Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuungana na viongozi wenzangu kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia baraka zake katika nyanja mbalimbali za ustawi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuungana na wananchi wa Jimbo langu la Mbulu Mjini kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ya kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi mwaka 2023/2024, hususan katika Jimbo langu la Mbulu Mjini. Tumepata fedha nyingi sana haijapata kutokea, hali iliyotuwezesha kutekeleza miradi iliyokwama kwa muda mrefu toka mwaka 1984. Mifano yake ni ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji Endayaya Tlawi na ujenzi wa Daraja la Gunyoda na barabara unganishi katika wilaya jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi na wananchi wa Mbulu Mjini kwa pamoja tunamwombea Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kheri na baraka tele kwa Mwenyezi Mungu na tunamuahidi ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2025, kwa kuwa matokeo ya utendaji wake na Serikali katika utatuzi wa kero na changamoto zilizowakabili wananchi wetu kwa muda mrefu tunayaona.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kutoa mchango wangu kuishauri Serikali kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na mapendekezo na maoni ya Kamati zetu zote nne:-
(i) Tunaiomba Serikali iangalie upya utaratibu wa kuboresha maslahi ya wastaafu nchini kwani kwa sasa kiwango kinacholipwa kwa wastaafu kila mwezi ni kidogo sana kulingana na hali halisi ya maisha kiuchumi;
(ii) Tunaiomba Serikali ijitahidi sana kutoa fedha za bajeti ya maendeleo tunazopitisha kila mwaka kwa kila Wizara kwani kitendo cha fedha nyingi kutopelekwa kwenye malengo yaliyokusudiwa kinakwamisha maendeleo ya nchi kwa ujumla;
(iii) Tunaiomba Serikali iangalie upya utaratibu wa kusimamia uendeshaji wa mashirika yanayojiendesha kwa hasara ili kuleta ufanisi zaidi kupata gawio kama ilivyotarajiwa; na
(iv) Tunaiomba Serikali iangalie utaratibu wa kuanza kujadili upya suala la kikokotoo cha pensheni ya wastaafu. Kwa kweli kila unapofanya mikutano ya hadhara na mikutano ya watumishi popote pale wamelalamikia jambo hili. Hivyo basi kuna haja ya Serikali kukaa meza moja na vyama vya wafanyakazi ili kupata maridhiano ya pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga hoja mkono hoja kwa asilimia mia moja na naomba kuwasilisha.