Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ngorongoro
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia Mapendekezo wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2024/2025.
Naomba niwapongeze Mawaziri wote wawili kwa kazi nzuri ya uwasilishaji wa hotuba zao ambazo zimesheheni mambo mazuri kwa Watanzania. Napenda kusema kwamba Nchi yetu kwa miaka yote haijawahi kuwa na shida ya mipango. Tatizo letu kubwa ni namna tunavyotekeleza mipango tunayojiwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapanga vizuri sana tunaandika kwenye makaratasi vizuri sana. Leo mwananchi akisikiliza huko nje anadhani kesho kutakuwa kuna mto unatoa maziwa, lakini kwa jinsi tunavyotekeleza inakuwa ni tatizo. Leo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, Profesa Kitila ukurasa wa 13 amesema kwamba; “Ili kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi unakuwa na athari chanya katika kuinua kiwango cha maisha ya watu wetu na kupunguza umaskini, mipango ya muda mrefu na mfupi ijayo itajikita katika kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi wetu unakuwa jumuishi, unapunguza umaskini, unazalisha ajira nyingi, unatengeneza utajiri na unachochea mauzo ya bidhaa zilizoongezwa dhamana nje ya nchi…” Katika aya ya mwisho amesema: “…kazo wa kipekee utakuwa katika kuchochea maendeleo kijamii na kiuchumi or rural social – economic development.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite katika maeneo mawili, kwanza suala la elimu. Nataka baadaye Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo anapokuja atuambie ni namna gani tunaweza kuwajumuisha wananchi wa vijijini ili waweze kushindana na watoto wa mjini. Leo mtoto anayesoma Shule ya Msingi ya Samunge, Kata ya Samunge, Wilaya ya Ngorongoro anawezaje kushindana na mtoto aliyeko Dar es Salaam. Yule mtoto aliyeko Samunge yeye anategemea jua ili asome, lakini aliyeko Dar es Salaam yeye anategemea jua na wakati huo huo anategemea umeme. Nadhani ni vizuri tujikite kuangalia katika suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni namna gani tunaweza ku-balance au kuweka sawia Walimu; Waziri atuambie kwenye mpango wake ni namna gani tunaweza ku-balance uwepo wa Walimu katika shule zetu za vijijini kwa sababu, leo tukiangalia kuna kipindi fulani Mheshimiwa Jenista alisema, ukiangalia kwenye shule za mjini unaangalia somo moja lina Walimu zaidi ya saba, somo moja mjini, lakini kule kijijini Mwalimu mmoja anafundisha zaidi ya masomo 12. Kwenye mpango wa Waziri aje atuambie kwa sisi tuliopo kule vijijini, ni kwa namna gani tunaweza kupata watumishi ambao watawafundisha watoto wetu kule chini. Sambamba katika sekta zote kwenye afya pamoja na elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la mifugo. Sisi wafugaji tunategemea ardhi kwa kila kitu, lakini kumetokea tatizo kubwa sana hapa, coordination ya Wizara zetu. Kwa mfano, leo tunaweza tukawa na Wizara ya Maji, Wizara ya Maji anapeleka maji labda kwenye kata fulani, lakini pia mtu wa mifugo anataka ajenge josho, lakini wakati huo huo anaenda kujenga josho eneo ambalo hakuna maji na Waziri wa Maji ataenda kuweka mradi wa maji katika eneo fulani ambalo mifugo hawaogeshwi kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Mpango wetu useme ni namna gani hizi Wizara ziongee, kwa sababu Wizara zikiongea itasaidia kutatua matatizo makubwa katika nchi yetu. Leo mtu wa Maji ni lazima aongee na mtu wa Mifugo, kwa sababu unaenda kutatua tatizo la maji ili kuogesha mifugo, tunahitaji maji, lakini mtu wa mifugo anaenda kujenga josho eneo ambalo hakuna maji, hiyo nayo ni misplacement ya resources, ni lazima tuzungumze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine Mheshimiwa Profesa natamani atuambie Mpango huu ni namna gani unaenda kutatua migogoro ya ardhi katika nchi yetu. Suala la migogoro ya ardhi limekuwa ni tatizo kubwa kwa miaka mingi. Mpango wa Waziri utuambie ni namna gani wanaenda kutatua migogoro ya ardhi. Leo ukienda kwenye wilaya nyingi za wafugaji kuna migogoro ya ardhi. Ukienda Longido kuna migogoro ya ardhi, Simanjiro, Kiteto na maeneo yote yanayozunguka hifadhi zetu kuna migogoro ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tukiangalia kwenye Wilaya yangu ya Ngorongoro, toka mwaka jana Serikali imetenga eneo la kilometa 1,500 wananchi wangu wameendelea kuumia kwa sababu hawana ardhi. Nataka Profesa akija hapa atuambie, mpango huu utaenda kuwasaidia hawa wananchi