Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hoja hizi mbili za Kamati ambazo zimewasilishwa vizuri sana na Wenyeviti wawili wa Kamati hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hoja hizi ni za Kamati zimegawanyika katika maeneo ambayo yanahitaji utekelezaji wa sasa hivi lakini mengine ni ushauri ambao unaendana na maelekezo ya Bunge ambayo mengine tutayatekeleza tunavyoandaa bajeti hizi mpya za mwaka wa fedha huu unaokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzipongeza Kamati niwapongeze pia Wabunge wote ambao wametoa michango yao na niwahakikishie kwa niaba ya Serikali tumepokea yale ambayo yanahitaji kwenda kufanyiwa kazi na yale ambayo yanahitaji ufafanuzi wa haraka nitaomba nifanye hivyo katika mchango wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zimetolewa hoja nyingi ambazo zinalenga zaidi kwenye masuala ya mtiririko wa fedha. Niwashukuru kwa wale ambao wamepongeza jitihada za Serikali ambazo zimefanyika katika miradi mbalimbali. Hoja kubwa ambayo imejitokeza na ilijitokeza hata jana na bahati mbaya sana sikuwepo nilikuwa sehemu ya Kamati ya maandalizi ya msiba ya mpedwa wetu Waziri Mkuu Mstaafu, lakini jambo hili la fedha za TARURA zipo namna hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja zile fedha za dharura ambazo tulitoa kauli hapa Bungeni tayari tulishatoa. Tulishatoa na utekelezaji wake unaendelea kwenye Wizara za Kisekta, kwenye Mikoa pamoja na kwenye Wilaya ambapo mahitaji yalikuwa bilioni 30. Mbali na hapo kulikuwa na nyongeza ya shilingi bilioni 350 ambayo tuliisema kwenye bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Wabunge tuelewane kwenye hili. Utaratibu wa fedha ya nyongeza tuliyoitamka kwenye bajeti ni wa P4R na tulisema hivyo hivyo wakati wa bajeti. Fedha ya P4R haitoki yote mara moja na ikagawanywa, inatoka kadri unavyotekeleza na sisi pamoja na wenzetu wa Wizara ya TAMISEMI tumeshaliongea hili na tulishakubaliana na tulishatoa ridhaa na nadhani mawasiliano hayo Waheshimiwa Wabunge mtakapoenda Mikoani mtayakuta. Kila mtu sambamba na mgao wake aliokuwa anastahili. Miradi itatangazwa, utekelezaji utaendelea na kadri wanavyotekeleza wataendelea kupata fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la TARURA ni moja ya kipaumbele namba moja na ni moja ya kipaumbele cha juu kwa Mheshimiwa Rais kwa sababu barababra hizo zinawagusa Wananchi wa Tanzania wa Vijijini. Vinawahusu wakina mama wajawazito, watoto wanaokwenda shuleni, vijana wanaofanya biashara, wakulima wanaobeba mazao yao kutoka mashambani kupeleka sehemu ambayo wanahitaji kuyafikisha, pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi. Ni barabara zinazofungua nchi, ni barabara zinazowaunganisha wananchi kutoka eneo moja kwenda eneo lingine, ndio maana bajeti yake iliongezeka katika kipindi hiki cha miaka mitatu, imeongezeka kwa takribani mara saba kutoka bilioni takribani 200 imekwenda takribani trilioni moja na bilioni mia tatu na hamsini kwenda mia nne. Kwa hiyo hili ni jambo ambalo ni la kipaumbele kwa Serikali na kila wakati Mheshimiwa Rais analisisitiza na sisi Wizara ya Fedha tunalizingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kimoja tu ambacho kilikuwa kinaleta tofauti ni pale ambapo utaratibu wetu wa utekelezaji wa miradi, unaenda kwanza unafanya manunuzi, ukishamaliza manunuzi tunaanza kutekeleza kwa certificate na kwa ile ya P4R inatekelezwa kufuatana na jinsi miradi inavyotekelezwa ile ambayo imetangazwa. Kwa hiyo, hilo ndilo linaloendelea na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, hata jana tu nilikuwa ni Mheshimiwa Waziri