Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Dr. Josephat Mathias Gwajima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nichangie kwenye hii taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili na Utalii. Kwanza nakushukuru wewe na pia namshukuru Mwenyekiti wa Kamati yetu ndugu Mnzava pamoja na wewe ambaye ni Mwenyekiti lakini ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuanza na Wizara ya Maliasili, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Wizara hii iliidhinishiwa kiasi cha shilingi bilioni 163 na katika fedha hizo Bunge liliidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 82 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Kwenye hizo fedha za miradi ya maendeleo kuna kiasi kama shilingi bilioni 14 ni fedha ya ndani na kuna shilingi bilioni 68.1 ni fedha ya nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ilikuwa na makusudio ya kukusanya shilingi bilioni 300 lakini mpaka kufikia Desemba 2023, Wizara hii imekusanya shilingi bilioni 76 peke yake. Ambayo ni asilimia 26 tu ya malengo yake ya kukusanya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni disaster, tena ni disaster kweli kweli; lakini bado wizara hii imetumia fedha. Yenyewe imekusanya shilingi bilioni 76 lakini yenyewe tayari imepokea fedha shilingi bilioni 194.8. Imepokea kutoka wapi kama yenyewe haina uwezo wa kukusanya? Ni kitu gani kinafanya hii wizara giant ambayo ardhi yote ya Tanzania iko chini yake, nyumba zote za Tanzania ziko chini yake na ishindwe kukusanya mapato; lakini tayari imepokea shilingi bilioni 194. Hii fedha imetoka wapi? Kwenye hii fedha iliyopokea imelipa madeni, imelipa fidia na imetatua migogoro. Tayari fedha hii iliyopokea imeshatumia tayari asilimia 95 ya hizi fedha. Yaani yenyewe haikukusanya vizuri, imepokea na imeshatumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Bunge lako linisikilize, shida ya nchi yetu ni kukosa mipango. Naipongeza sana Serikali kwa kuiongezea Tume ya Bajeti ya matumizi bora ya ardhi kutoka kuwa na bajeti ya shilingi bilioni 4.8 mwaka jana 2022/2023 kufikia mpaka shilingi bilioni 8, 2023/2024. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuongea mambo, Wizara ya Ardhi na Maendeleo na Makazi is a sleeping giant. Ni wizara ambayo inaweza kuiletea nchi yetu fedha nyingi sana, Nchi ya Tanzania ina karibu square kilometer za mraba 945,000. Nchi yetu ina idadi ya vijiji 12,318, Kata 3,564, Tarafa 570 na kati ya hii vijiji vilivyopimwa hadi kufikia sasa ni vijiji 10,744.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vilivyoandaliwa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ni vijiji 3,681. Vijiji ambavyo havijaandaliwa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ni vijiji 8,637 na eneo ambalo limekwisha kupimwa na kupangwa la mjini ni asilimia 30 tu ya mijini imekwisha kupangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana kuona mahali ambapo Mwenyezi Mungu ametupa ardhi kubwa ili kwamba kupitia ardhi hiyo tupate mapato; lakini hatuwezi kukusanya mapato na matokeo yake tunaishia kuwa tunakopa mahali ambapo sisi wenyewe tungeweza ku-run nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano, kama ardhi yote ya Tanzania ikapimwa, kila kipande cha ardhi ya Tanzania kikapimwa na kikawa na hati, hii inamaana kwamba kila kipande cha ardhi ya Tanzania kiwe kinamilikiwa na mtu binafsi au taasisi au na shirika, kitalipiwa kodi ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi yote ya Tanzania ikapimwa, kila kipande cha ardhi ya Tanzania kikapimwa na kikawa na hati. Hii ina maana kwamba kila kipande cha ardhi ya Tanzania, kiwe kinamilikiwa na mtu binafsi au na taaasisi au na shirika kitalipiwa kodi ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mifumo ya Kiserikali ikaunganishwa, Wizara ya Mheshimiwa Nape wakaamua kuunganisha mifumo na Wizara ya Ardhi; kwamba kila kipande cha ardhi kikawa na hati na wakatengeneza mfumo ambao kila ukifikia wakati fulani ule mfumo una-generate control number, unamtumia mtu mahala popote alipo na fedha inalipwa kutokea popote pale alipo. Fedha itaanza kuingia kupitia Wizara ya Ardhi kwa namna ambayo huwezi ku-emagine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni aibu kubwa tena kubwa sana a giant Ministry kama Wizara ya Ardhi inaweza kukusanya shilingi bilioni 76 kwenye malengo yake ya shilingi bilioni 300. Hili ni jambo tunahitaji kuliangalia tena na tena. Kwa hiyo ningeomba sana hii Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi iongezewe fedha ili hatimaye nchi yetu yote tuipime, narudia tena, nchi yote ipimwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna faida za kupima nchi yote. Kwanza, tunaepuka migogoro ya ardhi, mbili tunaipa ardhi thamani na kuwasaidia wananchi wetu waweze ku-mortage ardhi yao wajipatie mapato yao. Tatu itatusaidia sana kwenye kukusanya mapato ya nchi. Ardhi ni mali ambayo kila mwaka utakuwa unategemea fedha na itakuwa inaingia kila wakati. Lakini leo ardhi yetu imekuwa a sleeping giant. Kwa sababu ya kutokupanga kwa ardhi yetu imesababisha kuwa na changamoto za wanyama waaribifu

