Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Kwanza namshukuru Mungu sana kuiona siku ya leo ya wapendanao. Vilevile nawapongeza Wenyeviti hawa wawili ambao kweli wamewasilisha hotuba zao hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo pia ya kushukuru kwanza kabla sijaanza kusema. Namshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kweli ametufanyia jambo jema katika Majimbo yetu sisi Waheshimiwa Wabunge. Ametuletea fedha za kutosha katika maeneo yetu kwa sekta zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hii, naomba niende moja kwa moja, kwa kuanzia na eneo letu hili; mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PIC. Ukiangalia Mwenyekiti wetu wakati anasoma wasilisho lake hapa, nataka niende kwenye upande wa Mashirika ya Serikali. Ukiangalia kwanza Benki ya Maendeleo (TIB), Benki hii nafikiri imeanzishwa kwa makusudi maalum ya kusaidia maendeleo katika nchi yetu na maeneo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sisi ambao tunatoka vijijini na maeneo ya wakulima, tulitegemea Benki hii iwe msaada mkubwa kwa maeneo yetu. Ukiangalia taarifa ya CAG inaonesha jinsi ambavyo Benki inadaiwa na inakwenda kufanya hasara. Mwaka 2021/2022, Benki imekuwa na hasara ya shilingi bilioni 129. Inaonekana wapo wadaiwa sugu ambao wapo katika eneo hili la mikopo ya Benki hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, ni vizuri Serikali ikaamua kuweka miguu yake chini ili hawa wadaiwa wanaoonekana sugu warudishe fedha hizi ili walau na wengine wakopeshwe. Ukiangalia Benki hii, hakika kama watapewa fedha hizi na madeni haya yakawa yanalipika bila kuonekana sugu, ni wazi mfuko huu utatanuka na Benki itakuwa inajiendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia, tumeona namna ya kuisaidia, hasa ukiangalia mashirika haya ya Serikali, yako mengi na mengine yanasababisha hasara. Ukiangalia NARCO, ukiangalia TTCL na mengine mengi ambayo sitaki kuyataja kutokana na muda, tunaona hawa ndugu ambao wanaendesha mashirika haya (menejimenti), ndugu hawa ni kweli wanajitahidi lakini ukiangalia mashirika ya Serikali yamekuwa yanaingia hasara muda wote. Kwa nini yanaingia hasara? Ni wazi kuna tatizo katika gap hili la kuajiri hawa watu na namna ya kuwapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Kamati na ushauri wetu, kwa nini isianzishwe namna ya kuwashindanisha hawa viongozi kwa mfano Mwenyekiti wa Bodi, Wajumbe wale, wa-apply wanapoajiriwa, kila mmoja a-apply na itafutwe Tume ambapo wao watakwenda kuomba pale, washindanishwe. Pawe na mechanism ya kuwashindanisha hawa. Hatuingilii Mamlaka ya Uteuzi, Mamlaka ya Uteuzi ipelekewe majina kama matano hivi, lakini mtu aajiriwe kwa competence. Kwa nini nasema hivi? Ukiangalia kwenye mashirika ya binafsi, yanaendelea na Benki zingine zinaendelea. Kwa nini hizi za Serikali haziendelei? Ni vizuri Serikali ikaleta Muswada wa kubadilisha sheria kidogo ili tukaweka namna ambayo itayasaidia mashirika ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa mfano MSD hapa, sitaki kusema vibaya, lakini sisi na wananchi kwa kweli mara nyingi tunaitegemea sana MSD. Kwa mambo gani? Kupeleka dawa, vifaa tiba, lakini ukiangalia kwenye bajeti ya mwaka jana, 2023, tumepitisha hapa shilingi bilioni 561 ili ikafanye kazi yake ipasavyo, lakini leo ukiangalia, fedha hizo hazijafika katika maeneo yetu. Hamjawapatia MSD, wanapelekaje huduma ya dawa? Wanapelekaje huduma ya vifaa tiba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amejenga hospitali nyingi na zahanati nyingi, lakini unafanyaje kazi hii wakati MSD haijapewa hela? Ombi langu, Serikali ikubali kupeleka fedha MSD ili ifanye kazi ya kuwasaidia wananchi. Maeneo mengi dawa hazifiki kwa wakati au vifaa tiba havipo. Ni wazi kwamba, ni vizuri tukaona namna gani ya kuisaidia MSD. Naomba Wizara ya Fedha ione namna ya kuisaidia MSD ni kupeleka fedha kwa wakati wake. Kuna kitu kinachoitwa budget circle. Ikifika muda wa kupeleka fedha, ipelekwe

Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda kwenye eneo hili la kwenye Kamati ya Bajeti. Namshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, amewasilisha vizuri hotuba yake hapa. Ukiangalia leo, Wakandarasi wengi hawajalipwa kwenye miradi mingi ya Serikali. Kwa hiyo, miradi haiendelei. Kama miradi haiendelei, basi ni wazi kwamba tutaona jinsi ambavyo miradi inapanda thamani. Natoa mifano, kuna mwaka hapa niliruka sarakasi nikililia Barabara ya Haydom, au tunaiita Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ile, nashukuru Mungu sana na nimshukuru Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, niishukuru sana Wizara, barabara imetangazwa, mkataba umesainiwa. Sasa kinachotokea kibaya ni kwamba haipewi pesa na kama haipewi pesa Mheshimiwa Mwenyekiti, tazama tumesaini Mkataba fedha hazipelekwi na kama fedha hazipelekwi maana yake ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mkataba muda unaondoka na muda unapoenda ni wazi kwamba, itafika mahali yule mkandarasi atatudai fedha na mkandarasi akidai fedha maana yake nini? Barabara kama ilikuwa itengenezwe kwa bilioni 300 kwa vyovyote itapanda iende kujengwa kwa bilioni 400. Hasa ombi langu kwa Wizara, pelekeni fedha hizi barabara zitengenezwe lakini twende tuangalie kama uwezo wa fedha ni mgumu au kupatikana kwa fedha inakuwa kuna ukata huo najua lakini ni vizuri basi ukaona barabara zipi zianze? Zipi zifuatwe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi ni vizuri kwa ushauri wangu tusisaini barabara nyingi ili walau tuzitengeneze kwa uhakika. Angalia saizi kwa kuwa barabara zinavyosainiwa Wabunge wengi tunalalamika habari ya kujengwa kwa barabara, barabara ikisainiwa maana yake haijatengewa bajeti ya maintenance ya kila mwaka na kama aikutengewa bajeti barabara hiyo inakuwa tena haijengwi, hakuna mtu anaefanyia maintenance, kama haifanyiwi maintenance maana yake ni kwamba wananchi wanapata shida kupita kwenye barabara ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi nikuombe sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu sisi tuna barabara ile, tuletee fedha ili mkandarasi walau aanze down payment. Kuna fedha ile ya mwanzo kabisa wapatieni wakandarasi waanze kujenga barabara, barabara hizi kwa kweli ni barabara za Kimang’ati, barabara zinazotakiwa kujengwa. Nasema hivi kwa sababu gani? Nasema hivi kwa sababu maeneo yetu barabara zisipojengwa maana yake hakuna namna tena ya kupeleka mazao kutoka mashambani kwenda viwandani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu la mwisho hapa wamenituma wananchi niwaombe kabisa Serikali mpeleke fedha. Basi kama hakuna fedha hizo za kujenga barabara basi mpeleke fedha za maintenance turudi kwenye utaratibu wetu ule wa kawaida. Sisi tulijua mambo yameenda vizuri, tunaenda kujengewa lami. Ninaomba kwa kweli leo kupitia maneno yangu haya pelekeni fedha ili barabara ifanye nini? ijengwe kama ikishindikana ile ya mkandarasi basi tupeleke fedha za maintenance, tuweke changalawe wakandarasi wafanye kazi na hii itatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia leo hapa bajeti yetu ni kweli tunakusanya au tunatumia? Lakini tuone basi tunavyokusanya tunatumia, ukiangalia bajeti cycle tunapitisha bajeti toka mwezi wa saba, mwezi wa nane unapita wa tisa unapita wa kumi unapita wa kumi na moja unapita wa kumi na mbili unapita wa kwanza wa pili mpaka sasa hivi fedha hazijapelekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unategemea nini? maana yake ni kwamba tumebakiza muda gani? Tumebakiza mwezi wa tatu, mwezi wa nne wa tano inakuja bajeti mpya tunapiga tena bajeti mwezi wa saba. Sasa kwa miezi mitatu kama hujapeleka fedha bajeti ya mwaka 2023 kuja 2024 fedha hazijaenda lini watalamu watapata nafisi ya kutengeneza bajeti? Ombi langu ebu tupeleke fedha kwa wakati ili fedha hizi zikafanye kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona muda wangu umekwisha. Nikushukuru sana, lakini niunge hoja mkono ninaomba fedha zipelekwe ili kazi ifanyike. Ahsante sana. (Makofi)