Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sina budi kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote wa Wizara hizi pamoja na Wenyeviti wa Kamati na Mheshimiwa Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya ndiyo tukaweza kutulia kwenye Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka kuzungumzia kuhusu vifaa vya kijeshi vinavyotaka kuingia nchini kupitia kwenye bandari zetu, hivi sasa kuna ukakasi. Kamati imekaa muda mrefu na imelizungumza hili jinsi ya kutenganisha vifaa vya kijeshi vinavyoingia katika bandari yetu. Hivi ni vifaa nyeti na vina ushuru mkubwa na vifaa hivi ndiyo roho ya Taifa letu na Watanzania kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado naiomba Wizara iliangalie kwa jicho la pili na itupe mrejesho hata kwenye Kamati, ni kwa vipi wanafanikiwa kuwezesha vifaa hivi kuingia na kuweza kuvitoa bila kuvichanganya na vitu vingine ambavyo havistahili kuwa navyo karibu au kuonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bajeti ya maendeleo ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania; safari hii wamepewa bajeti ndogo ya maendeleo, ambayo ni 35 percent. Jeshi ni chombo cha kuaminika, linahitaji kushughulikiwa na linataka kufanya maendeleo. Maendeleo yakipatikana katika Jeshi, ndiyo maendeleo ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninaiomba Wizara ya Fedha suala hili waliangalie, waweze kuwapatia pesa zilizobakia na waweze kumaliza majukumu yao kwa wakati ili Jeshi letu liweze kufanya kazi zake za maendeleo kwa wakati waliojipangia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo linatisha; jambo hilo ni usafirishaji haramu wa binadamu hasa wanawake na watoto wa Kitanzania, suala hili lipo na linafanya kazi hapa Tanzania. Vijana wetu wanarubuniwa kwamba kuna kazi nchi za nje na anaambiwa utapewa kazi fulani, anakwenda kule kwamba akaifanye kazi hiyo. Kuna ma-agent wa Tanzania wanasimamia masuala hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nina wasiwasi na Idara ya Uhamiaji, kwa sababu wale vijana wanapokuwa wanakwenda katika hizi safari zao za ughaibuni, wanakuwa wana vielelezo kamili na wanajua ninakokwenda kuna manufaa kamili, lakini akifika huko anakuta siyo maadili ya Kitanzania, anatakiwa akajiuze au akafanye kazi ambayo siyo. Anapofika akiliona lile anakuwa hataki kufanya anaambiwa umeshafika, ananyang’anywa passport na anateswa na akionekana mtukutu wanamfungia hata ndani na hawampi chakula. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Serikali nataka mliangalie hili, kwamba vijana wetu wanawake na watoto wanalaghaiwa, wanakwenda nje na wanapotaka kurejeshwa wanakataa kuwarejesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Wizara…
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Fakharia, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Njau.
TAARIFA
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda nimpe taarifa Mama yangu Mheshimiwa Fakharia ambaye anachangia vizuri sana kwamba suala hili limekuwa sugu, lakini pia tatizo ni mchakato wa kutoka hapa. Wale watoto wa kazi wanapotoka hapa kuelekea huko, hakuna ukaguzi wowote unaofanyika na hivyo kuonekana kwamba kuna chain ambayo inatokea hapa nchini kuelekea huko nje. Kwa sababu biashara hii ni kubwa kimataifa, ahsante sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Shomar, unaipokea taarifa hii?
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninaipokea kwa mikono miwili, kwa sababu hili jambo lipo, na linaonekana ingawa limejificha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Wizara ya Mambo ya Ndani, hili suala wameliona na wanalifanyia kazi; lakini ningeomba washirikiane na Wizara ya Mambo ya Nje. Kwa sababu Balozi zetu kule baadhi yetu hawazijui na wale vijana hawana mbinu za kufika kule, utakuta mateso. Ingawa Wizara ya Mambo ya Ndani, imefanya mbinu baadhi wameweza kuwarejesha kwa kutumia mbinu zao za mikakati ili warejee nchini wawaokoe watoto wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija nakuja na swali la Jeshi letu la Magereza. Kwanza nalipa pongezi. Tulikuwa tunapiga kelele hapa ndani kwamba Jeshi la Magereza limerundika wafungwa na watu kule ndani. Hivi karibuni tulikaa tukazungumza nao na kelele za Wabunge, utakuta mrundikano uliokuwepo ndani umepungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa idadi ile iliyokuwa ichukue watu Jeshi la Magereza imeshuka na bado tunaendelea itashuka, maana kuna wengine wanatakiwa kurudishwa kwao hawana fedha hadi Wizara ya Fedha, iwape fedha; baadhi ya wafungwa ambao wameshamaliza muda wao itoke fedha watoke tuweze kupunguza ongezeko la wafungwa ndani ya Magereza. Magereza hongereni, kelele za Wabunge, mmezisikia na kila siku mmekuwa mkiambiwa lakini mmejitahidi kupunguza angalau sasa hivi mtu akija Magereza, anaona uwezo wenu wa kuweza kudhibiti wafungwa na wapi watakaotoka na wingi watakaokubalika kukata upili na wao watoke ili Magereza yetu ikae kwa usafi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie miundombinu ya Magereza. Miundombinu ya Magereza si rafiki kwa sababu Magereza yetu yamejengwa tangu wakati wa ukoloni, na vilevile hayako vizuri. Kutokana na hilo ni lengo moja la Mambo ya Ndani kwa kushirikiana na Idara ya Majeshi na Magereza wabuni mbinu ya kuweza kujenga Magereza mapya tena ya kisasa ili Mtanzania atakapokuwepo Gerezani ajione yuko sehemu salama na aweze kupata mafunzo ili akitoka aweze kufanya kazi ya kuweza kuyaondoa yale aliyokuwa amefanya uhalifu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachana na hilo, hata Sheria za Magereza, sheria zao za kikoloni, nyingi zimefanyika wakati wa ukoloni na hivyo zinahitajika kubadilishwa. Naiomba Wizara ituletee Bungeni sheria ambazo zinaendana na wakati huu wa Tanzania. Ziendane na wakati ili na wale wafungwa wataokuwepo kule Gerezani au wakishahukumiwa au wakishashtakiwa iwe kila kitu kinakwenda kwa mujibu wa taratibu za kisasa za kileo siyo zile tulizoziacha za kikoloni. Kwanza za kikoloni utamkuta mtu ameshitakiwa amehukumiwa lakini hawezi kutekelezewa zile hukumu zilizokuwepo pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache, naunga mkono hoja. (Makofi)