tumeongea hili, na Mheshimiwa Naibu Wazri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Ndejembi alilielezea vizuri. Hii ni fedha ambayo tuliisema ndani ya Bunge na ndani Serikali tumekubaliana kwamba utekelezaji wa miradi hiyo itasainiwa na kazi itaendelea na tutaenda kutekeleza kama ambavyo tulisema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo lilikuwa linajitokeza lilikuwa ni suala la tax refunds. Kule tulikotoka kuna wakati kulitokea matatizo kwenye madai ya refund (madai ya marejesho ya kodi). Ulitokea utaratibu ambao haukuwa mzuri kwa baadhi ya wale wasiokuwa waungwana. Yalikuwepo makampuni yaliyokuwa hayafanyi biashara ya kuuza bidhaa, yalichokuwa yanafanya, yalikuwa yanazalisha risiti wanaenda kudai fedha. Kwa hiyo, tulikuwa tunakusanya makusanyo, unayaona ni makubwa lakini ndani yake kunakuwa na baadhi ya makampuni wanapeleka risiti. Ukiziangalia unaona kama ni halali vile lakini kumbe zimetengenezwa bila bidhaa. Jambo hili lilisababisha tupeleke utaratibu mkali wa kukagua zile risiti, kukagua kila ki-item. Jambo hili lilisababisha mrundikano wa mahitaji yale ya marejesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tulivyoona mrundikano ule unakuwa mkubwa katika siku za hivi karibuni ambapo tumeboresha mifumo, tumeanza utaratibu wa kukagua miamala ambayo ni shuku, yaani baadhi ya makampuni ambayo hayaaminiki tunayafanyia ukaguzi wa kipengele kwa kipengele na yale mengine tunayakagua kwa sampling. Kwa hiyo, tumeshapunguza kwa kiwango kikubwa sana haya masuala ya refunding na mamlaka ya mapato inafanya vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea jambo la MSD, tunaendelea kuongea na wenzetu wa Wizara ya Kisekta na kuna mpango ambao tunaufanya nadhani tutakapokuja kwenye kipindi cha bajeti tutakuwa tumeelezea fedha ambazo tutakuwa tumeshazipata. Kwenye yale ambayo yalitolewa kwenye upande wa maazimio, ilikuwepo ile habari ya marekebisho ya takwimu, kanuni ili tuweze kuwa tunakaa na Kamati kabla ya kwenda kuandaa zile kodi ambazo ni za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hatuna pingamizi na Kamati tunakubaliana nalo. Kwa hiyo hilo ni jambo la Kibunge na sisi tunakubaliana nalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miradi ya maji na sisi tunakubaliana na Bunge. Wizara ya Fedha pamoja na Wizara ya Maji Serikalini hicho ndicho ambacho tunatekeleza. Kwanza ilikuwa tupate mitambo, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais mitambo imepatikana. Tunapoandaa bajeti huku tunapokwenda tutaandaa bajeti ambazo zitawezesha halmashauri zetu kuweza kuchimba visima. Visima si bei kubwa sana, ziwe na mafungu ambayo yatawezesha kuchimba mabwawa na hili ni jambo ambalo kwa huku tukikopita ambako hatukuwa na mitambo hakukuwepo na utaratibu wa aina hiyo, lakini tunapokwenda ni jambo ambalo litaenda kufanyika kwa namna hiyo. Wizara inafanya vizuri sana kuratibu jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye upande wa Kamati ya PIC wameelezea na limejitokeza kwa kiwango kikubwa jambo la Muswada ambao unaongelea mamlaka ya uwekezaji. Muswada huo haujapotea upo. Waheshimiwa Wabunge, Serikali imekuwa na nia njema kwenye jambo hili na kwa kuwa Serikali ndiyo imeleta na ndiyo iliyokuwa inapika jambo hili imeona ikamilishe ililete likiwa limeiva zaidi. Kwa hiyo, mimi sidhani kama ni tatizo. Tunamalizia consultation ndani ya Serikali, tutakuja ndani ya Kamati na baadaye tutakuja ndani ya Bunge. Hili ni jambo ambalo Serikali ina nia njema na inataka itengeneze kitu ambacho kitakuwa na manufaa mapana kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yale