Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Hamad Hassan Chande

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kojani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fusa hii. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Rahim, mwingi wa rehema, mwenye kurehemu kwa kutuwezesha kuwepo katika Bunge hili na mijadala yetu tukiwa katika hali ya uzima na afya. Pili, nikushukuru wewe kwa kunipa fursa hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia, wametoa ushauri mzuri, wametoa hoja njema za kujenga, lakini sitoweza kujibu moja baada ya nyingine, naomba uniruhusu niweze kutoa maelezo kwa hoja chache.

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo hoja kwanza ambayo imetolewa na Ndugu yetu Mheshimiwa Kilumbe, katika hoja yake anashauri kwamba, wakandarasi na wazabuni Serikali iwalipe kwa wakati, tunalitambua hilo na Serikali inaendelea kulipa madeni ya wakandarasi na wazabuni siku hadi siku. Hivi ninavyoongea sasa hivi mpaka kufika leo tayari bilioni 882.5 zimeshalipwa kwa wakandarasi. Hivyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine kwamba kadri fedha zitakavyopatikana, basi madeni hayo yatalipwa kwa wakandarasi wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ilikuwa ni hoja ya Mheshimiwa Kilumbe, anasema kwamba PPRA waimarishe mfumo wa NeST. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wenzangu kwamba Mfumo wa NeST uko vizuri sana, ni mfumo wa kizalendo, ni mfumo ambao taarifa zetu ziko salama ikilinganishwa na mfumo uliokuwepo nyuma TANePS, kwamba taarifa zetu zilikuwa zipo nje ya mawanda yetu, leo kupitia NeST taarifa zetu zipo salama na bahati nzuri wanaosimamia mfumo ule ni wazalendo yaani ni wananchi wa Tanzania wenyewe, hakuna mtu mgeni ambaye anausimamia mfumo ule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mfumo huu utaendelea kutoa mafunzo mazuri kwa wazabuni wote nchini, hivi ninavyozungumza sasa wazabuni 2,170 tayari wameshapatiwa mafunzo na milango iko wazi. Katika hili nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumpongeze sana Mheshimiwa Rais, kwa fedha nyingi ambayo ameiweka pale kwa ajili ya utekelezaji na ujenzi wa mfumo huu. Hapa Mkurugenzi Mkuu, Ndugu yetu Maswi apewe maua yake kwa usimamizi mzuri wa PPRA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine imetolewa na Mheshimiwa Mariam Nyoka, kwamba fedha bilioni moja itolewe kwa ndugu zetu wenye ulemavu, fedha hii tayari imeshatolewa na imeshafika kunapohusika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya mwisho ambayo nitazungumza ni hoja ya Mheshimiwa Innocent Bilakwate, anasema kwamba Serikali iendelee kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kudai risiti wakati wa manunuzi. Kwa kweli suala hili ni changamoto, naomba niwaombe Wabunge wenzangu na wananchi wote, tuwe na utamaduni wa kudai risiti tunaponunua na wale wafanyabiashara wawe na utamaduni wa kutoa risiti, yaani iwe kama ni utamaduni wetu kama vile mtu akiamka asubuhi anatafuta maji kuosha uso ama kuoga basi akifanya manunuzi lazima atoe risiti na mteja adai risiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo kaulimbiu inayosema tuwajibike. Ni lazima tuwajibike, suala la ukusanyaji wa kodi lisiwe ni suala la Serikali na TRA peke yake, suala hili liwe ni wajibu na jukumu la kila mtu hapa nchini kwa sababu maendeleo yetu yanahitaji makusanyo yetu ya fedha. Leo kila Mbunge tunatoa hoja kwamba barabara yangu imefanya hivi, barabara yangu imebomoka zinahitajika fedha, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tuwajibike.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tumetengeneza kwamba mteja wajibu wake ni kudai risiti halisi na thamani ya kile alichokinunua, lakini mfanyabiashara wajibu wake ni kutoa risiti, tena risiti halisi na thamani ya kile ambacho amekiuza. Nini wajibu wa TRA? TRA wajibu wake ni kukusanya kodi kwa ufanisi, kwa uhalisia bila kutumia nguvu na fedha hiyo kuirudisha Serikalini na wajibu wa Serikali unaonekana ni kupeleka maendeleo kila sehemu, kujenga miradi ya maendeleo na mwenye macho haambiwi tazama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kila jimbo, kila wilaya inaonekana miradi ya maendeleo iliyofanyika kama siyo afya, basi miradi ya elimu kama siyo elimu basi miradi ya barabara. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge, kwa yale ambayo hatujayajibu, basi tunayachukua na tutajibu kwa maandishi na tunaenda kuyafanyia kazi. Ahsante sana. (Makofi)