Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa na mimi leo kuchangia. Kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema lakini pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya lakini pia niipongeze Kamati hii ya Ardhi, Nyumba, Maliasili na Utalii kwa kazi kubwa ya uchambuzi ambayo imefanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo nilitaka nichangie mambo machache sana. Nianze kwa kusema yafuatayo. Sekta ya Ardhi ama Wizara ya Ardhi tukubaliane ya kwamba ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wetu wa nchi yetu hii ya Tanzania. Sekta ya Ardhi imebeba mambo mengi sana. Tunapozungumzia habari ya maendeleo ya ukuaji wa uchumi hatuwezi kuacha kuizungumzia Sekta ya Ardhi. Tunapozungumzia habari ya uwekezaji ni lazima tuguse ardhi. Tunapozungumzia habari ya kilimo ni lazima tuguse ardhi. Sasa ni namna gani hii Wizara ya Ardhi imejipanga kikamilifu kuhakikisha ya kwamba inatumia ardhi hii katika kuonesha ya kwamba inaleta mchango mkubwa wa uchumi kwenye taifa letu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Ardhi katika nchi yetu nadhani imekuwa ni tofauti kidogo, na hasa ukiangalia namna ya mipango ya matumizi bora ya ardhi katika nchi hii umeona kuna changamoto kubwa. Mheshimiwa Gwajima amezungumza hapa, ametaja ukubwa wa nchi yetu hii, kwamba ina ardhi kubwa, square meter za mraba zaidi ya 940 na zaidi lakini tukubaliane tu, kwa hali tuliyofikia kwa sasa nikitazama namna Sekta ya Ardhi ilivyojipanga kwenye nchi yetu hii, mimi naona kama hatuna ardhi kwa sasa. Kwa nini nasema kwamba hatuna ardhi, ni kwa sababu ya mipango ambayo Wizara ya Ardhi imechelewa kuhakikisha ya kwamba inaleta mipango mizuri ya matumizi bora ya ardhi kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii utaona Waziri Bashe ana mipango mizuri sana ya kuinua Sekta ya Kilimo kwenye nchi hii. Lakini swali la kujiuliza hapa, hiyo ardhi ambayo Mheshimiwa Waziri wa Kilimo anatamani anyanyue Sekta ya Kilimo ipo wapi? Utaona kwamba mipango mibovu ya ardhi ambayo huko nyuma imeweza kuchukuliwa, hawakuweka mipango mizuri ya kutenganisha maeneo kwenye nchi hii. Ndiyo maana umeona tukijaribu kuangalia uwekezaji wa mashamba makubwa kwenye nchi hii hatuwezi kupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukienda kwenye maeneo yetu hakuna matumizi na mipango mizuri ya ardhi. Kwamba wapi ardhi ya mifugo, wapi ardhi imetengwa ya wafugaji? Ipo wapi ardhi imetegwa kwa ajili ya shughuli za kilimo, ipo wapi ardhi imetengwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda? Hakuna, ni vise versa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda kwenye maeneo yetu utaona hakuna sheria ambayo imewekwa inayom-protect mtu na inamzuia mtu kuwekeza kitu chochote kwenye maeneo yoyote; na ndiyo maana umeona leo hii ukienda kwenye ardhi, kwenye ardhi kwa mfano kwenye Jimbo la Msalala, hatuna maeneo ambayo tumeyapanga kwamba maeneo haya yatakuwa mahususi kwa ajili ya kilimo tu peke yake; na hakuna mtu yeyote yule atakayeweza kupewa permit ya ujenzi either wa nyumba za kudumu kwenye maeneo hayo. Tuyaache yawe ni