Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuwa mmoja wa wachangiaji katika bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja mapendekezo yote ya bajeti ambayo yamewasilishwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Naipongeza Serikali kwa mambo makubwa inayofanya, kwa kipindi cha miaka minne ya Mheshimiwa Rais mambo mengi yamefanyika katika majimbo yetu na wananchi wote wanafahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana kwenye bajeti hapa nililalamika sana kuhusu mambo mbalimbali ambayo yalikuwa yanawatatiza wananchi wangu katika Jimbo langu la Igalula, lakini kwa kuwa Serikali ni sikivu, mambo mengi yamefanyika ikiwemo ahadi za viongozi ambapo nililalamikia hapa kwamba, walikuwa wanakuja kwenye majimbo yetu, wanatoa ahadi, halafu wanaondoka moja kwa moja na kilio kile walikisikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nililalamikia wodi waliyokuwa wameanzisha wananchi, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikwenda pale Imalakaseko akaahidi shilingi milioni 80 na leo milioni 80 imekwishakwenda na wodi imeshakamilika. Nawashukuru sana Serikali na namshukuru Mheshimiwa Jenista, aliisimamia kwa nguvu zote akasema yote yatakwenda, kwa hiyo niishukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado kuna changamoto chache chache ambazo bado hazijakamilika, lakini kwa usikivu wa Serikali naomba nikumbushe kwamba, tarehe 17 Mei, 2022, Mheshimiwa Rais alikuja katika Mkoa wa Tabora katika ufunguzi wa Barabara ya Chaya - Nyahua. Alipokuwa jimboni kwangu tulimpelekea maombi kadhaa, baadhi ya maombi aliyatolea ufafanuzi na akatoa maelekezo kwa Mawaziri. Ombi la kwanza, Mheshimiwa Rais, alitoa maelekezo ijengwe Shule ya Msingi Igalula ambayo Mradi wa SGR umepita, akatoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mkuu ile shule ijengwe, lakini mpaka leo shule bado haijajengwa. Kwa hiyo naikumbusha Serikali ahadi ya Kiongozi wetu Mkuu ilindwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, tulimwomba ujenzi wa Daraja la Loya katika Mto Loya ambalo kila mwaka wananchi wanakufa kwa sababu ya kutokupitika. Katika ahadi hii alitoa maelekezo, naiomba niikumbushe Serikali. Serikali yetu ni Sikivu, nadhani wamekwishasikia na watu wapo hapa watafanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kwamba nina maombi machache, kwa kuwa sisi kazi yetu ni kuleta matatizo ya wananchi na Serikali kusikiliza matatizo ya wawakilishi wa wananchi. Ombi la kwanza, sisi Jimbo la Igalula tumepitiwa na mradi mkubwa wa SGR na baadhi ya maeneo ulikopita ni kwenye makazi ya watu. Kwanza nianze kuishukuru Serikali imekwishaanza kulipa fidia. Nilileta hapa maombi kwamba kuna watu waliifuata reli, leo Mheshimiwa Rais baada ya kuyasikia maombi hayo wale waliokuwa wameifuata reli walitakiwa wasilipwe hata shilingi 10, kwa mapenzi ya dhati ya Mheshimiwa Rais, leo wamelipwa kifuta jasho kwa sababu walikuwa wamekwishaendeleza maeneo hayo. Wananchi haoa wamenituma nitoe shukurani kwa Mheshimiwa Rais, fedha hizo wameshazipokea na wamekwishaanza ktengenezea makazi sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna changamoto ya baadhi ya watu ambao bado hawajalipwa fidia wa katika Kata za Goweko na baadhi katika Kata za Igalula. Niiombe Serikali, tathimini kisheria ikipita miezi sita lazima wakafanye tathmini upya na leo imekwishapita zaidi ya miezi 10 na kidogo. Kwa hiyo niiombe Serikali kabla ya Bunge hili la bajeti kuisha, watu wote wa Jimbo la Igalula ambao walitakiwa walipwe fidia katika Mradi wa SGR, basi wawe wamelipwa na kama watakuwa hawajalipwa basi Serikali warudi wakafanye tathmini upya ili sasa tuendane na matakwa ya sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la kulipa makaburi, wameleta kizungumkuti kule, wananchi tulikwenda tukawaomba tuhamishe mahali ambapo walikuwa wamewazika wapendwa wao na wananchi waliunga mkono juhudi za Serikali, lakini wananchi kila siku wanaahidiwa wiki ijayo, wiki ijayo. Wananchi wa Kata za Igalula, Kata za Goweko, Kizengi pamoja na Tura wametoa maeneo kwa nia ya dhati ili kuendeleza mradi wa Serikali, wakahamisha makaburi yao, lakini mpaka leo hakuna kinachoendelea. Niiombe Serikali waweze kuwalipa wananchi hao hasa waliotoa maeneo yao kwa mapenzi ya dhati ya kupisha Mradi wa SGR.