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye taarifa ya Kamati hii wameazimia, naomba nisome kidogo kwenye changamoto za wanyama wakali na waaribifu. Kamati inaazimia kwamba, Serikali ihakikishe inakamilisha zoezi la kuondoa shoroba za wanyama wakali na waharibifu 18 ilizojipangia katika mwaka 2023 mpaka mwaka 2024 ili kupunguza mwingiliano wa shughuli za wananchi na wanyama hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shoroba ni nini? Shoroba ni njia ambazo wanyama huwa wanapita traditionally. Wanyama kama tembo wana kumbukumbu ya ajabu sana. Tembo akipita barabara fulani akaenda baada ya miaka mitatu anarudia kwenye barabara hizo hizo. Zipo njia ambazo wanyama wanapita traditionally ambazo zinaitwa shoroba au njia za wanyama. Sababu mojawapo inayofanya wanyama tembo wanatoka kwenye hifadhi wanaingia kwenye nyumba za watu na kuharibu maisha ya watu ni kwa sababu kwenye maeneo ya shoroba ambazo wanyama wangepita Serikali yenyewe imejenga nyumba maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na inashangaza sana wanaposema kwamba wanataka kuondoa shoroba 18. Nikupe mfano. Moja kati ya maeneo ambayo ni shoroba zimejengwa. Halmashauri ya Mvomero imejenga ghorofa kwenye shoroba ya wanyama. Leo wanaposema hapa wanakwenda kuondoa shoroba, utakwenda kubomoa Halmashauri ya Mvomero? Mojawapo ya maeneo ambayo ni shoroba zimejengwa kuna Chuo Kikuu kimojawapo kimejengwa kwenye shoroba. Mojawapo ni airport moja imejengwa kwenye shoroba ya wanayama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mkituambia kwamba mtakwenda kuondoa hizo shoroba huwezi kutushawishi utakwenda kuharibu Halmashauri ya Mvomero au uharibu airport…

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa.

TAARIFA

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na namuunga mkono Mheshimiwa Askofu Josephat Gwajima kwa mchango mzuri. Ameeleza kwa habari ya airport iliyojengwa kwenye shoroba ni airport ya Kilimanjaro. Ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Josephat Gwajima umepokea hiyo taarifa?

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa ya ndugu yangu Mheshimiwa Kunambi. Kwa hiyo hizi ni Taarifa za Wizara sio taarifa za kwangu. Sasa kitu gani kinachosababisha Halmashauri iwe na building permit ya kujenga kwenye shoroba? Kitu gani kinachosababisha airport iwe building permit ya kujenga kwenye shoroba? Kitu gani kinachosababisha university iwe na building permit ya kujenga kwenye shoroba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kukosa mipango ya muda mrefu ya matumizi bora ya ardhi. Kama nchi yote ingepangwa tayari pangejulikana eneo hili ni shoroba, eneo hili ni mbuga ya wanyama, eneo hili ni kijiji; na kwa namna hiyo wanadamu wasingefanya shughuli za wanadamu kwenye shoroba za wanyama na tukaingia kwenye haya tuliyonayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mpango tunaojaribu kuufanya wa kuwaokoa wananchi wetu wa wanyama waaribifu hautafanikiwa kama hatujaingia kwenye mipango bora ya ardhi. Nashukuru sana Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kwa makusudi kuongeza fedha kwenye Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi mwaka huu, angalau itasaidia lakini niseme jambo moja. Kama tusipoipanga nchi yote tutapata matatizo. Kwa sababu leo hii mwananchi mmoja anahamia mahala fulani, anafika pale anajenga nyumba yake, akijenga nyumba yake anavuta na umeme wananchi wenzake nao wanamuona wanajenga karibu wanaanza kuongezeka inakuwa Kijiji lakini tungekuwa tumepanga vijiji vyote, tumepanga nchi yote hii ingetusaidia sana kama taifa tusingekuwa na migogoro ya ardhi tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbuka hii fedha shilingi bilioni 194 iliyotolewa inatatua migogoro hiyo hiyo, inalipa fidia hizo hizo, inajaribu kulipa madeni yale yale lakini nakuomba sana tuisaidie Serikali, tuazimie kwa nguvu zetu zote kuwa mipango ya muda mrefu, nchi yote ipangwe. Kila kipande cha ardhi ya Tanzania iwe kichuguu, iwe barabara, iwe njia panda, ipangwe ili iwe sehemu ya kuipa Serikali fedha. Tutasaidia sana nchi yetu kupata fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo ningependa kulikazia sana. Hebu tuone ukweli uliopo kati ya hii fidia inayolipwa kwa wananchi walioshambuliwa na wanyama waharibifu, ni kidogo sana. Ni kweli there is no value for human life, there is no amount that can be paid for human life it is true. Hakuna kiwango kinachoweza kulipwa kwa maisha ya mwanadamu lakini angalao wale wanaoshambuliwa na wanyama wawe na faraja fulani. Naomba sana hayo maazimio ya Kamati Serikali iyazingatie sana na iyafanye vizuri. Lakini nchi lazima ipangwe. Nchi isipopangwa tunajiandaa tena kutengeneza migogoro mingine tena, tutakuwa tunalipa migogoro tena na tena na hatutafika mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, sasa Tanzania yote ipangwe; na Wizara ya Ardhi msipokuja na bajeti ya kupanga Tanzania yote kwenye Bunge lijalo nitashika shilingi mpaka mwisho kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi yetu Tanzania. Ahsante sana. (Makofi)