Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote ningependa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo amekuwa kila mwaka akituidhinishia bajeti katika sekta hii ya miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais tangu ameingia madarakani kwa kipindi hiki kifupi ameweza kulipa hata madeni ambayo yaliachwa 2015 mpaka sasa hivi. Licha ya kwamba madeni haya yamekuwa yakilipika lakini bado sekta hii ya miundombinu imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa sana ya ufinyu wa bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hapa Bungeni imekuwa ikija tunawapitishia bajeti ya miundombinu, lakini cha kushangaza fedha zile zimekuwa hazifiki kwa wakati katika Wizara hii ya Miundombinu, na fedha zile zimekuwa pia zinacheleweshwa na kufikia hatua kwamba wakandarasi wengi wameshindwa kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tunajua kwamba ina mikakati mingi, lakini Serikali pia inabidi iangalie kwa wakati huu nini cha muhimu cha kufanya? Tunaelewa barabara ni siasa, na barabara hizi kama ni siasa kwenye kila mwaka tunapopitisha bajeti ni lazima tuangalie kipaumbele chetu ni kipi, lipi litakuwa ni la kimkakati kuliko hivi sasa hivi Serikali inachokifanya. Tunaidhinisha bajeti ya shilingi trilioni moja, haifiki; Waheshimiwa Wabunge wengi wanakuja hapa wanalalamika kuhusu Barabara, kwamba hatujafikiwa. Hii inakuwa inaleta sintofahamu katika majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ifike mahali kama imeamua kutekeleza miradi ya barabara ilete fedha kwa wakati na iweze kutekeleza barabara hizi kwa kipindi cha bajeti ili iweze kutoa hizi sintofahamu. Kwa mfano, kwa mwaka jana mpaka Disemba miradi iliyokamilika ni 94 na miradi ambayo bado inaendelea ni miradi 69 na bado Serikali inadaiwa bilioni 796 mpaka kufikia Disemba. Kumbuka fedha hizi zinachajiwa na riba na hii kuifanya Serikali kuingia kwenye riba na kupoteza fedha nyingi zinazoenda kwenye riba. Kwa hiyo kama Serikali mimi ningeiomba ili tujisaidie tusiingie kwenye hizi changamoto tupitishe vile ambavyo tunaviweza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna tatizo lingine katika Road Fund. Serikali inaidhinisha pia barabara mpya huku kuna barabara 71 zimebaki zikiendelea kuwa mbovu, ambazo ni barabara kongwe. Sasa hivi nitamwona Waziri Bashungwa anahangaika mara utamwona Shinyanga, mara Dar es Salaam barabara zimekatika, na kuna tishio kubwa la mvua za El-Nino linaendelea na barabara madaraja yamekatika, zinahitajika fedha, lakini ukija kuangalia Road Fund yenyewe haina fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili Road Fund ijiendeshe inahitaji shilingi trilioni mbili na mpaka tunavyoongea hivi Road Fund yenyewe haina hiyo bajeti ya kuweza kutengeneza hizi barabara zilizokatika. Road Fund pia wana changamoto ile ile kama iliyoko TANROADS, fedha kutokufika kwa wakati. Tumeshaongea mara nyingi sana na Waziri wa Fedha, tumekuwa tukimwita aweze kuidhinisha fedha hizi kwa wakati. Siwezi kuelewa changamoto wanazozipitia Serikali labda kwamba hela hakuna kwenye kapu la Taifa, lakini lazima tuangalie. kwasababu barabara hizi zinapokatika, miundombinu hii inapokatika wananchi watashindwa kutoka kwenda kazini na pia Serikali itashindwa kupata mapato, kwa sababu barabara nayo ni mapato. Tutashindwa kusafirisha mazao, tutashindwa kufanya shughuli nyingine za kuingiza kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi pia nashauri, na hata Kamati pia imeshauri; Road Fund itengewe chanzo kingine cha mapato. Kwa mwaka Road Fund inahitaji shilingi trilioni mbili, na mpaka tunavyoongea sasa hivi kiasi kilichoidhinishwa ni bilioni 300. Kutoka kwenye trilioni mbili tunachokihitaji mpaka sasa hivi imeidhinishwa shilingi bilioni 300. Kwa jinsi gani utaona barabara nyingi zitabaki na mashimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna barabara mpya, barabara zile za zamani zinaendelea kuwa chakavu. Kwa mfano ukiangalia hii Barabara ya Dodoma – Morogoro ina mashimo mengi nayo inahitaji hela; na hii barabara ni kubwa, lakini ukija kuiangalia hata sasa hivi bado tuna suasua kuitengea bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nipende kuishauri Serikali tunapoamua kuingiza barabara mpya kujenga barabara mpya; TANROADS kwa mwaka inahitaji shilingi trilioni tano. Hebu tuangalie tunaweza tukaipata shilingi trilioni tano au tupunguze barabara mpya tu-deal na hizi barabara za zamani 71 ili tuweze kuendelea kuunganisha hii mitandao na maisha ya wananchi yakaendelea kwa kawaida kuliko kuendelea kuingiza barabara mpya kwenye mtandao wa TANROADS ambazo hatutaweza kuzihudumia na hii ikawa ni changamoto katika Serikali yetu? Kwa sababu mwisho wa siku tutamaliza kutengeneza barabara mpya tutajikuta tunarudi kutengeneza hizi barabara za zamani ambapo na Serikali itakuwa imeingia hasara kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia jambo lingine ningependa kuishauri Serikali. Mnazuia maeneo ya wananchi, mnawataka wananchi wapishe yale maeneo kwa ajili ya kulipwa fidia lakini hapa imeshaonekana Serikali haina uwezo wa kulipa fidia kwa wakati. Kingine kwa mwaka jana wa fedha Serikali ilitakiwa kulipa shilingi trilioni saba fidia lakini TANROADS kama TANROADS wametengewa shilingi trilioni moja; utaona kwa namna moja tunapitisha mambo utelekezaji ni mdogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi naomba kama yale maeneo Serikali inajua kabisa wameyapiga X ili wananchi wasiyatumie, na wameyazuia, waache wananchi kwa kipindi hichi waendelee kuyatumia maeneo yale kuliko kuendelea kuyazuia, hawawalipi fidia, wananchi wamewaondoa na haijulikani. Licha ya hivyo Serikali ikiwa inakuja kulipa fidia inailipa fidia ambayo haiendani na gharama ambazo zipo kwa wakati huo, na hii huwaletea wananchi changamoto sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi nina imani na Serikali yangu na nina imani na jinsi ambavyo Mawaziri wanavyojituma katika kufanya kazi lakini tunapoelekea mwaka huu mwingine wa fedha kwa kweli tufanye pale ambapo tunahisi tunaweza; na tusiwe na ahadi nyingi ambazo hazitekelezeki ambazo mwisho wa siku huko kwenye majimbo yetu ni changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano hata mimi kwangu kuna Barabara ya Bulyankulu. Kila siku tunapewa ahadi tunaenda kusaini, tunaenda kusaini lakini mwaka wa fedha huu unaisha na wananchi wanaimani sana na Mheshimiwa Rais, wanaimani sana na Serikali na wanaimani na Chama Cha Mapinduzi; lakini wanavyoona ukimya kila siku kwamba wanakaa ahadi inatolewa hazitekelezeki imani ile inazidi kupotea, ahsante sana. (Makofi)