Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ruangwa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI MKUU: Ahsante, shukurani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nataka nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima wa afya hata leo tumeweza kukutana kwenye Kikao hiki cha Sita cha Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge la Kumi la Mbili kwa ajili ya kuhitimisha mjadala kuhusu hoja ya bajeti ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kutumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Mbunge na Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Mabunge ya Dunia kwa namna ambavyo analiongoza Bunge letu kwa umahiri mkubwa. Nashukuru na kukupongeza sana wewe binafsi pamoja na Wenyeviti wote wa Bunge kwa Uongozi wenu imara na thabiti. Sina shaka Waheshimiwa Wabunge wenzangu watakubaliana nami kuwa wameweza kuongoza vyema kipindi chote cha mjadala kuhusu hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka wa fedha 2024/2025. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru na kuwapongeza sana Wenyeviti na Wajumbe wote wa Kamati za Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kwa michango yao muhimu ambayo wameitoa mbele ya Bunge lako Tukufu. Nikiri kwamba maoni na ushauri wao wakati wote umekuwa ukileta tija kubwa kwenye hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote kwa hoja na michango yenu yenye tija katika kipindi chote cha mjadala wa hoja ya Bajeti ya Waziri Mkuu. Nataka nitumie nafasi hii kuwahakikishia kwamba Serikali wakati wote itazingatia maoni yao na ushauri walioutoa katika mipango na utekelezaji wa majukumu yake kwa ustawi wa maendeleo ya wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mawaziri wa Sekta na Naibu Mawaziri waliochangia hoja ya Bajeti ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii pia kuwashukuru Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Idara, Mashirika, Taasisi na Wakala wa Serikali kwa ushirikiano mkubwa walioutoa na kufanikisha hoja ya Bajeti ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge. Nawapongeza sana Watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya katika hatua zote za maandalizi ya hotuba ya bajeti hadi tunapoelekea kuhitimisha mjadala wa hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Vilevile nawashukuru kwa ushirikiano walionipa ambao wakati wote ambao umeniwezesha kutimiza majukumu yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, salamu za pole; wakati tukiendelea na Mkutano huu wa Kumi na Tano wa Bunge lako Tukufu, mnamo tarehe 9 Aprili, 2024 tuliondokewa na mpendwa wetu Mheshimiwa Ahmed Yahya Abdulwakil aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kwahani. Sina shaka Waheshimiwa Wabunge wenzangu watakubaliana nami kuwa Mheshimiwa Ahmed Yahya Abdulwakil alikuwa ana uwezo mkubwa na ushawishi wa kipekee ndani ya Bunge hili na mchango wake utakumbukwa daima.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kutoa salamu za pole kwa wana CCM wote, familia, ndugu na jamaa wa marehemu, wananchi wa Jimbo la Kwahani na Watanzania wote kwa ujumla. Niwaombe Watanzania wote tumwombee marehemu kwa Mwenyezi Mungu apumzike mahali pema peponi.
WABUNGE FULANI: Amina.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni wapo Watanzania wenzetu waliopatwa na majanga mbalimbali yakiwemo ajali za barabarani, mafuriko na mengine yaliyosababisha vifo na uharibu wa mali. Kwa masikitiko makubwa naungana tena na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa salamu za pole kwa waathirika wote wa majanga hayo. Nitumie nafasi hii kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki waliowapoteza wapendwa wao kutokana na majanga hayo. Tumwombe Mwenyezi Mungu awajalie uponyaji wa haraka majeruhi wote na kuwapa pumziko la amani marehemu wote.
WABUNGE FULANI: Amina.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mjadala huu ukiendeshwa, Waheshimiwa Wabunge 129 wamechangia hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kati yao Waheshimiwa Wabunge 119 walichangia kwa kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge 10 walichangia kwa maandishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kutumia nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia Hoja ya Waziri Mkuu. Ningependa kuwataja majina yao, lakini kutokana na ufinyu na muda naomba uridhie nisiwataje na badala yake majina yao yaingizwe kwenye Hansard.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wametoa ufafanuzi wa hoja nyingi zilizowawasilishwa na Waheshimiwa Wabunge wakati tukiendelea na mjadala wa Hoja ya Waziri Mkuu. Sikusudii kuzirudia, lakini nataka nishukuru kwa michango yao tena na kwamba tutaendelea kuzifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilihakikishie Bunge lako Tukufu kuwa Waheshimiwa Mawaziri wataendelea kufafanua zaidi baadhi ya hoja zilizoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge kwenye mjadala huu wakati wakiwasilisha hoja za bajeti za sekta zao. Kadhalika kama ilivyo ada Serikali itatoa ufafanuzi zaidi kuhusu hoja zilizosalia kwa maandishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Waheshimiwa Wabunge wanavyofahamu kwamba tayari tumetimiza miaka mitatu ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni jambo la kujivunia kuwa katika kipindi hicho cha miaka mitatu ya uongozi wake Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mambo makubwa kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa Taifa letu. Sisi sote ni mashahidi kwamba amekuwa kinara