Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

Hon. Eng. Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia taarifa ya Kamati ya Miundombinu. Naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema.

Mheshimiwa Naibu Spika, mapinduzi ya sekta ya mawasiliano yanachangiwa kwa kiasi kikubwa sana na Kamati hii ya Miundombinu. Hivyo nawapongeza sana na tunaendelea kuwashukuru sana kama Serikali kwa kuendelea kutushauri na kutusimamia, na pale ambapo tutahitajika tutashirikiana vizuri ili kuhakikisha kwamba Serikali yetu inaendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuongelea maeneo mawili. Eneo la kwanza ni safari ya Tanzania kuelekea kwenye uchumi wa kidijitali. Uchumi huu unahitaji miundombinu ya kidijitali, na miundombinu hii ni pamoja na ujenzi wa mikongo ukianzia mkongo wa baharini, mkongo wa Taifa, last mile connectivity ambayo inahusisha minara pamoja na fiber mlangoni kwako.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya nini? Upande wa Mkongo wa Baharini Serikali inaendelea kuvutia wawekezaji ili tuweze kuwa na mikongo mingi ili kuhakikisha kwamba tunashusha gharama ya matumizi ya internet. La pili, ni ujenzi wa Mkongo wa Taifa, Mheshimiwa Rais alipoingia madarakani alitoa kiasi cha shilingi bilioni 170 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba mkongo wa mawasiliano unajengwa na kufika katika Wilaya nyingi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkongo wa Mawasiliano ni moja ya ecosystem katika miundombinu ya mawasiliano. Tunapoanza na mkongo wa baharini, tunakuja mkongo wa Taifa, tunapokuja kwenye last mile connectivity, sasa tunafika kwenye minara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kipindi cha kuanzia 2021 - 2023 imeweza kutoa fedha za ujenzi wa minara 1,070 yenye gharama ya takribani shilingi bilioni 170.978. Minara ambayo bado ipo katika hatua za utekelezaji ni minara 758 ambapo minara 320 inatokana na fedha za ndani na minara 438 inatokana na fedha za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua kwamba kuna maeneo ambayo bado yana changamoto na Mheshimiwa Rais anaendelea kutafuta fedha ambazo zitakuja kutatua changamoto katika baadhi ya maeneo. Tayari Mheshimiwa Rais ameshapata fedha kwa ajili ya kuongeza minara mingine 636, lakini katika minara hiyo kuna minara ambayo itaenda kujengwa katika maeneo yenye changamoto ya TBC, minara ambayo ni takribani 15.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo ambayo minara tayari imeshajengwa na Waheshimiwa Wabunge wameonesha changamoto ya minara kuwaka asubuhi na mingine inawaka kwa masaa machache baadaye jioni inakuwa haipatikani.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshatoa maelekezo kuhakikisha kila mtoa huduma anapojenga minara ya mawasiliano cha kwanza ni lazima iwe na huduma ya internet. Jambo la pili, ni kuhakikisha kuwe na source ya power tatu; ya kwanza ikiwa solar, ya pili ikiwa betri na ya tatu ikiwa generator. Tunaamini kwamba kwa kufanya hivyo, hata kama solar itakosa nguvu, basi betri itaweza kusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongea kidogo kuhusu suala la ujenzi wa Chuo cha ICT. Mheshimiwa Rais tayari ameshaelekeza na Mshauri Elekezi ameshafika kutoka South Korea na kazi ameshaanza tayari toka tarehe 29 Januari. Hivyo tutegemee kwamba ukamilishaji wa chuo hiki kitawasaidia Watanzania kuwajenga katika maarifa zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile suala la kuwa na ICT hubs, tayari Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa kiasi cha dola milioni sita kwa ajili ya kujenga ICT hubs katika maeneo ya Dodoma, Dar es Salaam, Tanga, Mbeya, Lindi, Mwanza, Arusha pamoja na Zanzibar. Lengo ni nini? Lengo ni kuandaa vijana wetu wawe tayari kuingia katika soko la kidijitali ili Tanzania yetu ifikie uchumi wa kidijitali.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongea kitu kidogo kuhusu suala la teknolojia zinazoibukia. Mheshimiwa Engineer Ulenga ameongelea kuhusu attacks katika critical infrastructure. Ni kweli kabisa, nchi za jirani hivi karibuni wawepambana na changamoto hii, lakini Serikali yetu tayari imeshaanda miongozo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Malizia.

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Serikali yetu imeshandaa miongozo mitano na tunapitia sera zetu ili kuhakikisha kwamba tunapambana na majanga haya yanayotokea. Mpaka sasa pamoja na kwamba nchi jirani zimeshapambana na haya majanga ya attack, Serikali yetu bado iko salama, mifumo yetu bado iko salama, lakini Serikali haitabweteka, itaendelea kuweka mkakati wa kuhakikisha kwamba mifumo yetu inaendelea kuwa salama zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)