Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Abdallah Jafari Chaurembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbagala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Kamati hii ya Miundombinu. Niseme ni miongoni mwa wajumbe katika Kamati hii ya Miundombinu, Kamati ambayo kila Mbunge hapa amekuwa akiangalia namna ambavyo tunaweza tukatekeleza wajibu wetu kuhakikisha miradi hasa ya barabara inatekelezwa kwa wakati na namna ambavyo imepangwa kwa mujibu wa bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wetu, Mama yetu Daktari Samia Suluhu Hassan, kwanza kwa kusikiliza kilio cha wananchi wangu wa Mbagala hususan wakazi wa Kisewe, Mbande mpaka Msongola kwa maana tulikuwa na kilio cha muda mrefu katika ile Barabara ya Mbande – Kisewe mpaka Msongola. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, mambo yanaenda vizuri na wananchi wanafurahi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; kwa dhati yangu ya moyo niwashukuru sana Wajumbe wenzangu wa Kamati tukiongozwa na Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Kakoso, kwa mapendekezo ambayo tumeyaleta kwenye Bunge hili. Mapendekezo ambayo tukiyasoma kwa kina yanaenda kuwa mwarobaini wa mambo tofauti tofauti katika idara zote ambazo zinasimamiwa na Kamati hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sasa baada ya Kamati kutoa mapendekezo haya, niwaombe Wabunge wote baada ya kuyasoma na kuyajadili hapa basi yawe ndio maazimio ya Bunge letu hili ili tuweze kuleta tija katika sekta mbalimbali ambazo zinasimamiwa na Kamati hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukisoma kwenye taarifa yetu, zipo changamoto ambazo zimeonekana katika Mamlaka ya Bandari na Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamechangia sana. Changamoto zile tukiziwekea maazimio katika Bunge hili naamini tunaenda kurekebisa mambo mengi pale bandarini na mapato ya nchi yetu yatazidi kuongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamezitaja changamoto karibu zote zile za bandari na a way forward nini tufanye katika kutoa hizo changamoto. Katika taarifa pia tumeonyesha changamoto zinazowakabili wenzetu wa TANROADS. Naomba nijikite hapo katika mchango wangu wa leo baada ya pongezi hizi ambazo nimezitoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika taarifa tumeainisha, moja ya changamoto ni ufinyu wa bajeti na wenzangu hapa wamechangia na mimi nachangia, endapo Wizara hii au TANROADS wakipata trilioni tano kwa kila mwaka tunaamini tunaenda kutatua matatizo makubwa ya changamoto ya barabara zinazotukabili katika maeneo yetu. Barabara nyingi zimeharibika, barabara nyingi zinahitaji matengenezo, kitu ambacho kutokana na fedha ambazo TANROAD wanazo 1.3 trillion hatuwezi kutoboa, hatuwezi kufika popote katika suala zima la barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakutolea mfano wa baadhi ya barabara, kwa mfano ile barabara inayotoka Mbagala Rangi Tatu – Kongowe mpaka kwenda Mwandege, barabara ile ni lango kuu la wenzetu wanaotoka mikoa ya kusini. Lakini barabara ile imekuwa haitengenezwi mara kwa mara kutokana na ufinyu wa bajeti, na hata inapotengewa bajeti kutokana na tatizo kubwa lililokuwepo la miundombinu tunajikuta fedha zile zinaweza ku-service maeneo mengine na hatimaye kila mwaka barabara ile imekuwa haitengenezwi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana Serikali endapo tutaongeza fedha mpaka kufikia trilioni tano basi changamoto nyingi za barabara zinaenda kutatuka katika maeneo mbalimbali, nilikuwa na mwenzangu Mbunge wa Kiteto naye ananikumbusha barabara zake kwa kunisogezea vi-memo. Hii itaonyesha ni jinsi gani changamoto ya barabara ilivyokuwa ni kubwa na hii inatokana na ufinyu wa bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika taarifa ya Kamati tumezungumzia sana kuhusiana na madeni ya wakandarasi. Unaweza ukaona suala la madeni ni suala dogo lakini athari zake linaenda kuongeza riba kitu ambacho fedha hizo tunazozipata nyingine badala ya kufanya maendeleo ya ujenzi wa barabara tunaenda kulipa riba kutokana na kuchelewesha kuwalipa wakandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana maazimio tutakayofikia hapa na niwaombe Wabunge wenzangu watuunge mkono Kamati yetu. Serikali waende kutekeleza, tutaenda kuokoa mambo makubwa sana katika sekta nzima ya Barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumezungumza suala la fidia, katika changamoto ya fidia hapa naomba tuelewane kidogo, TANROADS hawawezi kujenga barabara ambayo kuna migogoro ya fidia au maeneo ambayo hayajalipwa fidia. Zipo barabara nyingi watu wamesimamishwa kuendeleza na bajeti zinapangwa kila mwaka lakini kwenye suala la ulipaji wa fidia kumekuwa na changamoto kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii niliyoisema hapa ya kutoka Kongowe – Kokoto mpaka kwenda Mwandege ni zaidi ya miaka 10 sasa wananchi wameambiwa wasiendeleze maeneo yao kwa ajili ya kusubiri fidia na barabara hii nayo inazalisha riba. Sasa ndugu zangu niwaombe sana Serikali maeneo haya kama tuna mpango kweli wa kuyaendeleza na kuyajenga basi tulipe fidia kwa wakati ili tuondokane na riba. Wananchi wale wa kutoka Kokoto mpaka Mwandege wanaendelea kukata tamaa siku hadi siku nyumba zao hazipangishiki, wananchi wanahama waliopanga katika nyumba zao, wanazidi kuwa maskini kadiri ya siku zinavyokwenda kwa ajili ya zuio lililofanyika pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nataka nimalizie kwa ndugu zangu wa TANROADS, wanafanya kazi nzuri sana lakini yapo maeneo wanazusha taharuki zisizokuwa na msingi. Kwa mfano barabara ya kutoka Msongola kuja Mbande – Kisewe – Majiatitu- Rangi Tatu wameweka X kwenye corridor zote za barabara bila kutoa maelezo yoyote, bahati nzuri ni mzawa wa Mbagala.

Mheshimiwa Naibu Spika, unapafahamu pale Majimatitu, eneo lile mwanzoni katika miaka ya 80 Kampuni ya ABUCO ililipa fidia upana wa barabara na wananchi wa pale wanajua barabara zilizolipwa zimelipwa upana gani na bahati nzuri miongoni mwa watu waliolipwa fidia alikuwepo pamoja na marehemu mzee wangu. Nimetafuta karatasi nimeona tumelipwa fidia mita 15 kutoka katikati ya barabara. Leo TANROADS wamekwenda kuweka X zaidi ya mita 30, wananchi wamekumbwa na taharuki, niwaombe sana TANROADS wakaondoe mgogoro ule kwa kuwaambia uhalisia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)