Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo ili na mimi niweze kutoa mchango wangu mdogo kwenye taarifa hizi zilizowasilishwa asubuhi. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kusimama ndani ya Bunge hili katika siku hii muhimu. Pia niwapongeze Wenyeviti wote wa Kamati zetu hizi mbili kwa wasilisho zuri ndani ya Bunge letu, hususani Mwenyekiti wetu wa Kamati Mheshimiwa Daniel Sillo kwa kazi nzuri anayotuongoza kwenye Kamati yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mimi ni mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Bajeti, naunga mkono taarifa yote iliyowasilishwa hapa na maoni yote. Tumefanya kazi kama ambavyo mmeiona na mnaifanyia rejea. Kwa hiyo nimpongeze sana Mwenyekiti na wajumbe wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia na mimi niongezee kwenye mchango wa Mheshimiwa Halima Mdee, kwenye ukurasa wa 28 kuhusu Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Kwanza, mimi lazima niipongeze Serikali ya Chama Cha Mapinduzi Awamu ya Sita, imefanya kazi kubwa. Wakati anaingia madarakani Mheshimiwa Rais Mama Samia alikuta mradi huu ukiwa kama asilimia 36 na kiasi cha trilioni mbili ndizo zilizokuwa zimelipwa. Kwa wakati wake zaidi ya trilioni 3.53 na maradi umefikia asilimia 95. Tunaozunguka mradi huu na Watanzania tunatoa shukrani za dhati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua mwishoni mwa mwezi huu pengine majaribio ya kuingiza umeme kwenye Gridi ya Taifa yatafanyika hongereni sana Serikali na Mheshimiwa Rais Samia, ametimiza ahadi yake ya kutekeleza kuendeleza miradi ya kimkakati. Kwa hakika amemuenzi Marehemu Dkt. John Pombe Magufuli kazi yake nzuri aliyoanzisha na Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo sasa kitakachosalia ni hii miradi ya jamii (CSR). Kama leo akienda CAG tena atakuta mabadiliko. Kupitia TANESCO Serikali imetuarifu kwamba inatarajia kujenga vyuo kadhaa kwenye mikoa ya Lindi, Kigoma, Dodoma na Tanga, ambapo zaidi ya bilioni 240 zitapelekwa huko. Pia, Halmashauri ya Rufiji na Morogoro Vijijini zimetengewa bilioni 10 kila moja kwa ujenzi wa hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna kupata kidogo tunaiomba Serikali na tunamshukuru Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Biteko ameahidi kufanya kikao cha pamoja na viongozi wote wanaopitiwa na mradi huu ili kuona namna gani taratibu zitafanyika ili sisi ambao tuko downstream tuweze kuongezewa kiwango hiki cha miradi ya jamii. Kiukweli hatujaridhika, lazima niseme ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili pia namsemea Mheshimiwa Mbunge Mohamed Mchengerwa kutoka Rufiji, amekuwa akipambana sana, ni miongoni mwa waasisi wa wazo hili ndani ya Bunge la ujenzi wa mradi huu. Kwa hiyo, naomba sisi kama Wananchi wa Rufiji, Serikali tunawapongeza, tunataka tugawane keki hii ya Taifa wote, lakini kwa hili kupewa asilimia tatu tu na Morogoro Vijijini tunaomba mfanye mapitio ya utaratibu huu muangalie mkataba unavyosema katika maeneo yale ambayo miradi mikubwa inafanyika ili CSR iweze kutenda haki na wengine wapate, lakini sisi ambao tuna wajibu wa kutunza mazingira yale wote kuanzia upstream mpaka downstream tufaidike na hii CSR.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, taarifa yetu imefanya tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya 2022/2023 na hii bajeti inayoendelea, takwimu zimeonesha namna gani Serikali imekuwa ikifanya vizuri kwenye kukusanya mapato, lakini suala si kukusanya mapato, suala ni sehemu ya mapato kupeleka kwenye miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nataka niipongeze Serikali yetu ya Awamu ya Sita kwa namna ambavyo imekuwa ikipeleka pesa za maendeleo. Miradi ni mingi na mimi leo ninaposimama hapa najisikia fahari sana katika mwaka huu wa fedha nimeweza kutembelea miradi 95 kupitia ziara ya Mwenyekiti wa Taifa Mama Mary Chatanda na Makamu wake Mama Zainab Shomari. Miradi