waweze kupata ardhi ya malisho kwa sababu hawana ardhi ya malisho mpaka sasa hivi. Kwa mfano kila siku hata leo kuna mifugo imekamatwa zaidi ya 834, wapo na wananchi wanaenda kutozwa fedha, lakini mpaka sasa zaidi ya mifugo 2,082 wametaifishwa, ni kwa sababu wananchi hawana ardhi kwa ajili ya kulisha mifugo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wafugaji wa kule kijijini tunategemea mifugo kwa ajili ya chakula, kwa ajili ya kusomesha watoto wetu, kwa ajili ya afya. Ni lazima sasa mpango huu uje utuambie hawa wananchi ambao hawana ardhi, kuanzia Ngorongoro ukienda Lake Natron ukienda maeneo ya Mara, wananchi hawa wanalia kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kwamba Mheshimiwa Rais wetu ana moyo wa dhati wa kuwasaidia wananchi na kuwaletea maendeleo, lakini tuangalie kwenye mipango yetu pamoja na Mawaziri wote, tuone namna ya kumsaidia kutatua changamoto zilizopo. Leo wananchi wa Ngorongoro wanasema angalau hata hao mifugo wakale tu kwa sababu hatuna namna, ni bora tufe polepole kuliko kufa kwa wakati mmoja, kwa sababu kama mwananchi unategemea mifugo kwa ajili ya chakula huna pa kulisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliambiwa hapa kwamba watu watachimbiwa maji, mpaka leo ni visima viwili na havitoi maji ambayo mifugo inatumia na ile mifugo ilikuwa inategemea maji kutoka eneo lile la kilometa 1,500 kwa ajili ya kupata maji. Walisema wataweka malisho hakuna, hakuna malisho ya aina yoyote sasa wale wananchi wataishije, mpango huu uje utuambie ni namna gani wanaweza kwenda kutatua changamoto za wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, kuna suala hapa wanazungumza, naomba mpango huu utuambie, je mpango huu unawahusu wananchi 100,000 wa Tarafa ya Ngorongoro ambao Serikali imewawekea vikwazo vya maendeleo kwa zaidi ya miaka miwili sasa. Hawapati maji, hawapati chochote. Mpango huu uje utuambie, Serikali ina mpango gani kwa ajili ya hawa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, …
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Shangai Kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ole-Sendeka.
TAARIFA
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge Shangai wa Ngorongoro juu ya hali ya tarafa yake ya Ngorongoro aliyoieleza, kwamba kutokana na urasimu ulioko katika Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro, hivi sasa kuna baadhi ya shule ambazo vioo vyake vimevunjika, vimepasuka na hawaruhusiwi wala hawapewi kibali cha kujenga. Kwa miaka hii miwili wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro kwa miradi ya maendeleo waliyokuwa wamepangiwa, miradi hiyo yote fedha zake zimesimama. Mpango huu utuambie ni Mpango wa Tanzania nzima isipokuwa Tarafa ya Ngorongoro ili tujue wananchi wa Ngorongoro watapangiwa mpango wao lini na kuletwa katika Bunge hili Tukufu.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Shangai unaipokea hiyo taarifa?
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa ya Kaka yangu, Mheshimiwa Ole-Sendeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema maendeleo jumuishi, maana yake tunalenga zaidi wale ambao wako nyuma kimaendeleo ambao ni watu wa vijijini ambao wanategemea kilimo. Kwa hiyo, niiombe Serikali kuhusiana na suala hili la Tarafa ya Ngorongoro pamoja na suala la Tarafa ya Loliondo na Sale, ni muhimu sana Serikali iangalie namna wale wananchi wanaangamia. Waziri aje na mpango mzuri wa kuwajali na wao kwa sababu ni Watanzania wanahitaji maendeleo. Tunaposema uchumi mzuri, ni lazima tunawaongelea na wao, lakini sasa tutakuwaje na maendeleo jumuishi kama kuna watu bado tunawauzia mifugo, haiwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la infrastructure; coordination yetu katika Wizara zetu, Wizara ya Maliasili na Utalii Mheshimiwa Rais alitangaza Royal Tour, lakini sasa hivi ukienda kwenye hifadhi zetu, nitolee mfano, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro pale getini. Wazungu hawataki silaha getini, kule ni hospitality industry, ni watu ambao wanaenda kwa starehe, lakini wanapoenda getini wanakutana na watu wenye silaha wanashangaa. Tutengeneze mifumo ya utalii ambayo itasaidia nchi yetu kupata mapato makubwa na Wazungu wanaokuja waende na kurudi tena. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa kengele ya pili hiyo.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kengele ya pili?
MWENYEKITI: Ndiyo.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)