Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kahama Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye Kamati hizi mbili. Bahati nzuri na Mheshimiwa Waziri wa Fedha yupo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala gumu linatusumbua sana sasa hivi Kanda ya Ziwa, hasa kwenye maeneo yetu ya machimbo ya dhahabu. Wachina wanaendelea kununua migodi midogo-midogo kwa wananchi, mimi hilo sina tatizo nalo, lakini suala hili ni jipya na wote ndiyo tumeliona na limeibuka sana wakati wa ziara ya Mheshimiwa Mwenezi wetu wa CCM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mchina anaununua ule mgodi wa wachimbaji wadogo, mgodi ule ulikuwa umeajiri watu zaidi ya elfu kumi mpaka elfu ishirini, lakini ulikuwa unazalisha kilo 20 za dhahabu kwa mwezi na Serikali inapata kodi na Halmashauri tunapata, lakini Serikali inapata kwenye mauzo ya bidhaa nyingine kama soda, pombe na vitu vingine anapata kodi na miji yetu inachangamka. Mchina akinunua ule mgodi kwenye mkataba wake hakuna panaposema anatakiwa azalishe kiasi gani cha dhahabu. Je, kama ataamua kutozalisha nini kitatokea kwenye ile Miji yote ya Geita, Kahama na Singida kwako Mheshimiwa Waziri wa Fedha, nini kitatokea? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala ni jipya na mara nyingi suala likija jipya na kwenye vitabu halipo na machimbo madogo-madogo yalikuwa haramu, wote mnafahamu, sasa hivi ndiyo tumesema yamekuwa halali. Sasa tutafanyaje? Kweli ni mwekezaji! Je, nini kitatokea? Ina maana ile Miji yote ya Kahama, Shinyanga, Geita, Singida, Miji yote itakufa automatically! kwa sababu hili suala linaendelea kwenye dhahabu, lakini linaendelea na kwenye samaki pia. Wachina wamefunga vizimba, wanavua sato kwenye vizimba wanauza kwenye soko la local. Wakiuza kwenye soko la local hawa wananchi wanaenda kuvua ziwani ambayo ni ajira yao ya kila siku, itatokea nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najaribu kuliweka kwenye alert kwa sababu sisi tunaotoka maeneo hayo tunafahamu madhara yake. Hakuna mahali ambapo yeye analazimishwa kwamba, kama mgodi huu ulikuwa unazalisha kilo 20 na wewe unaununua kutokea leo, ndani ya siku fulani na wewe uzalishe zaidi ya kilo 20 ili sisi Halmashauri ianze kupata pesa na Serikali wewe upate hela, vinginevyo hata wewe Serikali hutapata hela kwenye dhahabu tena kwa sababu dhahabu yote atakuwa amei-hold chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niliseme, sikatai uwekezaji lakini kwa kuwa ni suala jipya, Kamati ya Fedha ipo, Kamati ya Bajeti, kaeni tuliangalie upya kwa sababu ni suala jipya kabisa duniani. Kwa hiyo, nimeona niliseme kwenye Kamati na Waziri wa Fedha kwa kuwa yupo linaweza likatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado mimi napingana sana na wataalam, wataalam wasipokubali kubali kubadilika tuko kwenye shida ngumu sana. Wabunge wote humu ndani tunalia habari ya Barabara, Mimi kwangu Kahama nimepata kilometa 21 za Benki ya Dunia, lakini sheria yetu ni ya zamani, unahitaji barabara ya mita sita mpaka mita nane, barabara inayoingia ndani ya Mji kwa mle ndani unahitaji Barabara ya mita nane au mita sita? Kwa nini isiwe barabara ya mita tatu? Badala ya kilometa 21 nikapata kilometa 50? Tukawa na one-way na one-way, hii unaingilia huku, unaingilia huku?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, hata Uswiss ambayo ndiyo tajiri na hela zetu zote tunakopa huko Mheshimiwa Mwigulu, si njia zote zina one way, magari hayapishani, unaingilia huku. Miji yetu ya hii ya Geita, Kahama, ni lini itakuja ipate msongamano wa magari kwenye maeneo ya majumbani? Tuwekewe barabara za mita tatu ili tupate barabara nyingi zaidi. Najaribu tu kuona kwa sababu, tusipotumia akili muda huu tutaendelea kumsakama Mheshimiwa Rais, lakini Mheshimiwa Rais anatukataza sisi kufikiri kweli? Yaani tunakatazwa kufikiri? Kwamba, hatuwezi kufikiri tofauti, lazima tulalamike tu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo suala la shule wote hapa ni mashahidi, wote tunaendelea kujenga shule, sasa hebu tuulizane wote, kama kila siku tutajenga shule hivyo viwanja tutavipata wapi? Au nchi nzima itaenea shule? Kwa nini tusiruhusu kwamba, watoto wasome, Jumatatu wasome watoto group hili, wengine waende Jumanne, hawa wengine waende Jumatano, litakuwa kosa? Hata kama tutakataa, sikatai, hakuna neno, lakini viwanja tunavyo? Lakini ile Jumamosi na Jumapili si watoto huwa wanakaa nyumbani, akili huwa inafyatuka wakienda Jumatatu? Walipoteza masomo? Tutaweza kujenga shule kila siku? Miaka 64 ya uhuru tunajenga shule? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wazee kule vijijini ukifika wanakwambia aah, sisi mambo ya shule tumechoka, huwa hamna hadithi nyingine mpya? Ni ujenzi wa shule kutwa nzima! Kwa nini watu wasisome Jumatatu wakasoma wengine, Jumanne wakasoma hawa wengine, hawa wakaenda tena Jumatano, litakuwa kosa gani?