katika Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020. Mheshimiwa Rais wakati wote amekuwa akionyesha busara, uhodari mkubwa, uzalendo, usikivu, uwajibikaji na kuwa mfano wa kuigwa ndani na nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kutumia nafasi hii kuungana na Watanzania wenzangu kumshukuru kwa uzalendo wake na namna anavyojitoa kulitumikia Taifa letu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali. Miradi hiyo inahusisha Sekta za Maji, Elimu, Afya na Miundombinu ambayo niliieleza wakati nilipokuwa nawasilisha hoja yangu. Naomba sasa nieleze kwa uchache mafanikio mengine yaliyopatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, ni kuleta maridhiano ya kisiasa, amani na utulivu wa kidemokrasia hapa nchini. Niendelee kutokuwa na mashaka na Waheshimiwa Wabunge wenzangu watakubaliana nami kuwa Mheshimiwa Rais ni kinara katika kuimarisha demokrasia vilevile haki za binadamu na utawala bora. Katika kipindi hiki cha uongozi wake tumeshuhudia utekelezaji wa falsafa yake ya 4R (Reconciliation, Resilience, Reform and Rebuilding). Kwa lugha ya Kiswahili ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Mabadiliko ambayo kwa hakika yamekuwa chachu ya kuimarisha siasa za ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na utashi wake, mwelekeo wa mitazamo na uendeshaji wa masuala ya kisiasa umebadilika na kuchagiza siasa za kistaarabu. Sote ni mashuhuda kuwa nchi yetu inaendelea kuwa na mshikamano, amani na umoja wa kitaifa. Hii inatokana na msisitizo wake kuhusu utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu, utawala bora na demokrasia.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza masuala ya demokrasia kwa vitendo, tumeshuhudia maboresho mbalimbali ya upande wa mifumo, sheria na uendeshaji wa shughuli za kisiasa hapa nchini. Licha ya hayo tumeshuhudia pia uwepo wa fursa zaidi za mijadala na maridhiano miongoni mwa makundi ya wadau wa demokrasia na masuala ya siasa hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni maboresho ya mfumo wa utoaji haki na Taasisi za Hakijinai katika kuhakikisha mfumo wa utoaji haki unaboreshwa. Mnamo tarehe 31 Januari, 2023, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliunda Tume Maalum aliyoipa jukumu la kushauri namna njema ya kuboresha mfumo wa utendaji kazi katika taasisi zinazohusika na hakijinai.
Mheshimiwa Naibu Spika, tume hiyo ilipokea maoni kutoka kwa wananchi na wadau wengine wa hakijinai na kutoa mapendekezo ya maboresho yanayohitajika kufanyika. Tangu tume ilipowasilisha mapendekezo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za maboresho ya mfumo wa utoaji wa hakijinai, ikiwemo kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa Taasisi za Hakijinai. Licha ya hayo Serikali inaendelea kufanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa kwa lengo la kuhakikisha kuwa, wananchi wanapata haki zao kwa wakati ili waweze kuendelea kufanya shughuli za maendeleo yao binafsi na Taifa zima kwa ujumla. Hii ndiyo dhamira ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kukidhi kiu na matarajio ya wananchi katika utoaji wa hakijinai kuanzia hatua ya uchunguzi, ukamataji watuhumiwa hadi utoaji wa hukumu yenyewe pale inapofanyika haki mahakamani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, ni matumizi ya TEHAMA na Lugha ya Kiswahili mahakamani. Katika hatua nyingine Serikali ya Awamu ya Sita, imeendelea kufanya jitihada kubwa ya kuimarisha matumizi ya TEHAMA ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia kutokana na mapinduzi ya nne ya viwanda hapa duniani. Jitihada hizo zimeanza kuleta mafanikio katika utendaji wa Serikali kwa kuunganisha Serikali yote (Wizara, Idara, Wakala na Taasisi zake) ili ziweze kusomana kwa kimfumo. Tumeanza kupata mafanikio tukianza na Mahakama ya Tanzania, ambapo mifumo mbalimbali ya TEHAMA imejengwa ili kurahisisha na kuhakikisha utoaji wa haki kwa wananchi unaimarika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mifumo hiyo ni pamoja na mfumo wa usajili, uendeshaji na usimamizi wa mashauri kwa ajili ya kurahisisha, kuharakisha na kuokoa muda wa mwenendo wa shauri mahakamani. Mfumo mwingine ni wa unukuzi na tafsiri ya mienendo ya mashauri mahakamani kwa lengo la kuwa na suluhu ya kudumu, ili kuwawezesha Waheshimiwa Majaji na Mahakimu kuondokana na adha ya kuandika kwa mkono mwenendo wa mashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni hatua kubwa sana katika mfumo huu unaorekodi sauti na kupeleka kwenye maandishi. Vilevile unaweza kutafsiri Lugha ya Kiswahili au Kiingereza kulingana na uhitaji na kwa upande mwingine Kanuni za Mahakama zimeanza kutafsiriwa sambamba na uandaaji wa mihtasari ya hukumu katika Lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wananchi kuelewa mwenendo wa mashauri yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni mafanikio kwenye Sekta ya Uzalishaji ambako kuna kilimo, mifugo, uvuvi na viwanda. Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuinua sekta ya uzalishaji. Kama tunavyofahamu uzalishaji kupitia Sekta ya Kilimo umeendelea kuongezeka na kuiwezesha sekta hii kuchangia 26% ya Pato la Taifa kwa mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, jitihada zinazofanywa na Serikali ni katika kuhakikisha kuwa, Sekta ya Kilimo inaendelea kutoa mchango mkubwa katika upatikanaji wa ajira, malighafi za viwandani, kuleta fedha za kigeni kutokana na mauzo ya nchi za nje, pamoja na kulihakikishia Taifa letu usalama wa chakula. Jitihada mbalimbali zinazofanywa zimewezesha nchi yetu kuwa na utoshelevu wa chakula kwa 124%.
