Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru sana kwa kupata nafasi ya kuchangia hoja hii muhimu sana lakini nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwamba muda kama huu mwaka 2021 nilikuwa Bungeni, mwaka 2022 nilikuwepo na mwaka 2023 nipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimeshuhudia kaguzi hizi zikifanyika na ningependa sana kupata taarifa mimi na Wabunge wenzetu kwamba ukaguzi ukifanyika na ikaonyesha kuna mtu mhalifu wa eneo fulani ni hatua gani zinachukuliwa? Au tunachukua ripoti tunatunza miaka mitatu, minne, mitano kumi kama kawaida? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpongeze Mheshimiwa Rais, Mama Samia, Mama wa Taifa. Kwamba ameongeza nguvu ya Serikali kumteua Mheshimiwa Doto Biteko, Naibu Waziri Mkuu kufanya kazi ya kusaidia Serikali lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya kazi kubwa sana na nzuri sana anapoenda katika Mikoa na Majimbo yetu kufanya ukaguzi na kuainisha wabadhirifu na mara nyingi kuchukua hatua katika umahiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amemteua pia Mheshimiwa Mchengerwa nimefurahi kazi imeanza kwa kasi kwa kuwajibisha watu ambao wanafuja fedha katika Halmashauri na Mheshimiwa Rais ameunda Kamati ambayo ilipitia Wizara ya Mambo ya Nje na Afrika ya Mashariki na kumuonyesha namna ambavyo kuna uozo na upendeleo katika ajira maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Rais Kamati ile isiishie pale iende ikachunguze Wizara ya Mambo ya Ndani, iende ikachunguze Ofisi ya Rais, TAMISEMI, iende kuangalia ma RAS, iangalia ma-RC iangalie ma-DED na ma-DC kweli wanaweza kufanya kazi waliopewa na kama wanamsadia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaombe Waheshimiwa Mawaziri wakitaka kutoa taarifa tunapochangia ripoti hii waangalie maswali ambayo wanaulizwa katika Bunge hili. Mbunge anatoa mishipa hapa anaomba apelekewe milioni hamsini kujenga zahanati wewe unatuambia kuna Mtumishi mmoja wa umma, Mtanzania mwenzetu amekula mabilioni anatembea na ma VX mtaana na bado tunampigia makofi. Naomba hili Waheshimiwa Mawaziri mliangalie sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapochangia hoja hii Mkaguzi Mkuu wa Serikali ni daktari ameenda amechunguza taarifa amekwambia hapa kuna wizi. Halafu wewe unaambiwa unaumwa malaria unasema hapana mimi siumwi hii siyo sawa, siyo sawa hata kidogo. Kwa sababu hiyo kasi ya Mheshimiwa Rais kutafuta fedha ni kubwa sana lakini bahati mbaya kasi ya kuiba fedha za umma imekuwa kubwa sana vilevile. Maana yake ni kwamba unachota maji unaweka kwenye mkono wako wa kushoto halafu huku kibaka mwingine anatoboa ile pakacha maji yanavuja kwa hiyo, mwisho wa siku hautajaza hilo pipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waheshimiwa Wabunge tena wengi hapa ni Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi karibu wote hapa. Kama kuna