Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASYA SHARIF OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni hii ya leo. Mimi nianze kwa kutoa shukrani, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai lakini na afya njema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi na wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kaskazini Pemba, nichukue nafsi hii kumpongeza Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoiendesha nchi hii ya Tanzania, pia nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wetu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Kamati yangu ya Maji na Mazingira na Wajumbe wote wa Kamati kwa namna tulivyoweza kushirikiana katika kujadili mambo mbalimbali. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso na Waziri wa Mazingira Mheshimiwa Selemani Jafo kwa namna wanavyotupa ushirikiano katika Kamati yetu hii ya Maji na Mazingira, tunawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niunge mkono hoja mapendekezo yote ya Kamati ambayo yaliwasilishwa. Nianze mchango wangu kwa kwenda kwenye hoja ya nyadhifa za kukaimishwa kwa baadhi ya watumishi kwa muda mrefu. Kumekuwa na changamoto kwa Wizara yetu ya Mazingira na Maji kwa nafasi ya Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo kukaimishwa kwa muda mrefu. Jambo hili halileti afya. Kama tunavyofahamu, unapomkaimisha mtu kwa muda mrefu kwenye nafasi, anakuwa hana amani na hana maamuzi sahihi katika utekelezaji wa majukumu yake. Jambo hili linaweza kushusha ufanisi wa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kadhia hiyo, uzoefu mara nyingi unasema watu wanaokaimishwa wanakuwa na tamaa kubwa, lakini hatma ya maisha yao yanakuwa ya wasiwasi. Hii ni hali ya mwanadamu, kwa sababu anafanya kazi zake kwa kujituma, lakini pengine muda umepitiliza haijulikani kama anatosha au hatoshi. Kama anatosha, kwa nini asithibitishwe kwa muda muafaka ili aweze kufanya kazi kwa kuleta ufanisi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwona Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania namna alivyotupa fedha na miradi mbalimbali katika Wizara yetu ya Maji na Mazingira. Hii ni namna ya kuona wananchi wanaweza kunufaika na maji lakini pia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Sasa ikiwa wataalam mbalimbali, wakiwemo Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo watakuwa wanakaimishwa mpaka muda unapitiliza; kama hafai awekwe pembeni apangiwe jukumu lingine, aletwe ambaye anafaa. Naamini watu wapo wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ushauri kwa Serikali kuzijaza nafasi hizi za kukaimishwa ili kuleta ufanisi katika utendaji wa majukumu katika Wizara hizo mbili nilizozisema za Maji na Mazingira pale ambapo kwa sasa watu wanakaimishwa na wamekaa kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)