Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa na Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha uliuoishia tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishi tarehe 30 Juni, 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezajiwa wa Mitaji ya Umma kuhusu uwekezaji wa mitaji ya umma kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Kwanza, nizipongeze sana Kamati hizi zote tatu; na kwa kweli hizi Kamati tatu ni Kamati ambazo zimepewa watu wanaojielewa, niwapongeze sana. hizi ni Kamati ambazo sisi kama Bunge tunatakiwa kuwapa maua yenu. Kwanza unaenda kuwahoji watu wengine wana nyota wanakuja na nyota na walinzi, lakini mmefanya kazi yenu vizuri, mmeleta Taarifa ili na sisi tuweze kuchakata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, mimi huu ni mwaka wa saba najadili taarifa ya CAG yangu ya saba hii. Kwa kweli tufike mahala tuoneane huruma. Niliwahi kusema humu ndani, kama Bunge tunaletewa hizi taarifa kwa ajili ya kuzungumza na kwenda nyumbani ni bora mkabadilisha utaratibu mkamaliza huko nje kwa nje. Kwa sababu, mimi ninajiuliza tunazungumza kila siku kitu kile kile. Ninataka nizungumze kitu kinaitwa KADCO; huyu ni nani kwanza; mimi ninataka kujua nyuma yake kuna nani? Kwa sababu mimi kabla sijawa Mbunge akina Zitto Kabwe wanakaa pale wanazugumzia KADCO, mpaka leo KADCO yule yule tunahangaika kwenye kila taarifa ya CAG.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nani yupo nyuma yake au na yenyewe ni Chalinze ile? Au nayo ni ile Chalinze ambayo ilikuwa haina mwenyewe nyuma yake? Kwa sababu, ninajiuliza kila mwaka tunazungungumza kitu kimoja kile kile. Ninakumbuka rafiki yangu Mbalawa mwaka jana, Mheshimiwa Songe Mbunge wa Itilima, ukasimama hapa kwenye kuhitimisha ukasema unairudisha TAA; sasa bado tena KADCO amekuja humu ndani. Na bado mwaka jana tumeona tena mwezi fulani amesaini tena mkataba na waarabu kuchukua Airport ya Arusha. Sasa mnatuchonganisha tu na watu, maana watu ni hawa hawa tunakutana mitaani. Kwa kweli kama Bunge hatuwezi kuwa na meno ya kutoa maamuzi na Serikali ikafanyia kazi hatuna sababu ya kuleta humu ndani. Mnakuja kututafutia uadui tu. Unamzungumzia IGP na General halafu unakutana naye huko. Sisi ni binadamu ukikosea kadogo si utamaliziwa hasira?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuchukue maamuzi kama tunamzia mtu tunafikia maamuzi. Mnaambiwa mtu ni mwizi, mnahakikisha ni mwizi, chukueni hatua lakini mkileta humu kwa kweli tuinafika mahala sasa tunakuwa tunanyamaza mkose wachangiaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kuzungumza kuhusu IPTL. Hii IPTL tangu Mheshimiwa Olesendeka; alikuwa role model wangu; namuangalia anahangaika, akina Kafulila pia, lakini mpaka leo tena. Watu wakasema fedha ya mboga zikalipwa fedha; leo tena na sisi kizazi chetu ameibuka humu tena anataka kulipwa. Ni deal gani hizi jamani? hata najiuliza hivi hizi fedha mnazipeleka wapi? Kwa sababu ni fedha nyingi mno zinatajwa kuibiwa, mbona kwenye benki mzungukoni hazimo? Niamini kwamba sasa mnazihamisha kweli kwenda nje au? Yaani ni matriloni ya fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Waheshimiwa Wabunge, mimi ninajiuliza; ukienda sehemu nyingi, ninaangalia hata ukiingia kwenye maduka bei za suti zimepanda kweli; na ukigusa shilingi milioni moja na laki mbili. Anakuja mwingine ananunua hata tano na kamoka kazuri na Kiingereza kingi, kumbe ni wezi. Ukimkuta mtu ofisini ameulamba vizuri amechomekea kumbe mtu ni mwizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, niwaombe, kama tuna uwezo wa kutoa maamuzi kuisaidia Serikali, kiukweli taifa hili linaibiwa fedha nyingi sana. Ukijumlisha hizi fedha tu zilizotajwa na CAG si fedha ndogo kwenye miradi ya maendeleo kama ingepelekwa. Ninadhani tuna maamuzi kabisa kama Bunge, sheria inaturuhusu kuchukua maamuzi kuielekeza Serikali; na msipotusikiliza basi tuchukue maamuzi kwenu wenzetu ambao tumewatuma mmechaguliwa kwenda kutuwakilisha huko kwenye Serikali. Kwa kweli fedha zinaibiwa mno, yaani unafika mahala, mimi elimu yangu ni ndogo najiuliza hivi definition ya shule ni wizi au ni kitu gani? maana mnatusumbua, wasomi ni wezi. Ukikutana naye supermarket amejaza machupa ya pombe ya gharama anakwambia how much, harry up, give me bill; kumbe ni fedha zetu hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani mimi ninajiuliza jamani. Itafika mahala tutakata tamaa hata kusomesha watoto kama definion ya elimu ni wizi ni bora tukafundishe watoto wetu wajitegemee kwa kulima. Namna hii hatuwezi kufika, lazima tufike mahala tuhurumie taifa. Hebu mwangalieni Mheshimiwa Rais anavyohangaika, kila siku tunaona mama wa watu anahangaika na fedha zinakuja. Na ninyi Mawaziri, unajua ukiuliza Mbunge humu ndani hakuna Mbunge hawaripotii (kutoa taarifa) wizi kwenye halmashauri zetu, mmemsikiliza Mheshimiwa Simbachawene; tunawaambia kila siku, mnaandika kwenye vi-diary kama unanisikiliza vile, lakini ukitoka unakachana ka-karatasi unakaacha hapo hapo. Sasa matokeo yake unakuja kutumbia sisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawaeleza kila siku wizi wote unaofanyika kwenye halmashauri; mara mchakato unaanza TAKUKURU, team, uchunguzi, mwaka unaisha ripoti ya CAG inakuja inasema tumepigwa shilingi bilioni sita. Nimezungumza, nilikuwa huku na mkurugenzi wangu, mpaka nimelia tangu Waziri akiwa Mheshimiwa Bashugwa. Nimemsema hadharani na document, chukua mwizi huyo, akatolewa kwangu akapelekwa Misenyi, katoka Ilemela kapiga 11 kwenye laki, katolewa Ilemela kaletwa kwangu kapiga shilingi bilioni tatu, katoka kwangu yupo Misenyi mwakani tunaye LAAC tena; sasa hayo ni mambo gani? Si ni afahdali tunyamaze tuwaachie?
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani mimi ninataka mniambie nyie wasomi, definition ya shule, mnafudishwa kutusaidia ambao hatukupata elimu au kutuibia? Maana ninajiuliza kitu kidogo; kwa wafanyabiashara ukikosea tu kosa dogo TRA wanakuja wanakwambia funga account, chukua fedha. Ninyi mnaotuibia matrilioni kwa nini mpo nje? Mimi sitaki kwenda hata mbali kusema kunyonga kwa sababu kunyonga hatutajua kwa Mungu anapata adhabu gani, anaweza kusamehewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufungue gereza. Tuna mashamba makubwa ya NARCO, fungua gereza, peleka gereza la kilimo walime mpaka warudishe zile fedha. Tunahitaji kupata nguvu kazi. Sasa, mwizi akijiuliza nikiiba nikikamatwa, kulima nadhani watu watanyooka; lakini kwa dizaini hii mzee, tunapigana taarifa. Huyu akizungumza, taarifa, taarifa. Tuogope kusema watu, hapana. Kwa kweli tumepigwa vya kutosha sisi kama Bunge; na Watanzania mkiangalia tokea jana wanavyolisema Bunge letu, ni Bunge la kiwango, lazima tutoke na jitu humu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawashukuru sana Mawaziri lakini watanisamehe. Unaweza ukapima, katika kipindi ambacho Waheshimiwa Wabunge wanataka kulieleza taifa ni kipindi hiki ambacho tunazungumza Taarifa ya CAG; lakini Mawaziri hawapo, wapo moja, mbili, tatu, wengine wapo huko kantini; hakuna u-serious. Kaeni hapa msikilize ili mjue tunachokisema humu. Na nimuombe hata Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Rais, futa safari zote mpaka watu wajadili hii taarifa ikamilike. Kwa sababu, matatizo haya tunawaeleza kila siku (diary) halafu ukitoka kantini mtu amesahau.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mnaanza!

