Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Ally Anyigulile Jumbe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nami kupitia Bunge hili Tukufu nipaze sauti ya kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa miradi mikubwa anayoifanya Wilayani kwangu na kwa Tanzania nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba nichangie kwenye eneo la bandari na hasa eneo ambalo ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi hii, nayo ni kwenye upakuaji. Ili bandari ifanye kazi vizuri ni lazima Watendaji na Watumishi wa Bandari wawe committed na wafanye kazi vizuri sana. Hili nataka niseme kwa watumishi wetu na viongozi wetu walioko pale bandarini wanafanya kazi nzuri ndiyo maana mpaka sasa tunalalamika kwamba meli ni nyingi sana, haya hayajatokea hivi hivi, ni kwa sababu watumishi wetu wakiongozwa na Mkurugenzi wa TPA wamejitahidi kuvutia wawekezaji wengi, wafanyabiashara wengi, lakini pia wamehakikisha shipping lines nyingi zimeongezeka kuja Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni jana tu nilikuwa naangalia taarifa ya habari wanatuambia wamepata shipping line ambayo inatoa mzigo China moja kwa moja mpaka Dar es Salaam bila kupitia bandari yoyote ile. Haya ni mafanikio makubwa sana. Tunataka tuseme Mheshimiwa Rais amefanya kazi nzuri sana mpaka tunapata mafanikio haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuendelee na ufanisi huu, ni lazima TPA wajiendeshe kibiashara. Makampuni mengi ambayo yanafanya biashara ya upakuaji kwenye bandari zikiwemo hata DP World ni makampuni ambayo yana asilimia kubwa ya Serikali kama ilivyo TPA, lakini kwa sababu Serikali zao ziliwawezesha na kuwapatia fedha wajiendeshe kibiashara, ndiyo maana wameweza mpaka kuvuka kwenda bandari nyingine na sasa hivi wanaonekana ni wakubwa. Nasi tunataka tufike huko, TPA nayo ianze kuvuka mipaka, ifanye kwa ufanisi hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa mfano, tukiwapatia fedha hasa za wharfage hata shilingi bilioni 35 mpaka 40, wanao uwezo wa kuanza sasa kujiendesha kibiashara, benki zikawaamini wakaweka fedha kwenye benki zikaanza kufanya kazinao kwa ujumla mpaka wakaweza kuwekeza kujenga magati mengine na kuhamisha eneo lile la Kurasini kwenda Kigamboni halafu hapa tukajenga magati mawili mpaka manne ili meli ziweze ku-park pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba sana Serikali hili ilifanyie kazi. Kwa vile tumeshaomba lifanyiwe kazi, ninafikiri sasa ni wakati sahihi wa kufanyia kazi na TPA kuanza kufanya kwa biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirudi kwa upande wa TANROADS. Wenzangu wote wameongelea kwamba tayari tunajiona tuna pesa kidogo kwenye bajeti za uendeshaji wa TANROADS. Naomba nikumbushe kwamba pamoja na ndege na reli, lakini uchumi wa nchi hii, mshipa ambao unafanya kazi kuilisha nchi hii ni barabara. Hatuna namna ya kukwepa ujenzi wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, kuna upungufu mkubwa. Ili tujenge barabara hizi, tunahitaji shilingi trilioni tano na hizi tungeziomba kwa mwaka huu bajeti inapokuja angalau ifike kwenye shilingi trilioni tano ili tuweze kufanya matengenezo na kujenga barabara ambazo ziko kwenye bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ubunifu uwe mkubwa sana katika kutafuta mapato hasa kwenye Mfuko wa Barabara. Tumezoea kwenye mafuta tu, naomba twende mbali tuangalie vyanzo vingine kama wenzetu wanavyofanya. Kuna distance tolling, nayo ni nzuri sana, inao uwezo wa kuongeza mapato. Pia tunao uwezo wa kutengeneza barabara za kulipia ambazo zitaenda kuongeza malipo kwenye Serikali na kufanya mfuko wetu utune. Tunaomba Serikali ihakikishe inakuja na vyanzo vya kutosha ambavyo vitafikia shilingi trilioni mbili ili tuweze kufanya matengenezo ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni suala la fidia za wananchi ambako barabara zinapita. Naomba katika hili nipaze sauti. Kuna wananchi wengi barabara zinapita kwenye maeneo yao lakini mpaka leo hii hawajapata malipo. Mfano mzuri ni barabara yangu ya Ibanda kwenda Kajunjumele. Wananchi wameendelea kusubiri malipo na wakati mwingine Serikali iliwapa matumaini kupitia Mkuu wa Wilaya, akasema tarehe tatu mwezi wa Kumi na Moja watapata fedha zao, lakini mpaka leo hawajapata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua Serikali yetu inapambana na inatafuta fedha kuwalipa wananchi. Tunaomba sana mahali ambako hatuna nafasi ya kujenga kwa sasa tuwaache wananchi waendelee na shughuli zao. Tuwaache wananchi waendelee na shughuli zao kuliko kuwasimamisha huku wakitegemea watapata malipo halafu malipo hayafiki kwa wakati. Tunaomba sana haya mambo yafanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la fidia ambazo zilikuwa zimeahidiwa. Jumla ya fidia zote ili Serikali iweze kulipa ni shilingi trilioni saba. Hili ni jambo kubwa sana, tunaomba Serikali izipitishe zilipwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ni ujenzi wa barabara ambao umekuwa ukisuasua, tunaomba sana TANROADS na Serikali wasimamie vizuri mikataba iliyopo. Vilevile mikataba iliyopo kwa sasa ninasema haina ufanisi mzuri na haisimami kwa upande wetu. Mheshimiwa Waziri amelazimika kuwaita wakandarasi kuzungumzanao wakati mikataba ndiyo ilitakiwa izungumze. Naona kuna sehemu kuna matobo na upungufu na kuna uwezekano kuna sehemu meno yetu kwenye mikataba ni ya plastic, badala ya kuwa meno ya chuma. Naomba hili la mikataba lisimamiwe vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishukuru sana Serikali kupitia Waziri wa Ujenzi na Waziri wa Fedha walipokuja Kyela kuwapa matumaini Wananchi wa Ikombe ambao hawajawahi kuona gari kwamba sasa wanaenda kutoa shilingi milioni 500 ili wananchi hawa waone gari. Nashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, naomba tuisimamie TAZARA. Hao wawekezaji wanaokuja, tunaomba waje na mkataba wetu na Zambia uangaliwe upya. Najua Wazambia wapo hapa, tunataka tuwaambie “injanji, tuefwaya iyambe.” Hiki ni Kichina cha Zambia. Tunataka reli ifanye kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nakushukuru kwa nafasi hii. (Makofi)