Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igunga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kufungua dimba jioni ya leo kwa ajili ya kuchagia taarifa zilizopo mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja ya Taarifa ya Kamati yetu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, iliyowasilishwa na Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Vita Kawawa na nimpongeze kwa umahili mkubwa ambao ameendelea kuuonesha katika kuisimamia Kamati yetu na kutuongoza vema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nichukue nafasi hii kuzishukuru na kuzipongeza Wizara zilizopo chini ya Kamati yetu tukianza na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. tunazishukuru sana Wizara hizi tatu na taasisi zilizopo chini yao kwa ushirikiano mkubwa ambao wameendelea kutupatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jioni ya leo nitachangaia maeneo manne. Nitachangia upande wa eneo la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Ulinzi na nitachangia kidogo katika Wizara ya Maji ambayo pia taarifa yao ipo mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Upande wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, nitachangia eneo la diplomasia ya kiuchumi, na ningependa jioni hii nijikite zaidi kwenye kipengele cha Utalii wa Mikutano (Conference tourism).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa dunia ilivyo na sisi Tanzania tukiwa sehemu ya dunia, tunakwenda katika mwelekeo wa Utalii wa Mikutano. Hapa kwetu nchini tuna Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) ambacho ndicho kimepewa dhamana kubwa ya kusimamia shughuli za mikutano ya kimataifa inayoendelea hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja ambalo tunahitaji kulifanya ili tuweze kusonga mbele, kwanza hii taasisi yetu ya AICC, jambo moja kubwa ambalo tunaweza tukafanya na kuipa uwezo mkubwa katika kusimamia jambo hili la utalii wa mikutano, initiative kubwa serikali mnaweza kufanya, jambo la kwanza hakikisheni taasisi hii mnaipa mamlaka kamili kama ambavyo Mheshimiwa Rais alivyosema na kutarajia iwe. Kwa sababu, ukiangalia wakati Mheshimiwa Rais akiongea na wakuu wa mashirika ya umma, matamanio yake yalikuwa ni kuhakikisha hii inakuwa ni mamlaka kamili ili iweze kujiendesha na kuweza kuingia katika ushindani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nchi za ukanda wa kusini mwa Afrika, washindani wetu wakubwa ni Afrika Kusini pamoja na Rwanda. Sasa, ukichukulia mfano Afrika Kusini wao wana kitu kinaitwa Durban International Convention Centre, ina uwezo (facilities) za kubeba na kuhudumia watu 10,000 kwa wakati mmoja ndani ya umbali wa kutembea (walking distance) ya dakika tano mpaka kumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Taifa ambao ni washindani bado hatujafikia hatua hiyo. Maana yake ni nini? Tuiwezeshe hii AICC ambayo inaendesha JNICC iliyopo Dar es salaam ipatiwe facilities. Kwa mfano pale Dar es salaam kuna ile hoteli inaitwa Southern Sun ilifungwa kipindi cha COVID, ambayo ipo katika mazingira yaliyopo around kabisa na JNICC. Serikali mfanye jitihada muweze kuipatia hii taasisi JNICC iweze kusimamia yale maeneo, zile hoteli ziweze kutengenezwa katika mfumo wa kuweza ku-host wageni wengi kwa wakati mmoja, tusiendelee kuwa na shughuli katika kumbi zetu za kimataifa na wageni wanakaa mbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta mikutano inafanywa JNICC pale Dar es salaam wageni wanalala Kunduchi, wengine wanakwenda kulala mpaka Chalinze, kule Bagamoyo. Wakati dunia kwa sasa ilipo, sehemu ambayo wageni wanafikia kufanya mikutano ya kimataifa ni suala la kushuka tu na lift au walking distance ya dakika tano na wamefika katika eneo la shughuli. Hii inaweza kusaidia kuchangia sana katika utalii wa mikutano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano. Ukienda pale Rwanda (Kigali International Convention Center), ile pale Kigali International Conventional Centre ina facilities za kuweza kuhudumia Marais 20 kwa wakati mmoja pamoja na details zao zote na ni suala tu la kutoka kwenye lift ghorofani na kushuka chini na kuingia kwenye mikutano. Hata hawachoki, yaani mtu is not bothered, hawezi kupata usumbufu. Facility inapokuwa mbali, kwa mfano Kunduchi au Bagamoyo, mtu anakuja kule Dar es Salaam City Centre unatoka kule unafika kwenye mikutano unaanza kusinzia, unafika kwenye mkutano unalala. Hatuwezi kuvutia utalii wa mikutano kwa mazingira kama haya. Tunawaomba Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje mlisimamie hili wapate facility, na tuachane na yale mambo ya zamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuchukue mfano pale Dar es Salaam around pale Julius Nyerere International Convention Center, kuna viwanja vingi. Kuna ile Botanical Garden ambayo inatumika tu pale kwa shughuli za kuaga kwa mfano misiba ya kitaifa, kama kuna mtu kafiwa. Ile mnaweza mkaihamisha mkaipeleka katika