Mheshimiwa Naibu Spika, sina shaka Waheshimiwa Wabunge watakubaliana na mimi kuwa, Mheshimiwa Rais amefanya jitihada kubwa kuimarisha Sekta ya Uvuvi. Utekelezaji wa ujenzi wa Mradi mkubwa wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko unaogharimu zaidi ya bilioni 289.5 ni kielelezo tosha cha dhamira yake njema ambayo pia Mheshimiwa Rais ameionesha hadharani. Tayari ameshatoa ridhaa ya matumizi ya shilingi bilioni 106.2 za kuendeleza ujenzi wa bandari hiyo, ambayo itachochea ukuaji wa Sekta ya Uvuvi na kuongeza pato la Wananchi kama ilivyoelezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 – 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Sekta ya Mifugo, vilevile tumeshuhudia ikiendelea kuimarika na kuwezesha kutoa ajira kwa wananchi milioni 4.5. Aidha, kutokana na jitihada zilizopo mchango wa sekta katika pato la Taifa umefikia 7.1% kwa mwaka. Uwekezaji kwenye viwanda umeongezeka, ili kuzalisha bidhaa kwa mahitaji ya ndani na kupata masoko ya bidhaa nje ili kuongeza pia pato la kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo Mheshimiwa Rais amelieleza ni mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Amelifafanua vizuri zaidi, lakini nataka nieleze tu kwamba, Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kupambana na tatizo la dawa za kulevya hapa nchini. Hii inatokana na ukweli kwamba, kundi la vijana ambao ni nguvukazi ya Taifa linalotarajiwa kuwakilisha maendeleo, ndiyo linaathirika zaidi na matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini. Licha ya tatizo la dawa za kulevya kuendelea kuwepo hapa nchini, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya katika kipindi kifupi, imefanya kazi kubwa sana. Tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa hatua anazozichukua za kuiwezesha mamlaka hii kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mamlaka inafanya kazi kubwa na nzuri, katika hili natoa rai kwa Taasisi za Serikali, Taasisi Binafsi, Mashirika ya Dini, Taasisi zisizokuwa za Serikali na Washirika wa Maendeleo na wananchi wote kwa ujumla, kutoa ushirikiano kwa mamlaka ili iweze kutimiza majukumu yake. Vilevile namwomba kila mmoja kwa nafasi yake, ashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa ya kulevya. Taasisi inaendelea kufanya kazi nzuri ya kudhibiti uzalishaji, usafirishaji, uuzaji na utumiaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza sana pia Waheshimiwa Wabunge kwa michango waliyoitoa kuhusu udhibiti na mapambano dhidi ya madawa ya kulevya, umoja ni ushindi. Hivyo basi, Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wananchi wote tushirikiane katika mapambano ya dawa za kulevya, kwa pamoja tutashinda, mapambano bado yanaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nieleze kidogo juu ya utekelezaji wa sera na fursa za kujikwamua kiuchumi. Serikali imeendelea kutekeleza sera mbalimbali za uwezeshaji wa makundi maalum ya wanawake, vijana na wenye ulemavu. Lengo likiwa ni kuhakikisha makundi haya yanashiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi hapa nchini. Utekelezaji wa sera hizo unafanywa kupitia Mfuko wa Uwezeshaji Kiuchumi, ambayo imeendelea kunufaisha makundi yote, wakiwemo wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2023/2024, fedha kiasi cha shilingi bilioni 743.7 zimetolewa kwa wanufaika zaidi ya milioni sita kupitia Mifuko na Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Katika utekelezaji wa sera ya ushirikishwaji Watanzania kwenye miradi ya kimkakati na uwekezaji nchini, wanawake na vijana wameendelea kunufaika kupitia miradi ya kimkakati na uwekezaji. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, jumla ya Watanzania 162,968 wamenufaika na ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuratibu masuala ya uzalishaji wa fursa za ajira nchini kwa kujenga mazingira wezeshi kwa wawekezaji na kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, fursa za ajira 2,489,136 zimezalishwa sawa na wastani wa ajira mpya 829,712 kwa mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuwezesha vijana ili waweze kujiajiri kushiriki kwenye shughuli za maendeleo na kuchangia pato la Taifa. Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, kiasi cha shilingi bilioni 3.19 kimeshatolewa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, ambazo zilitumika kutoa mikopo kwa ajili ya kuwezesha miradi 148 katika Sekta za Kilimo, Viwanda na Biashara katika halmashauri 62.