Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Mchango wangu utaanzia pale kwenye taarifa aliyopewa mdogo wangu, Mbunge wa Igalula; kwamba tusizungumze mambo kiujumla jumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mosi, tutazungumza kiujumla jumla kwa sababu taasisi zimetajwa kiujumla jumla halafu sasa tutawasaidia kuwataja waliohusika. Naanza na ukaguzi maalum uliofanywa kwenye Mfuko wa Tuzo na Tozo na Kufa na Kuzikana katika Jeshi la Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kifungu cha 66(3) cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi Sura Na. 333, kimeainisha kuwa Inspecta Jenerari wa Polisi ndiye mwenye mamlaka ya fedha kwenye mfuko huo. Mwaka 2018 mpaka 2020/2021 Inspecta Jenerari wa Polisi alikuwa Sirro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mfuko huu, umetajwa ufisadi wa shilingi bilioni moja. Anayeidhinisha fedha hizi, alikuwa Simon Sirro, mleteni kokote aliko aje apambane na hali yake. Hamuwezi mkafumbia macho hivi vitu. (Makofi/Vicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mfuko huu umeanzishwa kwa dhamira moja ya saidia Askari wadogo wa Jeshi la Polisi. Wakifiwa na wenza wao zisaidie zile familia. Wanaopambana na Jeshi, wanaopambana kwa damu na Jasho katika kulinda nchi hii kwa kupambana na majambazi, wakipata madhara hizi fedha ndizo ziwasaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko huu wanaochangia ni askari wenyewe kwa kufanya kazi ya ziada kulinda kwenye migodi, benki na taasisi mbalimbali; halafu wanatokea vingozi wao wana-take advantage kwa ile nidhamu ya kijeshi kwamba hawawezi kuhoji, wanawadhurumu askari wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuulize leo Sirro yuko wapi, si ni Balozi? Arudishwe aje abebe mzigo wake. Hakuna Bunge la kulinda watu wa namna hii. Kuna wengine wametajwa waziwazi, leo ni Naibu Katibu wa Maliasili na Utalii. Katajwa waziwazi, tena tu baada ya Ripoti ya CAG anapata promotion. Why? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo askari hawa mbali na fedha zao kutafunwa kwenye huu Mfuko wa Tozo wanaochangia kwa jasho lao kwenda kulinda kwenye migodi fedha zao hazijulikani zilipo. Halafu unaambiwa alikuwa tu anachukua anaidhinisha, anatoa BOT anapeleka huku, anatoa huku anapeleka huku. Kati ya Kombania 62 amapeleka kwenye Kombania tano tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za ulinzi wa nchi hii, askari wanatoa mikoa yote. Watu wanasema alipeleka kwa washikaji zake, mimi sijui. Askari wana uchungu, na ndiyo hawa hawa wakistaafu wanakuwa wanapata kikokotoo cha shilingi milioni 17. It is not fair, si sawa. Mimi ni Mbunge naenda kwa term ya tatu; tumekuwa tukijadili sana vitu hivi, vinakera. Haya, tuliwanong’onezaga nyie kuhusiana na ufisadi wa MSD hamkuchukua hatua mapema, CAG akasema. Wengine tuna uwezo wa kupata taarifa mapema. Haya mmempeleka wapi; nasikia amerudishwa Jeshini. Is it fair, mnataka tunyamaze? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukienda katika Mfuko wa Kufa na Kuzikana, mlezi ni IGP, na wa kipindi hicho alikuwa ni Simon Sirro. Ubadhirifu kwenye Mfuko wa Kufa na Kuzikana ni shilingi bilioni 4.6. Waheshimiwa Wabunge, fedha katika mfuko huu ni michango ya elfu tano ya kila mwezi ya watumishi wa Jeshi la Polisi. Walivyodai uitwe mkutano mkuu ili wahoji matumizi hakuna kilichofanyika. Miaka mitatu, mitano halafu leo nasikia wakati CAG anafanya uchunguzi walivyoenda kumhoji IGP msaafu anasema, huyo aliyehusika eti ametoweka; kweli, mtumishi wa Jeshi la Polisi katoweka na nyaraka? Mnataka tuyavumilie hayo? Aliyekuwa kiongozi wa ulinzi wa Jeshi anatoa amri; yeye anahusika na hivi vitu halafu mnampa Ubalozi. Arudishwe apambane na hali yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi mwenye sifa tutampa; na ninachukua fursa hii, maana huu uchunguzi haukuanzishwa bure; aliye-engineer alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara hii. Sijui leo yuko wapi, Mungu amsaidie. Labda alinusa harufu ya rushwa. Kwa unyenyekevu mkubwa na kuipenda nchi yake akaagiza haya yafanyike. Inawezekana akaondolewa lakini watu kama hawa ndio tunu ya kulinda, wanaonusa harufu za wezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, atakayefanya vizuri tutamsifia na atakayefanya vibaya, popote alipo aletwe apambane na hali yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayasema haya kwa uchungu. Haya nije kwenye halmashauri. Ubadhirifu wa shilingi bilioni 11 ya makusanyo yaliyotakiwa kwenda benki kupitia POS, shilingi bilioni 11 watu wamekusanya wameweka mfukoni. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine baada ya kuona zimepelekwa hizi Mashine za POS kwa ajili ya kuzuia wizi; wengine walizima. Chamwino walizima mashine ya POS kwa siku 1,905, Uvinza walizima mashine ya POS kwa siku 1,133, Ushetu walizima mashine ya POS kwa siku 397, Sengerema walizima mashine ya POS kwa siku 185. Mnajua kwa nini wanafanya hivyo; ni kwa sababu tunawalea. Hawa wakurugenzi wapo. Halafu anakuja kwenye Kamati anakwambia, unajua tumewapeleka TAKUKURU. Tukawauliza muda gani wanadai miaka mitatu, kwa nini tusiseme kwamba TAKUKURU ni kichaka? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi bilioni 11 za makusanyo kwenye majimbo yenu watu wametafuana; halafu wanatuambia wanapelekwa TAKUKURU; wengine bado wapo kwenye vituo vya kazi. Halafu mnataka tuyanyamazie haya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka wakati Rais anapokea ripoti alivyozungumzia mikopo hii ya asilimia 10, fedha ambazo hazijakusanywa zimeongezeka kutoka bilioni 47 mpaka bilioni 88. Mchanganuo wake sasa, mchanganuo wake unaambiwa milioni 900 ni vikundi hewa. Milioni zaidi ya 700 eti vikundi watu wamechukua mkopo halafu wakagawana. Bilioni 2.5 eti vikundi sasa hivi havijishughulishi na kazi yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwaambie, watoaji mikopo Mwenyekiti ni Mkurugenzi, yuko Afisa Maendeleo, yuko DT, yuko Afisa Mipango, inakuwaje kuna vikundi hewa vinapewa mikopo? Inakuwaje kuna vikundi vyenye thamani ya bilioni 2.5 eti havifanyi biashara? Inakuwaje eti kuna vikundi vya thamani ya milioni 700 eti watu wamepewa mikopo halafu wakagawana? Mnajua kwa kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni ya mikopo imesema wazi kabla hujatoa mikopo, lazima ukatoe elimu, lazima utembelee vikundi, lazima ujiridhishe na biashara wanayofanya. Halafu wanakuja kuleta majibu mepesi kwenye pesa zaidi ya bilioni 88 ambazo zingejenga zahanati, ambazo zingejenga vituo vya afya, wako ofisini. Sasa namshauri Rais …