mengine ambayo yalihitaji ufafanuzi wa masuala ya kampuni tanzu na zile nyingine nadhani ni mambo ambayo yatatolewa ufafanuzi. Yalitolewa yale ya usimamizi, hatuna pingamizi na Kamati na sisi tutaendelea kuyafanyia kazi kwa ukaribu zaidi ili kuweza kuhakikisha kwamba yanasimamiwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la TIB mmesikia tutakaa ndani ya Serikali ili tuweze kupata majibu yaliyo halisi. Tutakaa na wenzetu wa TIB na wenzetu wa ofisi ya TR ili tuweze kupata majibu. Tumepokea pia masuala ya ushauri ambayo yametolewa kuhusu kuangalia upya barababra zinazopita mijini pamoja na mambo mengine yote ambayo Waheshimiwa Wabunge waliyasema tumeyapokea. Pia na yale ambayo Waheshimiwa Wabunge mmeyaongelea yanayohusu kutoa fedha, ameongea ndugu yangu Mbunge wa Mbulu Mheshimiwa Flatei na pacha wake Mheshimiwa Issa walinikuta hapa kwenye kiti. Tangu asubuhi nilikuwa napokea Mbunge mmoja mmoja hata wale ambao hawajaongea, wameleta hoja zinahusiana na mtiririko wa fedha. Waheshimiwa Wabunge tumeyapokea, tulikubaliana hata siku ya briefing, mtakaporudi Majimboni tutakuwa tumeachilia hizo fedha ambazo zilikuwa bado hazijaenda kwa ajili ya kutekeleza miradi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge ni vile tu kwenye nchi yetu kila jambo ni kipaumbele, tuna mambo mengi na yote yana umuhimu. Kwa hiyo hata fedha ndivyo hivyo tunavyozigawa. Yanatokea masuala ya Bwawa la Mwalimu Nyerere, masuala ya reli, masuala ya elimu ya juu. Elimu ya Juu bajeti yake ni kubwa sana na ni kwa ajili ya watoto wetu. Ukienda elimu bila ada ni jambo la msingi sana, ukienda kwenye afya ni jambo la msingi sana. Ukienda kwenye hizi barabara zote ukiweka mpaka hizi dharura zinazojitokeza yote ni mambo ya msingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokifanya tunagawanya keki ile inayopatikana, tunatengeneza mtiririko kufuatana na mahitaji haya yanayojitokeza lakini pia na ukubwa wa keki yenyewe ambayo inakuwa ipo katika wakati huo. Kwa maana hiyo hoja zenu zote tumezipokea na sisi ndani ya Wizara tutaongeza spidi hiyo ya kuweza kuhakikisha hakuna mradi unaosimama kama ambavyo Mheshimiwa Rais amekuwa akielekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi wenyewe ni mashahidi mnaona kwamba nchi yetu ni construction site, kila eneo kuna shughuli mojawapo ya maendeleo inafanyika, kama si kituo cha afya itakuwa shule, barabara au itakuwa shughuli nyingine za umwagiliaji ama nyingine ambazo ni za umuhimu na zinalingana umuhimu. Tumepokea yale mengine yote yanayohusiana na mazingira bora ya biashara, uwekezaji, kuongeza mtaji TIB na wiki ijayo tu tunaendelea na utaratibu ule tulioahidi kwa ajili ya TIB na TADB zote hizo tunaenda nazo sambamba, tulikuwa tunafanya baadhi ya tathmini na tunaamini tutazikamilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata yale ya kuangalia baadhi ya mashirika ambayo hayafanyi kazi, Mheshimiwa Rais alishaelekeza na hatua mnaziona. Kwa ukubwa na wingi wa mashirika tuliyokuwa nayo huwezi ukaya-merge ndani ya siku moja, ukifanya hivyo unaweza pia ukafanya kwa makosa ikaleta hasara. Kwa hiyo kazi hii ni endelevu, inaendelea na inafanyika kwa umakini ili iweze kuleta tija. Naamini kwa ripoti hizi ambazo mmeendelea kuzipata, TR ameendelea kuzitoa, Waziri wa Uwekezaji Kaka yangu Profesa Kitila ameendelea kuzitoa ninaamini Bunge litaendelea kuona utekelezaji wa haya maelekezo ambayo mnayatoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili ya muda naunga mkono hoja na ninawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango mizuri waliyoitoa. Ahsante sana. (Makofi)