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imetoa mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi, kurasimisha na kuendeleza biashara kwa vijana katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI hivi karibuni itatoa taarifa ya mfumo utakaotumika kutoa mikopo ya 10% kutoka katika halmashauri zetu nchini ili wajasiriamali waweze kuendesha shughuli zao za kibiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la utunzaji wa mazingira, sote tunatambua kuwa uhifadhi wa mazingira una umuhimu mkubwa katika maisha yetu ya kila siku, kwa kuwa unatuwezesha kupata mahitaji muhimu ikiwemo maji, chakula, madawa, malighafi za viwandani, pamoja na nishati ya umeme itokanayo na maji. Ni ukweli usiopingika kuwa upatikanaji wa mahitaji haya, unaharakisha maendeleo yetu ya kiuchumi na kijamii, hivyo, tuna kila sababu ya kutunza mazingira ili nayo yaweze kututunza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu huo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa faida yetu na vizazi vijavyo. Vilevile, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mara kwa mara amekuwa akitukumbusha kuhusu utunzaji wa mazingira yetu. Nitumie nafasi hii kuungana na viongozi wetu, kuzungumza kwa uchache kuhusu uhifadhi wa mazingira hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na uharibifu mkubwa wa mazingira ambao kimsingi unasababishwa na ukataji wa miti hovyo kwa matumizi ya nishati. Kilimo kisicho endelevu kinachofanyika kwa kukata miti na kuchoma mashamba ikiwa ni njia ya kurahisisha maandalizi ya shamba. Sababu nyingine ni ufugaji holela usiozingatia uwezo wa eneo la malisho, ambao umesababisha mifugo kuharibu ardhi na maeneo mengine yaliyohifadhiwa ikiwemo vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kuwa athari za uharibifu wa mazingira ni mbaya kwa kuwa, huathiri masuala ya kijamiii na kiuchumi mathalani mara kadhaa tumeshuhudia vifo vya mifugo kutokana na ukame na uhaba wa maji, vilivyotokana na mabadiliko ya tabianchi yaliyosababishwa na uharibifu wa mazingira. Vilevile mvua nyingi kupita kiasi zimeendelea kusababisha athari kubwa nchini, ikiwemo mafuriko, vifo, na uharibifu wa miundombinu mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu wa uhifadhi wa mazingira, nitumie fursa hii kusisitiza masuala yafuatayo:-
(i) Viongozi wote kuanzia ngazi za vijiji hadi mikoa, wasimamie kikamilifu utunzaji wa mazingira na suala hili liwe ajenda ya kudumu katika vikao vyote katika ngazi hizo; (Makofi)
(ii) Viongozi wa Mikoa na Wilaya wasimamie utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu athari za kuchoma misitu hovyo, pia kufuga bila kuangalia uwezo wa maeneo ya kulishia, kufanya shughuli za kilimo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na kuondokana na tabia ya kukata miti hovyo;
(iii) Halmashauri zote nchini, zisimamie kikamilifu sheria ndogo za uhifadhi wa mazingira na kuwachukulia hatua wale wote wanaofanya uharibifu wa mazingira yetu;
(iv) Taasisi za Uhifadhi wa Misitu (TFS) na halmashauri ziandae vitalu vya miti inayoendana na ikolojia ya maeneo yao, kuigawa kwa wananchi na kuhakikisha inapandwa na kukua. Hatua hii iendane sambamba na kusimamia upandaji wa miti kwa kila kaya. Vilevile TANROADS na TARURA wahakikishe wakandarasi wanapanda miti pembezoni mwa barabara katika kila mradi wa ujenzi wa Barabara. Kwa kufanya hivyo itasaidia upandaji na utunzaji wa mazingira; (Makofi)
(v) Wananchi tuendelee kushirikiana na Serikali katika uhifadhi wa mazingira ili kuepusha madhara yanayotokana na uharibifu wa mazingira ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuzungumzia mabadiliko ya hali ya hewa. Kasi ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani inaendelea kuongezeka kila mwaka na athari zake zimekuwa kubwa. Tathmini ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani, limeonesha kuwa wastani wa ongezeko la joto kwa 2023 ulifikia nyuzi joto 1.4 kwa kipimo cha selsiasi (Celsius) na kuvunja rekodi ya kuwa mwaka wenye joto kubwa zaidi katika historia ya dunia. Kwa upande wa Tanzania, wastani wa ongezeko la joto kwa mwaka 2023 ulifikia nyuzi joto 1.0 kwa kipimo cha selsiasi. Pia ulivunja rekodi kwa kuwa mwaka wenye joto kubwa zaidi katika historia ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ongezeko la joto limesababisha uwepo wa El-Nino ambayo imeambatana na mvua kubwa na mafuriko hapa nchini. Oktoba hadi Desemba, 2023 kulikuwa na ongezeko kubwa la mvua, ambapo jumla ya milimita 534.5 zilipimwa ikilinganishwa na milimita 227.2 kwa mwaka 2022, ikiwa ni ongezeko la 135.5%. Vilevile ongezeko hilo la mvua limeshuhudiwa katika kipindi cha Januari hadi Aprili, 2024 na kwa mujibu wa Taasisi ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema mvua zitaendelea kunyesha hadi mwezi Mei, 2024 kwenye Mikoa ya Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi, Ukanda wa Mikoa ya Kusini mwa Tanzania na Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo kwa nchi mbalimbali duniani, nchi yetu imeendelea kupata mvua nyingi zaidi ya wastani kutokana na mabadiliko ya tabianchi, ambayo yamesababisha maafa mbalimbali. Maafa hayo ni pamoja na vifo, uharibifu wa mazao, makazi, mali za wananchi, miundombinu kama vile barabara, madaraja na reli. Kama mnavyofahamu maeneo mengi yameathirika na mvua. Mikoa ambayo imeathirika kwa sasa ni Mikoa ya Arusha, Lindi, Manyara, Kigoma, Morogoro, Pwani na Mbeya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya Maafa Kitaifa kwa kushirikiana na Kamati za Maafa za Mikoa na Wilaya, zimeendelea kuchukua hatua mbalimbali kurejesha hali katika maeneo yaliyoathirika ikiwemo Wilaya ya Rufiji, eneo la Muhoro; Wilaya ya Kibiti, eneo la Delta; Newala, Lindi Mjini, Liwale, Arusha, eneo la Kisongo; Mkoani Morogoro Malinyi, Wilaya ya Kilombero; kule Mrimba maeneo ya Masagati na Utengule na kule Mbeya kulikotokea maporomoko ya udongo kutoka milimani eneo la Kawetere.