Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo ingekuwa Kanuni inaruhusu, tungekwenda moja kwa moja kupiga kura, hata hivyo, acha nichangie.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami naungana na wenzangu kumpongeza sana kiongozi wetu, Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa bajeti yake nzuri sana na kwa jinsi anavyotusimamia. Nawashukuru na kuwapongeza Mawaziri wenzangu katika Ofisi yake kwa jinsi ambavyo wanatuongoza vizuri. Namshukuru sana dada yangu, Mheshimiwa Jenista Mhagama. Yeye ni zaidi ya kiongozi na ni mlezi, tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia maeneo mawili tu ambayo yamejitokeza katika eneo langu. La kwanza, ni hoja kutoka kwa Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini ambaye alihoji na kutoa ushauri kuhusu Taarifa za Sensa. Ameuliza ni namna gani Serikali inatumia taarifa hizi kwenye mipango ya maendeleo ya nchi?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima nikiri, ni kweli kwamba, Taarifa za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 imesheheni takwimu muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Taarifa ile inatupa muundo mzuri wa kuangalia aina ya watu ambao tunao kwa maana ya idadi ya watu. Tuna mifano mitano ambayo inaweza kusaidia, moja, ni 76% ya Watanzania, kwa mujibu wa taarifa hiyo, wapo chini ya miaka 35; 42.8% ya Watanzania wote wapo chini ya miaka 15; 19% ya Watanzania wote hawa wana umri wa kwenda shule kwa maana ya miaka saba na kuendelea; na 65% ambayo ni theluthi mbili ya Watanzania wanaishi maeneo ya vijijini na ya mwisho katika muundo huo ni 36% ya kaya zote hapa Tanzania zinaongozwa na akinamama, yaani mama ndio mkuu wa kaya. Hii maana yake ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuzingatia takwimu hizi ni lazima ichague vipaumbele kwa umakini na kipaumbele cha kwanza ni lazima uwekeze katika elimu kwa sababu Taifa lina idadi kubwa. Kimsingi Taifa letu ni Taifa la watoto na vijana, kwa hiyo, ni lazima uwekeze katika elimu na kwa sababu hiyo, sera zetu zimeweka kipaumbele katika elimu, katika afya na katika lishe kwa sababu, ni lazima hawa watoto na vijana waandaliwe vizuri. Kwa hiyo, ni lazima matumizi ya takwimu yatuelekeze huko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwelekeo wa sera za Serikali ya Awamu ya Sita ni kukazania sana maendeleo vijijini kwa sababu, kwa takwimu hizi idadi kubwa ya wananchi wetu ipo kule. Ndio maana utaona kwa sasa sekta za kilimo zinapewa msukumo mpya na ndio sababu Mheshimiwa Waziri wa Kilimo asubuhi ameeleza jinsi ambavyo bajeti imeongezeka. Pia ndio maana Sekta ya Mifugo na Uvuvi inapewa msukumo mkubwa, lakini ndio maana tunazungumzia habari ya miradi ya umeme vijijini ili kuhakikisha wananchi wetu wanapata unafuu wa maisha na hii sababu tunawekeza sana kwenye maendeleo ya miundombinu ya barabara vijijini kupitia TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yote hiyo inaonesha kwamba, tunazitumia takwimu hizi kwa ajili ya kuweka vipaumbele vyetu sawasawa. Nawaahidi Waheshimiwa Wabunge kwamba, katika Dira ya Maendeleo ambayo tunaiandaa, takwimu hizi zitatumika kikamilifu kwa ajili ya kutuelekeza kwa miaka 25 mingine ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Sita pia inaendelea kuwajengea uwezo wanawake kwa sababu, kwa takwimu ambazo nimezieleza hapa ile hoja ya zamani kwamba, baba ni kichwa cha familia inaanza kupitwa na wakati. Kwa sasa baba na mama wote ni vichwa vya familia na katika kila familia 10 hapa Tanzania familia nne mama