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Karibu.



TAARIFA

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonekana Mawaziri hatupo. Ninaomba Mawaziri tusimame ili tuonekane.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma endelea na mchango wako.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamheshimu Mheshimiwa Simbachawene, tuangalie Mawaziri na Naibu Mawaziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajiuliza kwa hesabu ya kawaida, taarifa inasema tuna wafugwa 3,100, wamemaliza muda wao wanakula. Ukisoma humu ni wafungwa wa nchi za nje. Sasa, shilingi bilioni tano kwa mwaka, ukipiga tu hesabu, kwa nini tusitoe hata Dream Liner tukawarudisha kwao Ethiopia? Kwa nini tunaendelea kuwalisha? Na kwa nini wale bure? Kwa nini tusifungue magereza ya kilimo tukaweweka huko tukapata nguvu kazi. Kwa nini unakaa na watu, huna kazi nao, hukumu yao imeshakwisha? Hamuogopi hata dhambi kwa Mungu kwa Mnawaweka watu magereza? Chukueni ndege. Kama tunatoa ndege kupeleka timu ya timu ya mpira, kwa nini tusitoe ndege kupeleka wakimbizi kwenye nchi zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni kuhusu TANOIL. Mimi nilikuwa Mjumbe wa Kamati ya Nishati, Mwenyekiti wangu Kitandula. Nilikataa hiki kitu kutoa fedha kuwapa TANOIL, nikawaambia zinaenda hizi fedha; znaenda kabisa hizi fedha. Leo tunazungumza short ya shilingi bilioni saba. Haki ya Mungu tuwe hai mwakani, shilingi bilioni 80 imeshaenda pale. Serikali msikubali kuanza kufanya biashara, mmefeli. Tumewapa mradi wa mabasi ya mwendokasi, barabara ya kwenu, magari ya bure leo yanatembea manne kutoka gari 300 na bado mnajenga mwendokasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye projector pale wanakwambia barabara ya Mbagala itakuwa hivi; unawekewa wazungu wanakimbizana kupanda gari kumbe wezi watupu. Wewe mabasi unaweka kodi, mchakato, gari imedondosha bolt unaambiwa wa kusaini yupo Dodoma. Mabasi yote yameisha, bado mnaenda kufanya kazi. Serikali kwenye suala la biashara acheni, tuachieni sisi watoto wa kitaa.