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa inatoka wapi? Haya Mheshimiwa Ng’enda.
TAARIFA
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa taarifa Mzungumzaji, Mzee wetu makini sana ambae ni think tank ya Taifa, kwamba hoja anayoizungumza ni hoja ambayo inawezekana katika fikra mpya. Kwamba, hata kutumia miundombinu ya shule moja kufanyika kama shule mbili au tatu inawezekana. Wanafunzi hawa wanaingia asubuhi wanatoka mchana, wengine wanaingia saa nane wanatoka saa kumi na mbili jioni. Vyoo vilevile, madarasa yaleyale, lakini wanaobadilishana ni wanafunzi, kuliko kuendelea kujenga shule na kujenga shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakubaliana ni kweli mwisho Miji yote itatapakaa shule tupu. Ahsante sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kishimba unaipokea hiyo taarifa ya Mheshimiwa Kilumbe?
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea kwa mikono sita. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tukubali kufikiri. Kama tutakataa kufikiri tutakuwa watumwa wa dunia na itakuwa ngumu mno kuishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kama tunakataa, tulipata ugonjwa wa Corona hapa, tulifunga kwa mwaka mmoja shule. Je, mlipata matatizo yoyote baada ya watoto kurudi? Walifeli? Kama walifeli mtuambie, kama hawakufeli tuendeni na utaratibu huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wa kiislamu wanasoma saa mbili au saa moja tu Kiarabu au Quran lakini wanakariri Quran tunawaona kwenye mashindano, atashindwaje mtu kuelewa kusoma? Utaratibu huu tunaotumia ni utaratibu wa Ulaya kwa ajili ya kuwekesha, ilikuwa ni sehemu ya kuwekesha watoto ndiyo maana wanawekeshwa Jumatatu mpaka Ijumaa, Bwana na Bibi wako kazini. Sasa sisi tumefuata utaratibu huo tutafilisika na tutakuwa tu watumwa. Kila ukifika kazi yako wewe ni kujenga shule, miaka kumi ya utawala wote tunajenga shule tu. Wanaoweza kusoma usiku wasome, tatizo ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna sababu yoyote ya kuanza kuchelewa kufikiri. Juzi hapa, kama sikosei, kwenye shule ya Chuo cha Kariuki cha Udaktari (Kariuki University), amefaulu msichana ambaye alimaliza udaktari, amesoma form one mpaka form four kwa miezi sita na wote tumemuona na amekwenda form five na six mwaka mmoja na ame-graduate Udaktari miana minne. Je, haliwezi kuwa wazo? Yaani hatuwezi ku-copy kwenye suala kama hilo tukaanza kwenda mbele ili kuendelea ku-save huo muda?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niliseme hili kwa sababu najua ni kero kweli. Sisi hiyo Miji yetu sasa imeisha, Miji yetu mingi ilijengwa katikati kwenye center, sasa hakuna pa kujenga shule, miji inaongezeka, tutafanyaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niliongee hili kwa sababu na Mheshimiwa Waziri wa Fedha yupo na wote tunamsakama Waziri wa Fedha. Sasa Waziri wa Fedha lazima uweke watu wa kufikiri kwenye ofisi yako ili kupunguza hizi pressure ambazo saa nyingine hazina sababu nyingine ya muhimu ambazo wewe unaweza kuzi-regulate na suala likaenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huo, nakushukuru sana. Ahsante sana. (Makofi)