ndio kichwa cha familia. Kwa hiyo, maana yake ni lazima sera zetu zituelekeze kwenye eneo hilo. Hivyo, namhakikishia Mheshimiwa Mwakasaka na Wabunge wengine kwamba, Taarifa na Takwimu hizi za Sensa tutazitumia vizuri kwa ajili ya kupanga mipango yetu ya maendeleo ya muda mfupi na muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo napenda kuchangia ni hoja ya Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, ambaye alihoji na kushauri kuhusu umuhimu wa kuimarisha sekta ya uzalishaji viwandani. Kwa kweli, aliongea kwa uchungu sana kwamba, tunaagiza karibu kila kitu na hatuuzi sana nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kueleza, pamoja na changamoto zilizopo ukweli ni kwamba, mwelekeo wetu wa sera kwa sasa tunapozungumzia ukuaji wa Uchumi, tunataka uchumi wetu ukue, lakini uakisi mambo ya msingi manne. Moja, uchumi huu ukue na uwe jumuishi na siyo ukue kwa baadhi ya watu; Pili, uchochee ajira kwa vijana na akinamama; Tatu, uchumi wetu utuelekeze kwenye kupunguza umaskini; na Nne, tunataka uchumi wetu tuwekeze kwenye kuongeza mauzo ya bidhaa zilizoongezwa thamani nje ya nchi. Kwa hiyo, suala la value addition ni suala la msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya Mheshimiwa Hasunga ni ya msingi na tunaizingatia, ndio maana ukiangalia katika miaka mitatu iliyopita kuanzia mwaka 2021 hadi 2023, utaona kwamba, katika sekta ya uwekezaji miradi mingi ambayo tunaivutia ni katika sekta ya uzalishaji viwandani. Ukiangalia katika miaka hii mitatu tumekuwa na miradi 1,400, lakini miradi 456 ambayo ni 45% ni katika sekta ya uzalishaji viwandani. Kwa hiyo suala la uzalishaji viwandani tunalipa kipaumbele kikubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, siyo tu data za kwenye makaratasi bali hata ukienda kwenye uhalisia utaona. Nitoe mifano michache, Septemba, 2023 Mheshimiwa Rais amezindua kiwanda kikubwa cha kampuni moja inayoitwa Sapphire pale Mkuranga. Hiki ni kiwanda ambacho kinatengeneza vioo vya kisasa vya ujenzi wa nyumba, floating glass. Kiwanda hiki kimewekeza pale takribani shilingi bilioni 832, kinaajiri vijana wa Kitanzania 1,600 na hiki ni kiwanda kikubwa kuliko vyote hapa Afrika Mashariki na ni kiwanda cha nne kwa ukubwa katika Afrika, viwanda viwili vipo South Africa, kimoja Nigeria na cha nne kipo Tanzania na 75% ya mazao yanayozalishwa pale yanauzwa nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie Mheshimiwa Hasunga na Waheshimiwa Wabunge kwamba, suala hili la kukazania uzalishaji wa viwandani, ni suala la kisera, lakini pia kiutekelezaji linakwenda vizuri. Kwa hiyo mwelekeo wetu unakwenda vizuri ndio maana ukisoma takwimu za Benki Kuu ya Tanzania za Mwezi Machi zinaonesha kwamba, mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi zimeanza kuongezeka na zimeongezeka kwa 14.7%. Mwezi Februari mwaka huu, tupo Dola za Kimarekani bilioni 14.3 na zinakwenda zikiongezeka. Kweli tuna changamoto, lakini mwelekeo ni mzuri. Tunapojadili masuala haya tusiangalie tu umbali uliobaki katika kusafiri, pia tuangalie tumesafiri umbali mrefu kiasi gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakwenda vizuri, kwa usimamizi wa sera hizo nasema mwelekeo wetu ni mzuri na tunaamini kwamba, mauzo ya bidhaa ambazo zimeongezwa thamani kutoka viwandani yataendelea kuimarika kwa sababu ndio sera yetu na katika miaka ijayo sekta hii itaendelea kutiliwa mkazo mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nichangie maeneo hayo mawili, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)