Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Mohammed Said Issa

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali hiki cha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitamalizia mchango wangu kwa mambo machache tu. Jambo la kwanza ni suala la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. Tulipitisha Sheria hapa, Sura namba 343 na 292 ambayo inahusiana na uchaguzi wa Wabunge, Madiwani na Uchaguzi wa Mheshimiwa Rais. Kwa kweli jambo hili lilikuwa ni jambo jema sana. Sasa basi, naomba, vyombo vinavyohusika tufanye utekelezaji wa jambo hili. Ni jambo la kufurahisha na la kupendeza, Mheshimiwa Rais ameshasaini sheria hii. Sasa, kwa sasa hivi chaguzi zinazokuja tuendelee na hii sheria kwa sababu juzi tumefanya chaguzi ndogo katika Kata 22, yaliyotokea ni yale yale ambayo yalinung’unikiwa kwenye chaguzi zilizopita kama ya 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni wakati wa kuwaondoshea wananchi kero zile ambazo walikuwa wanahitaji ziondolewe. Kwa hiyo, napendekeza tuendelee katika uchaguzi utakaokuja wa Serikali za Mitaa na hii Tume Huru iundwe kabisa isiwe tu tumepitisha jina. Iundwe kabisa, iendelee kufanya kazi ili tuweze kuwapatia wananchi haki waliyokuwa wanaitaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, tumepitisha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, sasa basi kule Zanzibar, Tume Huru hii ya Taifa ya Uchaguzi ilikuwa inawakilishwa na Tume ya Taifa ya Zanzibar (ZEC). Kwa hiyo sasa kule hakuna Tume Huru ya Zanzibar. Sasa iwe ni marufuku kutumia wakala yule kwa sababu wale siyo huru, tunataka huru. Kama ikiwa hapa ni huru, Tanzania ni huru basi na Zanzibar iwe huru. Kwa vile haijawa huru basi uchaguzi unaokuja, ZEC isiwe ni wakala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia mchango wangu, naomba niguse suala la Bwawa la Mwalimu Nyerere...

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

TAARIFA

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Uchaguzi unaofanyika upande wa pili wa Muungano ili kuthibitisha uhuru wake ni pamoja na yeye kuwepo ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, sioni sawa kama Mheshimiwa Mbunge anatoa tuhuma kwamba uchaguzi uliofanyika kule siyo huru na Tume kule siyo huru. Misingi ya sheria iliyobadilishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inahusu Tume ya Uchaguzi ya Tanzania. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, taarifa hiyo.

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa yake siipokei...

NAIBU SPIKA: Ukiendelea sana utakuwa unajitoa kwenye Kiapo cha Bunge hili...

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, sipokei taarifa na ndiyo maana tulibadilisha sheria ya kuwa Tume Huru ya Uchaguzi. Kama na yeye anakataa siyo Tume Huru ya Uchaguzi, tungebakia kule kule kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kwa maana hiyo, kule Zanzibar wakitaka iwe Tume huru na wao wabadilishe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea na mchango wangu. Jambo la pili ni suala la Bwawa la Mwalimu Nyerere. Wananchi wa...

NAIBU SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa, dakika tano zako zimekwisha.

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, aaaahhha, haijafika. (Vicheko)

NAIBU SPIKA: Sasa Sheikh...

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, haijafika mbona nimeangalia.

NAIBU SPIKA: Sasa una...

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba basi nimalizie mchango wangu kidogo dakika moja...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mohamed, mimi nakwenda kwa mujibu wa kanuni. Dakika tano zako ulizoziomba zimekwisha.

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie mchango wangu dakika moja.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mohamed, kaa chini tafadhali. (Makofi)

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)