Wizara ya Mambo ya Nje wakapewa hawa watu wa AICC chini ya JNICC wanaunda pale na wanaweka utaratibu inakuwa ni sehemu ya facilities zao. Kama kuna shughuli za kimataifa, au kitaifa kama hii kwenda kuaga pale viongozi, basi mnapewa kwa muda lakini baadaye inaendelea. Tusiache haya maeneo kuendelea kubaki wazi matokeo yake yanaishia kuwa tu sehemu za watu kuoshea magari, parking za magari mjini na viwanja vipo mjini ambavyo ni very prime, ambavyo vinaweza vikafanya kazi kubwa ya kukuza utalii katika nchi yetu na tunaweza tukasonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hii itasaidia katika ukuzaji wa mapato. Niwape mfano, hawa AICC kwa muda mfupi baada ya Mheshimiwa Rais kufanya mabadiliko ya kupeleka Mkurugenzi Mkuu mpya, ndani ya mwaka mmoja wameweza kuongeza mapato kwa zaidi ya asilimia 30. Sasa, tukiwafanyia hiyo development kubwa kama hizi, tukawapa facilities maana yake itasaidia hata kuongeza katika Pato la Taifa na uchumi wetu utakuwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nashukuru sana kwa hii nafasi lakini niishauri Wizara katika hilo jambo ambalo unaweza ukalisaidia liweze kusonga mbele. Sehemu ya pili, ningependa kuchangia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Kumekuwa na changamoto kubwa sana kwenye suala la ajira kwa vijana nchini. Wanapokwenda kwenye ajira hususani za vyombo vya ulinzi na usalama kuna kigezo kimewekwa cha JKT. Sasa, Wizara mje na mpango. Je, wale ambao hawajapita JKT nini kitafanyika watakapokuwa wana-qualify sifa nyingine za ajira? Kwa mfano, umri unamruhusu, taaluma inamruhusu lakini hakwenda JKT. Tunaomba Wizara mliangalie hili na mje na solution ambayo itaonekana hatuwabagui hawa vijana. Kwa mfano, tunaweza tukaamua kwamba, huyu mtu kama ana sifa za ajira za kiumri na kitaaluma, akiajiriwa, kabla hajaingizwa kwenye payroll aende kwanza mafunzo ya JKT kwa miezi sita. Hakuna ambaye atakataa kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni option kuliko sasa hivi unaweka preliminary prerequisite unasema kwamba, ili aajiriwe lazima kwenda JKT. From day one huyu mtoto umekwisha m-exclude. Mtoto amehangaika amesoma miaka 20, mtoto wa mkulima, mtoto wa mfugaji, wazazi wake wamehangaika wamewekeza kwenye maarifa amemaliza chuo kikuu, leo anakuja kuwa excluded kwa kigezo ambacho anaweza aka-qualify hata akiwa ameingizwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisema kwamba ili aingizwe kwenye mfumo, aende kwenye mafunzo kabla hajaanza kulipwa mshahara, hakuna ambaye atakataa hata kama ni mwaka mmoja. Naomba Wizara mtoe solution inayoeleweka katika hili jambo ili tuweze kuwasaidia hawa vijana wa Kitanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ni Wizara ya Mambo ya ndani ambayo inahusika na usalama wa raia na mali zao. Niipongzeze pia wizara nao wanakwenda vizuri. Vilevile, kuna ule mkakati wa kujenga vituo vya polisi Kata, tuwaombe Wizara waongeze kasi. Eneo la pili ni kujenga na kuboresha makazi ya askari wetu. Hili nalo Wizara waliangalie na waweke mkakati mzuri katika kuhakikisha kwamba wanaboresha makazi. Hata ukiangalia mfano mzuri pale Dodoma Central line, wana eneo kubwa ambalo ni very prime. Kwa hiyo, wanaweza wakafanya utaratibu wakaongea na wadau, tukapata na tukawawezesha askari wetu wakapata makazi mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho la nne ambalo ningependa kuchangia kwa kifupi ni Taarifa ya Wizara ya Maji iliyowasilishwa. Mheshimiwa Aweso, ni moja ya Mawaziri ambao sisi vijana wenzie tunamtumia kama role model. Tunamtakia heri katika kusimamia hii miradi. Hata hivyo, tumpe tu tahadhari. Ni kwamba, wakandarasi wengi wanataka kumrudisha kwenye lile suala la miradi chechefu. Alipambana sana kwa miaka mitatu kufuta hii miradi chechefu. Aangalie wasimrudishe nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandarasi anapopewa mkataba wa miezi 18, anafika hatua anamaliza mkataba, unafika muda wa kuhuisha mkataba unaoisha Mradi haujafika hata asilimia 50. Hawa watu watakukwamisha kaka yangu. Jipange, hakikisha unawasimamia vizuri. Kama ulivyo na jitihada siku zote, tunakujua, wewe ni mchapakazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti ninampa mfano mmoja, pale jimboni kwangu Igunga kuna mradi wa bilioni 20, mkandarasi anatakiwa amkabidhi mwezi wa nne lakini mpaka sasa anachezea kwenye asilimia anaitafuta 50. Hawa watu bado hawana dhamira njema kwenye Wizara yake, awabane vizuri wasije kukurudisha nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache nakushukuru sana. Niipongeze Serikali kwa kuendelea kuhakikisha inaisimamia vizuri diplomasia chini ya mwanadiplomasia namba moja Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameifungua nchi na sasa umeona hata kule yuko na Rais wa Poland. Haya yote ni matunda mazuri ambayo naamini tukitumia hii diplomasia yetu itatusaidia katika kukuza utalii wa mikutano na diplomasia yetu itaendelea kukua. Ahsante sana. (Makofi)