maeneo ya kilimo tu. Itatuwezesha kumwezesha Waziri wa Kilimo kuja na mkakati wa kuja na mkakati wa kuhakikisha ya kwamba anawezesha sekta ya kilimo kwenye eneo lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake ni nini? Kwenye eneo hilo hilo tulilotenga la mashamba ndiko kunakojengwa nyumba, eneo hilo hilo la makazi ndiko kunakojengwa viwanda, eneo hilo hilo la makazi ndiko shughuli zozote zile zinaendelea kwenye maeneo hayo. Matokeo yake ni nini; tunapokuja kwenye kuanza kutafuta maeneo ya uwekezaji katika maeneo ya kilimo na maeneo mengine tunakosa maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana, Wizara ya Ardhi ni wakati sasa umefika wa kukaa na kujitadhimini ni namna gani bora ya kukaa na kujifumbia kuanza kuweka matumizi bora na kupanga mipango bora ya matumizi ya ardhi kwenye maeneo yetu ili tuweze kuwa na ardhi itakayotuwezesha kuwekeza kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kuna wawekezaji walitoka nje ya nchi wakaja kwenye Jimbo la Msalala, wakawa wanahitaji eneo la uwekezaji wa kilimo hekta elfu kumi tulikosa. Leo kuna wawekezaji wanakuja wanataka kuwekeza kwenye mashamba makubwa lakini hatuna mashamba hayo, ni kwa sababu hatukuwa na mipango mizuri ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninaomba nizungumzie suala la migogoro ya ardhi. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi, Ndugu Makonda kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. Niombe Wizara ya Ardhi, hebu iangalieni Wizara anayofanya Katibu Mwenezi Ndugu Christian Paul Makonda, migogoro mikubwa, changamoto kubwa kwenye mikutano ile ni migogoro ya ardhi. Mimi jimboni kwangu tuna migogoro ya ardhi mingi sana. Ukienda kwenye Kata yangu moja ya Jana tumekuwa na migogoro ya ardhi watu wanaporwa ardhi zao, wanadhulumiwa ardhi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia utaratibu wa namna ya kutatua migogoro hii hasa kupitia mabaraza haya imekuwa ikiwanyima haki ya wamiliki wa ardhi na wadai wa ardhi kupatiwa haki zao kwa wakati. Ni wakati sasa Wizara ya Ardhi kupitia upya mabaraza haya; na ikiwezekana tutenge fedha kuyawezesha mabaraza haya yawe yanakaa mara kwa mara ili kuweza kutatua matatizo ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini leo utaona mtu anapeleka kesi yake kwenye Baraza la Ardhi la Kata, linakaa labda mara mbili kwa mwaka na wakati mwingine hawana bajeti linaweza lisikae. Maana yake ni nini? Mgogoro wa ardhi ambao walipaswa kupata hati mapema inamchukua ndani ya miaka minne hadi mitano mpaka kupata hati yake ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni uwekezaji kwenye maeneo ya madini. Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri naomba mnisikilize vizuri. Ni wakati sasa umefika wa Mtanzania ambaye Mwenyezi Mungu amemjalia kumpa neema ya kumiliki ardhi kwenye eneo hilo, na kupitia umiliki wake wa ardhi kwenye eneo hilo akamjalia uwepo wa madini chini ya ardhi hiyo anayoimiliki. Sasa kumekuwa na changamoto ya fidia kwenye maeneo hayo. Pindi muwekezaji anapopatikana kwenda kuwekeza kwenye maeneo hayo, utaratibu wa fidia unaotumika