niliyopangiwa mimi tu kama Mjumbe ina thamani zaidi ya bilioni 90, lakini miradi ambayo nilihusiana na viongozi wetu ya kimkakati ina thamani zaidi ya bilioni 444, lakini kiujumla UWT Taifa ambao tuliamua kwa dhati kabisa kwamba, tuende Kata kwa Kata tuitembelee hii miradi, tuone kazi nzuri ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, tumetembelea miradi zaidi ya trilioni mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa sababu kuona ni kuamini. Mimi binafsi nimeona na Kamati ya Utekelezaji tumeona, hakuna Kijiji nchi hii ambacho hakina mradi. Licha ya kuona tumepokea salamu za shukrani kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wasaidizi wake, hongereni, wananchi wamefurahi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mafanikio yasiyokuwa na changamoto, licha ya miradi tuliyoiona, ipo miradi ambayo Wakandarasi wamefanya kazi bado wanadai. Hapa nijielekeze kwenye miradi ya maji, naiomba sana Serikali kwenye Mfuko wa Taifa wa Maji, Mheshimiwa Waziri Mwigulu umefanya kazi nzuri, lakini bado una dhamana ya kuendelea kuunga mkono kutuliwa ndoo kichwani kinamama. Miradi iliyoanzishwa ambayo mingine imekwama, nautolea mfano mradi wa Kijiji cha Ibiwa - Bahi, Mkandarasi amepewa mradi wa kujenga milioni 700, ameanza mwenyewe, mpaka ninaposimama hapa tangu apeleke certificate mwezi wa saba mwaka jana ya kwanza milioni 186 hajalipwa. Sasa niiombe Serikali katika mazingira ya namna hii, Wakandarasi wanataka kuuziwa mali zao, basi kaeni na benki muweze kuwapa assurance kwamba, hawa tunawatambua, hawa tumewapa kazi, lakini malipo yao tutawalipa kwa sababu, tunatambua kazi inayoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hiyo kazi nzuri nafurahi, Kamati tumesema kwa mara ya kwanza Serikali hii ndiyo imenunua mitambo ya kuchimba visima. Na Kwa kuwa, bado vijiji vingine havina maji tunakuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa ushirikiano na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Waziri wa Maji muone namna gani mtaweza kuweka kanuni zile Halmashauri zetu ziweze kutenga fedha au kutoa ruzuku ili mitambo hii ilete tija vinginevyo itapata kutu, itaharibika na tija ambayo haitafanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kupitia Bunge hili napenda niseme wazi sisi kama Kamati tunaona Serikali yetu ni Sikivu. Tuliishauri irejeshe Tume ya Mipango imerejesha. Tuliishauri ifanye mapitio ya Sheria ya Manunuzi tumeipitisha Bungeni. Tuliishauri Sheria ya Ubia Binafsi na Serikali (PPP) imefanya. Hivi karibuni kwa kuona namna gani Sheria ya Manunuzi ile asilimia 30 tunayotenga kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo, wafanyabiashara wa kati na makundi maalum kwa mara ya kwanza Serikali imeandaa mpango wa kuwahusisha makundi yale na kuona kwamba, jambo hili linatekelezeka tofauti na kipindi cha nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. Lazima tumpongeze na tunapompongeza maana yake tunaona kazi inayoendelea. Pamoja na changamoto hizo, lakini nikushauri Mheshimiwa Waziri bajeti inayokuja nikuombe kama haya madeni hebu yaangalie, pengine tupange mipango michache, miradi michache ili miradi ambayo bado inatekelezwa iweze kumalizwa kisha tuanze mipya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze TRA kwa makusanyo mazuri, Mwezi Disemba wamevunja kiwango tena trilioni tatu tangu mamlaka hii ianzishwe mwaka 96, lakini niendelee kuwaomba Watanzania tulipe kodi kwa hiyari, tudai risiti, tutoe risiti, lakini mifumo inayoendelea kuboreshwa TRA iwe makini ili isiwabughudhi wafanyabiashara mara mtandao uko chini, mara nini, kwa hiyo tuone kwamba tunahitaji fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya kwa sababu, mengi yapo kwenye Kamati yetu, napenda kukushukuru, napenda kukupongeza Mheshimiwa Waziri Mwigulu, Wizara ya Fedha na Mipango yote kwa kazi nzuri unayoifanya, miradi ya kimkakati inaendelea vizuri. Ahsante sana. (Makofi)