Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Pangani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, niweze kukushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami kuweza kuchangia Hoja za Kamati zote mbili zilizowasilishwa mbele yako, Kamati ya Maji na Mazingira pamoja na Kamati ya NUU. Asiyeshukuru watu hata Mwenyezi Mungu hawezi kumshukuru. Natumia nfasi hii kwa dhati kabisa ya moyo, kuishukuru Kamati yetu ya Maji na Mazingira kwa kazi kubwa na nzuri ambayo imefanya katika Wizara yetu ya Maji. Kutokana na Kamati hii, leo tumepata pongezi mbalimbali kupitia Waheshimiwa Wabunge, lakini kazi kubwa ambayo imefanywa na Wizara ya Maji, ni maoni na ushauri ambao umetokana na Kamati yetu ya Maji na Mazingira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mwenyekiti wa Kamati, Mzee wangu Mheshimiwa Jackson Kiswaga, mweledi, Mwenyekiti bingwa ambaye amefanya kazi kwa ushirikishwaji mkubwa sana juu ya Wajumbe wake pamoja na Makamu Mwenyekiti Mama Anna Lupembe. Nataka kuwahakikishia Kamati yetu, mimi Jumaa Aweso pamoja na timu nzima ya Wizara ya Maji, mapendekezo ambayo mmeyatoa, moja nayaunga mkono na tumejipanga kuyatekeleza ili kuhakikisha kwamba tunayafanikisha malengo na dhamira ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kumtua mwanamama ndoo kichwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu kutoa ufafanuzi mchache ambao umezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge. Moja, malipo ya Wakandarasi. Ni ukweli usiopingika kabisa kwamba utekelezaji wa miradi ya maji unategemeana na fedha na pasipo utoaji wa fedha maana yake utekelezaji wake unakuwa wa kusuasua. Natumia nafasi hii kumshukuru sana Waziri wa Fedha, hivi karibuni tumeshapokea shilingi bilioni 23 katika kuhakikisha tunawalipa wakandarasi ili miradi ambayo tumeianzisha isikwame juu ya utekelezaji wake. Nataka kuihakikishia Kamati, na tumekwishaanza kulipa kuhakikisha kwamba kazi inaendelea. Nawasihi sana wakandarasi, wale wote ambao tumewalipa fedha hizi kwenda kufanya kazi na sisi kama viongozi wa Wizara tutakwenda kusimamia na kufwatilia kuhakikisha kwamba wananchi wanakwenda kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ni juu ya suala zima la ulindaji na utunzaji wa vyanzo vya maji. Wizara ya Maji, uhai wake ni uwepo wa rasilimali za maji; pasipokuwepo na rasilimali za maji, Wizara haipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema ni kwamba, maji ni usalama wa Taifa. Panapokuwepo maji toshelevu tuna uhakika wa nishati, panapokuwepo na maji toshelevu tuna uhakika wa kilimo cha umwagiliaji na tuna uhakika wa chakula, panapokuwepo na maji toshelevu uchumi wa Taifa hili utakuwa imara zaidi. Nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, pamoja rasilimali hizi zimeumbwa na Mungu, lakini tuna haki na wajibu wa kulinda na kuzitunza kwa pamoja. Eneo la ulindaji na utunzaji wa rasilimali za maji si jambo la Wizara ya Maji pekeyake, ni jambo mtambuka, kwa maana linahitaji ushirikishwaji wa pamoja. kwa lugha nyepesi ambayo nataka kuzungumza, jamii ipo na Viongozi wapo. Ukiwashirikisha utafanikiwa, usipowashirikisha utakwama. Baada ya kuona uharibifu wa vyanzo vya maji, nilikuja hapa katika Bunge lako Tukufu kuja kuomba mabadiliko ya Sheria juu ya ulindaji na utunzaji wa vyanzo vya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii kulishukuru sana Bunge lako Tukufu kwa kuhakikisha kwamba tunakuwa na jukwaa la pamoja juu ya ulindaji na utunzaji wa vyanzo vya maji. Natumia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Spika wa Bunge, kwa busara yake kwa kuunda sasa Kamati ya Maji ambayo inahusiana pia na Mazingira. Nina imani tunakwenda kuwa na mustakabali mkubwa kwa ajili ya kulinda na kutunza vyanzo vyetu vya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hata Tarehe 12 ya Mwezi huu, Dar es Salaam pale Chuo Kikuu, tutakuwa na jukwaa la wadau wote wanaohusiana na mambo ya Maji. Kama nilivyosema hili ni jambo letu kwa pamoja na Waheshimiwa Wabunge, ulindaji na utunzaji wa vyanzo vya maji unaanza na mimi, unaanza na wewe, unaanza na