hauzingatii kwa kuangalia thamani ya ardhi kwenye eneo hilo. Pia imeenda kwa kuzingatia thamani ya kuangalia maeneo haya yapo vijijini bila kuangalia mali iliyo kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo utaona; kuna mgogoro mmoja, na naomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri huu mgogoro ukatatuliwe. Tuna mgogoro kwenye Kata moja ya Mwakata. Kuna mwekezaji alikuja akakuta kijiji kipo pale anaitwa Kanuck, akawakuta wananchi wanaishi pale na wanaishi pale na wanaendeleza shughuli zao pale, akapata leseni ya uchimbaji wa madini kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa sheria zetu ni kweli amemiliki leseni na anahitaji kulipa fidia lakini kwa mara ya mpaka tunavyozungumza hivi leo, bado wananchi wa Mwakata hawajapatiwa fidia ya maeneo yao. Hata tathmini waliyofanyiwa mwanzoni, tathmini inafanyika lakini pia kumekuwa na watumishi ambao si waaminifu. Mwekezaji anawapa dhamana Wizara ya Ardhi kwenda kufanya tathmini, tathmini inayofanyika inafanyika bila kuzingatia thamani ya madini; na thamani ya mali zilizopo pale. Alipaswa kulipwa milioni kumi, anaambiwa alipwe milioni moja laki tano wakati ardhi ile inamiliki zaidi ya mabilioni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kutokana na kile ambacho kimeshafanyiwa udhamini bado ucheleweshaji wa malipo unachukua muda. Mathalani unakuta kuna kesi moja Bulyanhulu, toka mwaka 2006 tunazungumza, watu wamefanyiwa tathmini mwaka huu malipo yao yanakuja kulipwa mwaka unaokuja, sheria imeshabadilika, ardhi imepanda thamani, wananchi wanagoma. Leo mnakuja kulazimisha kulipa fidia kipindi ambacho uthamini umefanyika lakini sio kipindi ambacho malipo yamefanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana, Wizara muweze kuweka msukumo pindi muwekezaji au mtu yeyote anaenda kufanya uthamini wa ardhi, malipo ya ardhi (fidia) ahikikishe ya kwamba analipa kwa wakati ili kuondokana na ucheleweshaji ambao utampelekea hasara mmliki wa ardhi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kule Mwakata mpaka tunavyozungumza leo wananchi bado hawajapatiwa malipo yao, fidia ya maeneo hayo; na Wizara ya Madini imeenda kuzuia shughuli za wananchi lakini wananchi wale hawajapatiwa fidia. Lakini cha kushangaza mwekezaji huyu ame…

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa inatoka wapi?

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mtaturu karibu.

TAARIFA

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nataka nimpe taarifa mchangiaji anayechangia vizuri kwamba ardhi ndiyo urithi pekee wa mwananchi. Sasa maeneo ambayo anaeleza yamekuwa yakijitokeza, wananchi wanafanyiwa tathmini na hakuna shughuli zinazoendelea kwa muda mrefu. Kwa hiyo mwananchi aendelee na shughuli na wakati huo mwekezaji aendelee na shughuli. Kwa hiyo ninataka nimpe taarifa kwamba anachosema ni sawa, kuna haja ya kuangalia sheria upya. Kwamba anayepewa leseni akishindwa katika muda fulani wananchi waendelee na shughuli zao ili wananchi waendelee kutumia ardhi hiyo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Iddi unaipokea hiyo taarifa?