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine nina maombi katika Ofisi ya Waziri Mkuu. Hapa wamezungumza na Waheshimiwa Wabunge wameuliza maswali hapa; sisi katika halmashauri yetu ya Wilaya ya Uyui tulileta mapendekezo ya kuiomba Serikali ione namna ya kulipunguza eneo la kiutawala ikiwemo kuomba halmashauri nyingine ya Kizengi. Mheshimiwa Rais alipokuja katika ziara Mkoa wa Tabora tulimpa ombi hilo, alituahidi akasema tengenezeni document kutokana na matakwa ya Serikali na bajeti zake ili siku wakihitaji kutoa maeneo ya kiutawala Wilaya ya Uyui ina sifa na uwezekano wa kupewa kwa sababu Wilaya ya Uyui kijiografia imekaa vibaya zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo mtu akitoka Tura kwenda kuifuata Halmashauri ya Wilaya ya Uyui, anatumia zaidi ya shilingi 20,000 lakini anatembea zaidi ya kilomita 200 na kidogo kwenda Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Uyui. Leo mgonjwa akipatikana katika Kata ya Loya anatakiwa kwenda Hospitali ya Wilaya yetu ya Halmashauri ya Wilaya ya Uyui anatembea zaidi ya kilomita 180 kuifuata kule huduma. Tukaona ni vyema sasa tupate halmashauri nyingine ambayo itakaa Makao Makuu katika Kata ya Kizengi na halmashauri hiyo tukasema itaitwa Halmashauri ya Kizengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali kupitia Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kuwa ni bajeti yake hii na tutasikiliza Ofisi ya Rais, TAMISEMI nini wamepanga kwenye bajeti hii, basi haya maeneo ambayo wananchi wanafuata huduma umbali mrefu waone namna gani ya kupunguza, ikiwemo kugawa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kuwa na halmashauri mbili na kuongeza tarafa moja ya Kata ya Kizengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maombi yangu mengine Wilaya ya Uyui pamoja na ukubwa wake tuna Mkuu wa Wilaya ana kata 30, leo Wilaya ya Uyui ina square kilometre za mraba 11,000 na Mkuu wa Wilaya ni mmoja. Sasa kumekuwa na changamoto ya kutokuwepo na gari la uhakika la Mkuu wa Wilaya. Niiombe Serikali, kwa kuwa hawa Wakuu wa Wilaya ni wasaidizi wa Mheshimiwa Rais, Wakuu wa Wilaya wanatusaidia kwenda kusikiliza kero wakati Mbunge akiwa katika majukumu ya kibunge na wakati Mheshimiwa Rais na Mkuu wa Mkoa wakiwa na majukumu mengine. Leo Mkuu wa Wilaya akishindwa kwenda kusikiliza kero kwa sababu ya kutokuwepo kwa uhakika wa usafiri basi, anaiangusha Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali yetu, Wakuu wa Wilaya wote wenye changamoto ya usafiri, ione namna gani ya kuwasaidia ili waweze kupata usafiri wa uhakika wa kwenda kuwasikiliza wananchi, akiwemo Mkuu wangu wa Wilaya ya Uyui ambaye amekuja kwa kasi, anakwenda kijiji kwa kijiji muda wote. Sasa ili asivunjike moyo, basi apate usafiri wa kufaa wa kuwafikia wananchi na kuwasikiliza kero zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Igalula pamoja na Tanzania nzima tumepata majanga ya kuongezeka kwa mvua, lakini kuna uharibifu mkubwa wa barabara hasa katika Barabara ya Goweko – Igalula - Ndevelwa. Awali mwananchi alikuwa anasafiri kwa shilingi 3,500 hadi 4,000, sasa hivi kwenda kuifuata huduma kwa kutumia hiyo Barabara ya Goweko – Igalula -Ndevelwa anatumia zaidi ya shilingi 20,000. Sasa anatumia shilingi 20,000 na muda anatumia kwenda huko ni zaidi ya masaa 10 ilhali zamani alikuwa anatumia zaidi ya masaa mawili kufuata huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali, Jimbo la Igalula tumepata athari kubwa ya barabara, ikiwemo barabara ya Igalula – Kigwa kilomita 19 ambayo haipitiki, Goweko – Manta – Kigwa haipitiki. Vilevile barabara ya Mpumbuli – Izumba kuna mashimo makubwa nayo ni changamoto kwa wananchi na haipitiki, Mabeshi – Loya haipitiki, Izumba – Matuga – Isuli imekatika madaraja na kwa hiyo haipitiki. Niiombe Serikali kwa hizi barabara zinazofungua uchumi ipeleke huduma kwa haraka ili wananchi waweze kupata huduma...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Venant Kengele ya pili hiyo.

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante kwa muda wako. (Makofi)