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hizo ni pamoja na kutoa misaada ya kibinadamu kwa waathirika, kurejesha miundombinu iliyoathirika, kutoa elimu kwa jamiii kuhusu kujikinga, kuchukua tahadhari na kuendelea kufanya tathmini ya kina ya athari na vyanzo vya maafa hayo. Kamati za Maafa za Kitaifa kwa kushirikiana na Kamati za Maafa za Mikoa na Wilaya, zinaendelea kufanya tathmini kwenye maeneo yote yaliyopata athari.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuchukua hatua kadhaa tena za haraka na za dharura ikiwemo uokoaji, kutoa chakula, maji, makazi ya muda, dawa, mbegu na huduma za unasihi, katika maeneo yaliyopata athari kubwa za mvua ambazo zinaendelea hivi sasa. Tunatoa pole kwa ndugu zetu walioathirika na mvua hizo na naomba wananchi wote kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua kubwa zinazoendelea kunyesha hapa nchini. Niwasihi sana wananchi, waendelee kuwa na subira pale wanapoona maji mengi yanapita hususani barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa waendesha vyombo vya moto vya usafiri na wavuka kwa miguu, kuchukua tahadhari ya kutovuka mahali popote wanapoona maji yanakatiza barabara, ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kama ambavyo imetokea eneo la kisongo kule Mkoani Arusha, kwa gari la wanafunzi kutumbukia kwenye shimo, kwa dereva kupinga, kukaidi na kupita kwenye eneo ambalo maji yanavuka bila kujiridhisha kama eneo hilo lina maporomoko au la.
Mheshimiwa Naibu Spika, TANROADS, TARURA na Shirika la Reli waendelee kuchukua hatua za haraka wakati uharibifu wa miundombinu ya barabara na reli unapoendelea kujitokeza. Hatua hizo ziendelee sambamba na kutoa taarifa kwa watumiaji wa miundombinu hiyo, kuweka alama za tahadhari na kuweka kambi maalum za matengenezo katika maeneo yaliyoathirika zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizikumbushe mamlaka za upangaji kuzingatia mipango ya matumizi bora ya ardhi pamoja na kusimamia upangaji wa makazi kwa kuzingatia sheria ya mipango miji. Aidha, Wizara ya Maji kwa kushirikiana na sekta mtambuka, waendelee na mkakati wa ujenzi wa miundombinu ya kuvuna maji ya mvua ikiwemo mabwawa na kuyahifadhi kwa ajili ya huduma za jamii na uzalishaji ikiwemo kilimo, pia majosho ya kunyweshea mifugo ili kupunguza athari za uharibifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwakumbushe watendaji wote wa Serikali kusimamia uratibu wa maafa kwa kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022 na kanuni zilizopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na Kukabiliana na Maafa wa mwaka 2022 umeweka bayana majukumu ya kukabiliana na maafa kwa kuanzia ngazi ya kijiji au mtaa, kata, shehia, wilaya, mkoa na Taifa, kupitia Kamati za Usimamizi wa Maafa zilizopo katika ngazi husika. Hivyo basi, nasisitiza kuwa, Kamati za Usimamizi wa Maafa katika ngazi zote ziendelee kuweka mipango madhubuti ya kutekeleza majukumu ya usimamizi wa maafa katika ngazi hizo pamoja na kutoa elimu kwa wananchi ya kutoishi maeneo ya mabonde ili kuepusha kutokea kwa maafa kama ambavyo sasa tunashuhudia kwenye maeneo yaliyoathirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuzungumzia mwelekeo na mwenendo wa maandalizi ya Dira Mpya ya Taifa ya Maendeleo. Tarehe 3 Aprili, 2024 wakati nawasilisha Hotuba yangu ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 na mwelekeo wa kazi zake kwa mwaka wa fedha 2024/2025, nililieleza Bunge lako Tukufu kuhusu mchakato wa maandalizi ya Dira Mpya ya Maendeleo ya Taifa. Niruhusu niwapitishe Waheshimiwa Wabunge katika mafanikio yaliyopatikana katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 pamoja na maandalizi ya Dira Mpya ya Taifa ya Maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025, umewezesha Taifa letu kuwa na mafanikio yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ni kuboresha hali ya maisha ya Watanzania ikiwemo utoshelevu wa chakula, kuimarika kwa huduma za jamii hususan afya, elimu na upatikanaji wa maji, ongezeko la idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi na utawala katika maeneo mbalimbali hapa nchini, kuongezeka kwa umri wa kuishi kwa Watanzania na kupunguza kiwango cha umaskini wa kutupwa kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuimarika kwa mazingira ya amani, usalama na umoja, ikiwemo kuzingatiwa kwa utii wa sheria na utawala wa kisheria kulikowezesha kupungua kwa matukio ya uhalifu wa aina mbalimbali, hususan mauaji, wizi wa watoto, unyang’anyi wa kutumia silaha, wizi katika barabara kuu, uhalifu wa kifedha na dawa za kulevya. Yale ambayo yanajitokeza yanaendelea kuchukuliwa hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuimarika kwa utawala bora ikiwemo utaratibu wa makabidhiano ya kiuongozi na kiutawala kwa amani na utulivu. Kuongezeka kwa kiwango cha haki za msingi za binadamu na kuendelea kupungua kwa kiwango cha