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hii ya ndugu yangu Mheshimiwa Mtaturu kwa mikono miwili na niongeze kwa kusema kwamba ikiwezakana basi Wizara ya Ardhi mtoe tamko, muwekezaji huyu kama hajalipa fidia asianze kufanya shughuli zake kwenye eneo hilo mpaka ahakikishe kwamba malipo yote yamefanyika kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo huyu anamiliki ardhi ya juu, huyu anamiliki leseni ya madini lakini kwa kuwa huyu anatakiwa amlipe anamwambia wewe unamiliki eneo la juu, wewe endelea na shughuli zako za juu halafu yeye anachimba chini kwa chini. Wakati huo huo huyu anaishi na nyumba zake na familia, milipuko inafanyika, yeye akiwa juu na huyu anafanya milipuko chini. Sasa swali langu linakuja; hivi Serikali, Wizara ya Ardhi, Wizara ya Madini kwa nini msikae pamoja mkaona namna gani ya kuwasaidia wananchi hawa wanyonge kuhakikisha na kwamba wanapewa fidia zao? Ili kuhakikisha ya kwamba muwekezaji analidwa lakini pia na wananchi wenye haki zao wanalindwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ni kesi kubwa ambayo inaendelea. Bulyanhulu tuna kesi nyingi sana. Tuna kesi moja ya toka mwaka 1996 mpaka leo bado haijapatiwa mwafaka lakini tuna kesi nyingine ya mapunjo ambayo tunasema ni haya haya kuchelewesha malipo. Uthamini ulifanyika na wakati unafanyika malipo ya ardhi yalikuwa bado hayatambuliki, yalikuwa yanatambulika malipo ya vitu vilivyomo kwenye ardhi peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kucheleweshwa malipo yao, mwaka ambao wanaenda kulipwa fedha zile tayari sheria imeshabadilika na inatambua sasa ardhi inaweza ikalipwa. Maana yake hawa watu wakaja wakadai walipwe ardhi yao upya lakini mgodi wa Bulyanhulu ulikaa chini na ukasema sawa, ukapitia upya na kuona sasa tutalipa; na wanakubali kulipa; lakini bado kuna watumishi ambao sio waaminifu ndani yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ambayo imetolewa na mgodi walipwe wananchi malipo yao ya ardhi, fedha ile ikaenda kwa watu wajanja na fedha ikalipwa kwa watu ambao hawastahili na migogoro ikaendelea kubaki palepale na wananchi bado tunaendelea kulaumu Mgodi wa Bulyanhulu wakati Mgodi wa Bulyanhulu hauna matatizo kwa sababu wenyewe wamekubali kweli ardhi hii ni ya wananchi na ikatenga fungu kutoka milioni 300 ikaongeza milioni 200 ikawa milioni 500 kwamba wananchi walipwe; lakini Kamati zilizoundwa zimeenda kufanya ndivyo sivyo na zikalipa watu ambao hawastahili, na wadai mpaka leo wanaendelea kulia na ardhi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba Mheshimiwa Waziri, ni wakati sasa umefika wa kwenda kumaliza migogoro kwenye Jimbo la Msaala, kwenye Kata ya Bulyanhulu. Wadai hawa wanadai toka muda mrefu sana, toka mwaka 2003 wengine wanadai toka mwaka 1996. Niombe ni wakati sasa umefika wa Wizara kwenda kutatua migogoro hii, migogoro ya ardhi ni mingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niombe, amezungumza Mwenyekiti wa Kamati, hapa kuna Tume iliundwa ya Mawaziri Nane kwenda kushughulikia migogoro, ikikupendeza hebu Bunge lako hili tunaomba taarifa ile ije iletwe hapa ili watuambie wamefikia wapi, kwa sababu sisi ndiyo tunaishi na wananchi na wananchi wanatarajia majibu kutoka kwao na sisi tuwapelekee majibu, migogoro hii imefikia wapi. Wakati mwingine migogoro hii haiishi kwa sababu bado inasubiri Kamati hii, imalize kazi yake. Kila mwaka tunasomewa hapa Kamati ile bado inaendelea. Kwa hiyo, niombe sana ikiwezekana basi Kamati ile ya Mawaziri iliyoundwa ilete taarifa hapa tujadili ili tuone imefikia wapi na tuweze kushauri kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ni suala zima la upimaji wa ardhi. Alizungumza mwaka jana Mheshimiwa Kunambi, akasema Wizara ya Ardhi ikitumia ardhi yake vizuri inaweza kuchangia pato kubwa sana kwenye