimetumika kwaajili ya umwagiliaji. Hii inamaanisha kwamba ni asilimia 2.8 tu ya eneo zima limetumika kwa shughuli hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hizi takwimu utaona kabisa kwamba tuna kazi kubwa ya kufanya. Hatuwezi kuondoa nakisi hii kama hatutatilia mkazo kwenye kilimo cha umwagiliaji. Tunayo mabonde mengi ndani ya nchi yetu, tunalo Bonde kule Ziwa Viktoria, tunalo Bonde la Ziwa Tanganyika, tunalo Bonde la Ziwa Nyasa na tunalo Bonde katika Mto Ruvuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yote haya yanahitaji kuendelezwa ili wananchi wetu, vijana wetu ambao tunawahimiza wajihusishe na shughuli za kilimo waweze kutumia kilimo cha umwagiliaji kama njia ya kujipatia riziki zao. Lakini bila kilimo cha umwagiliaji…
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa.
TAARIFA
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na msemaji sasa hivi kuhusiana na maeneo ambayo yamekuwa identified kwa ajili ya umwagiliaji. Ningeomba wakati Serikali inakuja ku-wind up hebu itutajie maeneo kwamba ni maeneo gani kwa sababu ukisema tu ukubwa bila kutaja maeneo yenyewe mwisho wa siku hatujakua kwamba ni wapi kama tumefanikiwa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa unaipokea hiyo taarifa ya ziada?
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea ni mchango mzuri. Kwa hiyo, utaona kwamba kuna maeneo mengi ambayo yanahitaji kuendelezwa kwa kilimo cha umwagiliaji. Mfano katika Bonde la Mto Ruvuma ukianzia Mtwara Vijijini hadi katika maeneo yangu ya Jimbo langu la Nanyumbu eneo lote hili halina eneo kwa ajili ya umwagiliaji jambo hili kwa kweli si sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba Mheshimiwa Kitila Mkumbo waliingize katika mipango ya maendeleo ili vijana wetu ambao tunawahimiza waende wakajishughulishe na shughuli za kilimo waweze kufanya shughuli hii mwaka mzima, vinginevyo watakuwa watu wa kusubiri mvua ya Mwenyezi Mungu ambayo kwa kweli haitaweza kumkomboa kijana huyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika ukiangalia vijana wetu wanahitaji nyenzo, nyenzo ambazo zitawawezesha wao kufanya kazi kwa bidii. Changamoto ambayo ipo na ukiangalia ile ripoti iliyotolewa na Kamati ya Bajeti wameeleza mgongano wa kimaslahi kati ya taasisi mbili. Kuna taasisi ya umwagiliaji ambayo ipo chini ya Wizara ya Kilimo, pia kuna bodi inayoshughulikia mabonde ya haya maeneo ambayo iko chini ya Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo wanawajibika katika kuandaa miundombinu lakini maji ni ya watu wa bonde la maji kwa hiyo matokeo yake mgongano huu unasababisha shughuli za kimaendeleo zisiende mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri Mheshimiwa Waziri na Bodi, hebu tukubaliane ni nani anayewajibika uendelezaji wa mabonde yetu haya kwa ajili ya shghuli za kilimo vinginevyo maji yote ambayo yanapatikana yataishia baharini na wananchi hawanufaiki chochote. Naomba sana jambo hili liangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni upatikanaji ya mitaji ya kilimo kwa ajili ya wananchi. Jambo hili siyo jepesi kama linavyoonekana, wananchi wetu kwa kweli wanahitaji mikopo. Ukiangalia takwimu ambazo Kamati yetu ya Bajeti imeeleza mwaka 2022/2023 karibu trilioni 2.6 zilitengwa kwa ajili ya utoaji wa mikopo mbalimbali kwa wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kushangaza asilimia Saba ya trilioni 2.6 ilitumika kwa ajili ya mikopo ya uzalishaji na asilimia 93 ilikwenda kwa ajili ya kununua mazao, maana yake asilimia 93 ilitumika kama ulanguzi tu madalali wa ununuzi na asilimia saba peke yake ndiyo ilitumika kwa ajili ya kuwapa watu mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili hatutaweza kutotoa sisi na kuondoa hii nakisi ambayo ipo. Tunahitaji tuzalishe kwa wingi ili tuweza kuingiza fedha nyingi za kigeni. Nitawapa mfano mmoja, mimi natoka ukanda ambao unazalisha sana korosho, mwaka juzi Mkoa wa Mtwara au kwa maana ya korosho yote tulizalisha tani 300,000. Mwaka jana zao la korosho lime-drop kutoka tani 300,000 hadi tani 182,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini