Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuweza kunipa nafasi nami jioni ya leo niweze kuchangia hoja zilizo mbele yetu. Awali ya yote, mimi ni Mjumbe kutoka Kamati ya Maji na Mazingira. Nachukua fursa hii ya kipekee kuwapongeza Mawaziri ambao wanashughulikia hii Kamati yetu. Kwa kweli ni watu ambao wanajitoa na wanatoa ushirikiano mkubwa sana katika Kamati. Kwa hiyo, nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kuchangia katika Sekta ya Mazingira. Nitaenda katika bajeti ya miradi ya fedha za maendeleo. Tunapanga bajeti ambazo hazina uwezo wa kutekelezeka. Hii inadhihirisha kwamba kwenye bajeti ya 2023/2024 fedha za miradi ya maendeleo zilikuwa ni shilingi bilioni 16.6 lakini fedha za nje zilikuwa ni asilimia 89, shilingi bilioni 15 na fedha za ndani zilikuwa ni asilimia 11, shilingi bilioni 1.6. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema bajeti haiwezi kutekelezeka kwa sababu fedha nyingi za miradi ya maendeleo tunategemea kutoka kwa wahisani. Kitu ambacho mhisani leo akikupa fedha yake, lazima atakufundisha namna ya kuitumia. Kwa hiyo, wewe hutakuwa na mamlaka ya kutengeneza matumizi unayoyataka wewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumegundua tuna changamoto nyingi sana za kimazingira. Tunazungumza mvua ambazo zimenyesha, na watabiri wanaendelea kututabiria mvua zinakuja kesho, kesho kutwa. Hii ni kwa sababu hatuna mipango mizuri. Fedha hatuna, tunategemea fedha za wahisani. Leo mhisani atakuletea fedha akwambie nenda kavune hewa ya ukaa, lakini kumbe wewe changamoto yako ni maji kuvuka kutoka kwenye bahari na kwenda kwenye visiwa vya wananchi. Hii haileti afya ndugu zangu, lazima tunapokaa kupanga bajeti zetu, tuhakikishe hasa kwenye fedha za maendeleo japo asilimia 50 tuwe na uwezo wa kuzitenga sisi wenyewe, tusitegemee sana fedha za kutoka nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ile shilingi bilioni 1.6, hadi kufikia Desemba, hiyo fedha yetu ya ndani, Wizara ya Fedha hawajapeleka hata shilingi 100/=. Sasa leo tutakaa tunalaumu, hatuna uwezo wa kuyaboresha mazingira vizuri, hatuwezi kuyatunza, ni kwa sababu sisi wenyewe hatujawa na seriousness ya kutunza mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunahudhuria kwenye mikutano mingi ya kimataifa, kuna COP 28 imeisha juzi tu. Mheshimiwa Waziri alishiriki, Mheshimiwa Rais amekwenda na mikutano mingi Mama anashiriki kwa sababu ni mdau mkubwa wa mazingira, lakini kama hatujabadilisha mustakabali mzima wa kutengeneza bajeti ya fedha za maendeleo na tukaamua kutoa fedha, itakuwa hizi kazi ni za bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kwenye suala zima la changamoto ya taka ngumu ambazo tunazo ndani ya Taifa letu. Leo hii tunazungumza kwenye halmashauri 185, ni halmashauri tano tu ndizo zinafanya proper waste management. Sasa ndiyo tunarudi kule kule, kwa sababu fedha hatuna. Mhisani akileta, atakwambia nenda kawarudishie ardhi kwanza, mimi ndiyo naona kwangu kipaumbele, lakini wewe kumbe una changamoto, taka zinakusumubua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo taka ambazo zinasambaa kwenye miji yetu ni changamoto, na ni mtihani kwa kweli. Maana sijui niseme ni asilimia ngapi kwa kweli. Kama ni halmashauri tano ndiyo ambazo zinafanya kazi ya kusimamia usimamizi mzuri wa taka ngumu, halmashauri 180 hazijafikiwa, tujue bado kazi haijafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi taka zinavyosambaa, mwisho wa siku wind force ikifanya kazi yake, taka zitarudi baharini, taka zinarudi kwenye mashamba ya wafugaji, wanyama wetu wanakula taka hizi, bahari inaenda inachefuka, inapata joto la taka hizi, lakini na viumbe vilivyokuwepo baharini vinateketea. Hii leo tunaipa mzigo mkubwa Wizara ya Afya, tunatibu magonjwa ambayo hata sometime na jina lake halijulikani, ni kwa sababu hatusimamii vizuri mazingira yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwanza kwenye hili suala la taka ngumu, nalo naomba Wizara walitilie msisitizo kweli kweli na wakalisimamie ili tupunguze matatizo mengi ambayo yapo ndani ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye usimamizi wa maji. Nitazungumzia issue nzima ya uchimbaji wa visima. Hili jambo kiukweli linasikitisha sana. Juzi wakati tuko Tabora kukagua miradi ya maji, anasimama Mkuu wa Mkoa anakupa taarifa, anakwambia, eti kwenye visima 22, visima nane vimechimbwa havitoi maji. Yaani asilimia 36 ya visima havitoi maji. Sasa najiuliza, kwenye Wizara tuna wataalamu au tuna vichefuchefu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake kuna watu kazi yao ni kwenda kufanya research kutambua eneo kama lina maji au halina. Sasa kama wameenda wamefanya utafiti wa kutosha na wakarudi kumwambia Waziri hapa maji yapo, tukapeleka jopo la watu wakachimba visima, kwa hiyo, maana yake tunakusudia nini? Kumkomesha Mheshimiwa Rais, kuikomesha Wizara au kumkomesha nani? Hili jambo halina afya kwa kweli. Yaani hiyo ni takwimu ya Tabora, tukizunguka na maeneo mengine ni hivyo hivyo kazi imekuwa ni hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wataalam wetu kama hawana uwezo, Mheshimiwa Waziri wasaidie wakapate mafunzo hata kama ni nje ya nchi, ukawape taaluma. Haiwezekani kila siku tunachimba visima halafu havitoi maji. Tunapoteza fedha za walipakodi wa nchi hii, tunapoteza fedha ambazo tungeweza kwenda kujenga shule watoto wetu wakasoma. Tungeweza kuzipeleka hospitali watu wetu wakapata dawa, lakini imekuwa ni mtihani, ni mtihani, ni mtihani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nilipitia kidogo Taarifa ya CAG anasema kwamba; “katika Sekta ya Maji…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Muda wako umeisha malizia.
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)