Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Mchango wangu mimi utajikita kwenye Kamati ya Bajeti page 28 na 29 ambayo amezungumzia masuala muhimu yaliyojitokeza, lakini eneo langu la msisitizo itakuwa kwenye eneo la Bwawa la Kufua Umeme ama Mradi wa Mwalimu Nyerere ambao gharama yake ni trilioni 6.56 na kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati mpaka Julai, 2023 tumelipwa trilioni 5.53 ambayo ni sawa na asilimia 84.35 ya Fedha za Mradi ambayo ni sawa na asilimia 100 ya malipo yote yaliyoidhinishwa kulingana na utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati ya Nishati ambayo ilitoa taarifa hapa Bungeni, imetuonyesha kwamba ujenzi wa bwawa hili umefikia asilimia 95.83. Sasa mimi hoja yangu inajikita katika maeneo mawili ama matatu; eneo la kwanza, nataka tupate majibu kuhusiana na miradi ya Corporate Social Responsibility. Kamati inasema Serikali ihakikishe kwamba jamii inayozunguka maeneo ya mradi inanufaika na mchango wa hisani kwa jamii (Corporate Social Responsibility). Sasa mimi nina nyaraka mbili hapa ambazo zinaniongoza, ambazo nilitaka mwisho wa siku Serikali itujibu kwa sababu hii ni taarifa ya Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Taarifa ya TANESCO ambayo ilipeleka mbele ya Kamati ya Bajeti mwezi Oktoba, 2021, lakini vilevile tuna Taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali iliyotoka mwezi Machi, 2023 kuhusiana na Ukaguzi wa Kiufundi wa Mradi wa hili Bwawa la Julius Mwalimu Nyerere. Ambaye na yeye alizungumzia hii miradi, hii nini? Corporate Social Responsibility, hii michango ya kijamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia nyaraka ya Serikali inasema kwamba, kwanza kwa sababu inalipwa kwa ukamilifu wake, maana yake mpaka 2021 shilingi bilioni 262.3 zilitakiwa ziwe zimeishatolewa kwa ajili ya kwenda kufanya miradi hii ya kijamii, bilioni 262, ile taarifa ya Oktoba, 2021 na taarifa hii ikasema kwamba Serikali iwasilishe miradi inayotakiwa kutekelezwa ambayo ni Ujenzi wa Uwanja wa Michezo katika Jiji la Dodoma na Ujenzi wa Barabara ya Kiwango cha Lami umbali wa kilomita 41 toka Station ya Funga hadi eneo la mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ikaenda mbele ikasema tarehe 26 Juni, 2021 kikao cha mkandarasi baada ya majadiliano, mkandarasi alichukua hoja hizo ambazo zilishwa na upande wa Serikali na akasema watakabidhi fungu lote la mradi wa kijamii ambao ni sawa na asilimia nne ya hiyo package nzima ya mradi kwa Serikali ili Serikali isimamie Mradi wa Ujenzi, isimamie ujenzi husika hii ni 2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija Taarifa ya Mkaguzi Mkuu ambayo imetoka 2023 ambayo ndiyo jicho la Bunge, anasema mkataba wa uwajibikaji wa kijamii kwa ajili ya Mradi wa Umeme wa Mwalimu Julius, ulieleza kuwa makubaliano ya kina kuhusu utekelezaji wa mradi wa uwajibikaji kwa jamii yanapaswa kusainiwa ndani ya mwezi mmoja baada ya kusaini mkataba. Hata hivyo hakuna makubaliano yaliyoafikiwa hadi Oktoba 31, 2022 ambao ni miaka mitatu na miezi kumi na moja baadaye. Mnatakiwa msaini ndani ya mwezi mmoja baada ya ule mkataba Mkuu lakini ambao ulikuwa ni 2018 inapokuja Oktoba 31, 2022 hakuna kilichosainiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameenda mbele anasema Miradi ya Kijamii ilitarajiwa kuwa katika nyanja ya afya, elimu na ilikuwa na thamani ya asilimia nne ya bei ya mkataba. Serikali iliainisha mipango ya kujenga vyuo vya ufundi stadi, elimu na kadhalika kwa gharama ya bilioni 270. Sasa mimi nataka tuambiwe hapa kwamba kwanza huu mkataba umeisha sainiwa? Kwa sababu hawa watu tumeambiwa mradi umefika asilimia 98 sijui 95 unakaribia kumalizika. Kuna bilioni 270 net hatuja ipokea, TANESCO kupitia Wizara ya Nishati inatuambia tunajenga uwanja wa mpira na barabara sababu ya AFCON na vitu vingine, sisi hatuelewi, mtatujibu nyie wakati huo huo jicho la Bunge linasema tulikuwa tunatengeneza miradi ya elimu katika uhandisi wa umeme na vitu kama hivyo. