Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Daniel Baran Sillo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Babati Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. DANIEL B. SILLO – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA BAJETI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa fursa nami niweze kuhitimisha hoja ya Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa taarifa ambayo iliwasilishwa leo asubuhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kupata nafasi ya kuchangia hoja na wote wameunga mkono. Tunawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge, ahsanteni sana. Pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Fedha ambaye pia umechangia kwa sehemu yako, tunakupongeza na kukushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitapita kwenye maeneo machache. Jambo la kwanza limezungumzwa na Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna haja ya kufanya tathmini ya watumishi wa umma (human resource audit). Jambo hili ni muhimu sana kwa sababu unapofanya tathmini ya watumishi wa umma, utatambua wangapi wanafanya kazi vizuri na wapi pana madhaifu. Hii itasaidia kujipanga upya ili kutekeleza kazi kwa ufanisi mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatenga fedha nyingi sana za miradi mbalimbali hapa nchini na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amekuwa akifanya ukaguzi na anakutana na madhaifu mbalimbali, kumbe pengine tungekuwa na wafanyakazi ambao wako mahiri, pengine kusingekuwa na changamoto kubwa ya aina hii. Kwa hiyo, tunaomba sana wanaosimamia fedha za umma pia wakaguliwe ili tuwe na ufanisi katika utendaji kazi wa Serikali. Naomba Serikali ifanye jambo hili haraka iwezekanavyo ili kuokoa fedha za umma zinazopotea katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nimezungumza sana habari za mikopo kwa sekta binafsi pamoja na mikopo kwa watumishi wa umma. Mfumko wa bei kwa wastani ni kati ya asilimia tatu hadi nne. Sasa kitaalam inatarajiwa basi hata riba ya benki isizidi mara mbili au ikizidi, hata mara tatu ya mfumko wa bei, lakini leo hii, kwa mwezi Julai hadi Desemba, wastani wa riba ni asilimia 13.34, wakati mfumko wa bei ni asilimia tatu hadi nne. Kwa hiyo, kuna haja kubwa sana kwa Wizara ya Fedha kwa kupitia Benki Kuu ya Tanzania kuhakikisha wanapata namna ya kuona kwamba viwango hivi vya riba vinapungua ili kuwanufaisha Watanzania, kuongeza wawekezaji na kukuza Pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 tunatarajia ukuaji wa pato la Taifa kwa asilimia 5.2 lakini, mchango wa sekta binafsi ni wa muhimu sana katika ukuaji wa uchumu na ndiyo engine ya uendeshaji wa uchumi. Kwa hiyo, tunaiomba sana Wizara ya Fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania kuangalia namna ya kufanya kwa viwango vya riba ili kuwahamasisha Watanzania wengi sana wawekeze na hatimaye kukuza pato la Taifa na uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mikopo ya watumishi wa umma. Sote ni mashahidi kwamba mikopo kwa watumishi wa umma haina gharama ya ukusanyaji, kwa sababu mishahara inakatwa moja kwa moja na Utumishi na kurejeshwa kwenye benki husika. Kwa hiyo, naomba sana Wizara ya Fedha iangalie jambo hili, watumishi wa umma wanaumia sana na ndio wanaobeba benki na Waheshimiwa Wabunge wamechangia suala hili kwa hisia kali sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna haja ya kuhakikisha kwamba mikopo kwa maana ya riba kwa watumishi wa umma iwe katika single digit (tarakimu moja). Asilimia moja mpaka tisa pale. Kwa sababu watu hawa ni watu ambao benki nyingi sana zinakopa hii consumption loans, ndiyo inaenda kwa watumishi wa umma, lakini riba ni kubwa sana, kwa hiyo, wanaumia sana. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara ya Fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania kuangalia namna bora ya kuhakikisha kwamba mikopo inakuwa kwa riba ya single digit. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni mkopo wa fedha za GCF ambapo Serikali imepata mkopo wa shilingi trilioni 2.4 ambao unakuja kwa miezi 40. Tunaipongeza sana. Tumesema kwenye taarifa ya Kamati, tunaomba sana Wizara ya Maliasili na Utalii pia ipatiwe sehemu ya fedha hizo za mkopo kwa sababu ni chanzo cha fedha za kigeni, kwa maana Sekta ya Utalii ukishaiboresha basi ni moja ya nyenzo ambayo inachangia sana kupatikana kwa fedha za kigeni kwa haraka. Kwa hiyo, tunaiomba sana Wizara ya Fedha na Wizara ya Maliasili na Utalii waandae utaratibu wa kuomba fedha hizi nanyi mpate mgao ili muweze kwenda kubotesha utalii hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na michango hiyo mizuri ya Waheshimiwa Wabunge, yako maeneo machache pia ambayo ningependa pia kuyasisitiza. Moja ni kubana matumizi ya Serikali. Ili kuongeza mapato ya Serikali na fedha kwenda kwenye miradi ya maendeleo kuna njia kuu mbili. Moja, ni kupanua wigo wa makusanyo; na pili, ni kupunguza matumizi ya fedha za Serikali yasiyo ya lazima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika kipindi cha miaka mitatu, yaani mwaka 2020/2021 hadi 2022/2023, Serikali imekusanya kati ya asilimia 95 hadi 97. Tunaipongeza Serikali kwa makusanyo hayo mazuri, lakini yako maswali mengi hapa Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wanauliza, mbona fedha haziji kwenye miradi? Serikali inafanya kazi kubwa, lakini ni kwamba tuna malimbikizo ya madeni ya huko nyuma, pia tuna utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya kimaendeleo na hivyo kuna ongezeko la matumizi yasiyo ya lazima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kubana matumizi kuna haja ya kuangalia upya mfumo wa ununuzi wa magari ya Serikali. Katika eneo hili, Serikali ikijibana mimi naamini kabisa kwamba fedha zitapatikana, zitabaki na zitaenda kwenye miradi yetu ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni malimbikizo ya madeni (arrears). Malimbikizo ya madeni ni changamoto ambayo isipotafutiwa suluhu ya haraka inaleta madhara makubwa katika utekelezaji wa bajeti ya Selikali. Baadhi yameshaanza kuonekana. Kwa mfano, katika utekelezaji wa bajeti ya nusu mwaka, kwa maana ya Julai hadi Desemba, 2023, fedha za maendeleo zilizotolewa na Serikali zimefikia asilimia 62, lakini Waheshimiwa Wabunge wamelalamika kwamba hawaoni fedha kwenye miradi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhalisia ni kwamba fedha zimeenda kwenye kulipia hati za malipo ya miradi ya nyuma kutokana na kuwepo kwa malimbikizo ya madeni ya wakandarasi, watoa huduma na wazabuni kama ambavyo tumetoa kwenye taarifa yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, kwa sasa taarifa zinasema, malimbikizo ya madeni ni karibia asilimia 12 ya bajeti, na ni kinyume na viwango vya kimataifa ambavyo havitakiwi kuzidi asilimia mbili ya bajeti ya Serikali. Kwa hiyo, tunaomba sana Wizara ya Fedha na Serikali kwa ujumla, mhakikishe kwamba malimbikizo ya madeni haya yanalipwa kwa wakati ili watoa huduma hawa pia waendelee kukuza uchumi katika familia zao na Taifa kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la msingi hapa ni kwamba, Waheshimiwa Wabunge tukubali na hii Serikali tuipongeze. Katika maeneo ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, ni Tanzania pekee ndiyo inatekeleza miradi mikubwa ya kimkakati; mradi wa Bwawa la Nyerere na mradi wa SGR. Kwa hiyo, fedha nyingi zinaelekezwa kwenye miradi hii mikubwa, lakini kuna mambo ya kufanya ili fedha zibaki ziende kwenye miradi midogo midogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ya kufanyika ni haya yafuatayo: -
(i) Kufanya tathmini na kuondoa misamaha yote ya kodi isiyokuwa na tija ili kuongeza mapato ya Serikali na kufikia lengo la misamaha ya kodi isiyozidi asilimia moja ya Pato la Taifa;

