Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Zahor Mohamed Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nianze kwanza kwa kuunga mkono hoja kwa Kamati zote mbili. Pili; naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini kuzipongeza Wizara na taasisi zote ambazo kwa kweli zinajitahidi kufanya kazi pamoja na mazingira kuwa magumu sana; lakini niwapongeze kwa sababu kutenda ni wajibu wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wenzangu wamezungumza mambo mengi sana. Sasa mimi naomba niya-summarize kidogo kwa kuleta maombi au ushauri kwa Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ningeomba Serikali, pamoja na jitihada zake za kupeleka fedha kwenye maeneo mbalimbali tukifanya ulinganisho kati ya miaka mitano, sita iliyopita na sasa tumepiga hatua kubwa sana kwenye kupeleka fedha za mendeleo. Kwa sababu mchakato wa maendeleo ni endelevu, maana yake ni kwamba kila siku lazima tutoke hatua moja kwenda hatua nyingine ya kimaendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti; maana yangu ni nini? Maana yangu ni kwamba ni lazima tuhakikishe kwamba mipango yetu tunayoipanga kwa kupitia bajeti yetu lazima tuiheshimu kwa sababu ndicho tulichokipangia tukiwa tunaamini kwamba makusanyo yetu yanalingana na mipango yetu. Ndiyo maana Serikali inatoa ceilings ili kuona kwamba hatuzidi kwa kulinganisha na makusanyo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Mbunge amesema hapa, na wenzangu wamesema kwamba kwa mfano wenzetu wa Zimamoto kwa kipindi chote hichi karibuni tunamalizia nusu ya mwaka hawajapewa hata senti tano ya maendeleo. Hiki ni chombo kikubwa sana, chombo kina kazi kubwa sana lakini bahati mbaya sana ni chombo kipya ambacho ni mwaka uliopita tulikitengeneza kuwa jeshi. Maana yake ili chombo kiwe jeshi lazima kiwezeshwe kifedha na mafunzo na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba sana kwa Serikali kwamba tuhakikishe kwamba tunawawezesha wenzetu hawa ili waweze kutulinda; kama ambavyo tunawawezesha Polisi angalau wameweza kufikia asilimia fulani. Ninawaomba sana, ninaiomba Serikali ihakikishe kwamba tunaliwezesha Jeshi hili la Zimamoto kwa sababu kwa kweli bado linahitajika kuundwa. Chombo hichi ni kipya kinahitajika kiundwe ili kiweze kufanya kazi kama ambavyo tunategemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ningeomba hapo hapo ambalo linafanana na hilo. Miaka miwli iliyopita tumekuwa tukizungumza sana hapa juu ya Serikali, hasa Wizara ya Fedha kufanya mgawanyo wa mafungu ya fedha kama Bunge lilivyopitisha. Sasa inasikitisha sana kila mwaka tunakuja hapa tunalalamika kwamba, kwa kweli hatujafika mahali tukaweza angalau kupeleka mafungu haya kwa mlingano. Tunaamua nani tumpelekee, nani tusimpelekee. Hivi vigezo nadhani Bunge lilishapitia, tumekubali huyu apewe fedha kwa kazi hii. Sasa mimi ningeomba sana, na niliomba huko nyuma tujitathmini tuone; je, tunachokipanga kama Bunge ndicho kinachotekelezwa kwenye mganwanyo? Jawabu lake inaonekana yako maeneo wanapata hela nyingi, yako maeneo bado hayapati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi tumeunda vyombo vingi hapa. Tunayo Wizara ya Mambo ya Nje, tunayo Wizara ya Ulinzi, tunayo Wizara ya Mambo ya Ndani; Hivi vyombo vinatulinda masaa 24; vinalinda mali zetu, vinalinda mipaka yetu. Sasa bahati nzuri au bahati mbaya sana ninadhani bado hatujavipa umuhimu ili kuhakikisha kwamba vyombo hivi ndivyo vinavyomulika mipaka yetu kwa nje, kwa angani na ardhini. Ninaomba sana Wizara ya Fedha wakati inafanya mgawanyo wa fedha hizi isivione vyombo hivi kwamba havina kazi, vina kazi kubwa sana, na ndivyo vinavyolinda uhuru wa kwetu sisi kama Watanzania, naomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba kusema hivi, kwamba miaka miwili pia iliyopita tulizungumza juu ya maendeleo ya viwanja vyetu ambavyo tumepewa kama Taifa kwenye nchi mbalimbali. Taarifa yetu imezungumza hapa kwamba bado viwanja vile vingi hatujaviendeleza na viwanja vile vingi maana yake uwezo kwa kunyang’anywa ni mkubwa. Sasa siyo kwamba Wizara hizi hazitaki kutekeleza lakini hatujazipa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma tuliwahi kutoa mfano; India pale kuna eneo moja kubwa sana tumepewa, lakini kwa sababu ya tamaduni zetu kuamini kwamba wenzetu wameganda kama tulivyoganda ilituchukua mida ya miaka mingi sana mpaka tukajenga. Tulinyang’anywa kiwanja kile tukapewa kingine kidogo ambacho angalau kimejengwa sasa hivi ndiyo tunafanyia shughuli zetu za kibalozi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana; tukivipoteza hivi kwa mazingira yetu hatuwezi kupewa tena maeneo yale yale. Wamezungumza wenzangu hapa Adis tumepewa viwanja viwili vizuri sana, pale DRC tumepewa viwanja vizuri sana, Msumbiji tuna viwanja viwili wengine tumekwenda kuangalia lakini jengo moja lile kama vile tuligaiwa lakini eneo moja liko empty na ni miaka na miaka hatujafanya lolote. Si kwamba Wizara hawataki lakini kwa sababu hatujawawezesha. Mimi naliomba Bunge; sasa Bunge lichukue dhamana yake, lichukue nafasi yake ili kulinda heshima ya Taifa letu mbele ya mataifa mengine, naomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ningeomba sana kwamba Jeshi au vyombo vyetu hivi tumevitaka sana kushiriki kwenye mfumo wa kushiriki kwenye mambo ya uchumi. Ningeomba tukajifunze; wenzetu wa Jeshi la Egypt wanashiriki na wanasaidia Pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 50, ni chombo cha jeshi hicho. Si kwa sababu wanaakili zaidi ya sisi lakini ni kwa sababu Serikali inawawezesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningeomba sana tuwezeshe vyombo vyetu hivi vikiwemo vyombo vya ulinzi kwanza kwenye kufanya utafiti lakini pili kuviwezesha ili viweze kushiriki kwenye uchumi wa Taifa. Kwa sababu bila ya kuviwezesha tutaendelea kuvilaumu lakini sisi hatuviwezeshi kuhakikisha kwamba vinafanya wajibu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ningeomba sana sana kwamba tuhakikishe kwamba sisi kama Serikali yale tunayoyapanga kama Bunge kuielekeza Serikali itekeleze naombeni sana tusimamie mipango yetu kuielekeza Serikali ili Serikali itekeleze matakwa ya Bunge kwa sababu ndiyo matakwa ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba tena kuunga mkono hoja; nashukuru sana. (Makofi)