Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibamba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISSA J. MTEMVU: Bismillah! Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi ambayo umenipa na mimi nichangie kwenye taarifa hizi za Kamati tatu za PAC, LAAC na PIC. Pia, natamka wazi mimi natokana na Kamati ya Hesabu za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza mchango wangu wa leo napenda kwanza kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo anaendelea kufanya kazi vizuri na maelekezo yake kwa ujumla wake, Wasaidizi wake wanayafanikisha kwa kiwango kinachofaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maneno ya awali tu, moja, ninayo slogan mwenyewe ambayo nimewahi kui-induce kwa marafiki zangu Waheshimiwa Wabunge wengine, ikiwa inaitwa ‘Kumtenganisha Mheshimiwa Rais na Mafisadi, kumtenganisha Mheshimiwa Rais na wezi!’ Hii ni slogan yangu ya muda mrefu sana. Leo nimefurahi Kaka yangu Mheshimiwa Ole-Sendeka ulipopata nafasi ya kutoa taarifa, ukasema uwatenganishe Waheshimiwa Mawaziri na wezi. Ukarudi chini kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, hapa niko tayari kutofautiana na haya maneno uliyoyaweka hapa. Mimi ninaamini Makamisaa wetu tumewapeleka kwenye Wizara mkamsaidie Mheshimiwa Rais, mkatusaidie Wabunge. Ndiyo maana mmekwenda wachache kule. Sasa, tunapofika sehemu na wewe pia tukutenganishe na hawa mafisadi, hao mafisadi tukawaita ni Maafisa Masuuli na Wasaidizi wao, sasa wewe unakuwa uko wapi? Umepewa instruments zote, una uwezo wa kuwafanya vyovyote katika Wizara ambazo mnazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nawaomba sana, ninyi pamoja na Wizara zenu mumsaidie Mheshimiwa Rais ili aweze kufikia yale ambayo anayatarajia.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Issa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora.
TAARIFA
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nafahamu ninayempa taarifa ni mtu anayejua Local Government vizuri sana, ni mtoto wa Local Government. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria zetu za Fedha za Local Government, sisi tuliopo humu ndani ni Wajumbe wa Kamati ya Fedha za Halmashauri za Serikali za Mitaa, kwa hiyo, mapungufu yote yanayotokea kule hata sisi humu ndani ni sehemu yake. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo....
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe taarifa...
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, aah, taarifa!
MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, ninaomba tusikilizane.
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Waziri, utaharibu ushirika wa Bunge ....
MWENYEKITI: Mheshimiwa Simbachawene endelea.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nakubaliana kabisa na Mheshimiwa Mtemvu kwamba iko haja, hatuwezi kutenganisha ni lazima wote tuwajibike, haya yanayotokea leo wote tunawajibika. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mtemvu endelea na mchango wako.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu kwanza ndiyo uwe muhimu lakini kwa heshima kubwa ambazo huwa ninampatia za asilimia mia moja kaka yangu Mheshimiwa Simbachawene..
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mtemvu na Waheshimiwa Wabunge, taarifa ni sehemu ya muda wako wa mchango, kwa hiyo, endelea na mchango wako.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wetu wana muda wao wa mwisho wa kuhitimisha, ambao watapata nafasi ya kutujibu vizuri lakini kwenye hili ambalo ili nipokee hii taarifa, ninataka kumwambia ni kweli anachokisema, Waheshimiwa Madiwani ni sehemu ya maamuzi kwenye Local Government, vipi kwenye Serikali Kuu? Mimi nimesema hapa ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, siyo Local Government, haya madudu ambayo sijaanza hata kuyasema yanatokea Serikali Kuu, huku sisi ni nani kule kwenye Serikali Kuu? Ni ninyi ndiyo mpo huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, taarifa hiyo ni nzuri, lakini kwenye upande mmoja wa local government ambapo ameniambia mimi pia ni mshiriki kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine la maneno ya jumla, kwa sababu sijaanza kuchangia, ni heshima kwa chama changu. Haya mambo ambayo yanatokea hivi kwenye kamati zote, heshima ya chama changu kwenye umma (public), mnaitikisa, kwa hiyo, yanatuuma sana. Ziada, ni heshima ya taarifa ya CAG kwa umma. Taarifa zina miaka zaidi ya mitatu au minne, business as usual. Hatuwezi kwenda hivi kama Taifa. Hoja zinakuja, majibu ni changamoto, wananchi wanapokea mwezi wa Tatu, tunakuja kujadili mwezi wa Kumi na Moja, na mambo bado hayaendi, tunaendelea kubishana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tujitahidi sana. Waheshimiwa Wabunge wengi wameelekeza au wametamani leo watoke na maazimio au kesho ambayo kwa kweli public itatuelewa. Sasa baada ya maneno yangu hayo ya jumla, nitatamani kuchangia katika maeneo mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni Tanoil. Kwenye taarifa humo naona hata nimenukuliwa huko. Ndani ya Kamati, nafikiri hapa nilikaa nao vizuri sana. Kwa sababu wengi wamezungumza kwa ujumla wa changamoto ziliyotokea ndani ya Tanoil, wala sitaki kufika huko. Kwa sababu