Waziri ataondolewa pale kwa uzembe ataingia kada wa Chama Cha Mapinduzi mwingine kama kuna Mtumishi mwingine atawajibishwa atakaeingia kwenye nafasi hiyo ni Mtanzania mwenzetu hili Bunge linasubiriwa na Watanzania kwamba mnasaidia Mheshimiwa Rais? mnawasemea Watanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imetoa mapendekezo, Kamati hii imetoa mapendekezo mazuri lakini yamepungikiwa uzito mimi nilitarajia watatuambia hapa baada ya Ripoti ya CAG wangapi wamefungwa kwa wizi wa umma? Baada ya ripoti hii watuambie wangapi wamefukuzwa kazi? Baada ya ripoti hii watuambie wangapi wametapika fedha za Watanzania masikini ambazo wamekula? Na wangapi ambao wana kesi Mahakamani ni mpaka tunavyozungumza hapa leo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii taarifa hatujapewa, ingependeza tupewe hiyo taarifa lakini Waheshimiwa Wabunge mkumbuke tunazungumza mabilioni ya fedha yameibiwa lakini Watendaji wa Vijiji hawana hata baiskeli nchi hii, Watendaji wa Kata hawana hata pikipiki na pikipiki walizopewa hawana spare, hawana mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, waratibu wa Elimu ya Kata nchi hii wanatembea kwa miguu kukagua elimu. Sasa hivi wanafanya mitihani ya form two wanaenda mvua zinanyesha, wananyeshewa wakitembea kwa miguu, hawana hata kirukuu cha kuwapeleka lakini wapo watu hapa wamevimbiwa fedha za Watanzania wao wanapigiwa makofi na Wabunge tuwashangilie, hii haikubaliki, hii haikubaliki na hatuwezi kuunga mkono uzembe huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge lazima wafahamu kwamba katika Majimbo yetu tuna watoto wanakaa chini nchi hii hawana madawati. Kuna walimu hawana nyumba za kuishi, kuna walimu wetu wanadai madai mbalimbali tunataka posho ziongezeke, vijana wetu wako mtaani tungepata fedha hii ikafanye kazi vizuri maana yake Serikali ingeajiri vijana wa Tanzania waliosomeshwa na Wachungaji, Wakulima, Wafugaji na wako mtaani. Kwa sababu Serikali ina fedha nyingi ya kuajiri watu hao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mjadala huu tutawaomba wenzetu waliofanya uzembe katika maeneo mbalimbali na mimi nina mapendekezo ambayo siyo laini sana nchi kama Korea kuna mpaka watu wananyongwa kwa makosa kama haya. Sasa ningependekeza wale wote ambao wamethibitika pasipo shaka kwamba wamekula fedha za Watanzania na Waheshimiwa Wabunge wa CCM uchaguzi ni mwaka kesho Serikali za Mitaa na 2025 nimesoma mitandao. Mheshimiwa Rais tumsaidie na Wabunge tufanye maamuzi hapa, wale wote walioiba bila kuwaonea hawa watu wanyongwe kwenye nchi hii watoke, tubaki na watu wema katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale watu wote ambao wameonekana ni wazembe na wana nafasi katika umma hawa wafukuzwe kazi zao, wakae mtaani lakini…there is no gain without pain ni lazima tuwe na sindano kama unaumwa Malaria utachomwa chloroquine ili upone japo ni chungu…

