Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Haji Amour Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makunduchi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuweza kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia miswada ambayo imewasilishwa hivi leo asubuhi, tulikuwa na Muswada wa Bajeti pamoja na Uwekezaji wa Mitaji ya Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabla ya yote hayo napongeza pia naunga mkono miswada yote miwili hiyo ambayo imewasilishwa leo hivi asubuhi, lakini pia kabla ya yote napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa maono yake na katika kuhakikisha kuwa mashirika yetu ya umma yanaleta tija na kuwa na ufanisi mzuri katika ufanisi wa mashirika hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo lipo na napenda kulizungumza kwamba mimi ni mmoja wa Wanakamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma na lengo langu kubwa hasa ni kuweza kuzungumzia masuala yanayohusu suala la Msajili wa Hazina. Msajili wa Hazina, mimi kwa kweli nitasema kwamba katika mtu ambaye nimeanza kujifunza baada ya kuingia katika Bunge nilikuwa naona kwamba kuna jina linaitwa Msajili wa Hazina na nikawa najaribu kuangalia kwamba Msajili wa Hazina ni kitu gani, nikawa ninasema kwamba suala la Usajili wa Hazina labda pengine nilikuwa nasema kwamba huyu ni msajili wa mali zote na ukweli hasa nikaja nikakuta kwamba yeye ni msajili wa mali zote za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kikubwa ambacho nilichokuwa najaribu kukiangalia, nilikuwa najaribu kuangalia majukumu makubwa ambayo ni ya Msajili wa Hazina ni yapi. Nikaja kikakuta kwamba Msajili wa Hazina ana majukumu mawili makubwa ambayo amepewa, jukumu la kwanza ni kupitia ama kuhakikisha na kufanyika mapitio ya kudumu ya shughuli na mwenendo wa kila mtu na taasisi ambazo Msajili wa Hazina anamiliki mali na anamasilahi katika mali kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu la pili bila kuathiri madhumuni ya jumla ya kifungu kidogo cha kwanza na katika kufafanua zaidi kifungu hicho, Msajili wa Hazina anatakiwa kuna mambo pale ambayo yametajwa karibu mambo 13. Bahati nzuri katika kujifunza kwangu nikawa najaribu kuangali huyu Msajili wa Hazina anafanya kazi kwa niaba ya nani? Nikaja nikapitia kwamba Msajili wa Hazina anafanya kazi kwa niaba ya Rais, maana yake yeye anafanya kazi kwa ajili ya kuzihifadhi au kuhifadhi masuala ya uwekezaji wa mashirika ya umma pamoja na mali zote zilizopo katika Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nimeweza kujifunza pale katika hali ya kuangalia namna ya utendaji kazi wa Msajili wa Hazina na kama Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, sisi mtu tunayefanya naye kazi ni Msajili wa Hazina. Kwa kweli nimeweza kujifunza mambo mengi sana pale na nikaja nikakuta kwamba katika mambo ambayo au katika majukumu ambayo anayoyasimamia Msajili wa Hazina ni kusimamia yale mashirika hasa katika masuala ya menejimenti zao katika uundwaji wa zile bodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kitu ambacho nilichokuwa nimekiona katika zile bodi maana yake kwamba inawezekana pengine kuna mashirika, kulikuwa kuna mapungufu makubwa zinawezekana pengine katika shirika moja linaweza likachukua miaka mitatu maana yake hakuna bodi. Sasa hii kwa kweli imekuja kupunguzia yale mashikira yetu ya umma na uwekezaji maana yake ule ufanisi ukawa hauwezi kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho ninachokizungumza kwamba usajili wa hazina kwa namna ambavyo ilivyopitishwa huko nyuma na utendaji wake na namna ambavyo ilivyokuwa inafanya kazi kule nyuma ilikuwa inafanya kazi kupitia Wizara ya Fedha, lakini Msajili wa Hazina anafanya kazi kwa niaba ya Rais, kuhifadhi zile mali au rasilimali zote za mashirika ya umma pamoja na uwekezaji wa umma. Sasa bahati nzuri imetokea bahati kwamba sasa hivi uwekezaji wa mitaji ya umma haukupitia Msajili huyu maana yake kapelekwa chini ya Ofisi ya Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo jema tunalolishukuru, lakini kitu ambacho kilichopo hii ni taasisi ambayo ni kubwa na kwa kweli kuna mambo ambayo inabidi tuweze kuyazingatia