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester Bulaya, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Shaban Ng’enda.

TAARIFA

MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa Taarifa dada yangu, Mheshimiwa Ester Bulaya, ambaye anazungumza kwa uchungu mkubwa sana tena kizalendo kwamba, mambo hayo ambayo yeye anayaona yana uchungu mkubwa katika ubadhirifu wa pesa za umma, ndio yanayowafanya Wabunge wa CCM waseme itungwe sheria ya kufanya watu wanaofanya hayo sasa wakatwe vichwa. Kwa hiyo, katika Bunge hili suala la ubadhirifu na wizi linawaudhi watu wote, Wabunge wote na wananchi wote wa Tanzania. Halina itikadi hili ndio maana Wabunge wa CCM wanasema tulete sheria ya kukata vichwa watu hawa. Dada yangu endelea. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester, Taarifa unaipokea?

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa ikitoka kwa kaka, senior, lazima niipokee, najua uzalendo wake wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati muafaka tukamshauri Rais, tuanze kuangalia sifa za Wakurugenzi, uteuzi wake. Mkurugenzi ndio CEO wa Halmashauri, anatakiwa awe na weledi wa kutosha, isiwe tu tunateuana kwa ajili ya kutoa zawadi, matokeo yake ndio haya, watu wanashindwa kutimiza majukumu yao kulisaidia Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Naunga mkono hoja taarifa zote tatu. (Makofi)