najua yameshaingia vizuri kwenye Hansard. Nitazungumza eneo dogo ambalo wengi hawajalizungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na upungufu wote huo, moja, hakuna monthly reconciliation ambayo ilitusababishia tupate opportunity loss ya shilingi bilioni 1.8. Vile vile zaidi ya tani mbili, shehena mbili za mafuta za thamani ya shilingi bilioni 16.2, ambazo tungeweza kuzipata, tumeshindwa kuzipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ni hiyo ya underpricing ambayo watu wameielezea, kwamba underpricing na hii niitolee tu mfano, niwaambie tu vizuri kwamba ipo hivi, mwaka 2022 Tanoil palikuwa kuna bei ambayo, na ndiyo mwaka ambao tumefanya biashara vizuri. Kwa sababu mwaka wa nyuma yake tumefanya biashara kwa miezi miwili tu na ndiyo maana tulikuwa na loss ya shilingi milioni 166, lakini mwaka huu tunazungumzia loss ya Shilingi bilioni 7.8 ni kwa sababu full year (mwaka mzima) tumefanya biashara vizuri, lakini shida hapa imetokea nini? Kuna bei elekezi shilingi 2,610, hiyo ndiyo EWURA. Wao wakaenda kuuza chini ya shilingi 78.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo wanayo, haki ya kupunguza kwa percent kutoka ile base ya EWURA. Kwa hiyo, hiyo ni management standard, hawakuitii, lakini hata ile ya EWURA hawakuitii. Kamati ilihoji juu ya kibali, lakini ikumbukwe sana Chief Internal Auditor wa TPDC, parent company alikiri kuwa walikuwa hawana kibali. Kuna mmoja akasema, sasa kama mpaka watu wanakili kwa sentensi moja, “hatukuwa na kibali na tumefanya.” Sisi bado tunawatafuta hawa? Kwa hiyo, tunawatafuta wa nini? Yyaani mambo yako wazi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya utetezi wao, wakasema walikuwa hawana wataalamu huko siku za nyuma, lakini najua CAG amepata wapi haya? Kuna mmoja alisema kule juu ya kwenye tozo na tuzo, Polisi kule. Kuna sehemu kuna watu, vijana wazalendo sana. Nataka niseme kwa sababu kwenye ripoti ya Kamati yetu tumesema iende forensic audit kule, wakafanye ukaguzi wa kiuchunguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna mtaalamu, kijana mdogo mwenye CPA yupo pale, ameenda kuwasaidia kutengeneza hizi hesabu, kaenda kuziona, madudu yote haya kayaona. Wamemwondoa, wamempa akasome magazeti, tena kwa kumuumiza kweli! Hatuwezi kufikia hapa. Hii mifano ipo, amezungumza kule Mheshimiwa Ester Bulaya, lakini ikumbukwe kwenye michango ya nyuma kidogo kaka yangu wa Kigoma Mjini aliwahi kumzungumzia Meneja wa TRA mipakani na baadaye mkamrudisha. Watu wanafukuzana. Mdogo wangu Mheshimiwa Mrisho Gambo, amewahi kumzungumzia hapa Internal Auditor mmoja Arusha, vijana wazalendo ambao tunatamani watusaidie kama Taifa ambapo ninyi mpo huko kama wasimamizi, hamwezi kuwasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, si hata management mngeshaona kuna kijana kaumizwa, kwa nini katolewa? Mimi ningelikuwa ndio nipo mle ndani kama Kamisaa, huyu ndio angekuwa Manager of Finance au Director of Finance wa pale, kama siyo sehemu nyingine. sasa mnaenda kuwaumiza. Kwa hiyo, hiyo haikuwa na afya sana. Kwa hiyo, natamani sana Mheshimiwa Waziri mfuatilie, yupo mtu kaumia juu ya kutoa siri ya jambo hili. Kwa sababu tunapeleka uchunguzi kule, mtakuja kukuta hasara imeenda mara 12. Siyo Shilingi bilioni saba tu, zaidi ya Shilingi bilioni 60 kwa mwaka ujao, na mtakuja kunikumbuka na kwenye Hansard itabaki kumbukumbu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili. Ni riba ya shilingi bilioni 113.8 ambayo anadaiwa TANESCO na kampuni ya Pan Africa Energy. Upo mkataba ambao umeingiwa kati ya Pan Africa Energy na TANESCO kwa ajili ya matumizi ya gesi, lakini mkataba huu una-requirement yake ambayo wameekeana, kwamba kila ankara ya mwezi inapozalishwa inatakiwa ilipwe katika muda waliokubaliana. Kutoilipa kwa wakati, maana yake nini? Maana yake kutakuwa kuna riba ya asilimia nne na hii riba inakuja juu ya LIBOR rate. Maana yake ni nini? Kama riba ni asilimia nne na mwaka huo hii London Inter-Bank Offered Rate (LIBOR) itakuwa yenyewe ina-vary, siyo fixed. Kwa sasa ni asilimia 5.1, inasababisha tulipe asilimia 9.1. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia Mkaguzi anaenda kukagua kwa huu mwaka 2021/2022 wa hesabu, zipo ankara 115 hazijawahi kulipwa. Maana yake nini? Maana yake ukiondoa deni halisi ambalo TANESCO analijua la kama Shilingi bilioni 245, tayari ndani yake kuna riba ya Shilingi bilioni 113. Hizi ni fedha nyingi sana. Maana yake kila mwaka ina-accumulate riba ya Shilingi bilioni 11. Sasa shilingi bilioni 11 kwa mwaka hizi fedha, mimi Mbunge wa Jimbo la Kibamba Wilaya ya Ubungo, Wilaya ya Changamoto, ndugu zangu hapa ningekuwa na zahanati ngapi? (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Mtemvu, malizia mchango wako. Muda wako umeisha.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima niseme ukweli…
MWENYEKITI: Malizia sentensi ya mwisho Mheshimiwa, muda umekwisha.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaunga mkono hoja, nina ushahuri wa dakika moja. Ni kwamba, tuangalie mamlaka zote za uteuzi, muangalie qualification za watu rather than nepotism ili Taifa hili liweze kwenda mbele. Vinginevyo, hatutaweza kufika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)