Pato la Taifa. Mimi nakubaliana naye kwa asilimia 100 nakuunga mkono leo Mheshimiwa Kunambi, kwamba kama Wizara ya Ardhi itajipanga vizuri inaweza ndiyo ikawa sekta ambayo inachangia mchango mkubwa kwenye Pato letu la Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitatoa mfano mmoja. Hapahapa Dodoma toka 2020 Miganga North, tayari wananchi eneo lile lilipimwa na baada ya kupimwa tukaambiwa tulipie fedha na wananchi wakalipia fedha, baada ya kulipia fedha mpaka leo toka 2020 bado wananchi wale hawajapatiwa hati zao. Tumefuatilia tukaambiwa kwamba bado Halmashauri imekosa kiasi cha shilingi milioni 50 tu, kwenda ku-approve ramani ili basi procedure za hati ziendelee. Maana yake ni nini? maana yake ni kwamba kukosa milioni 50 kunaikosesha mapato Serikali zaidi ya mabilioni kwenye eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Mheshimiwa Naibu Waziri, hebu nendeni mkaone namna gani manaweza kuonyesha ya kwamba mnatatua migogoro hii na mnasimamia vizuri kwenye maeneo haya; lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, baada ya kuona kuna umuhimu mkubwa wa kupanga maeneo yetu alitoa fedha kuzipeleka kwenye baadhi ya Halmashauri, hata Halmashauri yangu ilipatiwa kiasi cha shilingi bilioni moja na milioni mia sita kwa ajili ya matumizi kupanga ardhi kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikajiuliza hivi hizi pesa tulizopeleka kule kwa ajili ya kupanga ardhi, tulijipanga vizuri. Tumepokea kiasi cha shilingi bilioni moja na milioni mia sita lakini namna ya uandaaji wa maeneo yale mimi wananishangaza mpaka leo, nilienda kufanya ziara kwenye maeneo mengine nimeona wenzetu wanapotaka kupanga maeneo, moja wanahakikisha kwamba wanapeleka miundombinu kwenye maeneo yale, kama ni barabara wanatengeneza barabara kwenye maeneo yale, kama ni maji wanapeleka maji, kama ni umeme unapelekwa umeme halafu baada ya hapo wanaanza advertisement ya viwanja vile ili viweze kuuzika na ile fedha iweze kurudi na wananchi waweze kupata kwenye maeneo yale, lakini kilichofanyika ni tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda kutumia zile fedha, tumeenda kufanya malipo kwenye maeneo yale lakini hatujapeleka miundombinu na wala hata kutangaza hatutangazi, matokeo yake vile viwanja haviuziki na Serikali inahitaji fedha zirudishwe. Sasa najiuliza huu mpango wakwenda kupanga miji kwenye maeneo hayo hivi mmejipanga kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Wizara ya Ardhi hebu pitieni fedha ambazo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezipeleka kwenye Halmashauri hizo muone nini kinakwamisha kuhakikisha kwamba viwanja vile vinauzika kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine …(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa muda wako umeisha.

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie la mwisho. Mheshimiwa Waziri hili alichukue, kumekuwa na uporaji wa maeneo ya wananchi hasa kwa Wakurugenzi wa Miji. Kuna eneo moja liko eneo la Nyamagana, eneo hili mmiliki anaitwa Mzee yuko pale, yule Mzee anamiliki lile eneo toka enzi za uhuru lakini leo hii Halmashauri ya Jiji la Mwanza imekuja pale na kutaka kulichukua eneo lile kwa nguvu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kulichukua kwa nguvu Mzee yule kaenda Mahakamani, Mahakama ikaamuru yule Mzee arudishiwe eneo lake liko Makongoro opposite na Benki Kuu, Mkurugenzi amekataa kumrudishia eneo hilo. Sasa niombe Mheshimiwa Naibu Waziri, haya mambo siyo mpaka Katibu Mwenezi, siyo mpaka Mheshimiwa Waziri Mkuu, siyo mpaka Mheshimiwa Rais, aende ninyi mnaweza kuyamaliza. Hebu wasilianeni na Wakurugenzi hawa muwaulize, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza shida yake ni nini, kwa nini anataka kupora eneo la mwananchi ambaye amalihangaikia kwa muda mrefu? Ahsante. (Makofi)