Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Judith Salvio Kapinga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya chini ya Serikali ya Awamu ya Sita. Kipekee nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri ambayo ameisoma hapa wiki iliyopita na pia nampongeza kwa kazi kubwa anayofanya ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri, dada yangu Jenista Mhagama na kaka yangu Deo Ndejembi pamoja na Waheshimiwa Naibu Mawaziri, kaka yangu Patrobas Katambi na dada yangu Ummy Nderiananga.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naunga mkono hoja na kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa dhati ya mioyo yetu kwa ushauri, maono na mapendekezo mbalimbali ambayo wamechangia katika Sekta yetu ya Nishati na hususani katika Sekta Ndogo tunazozisimamia za Umeme, Mafuta pamoja na Gesi. Tumepata jumla ya wachangiaji 13 na yamkini naweza nisijibu hoja moja baada ya nyingine, lakini nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba, kila hoja ambayo imezungumzwa hapa tumeipokea kwa uzito wa kipekee sana na zile ambazo zinaweza kutekelezeka, tunapenda kuwahakikishia kwamba, tutazitekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na nishati safi ya kupikia. Waheshimiwa Wabunge wameeleza umuhimu wa kupunguza bei ya nishati safi ya kupikia, hususani gesi ili kuwawezesha Watanzania wengi zaidi waweze kutumia nishati hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha matumizi fanisi ya nishati safi ya kupikia na ili kuweza kuchagiza matumizi ya nishati safi ya kupikia ni lazima nishati hii iwe na sifa kuu nne. Moja, ni lazima ipatikane kwa urahisi; Pili, ni lazima matumizi yake yaweze kuwa rahisi; Tatu ni lazima iwe na unafuu wa bei; na Nne, ni lazima iwe nishati salama ambayo inalinda usalama wa watumiaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha masuala yote haya na hususan suala la unafuu wa bei, Serikali ya Awamu ya Sita imeshaanza kutekeleza mikakati mbalimbali kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanatumia nishati safi ya kupikia. Mojawapo ya mikakati hiyo ni kupunguza gharama za awali ambazo zinahusiana na kuanza matumizi ya nishati safi ya kupikia hususan vifaa pamoja na majiko ya gesi. Hii ni kwa sababu changamoto kubwa ilikuwa ni kwa wananchi kuanza kufanya matumizi kwa sababu gharama za awali huwa ni kubwa kwenye kupata vifaa pamoja na majiko. Jambo hili tayari tumeshaliwekea mikakati mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, tumeshaanza kutoa ruzuku ya mitungi ya gesi kwa ajili ya watumiaji mbalimbali wa Tanzania. Pili, kupitia miradi tunayoitekeleza na wabia wetu wa maendeleo hususan Umoja wa Ulaya pamoja na Wakala wetu wa Nishati Vijijini tayari tumeanza kuwawezesha mawakala wanaouza gesi mijini na vijijini kwa kuwapa ruzuku ili gesi inayoenda kwa mtumiaji wa mwisho iweze kuwa na gharama nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia mradi tunaoutekeleza na Umoja wa Ulaya, wananchi wataweza kupata unafuu kwa 45% mpaka 60%. Vilevile, kupitia miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini wananchi wataweza kupata unafuu kati ya 25% mpaka 30%. Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwenye suala la kuanza matumizi ya nishati safi ya kupikia Serikali imejizatiti kupunguza gharama ili Watanzania wengi waanze matumizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tunayo mikakati ikiwemo kuboresha upatikanaji wa malighafi na miundombinu ya uzalishaji, upokeaji, uhifadhi na usambazaji wa nishati safi ya kupikia. Tunafanya hivi kwa sababu tukiboresha upatikanaji wa malighafi na miundombinu nishati safi ya kupikia itakuwa na bei rahisi kwa sababu tutakuwa tume-balance economic scale. Pamoja na mikakati hiyo kwa sasa hivi tunafanyia kazi kuhuisha na kuoanisha sera, sheria, kanuni na miongozo wezeshi itakayofanikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni mikakati michache ambayo tunayo kuhakikisha kwa kadri ya maoni ya Mheshimiwa Rais ambaye ndio champion namba moja wa nishati safi ya kupikia, ikifikia 2033 Watanzania wengi wawe wanatumia nishati safi ya kupikia. Niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge agenda hii ya Mheshimiwa Rais ipo katika mikono salama sana ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili uweze kuzalisha tani moja ya mkaa unahitaji kuchoma magogo kati ya tani 10 mpaka 12. Ndio maana ni lazima tulinde mazingira yetu kwa wivu mkubwa sana na ndio maana ni lazima Waheshimiwa Wabunge na wananchi tuhamasishane kwenda kwenye nishati safi ya kupikia ili tuweze kutunza mazingira haya kwa manufaa yetu sisi na manufaa ya vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hoja hiyo Waheshimiwa Wabunge wamezungumza hapa kuhusiana na hoja ya kupeleka umeme kwenye vitongoji. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kama ambavyo tumefanya kwa ufanisi mkubwa sana Mradi wa Kupeleka Umeme Vijijini na mpaka leo hii tumebakisha vijiji 468 tu kati ya vijiji 12,318, ndiyo hivyo tutahakikisha vitongoji vyote ambavyo ni 31,532 visivyo na umeme vitapata umeme ndugu zangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vitongoji hivi ni vingi, jumla ya vitongoji tulivyo navyo ni 64,359 na mpaka leo hii kwa kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita tumeweza kupeleka umeme kwenye vitongoji 32,827. Kwa hiyo, utekelezaji wa kupeleka umeme kwenye vitongoji unaendelea. Niwahakikishie kama Mheshimiwa Rais anavyosema, maendeleo ni hatua tutaenda hatua kwa hatua kuhakikisha umeme kwenye vitongoji unapelekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)