(ii) Kila mtu anayestahili kulipa kodi, alipe kodi stahiki na kwa haki ili kuongeza mapato ya Serikali;

(iii) Kuharakisha zoezi la uhakiki wa madeni ili kuepuka riba na adhabu na kuwaondolea wadai madhila haya;

(iv) Kuimarisha kitengo cha Mkaguzi Mkuu wa Ndani ili aweze kufanya ukaguzi kwa wakati; na

(v) Utungaji wa Sheria kwenda sambamba na utungaji wa Kanuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lako Tukufu limekuwa likitunga sheria mbalimbali, lakini baadaye sheria inachelewa kutekelezwa kwa sababu tu Kanuni bado haijatengenezwa. Changamoto inakuwa kubwa pale ambapo kwa mfano, umetunga sheria kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato, unapochelewesha kutengeneza kanuni maana yake unapoteza mapato ya Serikali kwa kipindi kirefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunashauri masuala yafuatayo kwa Serikali: -

(i) Utungaji wa sheria mpya uende sambamba na utungaji wa kanuni zake ili kurahisisha matumizi ya sheria mpya;

(ii) Kuwepo na muda maalum wa uandaaji na kupitishwa kwa kanuni mpya baada ya sheria kutiwa saini na Mheshimiwa Rais ili sheria mpya na kanuni zake kuanza kutumika mara moja; na

(iii) Kwa zile sheria ambazo hazitegemei sana uwepo wa kanuni, basi sheria hizi ianze kutumika mara moja iwezekanavyo ili isisubiri kanuni na tuendelee kukusanya mapato ya taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni changamoto ya upatikanaji wa fedha za kigeni hapa nchini. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, wote ni mashahidi kwamba kumekuwa na changamoto kubwa sana za uhaba wa fedha za kigeni hapa nchini, lakini tunapongeza juhudi mbalimbali za Serikali. Sisi Kamati ya Bajeti tumekutana na Wizara ya Fedha pamoja na Benki Kuu, zile juhudi mbalimbali ambazo zimeendelea na mojawapo kubwa ambalo tunaishauri Serikali ni kuhakikisha kwamba tunaongeza uzalishaji wa bidhaa za ndani ili kupunguza gharama za uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi. Hili ni jambo la msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, takwimu zinaonesha, kwa mfano, kati ya kipindi cha Julai hadi Desemba, 2023 thamani ya bidhaa na huduma zilizoagizwa kutoka nje ilipungua kwa asilimia 8.3 na kufikia dola za Marekani milioni 8,622.8 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 9,405.8 katika kipindi hicho cha mwaka 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizi, Kamati yetu ya Bunge ya Bajeti, inaishauri Serikali kuchuka hatua zifuatazo ili kuweza kunusuru jambo hili la ukosefu wa fedha za kigeni hapa nchini: -

(i) Kuchochea matumizi ya gesi iliyogandamizwa (compressed natural gas) ili kupunguza mahitaji ya mafuta ya petroli ambayo yanachangia takribani asilimia 21 ya thamani yote ya uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi. Kwa hiyo, jambo hili tukilifanya vizuri tutapunguza kutoa matumizi ya fedha za nje kuagiza bidhaa hizi nje ya nchi;

(ii) Kuboresha miundombinu ya Sekta ya Utalii, kwa sababu ni sekta ambayo imedhihirisha kuongeza mapato ya fedha za kigeni hapa nchini;

(iii) Serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi pamoja na kuongeza wigo wa bidhaa zinazouzwa nje ya nchi kwa maana ya export promotion;

(iv) Kuongeza thamani ya mauzo nje kwa bidhaa zetu za asili ili yapate bei stahiki katika soko la dunia; na

(v) Malighafi za miradi inayotekelezwa hapa nchini, zinunuliwe kwanza ndani mpaka tutakapokuwa na upungufu ndiyo tuweze kuagiza nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua hizi zote nilizozitaja zitaongeza ujazo wa fedha za kigeni hapa nchini, kwa maana ya mzunguko wa fedha za kigeni hapa nchini na kupunguza mahitaji ya matumizi ya fedha za kigeni kwa ununuzi wa bidhaa za kigeni nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uko mtazamo kwamba Serikali itumie akiba ya fedha za kigeni ili iweze kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni hapa nchini. Akiba ya fedha za kigeni ambazo zinatunzwa zina sababu kuu maalum. Tukizitumia kuongeza ujazo wa fedha tutaharibu dhima nzima na malengo ya Serikali katika eneo hili.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DANIEL B. SILLO – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA BAJETI: Katika eneo hili, mtazamo huu siyo sahihi kwa sababu unaondoa dhana nzima ya akiba ambayo inatumika wakati wa majanga, wakati ikitokea bahati mbaya ya vita au kwenye mtikisiko mkubwa wa uchumi hapa duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ndiyo maeneo machache ambayo nilipenda niyatolee ufafanuzi. Pia, narudia kuwapongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote mliochangia hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti. Tunaamini haya yote mmeyachukua na mtayafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu sasa lipokee Taarifa ya Kamati na likubali Maoni na Mapendekezo yote ya Kamati kuwa Maazimio ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.