Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja ya hotuba ambayo imetolewa na Mheshimiwa Waziri wetu Mkuu, ambayo imebeba vitu vingi sana kwa maslahi ya Taifa letu. Naomba nichangie mambo machache pengine kwa haraka haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya kwanza iliyowekezwa kwenye Wizara yetu ni kuwezesha Mamlaka ya Bandari ili kuongeza wigo wa kukusanya mapato. Serikali ya Awamu ya Sita inaenda kuingia katika rekodi ya Serikali ambazo zinafanya mapinduzi makubwa sana kwenye upande wa bandari. Ukianza kabisa tunao mradi mkubwa wa DMDP ambao tumeboresha gati namba moja mpaka gati namba saba na gati namba nane mpaka namba 11. Mradi huu ni wa shilingi trilioni moja. Pia, juzi tarehe 26 Mwezi wa Pili, 2024 tumesaini mkataba mkubwa wa kujenga matenki ya kuhifadhia mafuta. Hili ni moja kati ya mambo ambayo tuna kila sababu ya kutembea kifua mbele kwa sababu yanagusa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, matenki haya yanakwenda kuhifadhi cubic litre 420,000, una gharama ya bilioni 680. Faida zake ni nini? Nitasema kwa ufupi. Moja, inapunguza siku za ushushaji wa mafuta katika meli kutoka siku saba mpaka siku mbili. Pili, inapunguza gharama za meli za kukaa bandarini. Tatu, inapunguza gharama za mafuta yenyewe kwa watumiaji. Hivyo ni mradi mkubwa ambao Serikali yetu imeelekeza nguvu kubwa sana na kuhakikisha tunafanya pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maboresho makubwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam, pia tumefanya uwekezaji. Tumempa mtu ambaye atatusaidia kufanya uwekezaji pale ndani, kuendesha ili kuongeza mapato zaidi. Sambamba na Bandari ya Dar es Salaam, tumefanya uwekezaji. Tunakwenda kufanya maboresho Bandari ya Kisiwa Mgao – Mtwara ambayo ni maalum kwa kusafirisha makaa ya mawe, cement na bidhaa chafu kutoka nchini kwetu kwenda mahali pengine. Tunafanya maboresho makubwa Mbamba Bay na mkataba umeshasainiwa na mkandarasi yuko site. Tunafanya maboresho makubwa Bandari ya Kemondo, Bukoba na North Mwanza, Ziwa Victoria kote huko ni kuongeza matumizi makubwa ya bandari zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi, inakwenda sambamba na ujenzi wa meli zetu. Tumesaini mkataba wa zaidi ya bilioni 600 hapo majuzi Kigoma ambao tunajenga kiwanda kikubwa cha kutengeneza na kukarabati meli pale Ziwa Tanganyika (ship yard). Pia, tunajenga meli mpya ya tani 3,500 ya mizigo Ziwa Tanganyika na Ziwa Victoria. Yote haya kwa umoja wake ni uwekezaji mkubwa kwenye upande wa bandari pamoja na vifaa ambavyo vinatusaidia kwa ajili ya kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwepo pia na hoja ya Bandari yetu ya Lindi, ambayo ni bandari inaendelea kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi wetu na sisi tunaendelea kuiboresha hatua kwa hatua ili matumizi yake yaweze kuendelea kuwa makubwa zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja nyingine kuhusu kuboresha na kupunguza changamoto mbalimbali ambazo zipo kwenye Bandari yetu ya Dar es Salaam, tunaiagiza Mamlaka ya Bandari kuendelea kukaa chini na kutazama changamoto ndogo ndogo ambazo ziko pale kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wananchi wetu wananufaika nayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa Viwanja vya Ndege. Serikali hii ya Awamu ya Sita, kupitia bajeti iliyopita na zinazoendelea tumeona uwekezaji mkubwa sana kwenye Viwanja vya Ndege. Kwa mara ya kwanza, karibu viwanja vyote vya ndege nchini vinajengwa, vinakarabatiwa ama vinaboreshwa kwa namna nyingine. Tuna Uwanja wetu wa Msalato mpya unajengwa hapa Dodoma, tuna Uwanja wa Mbeya upo hatua za mwishoni umeshakamilika, tuna uwanja wa Kigoma, Mpanda, Tabora, Mtwara na maeneo mengine. Uwanja wa Arusha (TAA), uwanja wa Mwanza (Jengo la