nakumbuka Mheshimiwa Rais, kuna siku alikaa pale akasema kwamba kuna haja ya kwamba mashirika ya umma maana yake kuweza kufanya reforming, kwa sababu kuna baadhi ya taasisi ambazo za mashirika ya umma maana yake yanaonekana kwamba hayana tija na kila mashirika ambayo hayana tija au hayana ufanisi ni vyema zaidi maana yake tukaweza kuyaondoa au tukafanya namna ya kuweza kuyaunganisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa bahati nzuri au nitasema bahati nzuri kupitia Waziri wa Uwekezaji ambaye ni mpya Mheshimiwa Kitila Mkumbo, ameleta muswada wa sheria kupitia katika Kamati yetu kuweza kuujadili. Muswada ule nitasema kwamba kama ni Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, kwa kiasi fulani maana yake sisi tumeupitia na tumejaribu kuuangalia isipokuwa tunasema kwamba ule muswada maana yake umekwama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali au sisemi kwamba umekwama, lakini nitasema kwa ule muswada kwa awamu hii maana yake haujapitishwa, lakini ni vyema maana yake kuishauri Serikali kwamba ule muswada ili kuwe na ufanisi wa mashirika ya umma maana yake ule muswada ningependa Serikali ulete Bungeni kuja kuujadili na kwa nini? Kwa sababu ule muswada unamuundo na unaweza ukaleta ufanisi katika mashirika yetu ya umma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashirika yetu ya umma sasa hivi utakuta kwamba Msajili wa Hazina anachokifanya yeye maana yake ni kitu ambacho ni kidogo ni namna ya ufuatiliaji wa yale mashirika, lakini kuna mambo maana yake yanakuwa yanamkwaza. Endapo kama utakuja ule muswada ni vyema tukajaribu kuupitia upya na tukajaribu pengine kuuangalia na vilevile, kama kuna uwezekano hata yule Msajili wa Hazina maana yake kama kuna uwezekano tukawa na chombo cha uwekezaji wa Taifa. Sasa tunapokuwa na chombo cha uwekezaji wa Taifa na mashirika yote maana yake yakawemo ndani ya kile chombo nadhani kwamba ufanisi pamoja na tija ya mashirika ya umma maana yake yanaweza yakawepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwa leo hii maana yake nijikite kwa upande huo lakini, la pili na la mwisho, nasema kwamba nije katika yale mashirika ambayo tunaita mashirika ambayo yenye kampuni tanzu. Kampuni tanzu kwa kweli ni kampuni ambazo zinazoongozwa na kampuni mama na kuwa na hisa zisizopungua asilimia 51. Kuna baadhi ya kampuni tanzu ambazo tumezibaini katika Kamati yetu, hizo kampuni tanzu ambazo zilizopo pale maana yake tunaziona kama ni mzigo au pengine kama ni kichaka kwa baadhi ya mashirika ya umma. Kwa mfano kuna shirika, kuna kampuni tanzu ambayo ipo katika Taasisi ya TANESCO, kampuni tanzu hii inatengeneza nguzo za umeme. Mwezangu kazungumza pale Mheshimiwa Kajege, lakini ukweli ukiangalia katika uhalisia kampuni hiyo imekuwa kama kichaka, wakati huo huo katika Taasisi ya TANESCO pia wana kampuni tanzu ambayo inashughulikia na masuala ya utengenezaji au pengine kusambaza miundombinu ya umeme, kampuni ile nayo utakuta kwamba wafanyakazi wa TANESCO ndiyo ambao wanatumika kwenye ile kampuni tanzu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kiuhalisia juu ya kampuni tanzu zile, ukitazama hasa kikanuni maana yake ule muundo wa zile kampuni tanzu maana yake hazifuati utaratibu, maana yake hata zile katiba zao maana yake huwezi ukazikuta miundo yao ya zile kampuni tanzu ukitizama hasa kiundani huwezi kuzitazama. Mimi naiomba Serikali pengine kupitia kwa Msajili wa Hazina haya mashirika yote ambayo yanaunda kampuni tanzu ni vyema maana yake Msajili wa Hazina naye akawa na percentage ili kuweza kuzisimamia vizuri kwa zile kampuni tanzu pamoja na kwamba kule kunakuwa na asilimia 51, lakini ni vyema pengine Msajili wa Hazina na yeye akawepo na share ya kuweza kuwa na ule usimamizi wa zile kampuni tanzu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nampongeza Mwenyekiti wangu kwa namna ya uwasilishaji wake wa Taarifa ya Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, pia nampongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti kwa kuweza kuwasilisha wasilisho lake. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, nasema kwamba naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)