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nadhani ni muhimu sana Bunge likapata majibu kuhusiana na eneo hilo, kwa sababu sisi ni kawaida yetu kupenda kuliwa lakini sisi kula vya kwetu ambavyo ni stahili yetu huwa hatutaki na ndiyo maana katika muktadha huo huo ninataka Serikali itujibu, itujibu kwa sababu hii ni Kamati ya Bunge wameongea na sisi tunachagiza kile ambacho Kamati ya Bunge inazungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa mkataba uliosainiwa 2018 mradi ulikuwa ukamilike 2022, Juni, tukasogeza mpaka Juni, 2023 tumesogeza tena mpaka Juni, 2024 sasa tunaambiwa kama ambavyo sisi tumekuwa tukilipa. Tukichelewesha barabara tunalipa, tukichelewesha kuwalipa Miradi ya Maji tunalipa. Sasa tunaambiwa hivi kulikuwa na Tozo ya Fidia ya Ucheleweshaji wa Mkataba wa takribani milioni 327.93 sasa ni hivi tumeambiwa kabisa kifungu cha 8(1) cha masharti ya jumla ya mkataba (…book of ninety-nine) kinaeleza kuwa iwapo mkandarasi atashindwa kuzingatia kifungu hicho kidogo cha pili cha kutimiza mkataba anatakiwa alipe fedha ambayo fidia ni 0.1 ya bei ya mkataba kwa kila siku iliyocheleweshwa. Sawa na bilioni 6.5 na fidia ya juu zaidi ya ucheleweshwaji ilipaswa kuwa asilimia tano ya bei wa ule mkataba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ucheleweshwaji huo wote niliouzungumza hao jamaa walitakiwa watulipe bilioni 327. Sasa mimi nataka Serikali ituambie hizi fedha zetu ziko wapi? Tuliingia mikataba, tumalize miaka mitatu ili mkandarasi anaelipwa kwa ufanisi kabisa hacheleweshewi ni kama vile ni mtoto anelelewa na kubembelezwa. Sasa kama hajatekeleza sehemu yake ya mkataba tunaka tuambiwe cha kwetu kilipo. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu ikaeleweka vilevile, kwa mujibu wa Wizara mwenyewe kupitia hii taarifa ya TANESCO walisema wazi, kwamba mkandarasi alikuja na kigezo eti ugonjwa wa COVID ndiyo ilikuwa sababu ya kuchelewesha. Serikali imejibu hapa ikasema walifanya uchunguzi wakajua hiyo haikuwa sababu kwa hiyo, msije mkaja hapa mkatujibu kwamba ohoo kulikuwa kuna visababu vimesababisha achelewe hatutaki visababu vyepesi. Tunataka kufahamu pesa yetu imekwenda wapi? Na fedha yetu tutaikusanya lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo nataka nilimalizie kwa udogo wake Kamati imezungmza kuhusiana na mazingira, kwamba Wizara ya Mazingira ihakikishe vyanzo vya maji vya mto viko katika utimilifu wake. Mkaguzi anatuambia hatarishi ya upungufu wa maji katika Mradi wa Julius Mwalimu Nyerere kutoka na shughuli za kibinadamu zisizodhibitiwa. Hii ni project ya trilioni 6.5 ni project ambayo leo tunazungumza deni la Taifa limeongezeka kutoka trilioni 74 mpaka trilioni 87 huu mradi pia unajengwa kwa mkopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkaguzi anatuambia naomba nimalizie Mheshimiwa. Kuwepo kwa shughuli za kibinadamu zisizodhibitiwa katika sehemu ya juu ya Mradi wa Julius Nyerere, katika eneo la juu ya mto kunahatarisha uhaba wa maji kutokana na matumizi haramu ya maji, vyanzo vya maji visivyolindwa, miundombinu mibovu ya umwagiliaji, kilimo cha biashara, mashamba makubwa, malisho ya mifugo na maeneo ya watu wa makazi mijini, mifereji ya umwagiliaji isiyosakafiwa inayopoteza maji kwa njia ya udongo na uvamizi wa mito uliosababisha uharibifu na kujaaa kwa udongo ndani ya mita 60 hivyo kusababisha ufinyu wa eneo la mto trilioni 6.5 ziko pale, tunategemea maji yatatiririka, kumbe hali ya zile njia za kupeleka maji ni dhohofu bin hoi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia mkaguzi anasema shughuli za kibinadamu zimesababisha kupungua kwa eneo lililotengwa na Mto Kilombero, eneo la Bonde la Ramsa Kilombero limepungua kutoka kilomita za mraba 7,950 hadi 2,193 sawa na asilimia 72, Serikali mpo mpo tu, tunasema Bwawa la Mwalimu Nyerere tumejenga litakuja kuwa… (Kicheko)