Abiria), uwanja wa Shinyanga Mkandarasi yupo site, Simiyu tupo katika hatua ya kutwaa ardhi na maeneo karibu yote nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni jambo la kutembea kifua mbele na kujidai kwa sababu kazi hii inakwenda kutunufaisha Watanzania, specifically kwa maana ya Mwanza kuifanya iwe ya kimataifa na nazingatia kengele yako ya kwanza imeshagongwa, tayari tunatoa wavamizi ili kutwaa eneo, tunaendelea na taratibu zetu za kisheria ili uwe wa kimataifa pamoja na kujenga jengo la abiria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana ya eneo la mwisho la reli, tunafahamu reli ni roho ya uchumi wa Taifa letu. Serikali hii ilipoingia madarakani tulikuwa na Reli ya TAZARA pekee yake kutoka hapa mpaka Kapiri Mposhi, Zambia iliyojengwa kipindi cha ukoloni miaka hiyo kilomita 1,600. Tunajenga reli takribani mpaka sasa hivi kilomita 2,300 kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza, kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma na kutoka Uvinza, Buhigwe mpaka Msongati, huu ni uwekezaji mkubwa ambao tunaufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo imejengwa hoja kuhusiana na lini tutaanza ujenzi wa Reli ya Kusini. Tunatambua kama Serikali umuhimu wa Reli ya Kusini (Mtwara Corridor) ndiyo maana moja, tumeanza kujenga bandari ya Cargo kama nilivyosema. Pili, tumeshamaliza upembuzi yakinifu, hatua iliyopo kwa sasa hivi tumeanza kutafuta Mwekezaji wa kuweza kuingia naye PPP ili kuweza kuanza kujenga reli hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi, ipo hoja ambayo imejengwa na Mheshimiwa Mbunge wetu wa Ifakara kuhusiana na Mlimba. Moja, tulikwenda eneo husika tumeona mafuriko yaliavyoathiri watu wa Ifakara pamoja na Mlimba kwa ujumla. Hatua ya kwanza, tulipeleka helikopta kupeleka vyakula, hatua ya pili, treni ya Mwakyembe inafanya kazi sasa hivi kutoka Dar es Salaam kwenda mpaka Mlimba, hatua ya tatu tunaendelea kufukua ili reli ile ibaki safi. Pia, ushauri wake kuhusu maboresho ya sheria tumeupokea. Mwisho katika eneo hilo, mabadiliko ya sheria tuko kwenye hatua mbalimbali tutayafanyia kazi na tukikamilisha tutaleta hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Venant Protas pia amezungumzia habari ya fidia na ujenzi wa shule, tunamuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tunakwenda kujenga shule katika eneo lake kama ambavyo tulikuwa tumeahidi hapo nyuma na makaburi yale aliyoyaeleza kwenye Kata nne kama sehemu ya fidia, pia tutakwenda kukamilisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, fidia ya majengo na makazi kama ilivyoahidiwa tutakwenda kukamilisha na naiahidi Mamlaka ya Reli, wenzetu wa TRC waende wakafanye mchakato waharakishe ili kuhakikisha kwamba fidia katika maeneo ya pale Igalula yanakamilika sambamba na kuanza mchakato wa kujenga shule hiyo kama ilivyoahidiwa na Viongozi wetu Wakuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na habari ya SGR kuhusiana na malalamiko ya wananchi wa kule Itigi wanaolipwa shilingi 200,000 kwa heka. Tunaiagiza Mamlaka yetu ya Reli pia iende ikafuate sheria, kwa mujibu wa sheria ndiyo wananchi wetu waweze kulipwa hizo fidia zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge Genzabuke, anaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita na namshukuru sana kwa kupongeza ni wachache sana wanaoweza kutambua kazi kubwa na uwekezaji mkubwa unaofanywa, Mheshimiwa Mbunge amelitambua hilo na ameiambia Serikali, juhudi ziongezeke. Tunamhakikishia kwamba tutaongeza zaidi juhudi kwa sababu tunafahamu namna pekee ya kujenga uchumi wa Taifa letu …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri kengele ya pili hiyo.

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo haya, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)