sisi katika kuhakikisha kwamba tunakwenda vizuri katika kwenye utunzaji wa vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo limezungumzwa na Kamati ambayo ni Mapendekezo ya Kamati juu ya kuwa na Mwongozo wa Taifa juu ya uvunaji wa maji. Mapendekezo haya ambayo yametolewa na Kamati, tumekwishayatekeleza. Mpango wa Mwongozo kwa ajili ya uvunaji wa maji huu hapa lakini nahitaji ushirikishwaji wa pamoja juu ya utekelezaji wake. Mwongozo huu unahitaji kusaidia jamii na taasisi mbalimbali katika kujenga Miundombinu bora ya kuvuna na kuhifadhi maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kama mnakumbuka nchi yetu, si maskini ama uhaba wa maji ya mvua. Leo tumeshuhudia maji ya mvua, mvua zinaponyesha yanaharibu madaraja, tumekuwa na mafuriko katika kila kona. Baada ya kuona agenda ya uvunaji wa maji na Mwongozo huu kuanza, Mheshimiwa Rais amefanya kwa vitendo. Ametupatia fedha kwa ajili ya ununuaji wa mitambo kwa ajili ya uchimbaji wa mabwawa, hizi ni jitihada za Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mikakati ambayo Mapendekezo yalikuwa yakitolewa kila mara na Bunge, utekelezaji wake ulikuwa ni changamoto. Kwa mfano, ujenzi wa mabwawa ya kimkakati katika Taifa letu. Bwawa la Kidunda, Bwawa la Farkwa, yalikuwa yapo katika document na makabati ya Wizara. Leo hii leo Bwawa lile ambalo tunakwenda kulijenga pale Kidunda, zaidi ya shilingi bilioni 300, fedha hizi, tunaenda kujenga kwa fedha za ndani, advance imeshatolewa na Mkandarasi yuko site kazi inaendelea. Haya ni mapinduzi ya kweli ambayo yamefanyiwa kazi na Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, hii kazi tumeshaianza na tumeshaanza kuchimba mabwawa maeneo mbalimbali na hata Mwenyekiti wa Kamati yetu hii pale katika Jimbo lake tuna bwawa kubwa ambalo tumelijenga la Masaka Dam. Huu ni mfano Dhahiri wa kuhakikisha kwamba ni dhamira njema ya kumtua mwanamama ndoo kichwani na kuhakikisha suala la uvunaji wa maji tunakwenda nalo kwa kimkakati zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kuhusu suala la Sera ya uhuishaji wake. Kwa upande wa Sera ya Maji ya Mwaka 2002, Mapendekezo ya Kamati tumeshaanza kuyatekeleza, Rasimu ipo tayari. Sasa hivi tunapokea maoni mbalimbali ya wadau ili kuhakikisha kwamba tunakuwa na Sera ambayo inaendana na mazingira ya sasa. Tumeshuhudia kabisa sasa hivi tumekuwa na mabadiliko ya tabianchi, Sera yetu ambayo tunataka tuiunde, iendane na mazingira ya kuhakikisha kwamba mnakabiliana na mabadiliko ya tabianchi na Mapendekezo ambayo yametolewa na Waheshimiwa Wabunge. Itoshe tu kusema, Mapendekezo na Maoni ambayo yametolewa na Kamati yetu ni zaidi ya consultancy, Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati yetu tuwape maua yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ambalo nataka kulizungumza, Wizara ya Maji imetoka mbali sana. Miaka ya nyuma Wizara ya Maji ilikuwa Wizara ya kero na lawama. Hata Bajeti ya Utekelezaji wa Miradi ya Maji ipo miradi ambayo ilikuwa imejengwa tangu Mwaka 1970. Ukienda kule Serengeti, kuna Mradi ambao unaitwa Mwigumu, tangu mwaka 1970 haujakamilika, tumekuja kuukamilisha ndani ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa nini? ni kwa sababu ya changamoto ya kibajeti lakini katika kipindi hiki cha miaka mitatu tumepata fedha nyingi sana kupitia Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Maji ambayo ilikuwa ni changamoyo leo tupo asilimia 77 vijijini na asilimia 88 upatikanaji wa maji mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni tulikuwa Ethiopia, World Bank, imeshukutanisha zaidi ya nchi 53. Wizara ya Maji imeongoza duniani, zaidi ya Nchi 53 tumeongoza kwa miaka miwili mfululizo. Hii ni kazi nzuri ambayo imefanywa na Bunge lako, hii kazi nzuri imefanywa na Kamati yako, na hii ni kazi nzuri iliyofanywa na Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Itoshe tu kusema kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni suluhu ya matatizo ya watanzania na tuendelee kumuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono Kamati yako. Ahsante sana, pamoja na wenzangu. (Makofi)