maana yake, maana yake kwamba tumepoteza fedha nyingi za kigeni ukilinganisha mwaka juzi na mwaka jana. Jambo hili kama hatutatilia mkazo tutaendelea kupoteza fedha za kigeni kwa sababu wakulima wetu ambao ndiyo tunaowategemea wazalishe korosho ili tupate fedha za kigeni wanashindwa kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo mkulima tunazungumza, mkulima anahitaji mkopo, mtu wa pamba kule anahitaji mkopo kwa ajili ya maandalizi ya shamba lake, mtu wa pamba anahitaji mkopo kwa ajili ya kulipa vibarua ili waweze kuanda shamba lake, mtu wa korosho anahitaji mkopo kwa ajili ya kupalilia mikorosho yake, mtu wa mikorosho anahitaji mkopo kwa ajili ya kununua viuatilifu vya kupulizia shamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya jambo kubwa sana la maana inatoa pembejeo kwa wakulima. Jambo hili nizuri kabisa na mimi naonga mkono mia kwa mia lakini, pembejeo pembejeo peke yake haitamsaidia mkulima. Naomba sana wakulima hawa wapewe mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani leo benki zetu za CRDB, NMB, Benki ya Kilimo hawatoi mikopo kwa wakulima wakati wakulima wote wa Kanda ya Kusini wanahifadhi fedha zao katika hizi benki, hili jambo siyo sahihi! Kama kweli tunataka kuhakikisha tunazalisha Korosho za kutosha na itatuingizia fedha nyingi za kigeni tuwapatie mikopo wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza nani mwenye kauli ya kuilazimisha benki hizi zifanye hivyo? Mheshimiwa Hussein Bashe - Waziri wa Kilimo mwaka jana alikaa na hizi benki kwamba toeni mikopo kwa wakulima lakini hakuna benki iliyofanya hivyo! Benki wanakuambia tunashindwa kutoa mikopo kwa sababu wakulima hawalipi, kwa hiyo wale wafanyabiashara walanguzi ndiyo wanapewa hela nyingi lakini wakulima wazalishaji hawapewi mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sana jambo hili litiliwe mkazo sana ili wakulima wetu waweze kupata mikopo, waweze kuzalisha kwa wingi.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa.
TAARIFA
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba kuna shida upande wa mikopo kwa wakulima hasa vijijini kwa sababu hawana collateral, hii inahitaji mabadiliko ya Sheria ya Ardhi ili watu wa vijijini nao wawe wanapata hati badala ya kuwepa hati nyingine ya kimila ambayo benki haitambui kama collateral.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Yahya unaipokea taarifa?
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na wazo zuri la Mheshimiwa Mbunge. Ni kweli kwamba wananchi wanahitaji mikopo na Serikali ipime ardhi lakini nataka niwaambie kwenye korosho mimi natoka katika eneo la korosho na ni mkulima wa korosho, mikorosho yote wananchi wote mikorosho yao inajulikana na wakulima na mabenki yote yanajua kila mkulima ana hekari ngapi, kwa hiyo inatoa mkopo kulingana na idadi ya mikorosho uliyonayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mkulima anayo account katika benki husika, kwa hiyo hakuna room ambayo itasababisha mkulima ashindwe kulipa huo mkopo. Benki wana sababu ambazo kwa kweli nashindwa kuelewa kwanini hawatoi mikopo kama lengo ni kumuondolea mkulima adha hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu naomba nichangie kipengele cha madini.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Yahya malizia muda wako nimekuongezea dakika moja kwa sababu muda umeisha.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Tumeambiwa hapa kwamba jinsi gani madini yanavyoongezea uchumi nchi yetu, lakini naomba nieleze kuna maeneo ambayo yanayo madini lakini wakati huo huo ni hifadhi za nchi yetu. Je, kuna mpango gani wa wananchi wanaoishi katika maeneo yale ili waweze kuchimba madini yale bila kuadhiri uhifadhi katika maeneo yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo tutakuwa tunalinda yale maeneo tukija kutaharuki madini yote yametoka na wananchi wanakuwa hawana chochote cha kujivunia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono na nakubaliana sana na wazo la Mawaziri wetu na nina imani katika mabadiliko haya machache ambayo watayafanya nina imani kwamba tutakwenda pamoja. (Makofi)