rushwa hapa nchini. Kuwepo jamii inayoelimika vema na inayojifunza ambapo idadi ya Watanzania wanaopata elimu rasmi imeongezeka katika ngazi mbalimbali ikiwa ni ngazi ya elimu ya msingi, sekondari na vyuo vikuu. Aidha, kumekuwa na ongezeko kubwa la nyenzo na fursa za kuwezesha kuendelea kujifunza kupitia uwepo wa majukwaa ya mitandao ya kijamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, uchumi wetu kuweza kukabiliana na ushindani katika nchi nyingine kulikochangia kuongezeka kwa mpango wa pamoja wa Sekta ya Viwanda, Ujenzi na Uzalishaji wenye pato la Taifa. Kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi kupitia Sekta Ndogo ya Uzalishaji na kuhimili kiwango cha mfumuko wa bei kwa chini ya tarakimu moja. Ongezeko la pato la Taifa kwa mwaka kwa wastani wa 6.7%, kati ya mwaka 2000 na 2021, kuimarika kwa miundombinu ya msingi na ya kiuchumi, hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, huduma za mawasiliano na huduma za umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, matarajio yetu kwa Dira Mpya ya Taifa ni mafanikio yaliyopatikana yanayotokana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 ambayo itafikia tamati ifikapo Juni, 2026. Sasa, tuko kwenye mchakato wa maandalizi ya Dira Mpya ya Taifa ya Maendeleo inayotarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2026/2027. Ni matarajio yetu kuwa, utekelezaji wa Dira Mpya utawezesha nchi yetu kupiga hatua zaidi kimaendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Dira Mpya pamoja na mambo mengine itazingatia masuala muhimu yafuatayo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kufungamanisha ukuaji wa uchumi na sekta za uzalishaji; Kuimarisha upatikanaji wa data kwa sekta isiyo rasmi ili kuweza kurasimisha shughuli na kutambua mchango wake katika ukuaji wa Uchumi; Kuboresha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini; Kuwepo kwa utaratibu jumuishi wa programu mbalimbali za utekelezaji wa Dira Mpya; Kutoa kipaumbele katika ufanisi wa Mashirika ya Umma wakati wa utekelezaji wa Dira Mpya; Kuimarisha ushiriki wa Sekta Binafsi ndani na nje ya nchi pamoja na kuwawezesha wenyeji kuwa na utayari wa kupokea na kushirikiana na wageni wanaokuja kuwekeza na kufanya biashara hapa nchini; na Kuweka mkazo zaidi katika suala la Maadili ya Taifa na kubainisha mapema viashiria hatarishi na namna ya kukabiliana navyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara nyingine natumia nafasi hii kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maandalizi ya Dira yetu Mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuzungumzia Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano. Wakati tunaelekea kutimiza miaka 60 ya Muungano wetu, sote ni mashahidi kwamba, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umedumu na umekuwa ni wa kipekee na wa kuigwa Barani Afrika na duniani kwa ujumla. Vilevile, sote tunatambua kwamba, jitihada kubwa zimefanyika katika kulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni Tunu ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, matunda ya Muungano wetu yanajumuisha kuimarika kwa utaifa, umoja, amani, utulivu na hali ya maisha ya wananchi kutokana na ukuaji wa uchumi wa pande zote mbili za Muungano. Aidha, kuingiliana kwa kuoleana pia nako kumeimarika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuendelea kuutunza Muungano wetu ulioasisiwa na kuenziwa kwa manufaa ya Watanzania kwa kizazi cha sasa na baadaye, Serikali ilizindua kitabu kinachoelezea chimbuko la historia hiyo, misingi na maendeleo ya Muungano. Vilevile, elimu kwa umma kuhusu muungano imekuwa ikitolewa kupitia vipindi vya redio na television. Tumepeleka magazetini semina, warsha, makongamano, Maonesho ya Kitaifa, ziara za viongozi, machapisho mbalimbali na mitandao ya kijamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo furaha kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa terehe 26 Aprili, 2024, nchi yetu itaadhimisha Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Maadhimisho hayo yataongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yatakayofanyika Jijini Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, matukio yaliyopangwa kufanyika ni pamoja na uzinduzi wa Maadhimisho ya Sherehe za Muungano ambayo yalifanyika tarehe 14, jana, kule Zanzibar. Matukio mengine ni uzinduzi wa maonesho ya Muungano yatakayofanyika tarehe 19 Aprili katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam. Kutakuwa na Tukio la Dua na Sala ya kuliombea Taifa letu siku ya terehe 22 Aprili, 2024 katika Uwanja wa Jamhuri hapa Jijini Dodoma. Natumia fursa hii kuwajulisha Watanzania kuwa, maandalizi yanaendelea vizuri na wote mnaalikwa kushiriki katika matukio hayo muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, matukio hayo ni muhimu katika kuimarisha Muungano wetu, ikiwa ni njia mojawapo ya kuwaenzi waasisi wa Muungano ambao ni Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume. Tunamwomba Mwenyezi Mungu aendelee kuwapa pumziko la amani waasisi hawa wa Muungano wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuzungumzia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wanafahamu kwamba Taifa letu mwaka huu litakuwa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, uchaguzi huu ni muhimu sana kutokana na ukweli kwamba, viongozi wa Serikali za Mitaa ni msingi imara katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Taifa letu. Licha ya hayo, Viongozi wa Serikali za Mitaa ni wasimamizi wa karibu wa shughuli za maendeleo ya wananchi na pia, wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha ulinzi na usalama wa wananchi katika maeneo yao. Kutokana na umuhimu huo, napenda kusisitiza kuhusu masuala yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, ni Watanzania wenzangu bila kujali jinsia watumie haki yao ya Kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa. Wale wenye uwezo wajitokeze kugombea nafasi za uongozi pamoja na kushiriki kikamilifu siku ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Watanzania wote wajitokeze kwa wingi ili kushiriki katika hatua zote za uchaguzi huo, ikiwemo Maboresho ya Daftari la Mpiga Kura.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbili, ni viongozi wa Serikali watumie kila fursa zikiwemo semina, warsha na mikutano kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika uchaguzi huo. Waweke mkakati wa kutoa elimu kwa umma ili waweze kuwajulisha wananchi kufahamu haki zao na wajibu wao katika kuchagua viongozi wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, ni wamiliki wa vyombo vya habari waweke mkakati wa kuhamasisha umma wa Watanzania kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Waandae makala maalum na vipindi maalum kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie utambuzi au kutambua mchango wa watumishi wa umma. Watumishi wa umma wana mchango mkubwa katika kutafsiri na kutekeleza maono ya Mheshimiwa Rais. Mafanikio tunayoshuhudia sasa katika utekelezaji wa mikakati ya maendeleo ya Taifa ni kutokana na kazi nzuri inayofanywa na watumishi wa umma. Natumia nafasi hii kuwapongeza kwa dhati watumishi wote wa umma kwa kujitoa kwao na kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo, nawakumbusha watumishi wenzangu kuimarisha ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi na kutekeleza kikamilifu wajibu tulionao. Watumishi wote tujikite katika kutatua changamoto na kero za wananchi, tuwafuate kwenye maeneo yao tukawasikilize na kutoa majawabu yanayohitajika. Kwa kufanya hivyo wananchi wataishi kwa amani na utulivu na kuendeleza shughuli za uzalishaji mali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nifafanue baadhi ya hoja ambazo zilichukua nafasi kwenye mijadala yetu. Hoja ya kwanza ilitolewa na Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mheshimiwa Kasalali Emmanuel Mageni, Mbunge wa Sumve, Mheshimiwa Ester Amos Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum na Mheshimiwa Janejelly Ntate James, Mbunge wa Viti Maalumu. Hoja ilikuwa ni Serikali kufanya maboresho ya ulipaji wa mafao ya wafanyakazi kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii na kwamba, Serikali iongeze wigo wa utoaji elimu ya kanuni mpya za mafao kwa watumishi, kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa kanuni mpya ya ulipaji wa mafao iliyoanza kutumika tarehe Mosi Julai, 2022 kwa kuzingatia tathmini ya uhimilivu na uendelevu wa Mfuko iliyofanyika katika kipindi husika. Serikali imesikia ushauri na kupokea maoni mbalimbali ya wadau wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, Vyama vya Waajiri na wafanyakazi wenyewe. Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha mafao kwa wastaafu na itaendelea kufanya tathmini ya kuzingatia sheria za kazi ili tuweze kufikia hatua nzuri ambayo haitazua malalamiko mengi. Aidha, kuhusu utoaji wa elimu ya kanuni za mafao kwa watumishi, Serikali itaendelea kutoa elimu ya uhifadhi wa jamii ikiwemo na mafao kwa watumishi kupitia njia mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, natumia fursa hii kumtaka Waziri wa Kazi na Ajira asimamie kuongeza wigo wa utoaji wa elimu ya mafao kwa watumishi kwa lengo la kujenga uelewa wa kutosha pamoja na mjadala ambao wanaendelea nao juu ya uwepo wa kikokotoo ambacho sasa kimekuwa kinatolewa ushauri na makundi mbalimbali ya wadau.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ilitolewa na Mheshimiwa Ahmed Shabiby, Mbunge wa Jimbo la Gairo, Serikali ihakikishe inaweka mikakati ya kuwezesha upatikanaji wa vyanzo vingi vya mapato ili kuwezesha upatikanaji wa Bima ya Afya kwa wananchi vijijini. Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023, imeanzisha Mfuko kwa ajili ya kugharamia Bima ya Afya kwa watu wasio na uwezo na kubainisha vyanzo vya fedha vya Mfuko huo. Serikali itaendelea kupokea mapendekezo ya uendeshaji wa mfuko, ikiwemo vyanzo vya mapato na kufanya maboresho kadri inavyofaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya wanyamapori kuvamia maeneo ya wananchi pamoja na mauaji ya watu kwenye hifadhi, iliyotolewa na Mheshimiwa Esther Nicholaus Matiko, Mbunge wa Viti Maalum. Serikali inatambua uwepo wa changamoto ya wanyamapori kuvamia makazi na mashamba na kusababisha madhara kwa wananchi wanaoishi karibu na hifadhi; madhara hayo ni pamoja na ulemavu, vifo na uharibifu wa mali. Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu ya kukabiliana na wanyama waharibifu, uanzishaji wa Vituo vya Ulinzi kwa Maafisa Wanyamapori. Kwa upande mwingine, kumekuwa na changamoto ya baadhi ya wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi na kusababisha migogoro baina yao na Askari wa Hifadhi, changamoto ambayo pia imekuwa ikisababisha majeruhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, natumia fursa hii kuwakumbusha wasimamizi wa hifadhi kuzingatia taratibu wakati wa kushughulikia changamoto za uvamizi wa hifadhi. Kwa upande mwingine, nawasihi wananchi kuheshimu mipaka ya maeneo yaliyohifadhiwa na kuacha tabia ya kuingia hifadhini kiholela, kuingiza mifugo, kufanya shuguli za kilimo ndani ya hifadhi na uwindaji haramu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa ni ya Mheshimiwa Kasalali, Mbunge wa Sumve ya utekelezaji wa ahadi za Mawaziri. Serikali inaendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 - 2025 na ahadi za viongozi katika maeneo mbalimbali kupitia mipango ya bajeti ya kila mwaka. Utekelezaji unafanyika na unaendelea mpaka mwezi Juni, 2025 ambapo ndio mwisho wa mwaka huu wa fedha kwa hiyo, ahadi zote ambazo zimetolewa zinatarajiwa kutekelezwa katika kipindi hiki kwa zaidi ya 90%.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hitimisho. Wakati nahitimisha Hoja hii ya Waziri Mkuu, naomba nitumie nafasi hii kuzungumzia masuala yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mafanikiko kwenye sekta ya michezo; sote ni mashahidi, katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita...
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naongeza dakika 30.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya michezo imepata mafanikio makubwa. Michezo inapendwa na Watanzania walio wengi na imekuwa ni chachu ya maendeleo na nguzo muhimu kwa ustawi wa jamii pamoja na kuitangaza nchi yetu Kimataifa na kuliletea sifa Taifa letu. Wabunge watakubaliana nami kwamba, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni mpenda michezo na amekuwa mstari wa mbele kusimamia ukuaji wa Sekta ya Michezo, maono na maelekezo yake yameleta mchango mkubwa na mafanikio katika sekta hii. Aidha, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa kinara katika kuongeza hamasa kwa wanamichezo wetu. Suala ambalo limechangia kuimarika kwa nafasi ya Taifa kwenye michezo mbalimbali ya Kimataifa hususan kwenye ngumi, riadha na mpira wa miguu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nampongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais kwa hamasa kubwa anayoitoa katika Sekta ya Michezo pamoja na kuhamasisha wadau mbalimbali kuchangia timu zetu, ili ziweze kufanya vizuri. Kama mtakumbuka, kupitia “Goli la Mama” mafanikio makubwa yamepatikana katika Mchezo wa Mpira wa Miguu. Katika hili, Mama amefanya mambo makubwa na kwa lugha ya sasa, “Ameupiga Mwingi na Apewe Maua Yake”. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, jitihada za Mheshimiwa Rais zimewezesha Vilabu vyetu vya Mpira wa Miguu kuendelea kung’ara Kimataifa. Katika Msimu wa Ligi wa 2023/2024, Tanzania imekuwa nchi pekee iliyoingiza timu mbili kwenye hatua ya Robo Fainali ya Mashindano ya Klabu Bingwa ya Afrika. Hatua hii ni ya kupongezwa na kujivunia kama Taifa. Hongera sana wachezaji wetu, hongera sana viongozi wa vilabu, hongera sana timu zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, natumia nafasi hii kuvipongeza Vilabu vya Yanga na Simba kwa kufikia hatua ya robo fainali. Nawapongeza sana kwa kucheza mpira wa viwango vya hali ya juu. Michuano yote ilikuwa mikali na kwa yeyote anayefahamu mchezo wa mpira wa miguu atakubaliana nami kwamba, wachezaji wetu walionesha umahiri mkubwa, viwango vya hali ya juu na waliweza kukonga mioyo ya washabiki wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, narudia kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao, ama kwa hakika wanalitendea haki jukumu la kuishauri Serikali, la kuwawakilisha wananchi pamoja na kuhakikisha kwamba, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 - 2025 imetekelezwa kama ilivyoelekezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, natumia fursa hii kutoa rai kwa Watanzania wote kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Serikali yake. Dhamira ya Mheshimiwa Dkt. Mama Samia ni safi ambayo ni kuwaletea maendeleo ya haraka Watanzania wote. Jitihada kubwa anaendelea kuzifanya hivyo basi, Watanzania wote tumpe ushikiano unaohitajika ili aweze kufanikisha utekelezaji wa maono, mipango na mikakati ya kuinua ustawi wa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo yote, sasa naomba Bunge lako Tukufu liridhie na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zilizo chini yake na Mfuko wa Bunge kama ilivyowasilishwa katika Hoja yangu ya tarehe 3 Aprili, 2024.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)