Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GHATI Z. CHOMETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika sekta hii ya miundombinu. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na nimesimama katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya katika nchi yetu katika kuwaletea maendeleo Watanzania wote. Kipekee pia niwapongeze sana Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wewe kwa jinsi mnavyoendesha Bunge letu Tukufu na kuhakikisha Bunge letu linaendelea kuimarika na kuendelea kuwa kidedea; hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niende kuchangia kuhusu Mamlaka ya Viwanja vya Ndege. Nimpongeze sana Waziri mwenye dhamana Mheshimiwa Prof. Makame Mbarawa na Naibu wake Mheshimiwa David Kihenzile na wafanyakazi wa Shirika hilo la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba Mamlaka ya Viwanja vya Ndege inamiliki au inahudumu viwanja vya ndege takribani 53. Katika viwanja hivyo 53 vipo viwanja vitano au havifiki vitano ambavyo ndivyo vinavyosimamia au vinavyohudumu vinavyovisaidia vile viwanja vingine ambavyo vinapelekea vile viwanja vya ndege au Mamlaka uchumi wake au jinsi ya uendeshaji unaendela kushuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wamesema changamoto nyingi zilizopo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege. Mimi nimeona pia nigusie changamoto moja. Tunatambua kwamba Serikali imeipa Mamlaka hiyo ya Viwanja vya Ndege kukusanya lakini pia na kupeleka gawio Serikalini. Makusanyo yale ya asilimia 70 ambayo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege inakusanya, wao kama Mamlaka baada ya kukusanya na kupeleka Serikalini, wao wanarudishiwa asilimia 15. Hii asilimia 15 wanayorudishiwa ni ndogo sana; na baadaye pia wanaweza wasirudishiwe hiyo asilimia 15. Hii inapelekea utendaji wao wa kazi kushuka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ombi langu kwa Serikali, ninaomba Serikali iliangalie hili Mamlaka iweze kuongezewa kutoka asilimia 15 basi ifike hata asilimia 40 ili kusudi Mamlaka iweze kujiendesha vizuri. Sambamba na hilo basi nashauri asilimia hiyo iliyopangwa na Serikali irudi kwenye Mamlaka kwa wakati ili Mamlaka iweze kujiendesha vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba Mheshimiwa Rais amelifungua anga, amewekeza fedha nyingi kwenye anga. Tunapoacha kuboresha viwanja vyetu sisi wenyewe kama Watanzania tunajishushia uchumi wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo naomba nichangie upande wa TANROADS; kwanza naomba nimpongeze sana Waziri pia mwenye dhamana Mheshimiwa Innocent Bashungwa na Naibu wake Mheshimiwa Engineer Godfrey Kasekenya; hawa Wamekuwa ni viongozi wazuri wanaomsaidia sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kule kwetu, nitolee mfano kule Mkoa wa Mara; tumepata miradi mingi ya barabara za lami; nampongeza sana sana Meneja wetu wa TANROADS Mkoa wa Mara, amekuwa ni Meneja mzuri anayesimamia miradi ya TANROADS vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua miradi ya barabara iliyoletwa; ulikuwepo Mradi wa Nata mpaka Sanzati kilometa 40; ule mradi ni wa muda mrefu, lakini Mheshimiwa Rais ametuletea fedha na ule mradi unaendelea mpaka sasa; tunamshukuru sana. Changamoto iliyopo pale ni ucheleweshaji wa fedha kwa mkandarasi. Naiomba Serikali ihakikishe inapeleka fedha zile kwa mkandarasi ili kusudi ule mradi uweze kumalizika kwa sababu ni wa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumepata mradi mwingine wa barabara mradi unaounganisha wilaya kwa wilaya lakini mpaka mkoa kwa mkoa; Mradi wa Tarime – Nyamongo mpaka Mugumu Serengeti kilometa 87. Mradi ule unaendelea mpaka sasa na fedha zimekwenda. Isipokuwa, mradi ulitakiwa kumalizika mwaka jana lakini mpaka sasa mradi haujamalizika. Changamoto iliyopo ni kusuasua kulipwa mkandarasi. Naiomba Serikali yangu iliangalie hili. Tunapochelewa kumlipa mkandarasi tunaenda kuongeza madeni zaidi na kuisababishia Serikali hasara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaelewa changamoto za wananchi wa Mkoa wa Mara, ameendelea kutupa Barabara. Tunatambua kwamba katika Bajeti ya 2023/2024 ametupa barabara ya Musoma - Busekera kilomita 92 lakini mpaka sasa ule mradi au ile barabara hakuna kinachoendelea mkandarasi hayupo. Kwa hiyo, naiomba TANROADS kupitia Serikali yangu iangalie ni namna gani mradi ule utaenda kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hajaishia hapo ametupa mradi wa Mika, Utegi mpaka Kirongwe kilomita 56, mpaka sasa wananchi wa Wilaya ya Rorya au Jimbo la Rorya wanatamani mradi ule uende kuanza ni kwa namna gani unaanza, wakitambua kwamba mradi ule umewekwa katika bajeti ya 2023/2024. Wananchi wanatamani kula matunda ya Serikali ya Awamu ya Sita, ninaiomba sana Serikali yangu iangalie ni kwa namna gani inaweza ikakamilisha au ikaanza pia na miradi hii ili kusudi sisi sote tuende kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nizungumzie suala zima la upande wa Shirika la Ndege. Tunatambua kwamba shirika la ndege Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amewekeza vizuri katika shirika hili la ndege na ameendelea kununua ndege nyingi katika nchi yetu, tulipokuwa siko tunakoenda, hii imeonesha ni jinsi gani Mama anaendelea kuchapa kazi. Kuna Mikoa ambayo inatamani kuiona ndege Air Tanzania, ndege yetu ya Serikali lakini mpaka sasa Mikoa hiyo ndege haijawahi kufika na wananchi wanasikia kila wakati kwamba Mama amenunua ndege. Wazo langu au ushauri wangu ni nini? Kamati ilitembelea Mkoa wa Mtwara ilikuta Serikali imewekeza pesa nyingi sana pale kwenye uwanja ule lakini ndege ya Air Tanzania haifiki pale, tatizo ni nini? Naiomba Serikali yangu iangalie kwa jicho la pili Mikoa ambayo Air Tanzania inaweza kufika ili kusudi wananchi wote tufaidike na hii keki ya Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)