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa, taarifa, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Maganga.

TAARIFA

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nataka nimpe taarifa mzungumzaji anaeendelea kuongea kwanza Viongozi wote wa Serikali wanaofuatilia mdahalo huu mimi toka mwaka jana nilisema bila kupitisha Sheria ya kunyongwa watu, wizi hatuwezi kuumaliza. Kwa hiyo, naungana nae kabisa kwenye Sheria ya kunyongwa sisi ni Wabunge tupitishe hiyo sheria ili kusudi tumalize biashara, ahsante sana. (Makofi)

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika michango mizuri ya Mheshimiwa Maganga ni pamoja na Taifa hili ambalo naipokea kwa mikono miwili…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waitara taarifa unaipokea?

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeishaipokea kabla hajamaliza kuongea. Mheshimiwa… (Kicheko)

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa, taarifa..

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waitara kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Anatropia.

TAARIFA

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa kwamba hii ripoti uliyoiona hapa ni roughly chini ya asilimia ishirini ya taasisi zote na Taasisi za Serikali Kuu. Kwa hiyo, sasa unaweza ukaona ni wangapi watanyongwa katika hii nchi? (Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waitara taarifa unaipokea?

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea hii ripoti, hii taarifa yake. Maneno yangu leo hayafanani na suti niliyovaa, naomba niseme hivyo. Sina maneno mazuri zaidi ya hayo, nachopendekeza kwa Waheshimiwa Wabunge ni kwamba tumekuwa tunajadili mambo ya msingi katika Bunge hili lazima tujue Watanzania wengi wapo nje sisi tuna wawakilisha. Bunge likihairishwa tarehe 10 Ijumaa ijayo kila Mbunge ataenda Jimboni kwake, mnaweza mkaona kiwango cha umasikini cha watu wetu ambao wanashindwa kupeleka watoto shule kwa sababu hawana uwezo wa kuwalipia watoto wale wanakuja kwa Wabunge tuwasaidie hata mpaka sare.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako watu ambao, kwanza tukiwanyonga hawa hatujawaonea itakuwa ni haki yao kwa sababu katika Utumishi wa Umma ukiacha sisi Wabunge na Waheshimiwa Mawaziri ambao wanaweza wakawa Mawaziri kwenye sekta ambayo hakusomea. Watumishi wote wa umma wamesomeshwa na Watanzania, wana vyeti ukiwaambia walete CV wanakujazia mezani mpaka huwezi kuonekana kwa mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake hawa wanafanya makusudi na wanaiba kitaalamu uzembe ulipo sisi ni sisi Wabunge kwamba, mtu ameishaiba, ripoti ipo, taarifa ziko mezani, vyombo vipo hawawajibishwi hivi nyie Waheshimiwa Watanzania na Viongozi wenye dhamana mnawafundisha nini watoto wetu? Kwamba wakue wakijua kwamba, wala hata ukiiba utahamishwa kutoka Wizara hii kwenda Wizara, kutoka Kitengo hiki kwenda Kitengo hiki na hakuna uwajibikaji? Nendeni mjifunze wenzetu walioendelea…

MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwongozo, mwongozo, mwongozo…

MHE. MWITA M. WAITARA: …unafanya makosa ambayo… muda wangu Mheshimiwa Mwenyekiti ulindwe…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwongozo.

MWONGOZO WA SPIKA

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mbunge wa Chama cha Mapunduzi, moyo unaniuma. Mbunge mwenzetu anapochangia kwenye taarifa kama hii inauma kuona wanaohusika, Mawaziri wanachati na simu, wanaongea na simu. Hawajali kile anachokiongea Mheshimiwa Waitara kama vile ni jambo linapita. Mimi binafsi inaniuma sana. Naomba mwongozo wako.

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Augustino Mulugo, basi mwongozo utatolewa baadaye. Mheshimiwa Waitara endelea na mchango wako.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mchango wa Mheshimiwa Phillipo ni muhimu sana. Waheshimiwa Wabunge wenzangu wa Chama Cha Mapinduzi, kwanza naomba niwaombe, dhamana tuliyopewa ni kubwa sana, na chama hiki ndicho ambacho kimetusaidia Watanzania kuwa hapa tulipo. Sisi Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi na tumefuatilia Mabunge yaliyopita, sisi ndio wenye dhamana na Serikali hii ni ya kwetu na hawa watu ni wa kwetu. Tukiwawajibisha sisi, ni sisi wenyewe. Msisubiri kuja kuambiwa, chukueni hatua, na hatua ni sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napendekeza, kama tutakuwa tunafanya ukaguzi, tunampa fedha CAG na magari anazunguka; Kamati zinakaa na tunalipwa posho; ripoti inakuja makabrasha ya kujaza makabati, tunayaacha eti mwakani tena tunaletewa ripoti kama hii. Mimi hiyo ikija mwakani kama nitakuwepo, Mungu akinipa uhai, siwezi kuchangia tena… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana…

MHE. MWITA M. WAITARA: …kwa hiyo tunataka tuone hatua zinachukuliwa kwa watu ambao wanamkwamisha Mheshimiwa Rais. Mama anatafuta fedha, anajaza kikapu halafu wako vibaka fulani hivi wanakula hela…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Waitara…

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii haikubaliki. (Makofi)