Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa nafasi lakini vilevile nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mchana huu na kutoa mchango wangu kwenye hotuba ya Kamati ya Miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu, Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoamua kuutembelea Mkoa wa Lindi alikuja Liwale pamoja na kwamba Liwale hakufikiki kwa barabara Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuona umuhimu wa Wananchi wa Liwale aliamua kuja kwa chopa wana Liwale tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niungane na hoja zote kwa maana ya Maazimio yote ya Kamati na niwapongeze Wanakamati na Mwenyekiti wao na maazimio yote nayaunga mkono lakini hapa na mimi naomba niongeze azimio moja. Kama ikikuridhia tuitake Serikali ipeleke fedha zote tulizozipitisha kwenye bajeti ya mwaka huu, hii tunayoitekeleza hasa kwa upande wa barabara kabla ya bajeti ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nijikite sana kwenye upande wa TANROADS na hapa ninapozungumza Wilaya ya Liwale iko kisiwani, hapa ninapozungumza Wilaya ya Nachingwea iko kisiwani. Wilaya ya Nachingwea inafikiwa na barabara tatu; Masasi – Nachingwea, Ndanda – Nachingwea na Nanganga – Nachingwea. Hizo barabara zote tatu zimeharibika hazipitiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Liwale inafikiwa na barabara mbili; Barabara ya Nachingwea – Liwale na Nangurunguru – Liwale, barabara hizo zote hazipitiki. Leo hii tunapozungumza Liwale hakuna mafuta kwa sababu malori yote ya mafuta yamekwama hayaendeki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninapoongeza azimio la kuitaka Serikali ipeleke fedha zote zilizopitishwa na bajeti iliyopita kwa sababu kwenye Wilaya yetu ya Liwale barabara yetu ya Nangurunguru – Liwale tulikuwa tumetengewa kilometa 72. Kwa hiyo utekelezaji wa bajeti hii itatupa afueni kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 16 Juni, mwaka uliopita mimi ni miongoni mwa watu walioshiriki kwenda kushuhudia Mkataba wa Ujenzi wa Barabara ya Masasi – Liwale kilometa 75 kwenye Mradi wa EPC+F. Leo maswali ni mengi kwa Wanaliwale; miradi hii inakwenda kutekelezwa lini? Kwa hiyo tunaiomba sana Serikali kuhakikisha bajeti iliyopitishwa hapa mwaka huu inatekelezwa ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikisema hivyo kwa kusisitiza zaidi nataka niwaambie Liwale hakufikiki. Hivi juzi kulikuwa na ratiba ya Mwenezi wetu Taifa, Ndugu Makonda, ilikuwa aje Liwale, lakini ratiba ile imefutwa anaishia Nachingwea kwa sababu Liwale hakufikiki kwa hiyo nataka muone namna Liwale ilivyo kisiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile niendelee kuunga mkono Kamati, tunazungumzia Bandari ya Mtwara. Ni kweli mwaka huu Bandari ya Mtwara imefanya vizuri, korosho zote za Mkoa wa Lindi na Mtwara tumezisafirishia Bandari ya Mtwara lakini kizungumkuti kinakuja inapozungumzwa Barabara ya Reli kutoka Mbamba Bay kwenda Mtwara. Mara zote majibu ya Serikali wanasema wanatafuta mbia. Mimi bado kichwani mwangu kuna maswali mengi ambayo hayana majibu. Kwa nini reli hii inatafutiwa mbia wakati kuna reli nyingine inayotoka Dar es Salaam mpaka Kigoma mpaka Burundi inajengwa na fedha zetu? Kwa nini miradi hii isiingizwe huko? Kwani Mtwara na Lindi kuna nini? Ni majibu ambayo Mheshimiwa Mwenyekiti akija kuhitimisha hoja tutaomba Mwenyekiti naye utusaidie. Kwambakatika jambo hili shida ya Lindi na Mtwara ni nini? Kwa sababu kila mwaka tukiuliza tunaambiwa hii reli itajengwa tunatafuta mbia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninayo taarifa, na kwenye bajeti nilisema, kuna mbia mmoja alijitokeza lakini yule mbia mpaka leo ameandika barua Wizarani hajajibiwa; kwa hiyo kuna shida. Tunataka tujue reli hii itajengwa lini, sambamba na uimarishaji wa Uwanja wa Ndege wa Mtwara? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Kanda ya Kusini tunautegemea sana Uwanja ule wa Mtwara kwa sababu ndio uwanja pekee unaokaribiana na maeneo ya kwetu. Hayo ndiyo mambo ya msingi nilikuwa niyazungumze kwenye hotuba hii ya Kamati ya Miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo mengi sana ambayo yanazungumzwa kwenye Kamati hii. Kwa mfano kama TANROADS wamesema wana tatizo la bajeti lakini tatizo siyo bajeti peke yake; hata hiyo bajeti kidogo je, inakwenda?

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maelezo mazuri sana kwenye hotuba ya Kamati tungeomba sana Mwenyekiti wa Kamati atuelezee, mpaka sasa hivi TANROADS wameshapokea fedha kiasi gani versus na bajeti tuliyowapitishia. Hii itatusaidia kuona ni namna gani utekelezaji wa bajeti kwenye Serikali yetu unavyokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninazungumzia kwenye upande wa mawasiliano. Upande wa mawasiliano natoa mfano upande wa Liwale tulikuwa na minara iliyojengwa na Halotel. Ile minara imejengewa sasa hivi ina miaka mitatu yote haifanyi kazi kwa sababu inatumia battery, na battery zimekufa. Kwa hiyo mawasiliano sasa hivi unapata kuanzia saa nne asubuhi mpaka saa 12 jioni, au pengine mpaka saa 10 jioni mawasiliano hakuna. Kwa hiyo tunaiomba sana Serikali kwenda kuboresha minara ile ili iweze kufikika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upande mwingine ni TBC. Hii redio ya Taifa au hii TV ya Taifa; kwa upande wa TV hatuna wasiwasi lakini kwa upande wa redio Liwale tunapata Redio Ulanga, Redio Msumbiji lakini TBC hampo kabisa. Kwa hiyo mimi naiomba sana Serikali kuhakikisha sisi watu wa Liwale tunapata mawasiliano ya TBC, kwa sababu ndiyo TBC ya kwetu na sisi ndio walipakodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, najua Mheshimiwa Mwenyekiti ndiye atakayekuja kuhitimisha hii; kwa hiyo nimuombe anisaidie kunipatia majibu ya haya na hili Azimio langu ninaloliongeza hapa akiridhia liingizwe; kwamba tuiombe Serikali, pamoja na bajeti ndogo wanayopata TANROADS basi miradi yote tuliyoipitisha hapa tuone inatengewa fedha kabla ya bajeti ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante mimi naunga mkono hoja zote za Kamati; ahsanteni sana. (Makofi)