MHE. ENG. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima Mdee, taarifa. (Makofi)


TAARIFA

MHE. ENG. LEONARD M. CHAMURIHO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa mzungumzaji kwamba katika taratibu za ujenzi suala la kuukata uchelewashaji au liquidated na certainty damages huwa lina-total mwishoni mwa mradi. Kwa sababu milipaji ni mmoja tu anaitwa client na mkandarasi huwa halipi, huwa anakatwa kwa hiyo kwa sababu mradi haujaisha hakuna tatizo. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninapotoa rejea ya jicho la Bunge ambalo lipo pale Kikatiba, ambalo linasema kuna bilioni 327 Serikali ilitakiwa iwe imemkata, haijakata mpaka sasa hivi na mkataba utakuwa umeisha tokea mwaka 2022, halafu mtu anasimama kunipoteza muda hapa…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima Mdee, Mheshimiwa Halima Mdee kama haupokei taarifa malizia…

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, sijapokea na siwezi kupokea taarifa ambayo haieleweki. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa malizia kwa sekunde kumi…

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimalizie kwa kusema kwamba tunadhani ni muhimu Serikali ikalieleza Bunge hili Tukufu mikakati dhahiri kama ambavyo Kamati ya Bunge imezungumza hapa mikakati dhahiri na shairi ya kulinda vyanzo vyote vya maji vinavyopeleka maji katika Bwawa la Mwalimu Nyerere. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kwa taarifa ambayo imetoka mwaka jana 2023 hakuna kitu kilichofanyika ndiyo maana tunaambiwa maagizo wa Mawaziri 31 bado hayajafanyiwa kazi. Sasa tunakuwa tuna Mawaziri, wanatoa maagizo, maagizo hayatekelezwi halafu anainuka mtu mwingine…

MWENYEKITI: Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. HALIMA J. MDEE: …huko mtaani anaenda analia chama hicho hicho…

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. HALIMA J. MDEE: Serikali hiyo hiyo, kazi zinakuwa hazifanyiki huku wanashindwa kule wanalia…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. HALIMA J. MDEE: … hatuwezi kuendesha nchi namna hii.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Halima.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunivumilia. (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima, ahsante sana. Nilimtaja Mheshimiwa Charles Kajege, Mheshimiwa Joseph Kamonga na Mheshimiwa Subira Mgalu ajiandae.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeunga mkono hoja ya Kamati. (Makofi/Kicheko)