Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia jioni ya leo. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa namna ambavyo ameniwezesha kwa kunipa afya njema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Halima Mdee ambaye ndiyo Mwenyekiti wangu wa Kamati ya LAAC kwa namna ambavyo amewasilisha vizuri hoja ya Kamati, lakini pia nampongeza Mheshimiwa Kaboyoka, Mwenyekiti wa PAC, mmewasilisha vizuri sana hoja za Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye mchango wangu mimi ninajikita kuchangia kwenye eneo la force account na niliwahi kuchangia mchango hapa unaohusu force account, naongea kwa uchungu sana, kwenye force account kuna fedha nyingi sana zinapelekwa kwa ajili ya miradi. Ni mabilioni ya pesa, lakini cha kusikitisha ukiangalia hapa kutoka kwenye Taarifa ya CAG kati ya miradi 175, miradi 24 ndiyo majengo ambayo yamejengwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna wazalendo ndani ya Taifa letu la Tanzania, lakini wakati huo huo kuna watu wengine ambao si wazalendo, yaani baadhi ya watumishi sio wazalendo.
Mheshimiwa Spika, hili Taifa la Tanzania litajengwa na sisi wenyewe Watanzania, haiwezekani tufikirie kwamba kuna watu watatoka nchi za Ulaya waje watujengee Taifa letu la Tanzania. Uzalendo unatakiwa ujae ndani ya mioyo yetu ili kusimamia fedha hizi za walipa kodi ambazo zinapelekwa kwenye hii miradi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kati ya miradi 175, ni miradi 24 kwa maana ya majengo ambayo yamepelekewa fedha nyingi za Serikali, ukitoa hapa majengo 24 tu ina maana majengo 151 hayako kwenye ubora. Ni nini maana yake? Majengo haya ndiyo ambayo wanapokuwa wanakwenda kukagua sasa kwamba hili jengo limesimamiwa na viongozi husika ambao walikuwa wanasimamia hayo majengo, matokeo yake mnakwenda kukagua hayo majengo tiles zinabomoka zenyewe, bado halijaanza kutumika. Mnaenda kukagua hayo majengo, maji yanamwagika, kwa sababu vifaa vile ambavyo wamefungia siyo high quality. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilichangia hapa kuhusu force account, nilipata simu tofauti tofauti hata voice notes niko nazo kwenye simu ambazo hata mafundi ambao wanawatumia huko kwenye mambo ya force account hata wao hawapendi haya. Walikuwa wananipongeza kwamba umesimama kuongelea force account, sisi kama mafundi utakuta tunawaambia kwamba hapa inatakiwa tuweke nondo milimita 16, wanasema tuweke nondo milimita 12. Sasa ubora utapatikana kutoka wapi? Lakini wakati huo huo kama itawekwa nondo milimita 16, kama zilitakiwa nondo nane sehemu husika zinawekwa nondo nne au tano, uimara utatoka wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaongea kwa uchungu sana, mimi nikiwa Mjumbe wa Kamati ya LAAC, hawa ma-engineer wa Tanzania wengi ni wazalendo na ni watenda haki, kama wapo ni wachache sana. Kwa nini nasema hivi, hawa ma-engineer ambao wanatakiwa wawekwe, ambao ndio wataalam, kati ya 859 wanakuwepo wataalam 213, nini maana yake? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika miradi utakuta Halmashauri moja ina miradi 150, ndani ya hiyo Halmashauri yupo Engineer mmoja na wakati huohuo Engineer mwenyewe hata usafiri wa kwenda kukagua hizo site kwamba basi ndiyo aweze ku-move aende hapa, aende hapa gari hakuna la kwenda kukagua miradi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali ilikuwa na nia njema kabisa ya kuanzisha force account lakini matokeo yake sasa yamkini walianza vizuri lakini kadri siku zinavyozidi kwenda force account inakuwa ni tatizo ni ugonjwa mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili linajieleza wazi taarifa ya CAG ya Ukaguzi wa hayo majengo, kama ndani ya majengo 175, majengo 151 hayafai, unategemea nini baada ya miaka 10 ijayo, si yatakuwa ni magofu tu? Hayo majengo yatakuwa magofu tayari tumepata hasara ambapo hizo ni fedha za walipa kodi pia tunatakiwa kuwa na uchungu wa haya majengo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, natamani sana kuishauri Serikali kama watadhani force account iendelee kuwepo basi miradi ama kama ni ukarabati, fedha isizidi milioni 50 ikizidi sana milioni 100, akini haya majengo tunayojengewa bilioni tatu, bilioni nne kwa force account. Juzi nilikuwa nasikiliza Tunduma kwenye ziara ya Mheshimiwa Makonda, shule ambazo zinakwenda kujengwa shule hii ni shule mpya, anapewa bilioni tatu, shule moja imejengwa kwa bilioni tatu, lakini ramani ni hiyo hiyo, shule nyingine wamejenga bilioni tatu zimekwisha na bado wanaitaka Serikali ipeleke fedha nyingine bilioni zaidi ya mbili ili wakamilishe shule.
Mheshimiwa Spika, wakati huohuo fedha zinaingizwa kwenye akaunti za shule, Mwalimu anaambiwa fedha zinaingizwa kwenye account yako usimamie shule mpya ndiyo inaenda kuanza kujengwa. Huyo Mwalimu lini amesomea Ukandarasi kwamba sasa Mwalimu anaacha kufundisha anaenda kuwa Engineer anaenda kusimamia majengo, wataandaa saa ngapi, maana Mwalimu wanamwambia yeye aunde Kamati, akiunda Kamati ambayo itakuwa inasimamia ujenzi huo kwa fedha mabilioni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, si tu Mkuu wa Shule hata wakati fulani fedha zinaingizwa kwenye account anaingiziwa DMO. DMO inabidi aunde kamati ya kusimamia majengo ya hospitali, sasa hawa wagonjwa watasimamiwa na nani, watatibiwa saa ngapi wakati wako busy kuangalia huku? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukizingatia kwa upande wa mashule hizo Kamati, wanashirikisha na wanakijiji ama wana mtaan pale wao ni wataalam hao unaowashirikisha na ukizingatia hawana posho, kwa hiyo hawawezi kuweka mkazo, kwamba lazima waende kule kusimamia, wanasimamia kwa posho ipi? Kwa maana bajeti hapa haipo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali na ninaishauri haya ninayoyaongea hata Wakurugenzi, wakija mbele si lugha nzuri sana, wakija mbele ya Mheshimiwa kwenye Kamati yetu pale tunavyowahoji, tunavyowabana, Mkurugenzi anaweza akawa ana miezi miwili tu hapo hajui chochote. Hawa wataalam ambao wapo wakiambiwa elezeni kuliendelea nini, wanakuwa hawana majibu, hawajui chochote yaani hata mimi ambaye si fani yangu ile najua hapa ningetakiwa nijibu nini, najua hapa nilitakiwa niongee nini, si fani yangu, lakini wenyewe ambao ndiyo wamesomea hawawezi kujibu, hawajui chochote. Pale kwenye Kamati ya LAAC, kwa kweli kwa wazalendo wa kweli pressure zinapanda kila siku unasikia uchungu moyoni jinsi fedha za Serikali zinakwenda ndivyo sivyo.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Hussein Amar.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa mzungumzaji haya anayozungumza ni kweli, kwa sababu tumeona hata kwenye ukaguzi wakati wa Mbio za Mwenge miradi mingi inakutwa ni mibovu na kuna wataalam.
SPIKA: Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo malizia mchango wako dakika moja, unaipokea taarifa hiyo.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ninaipokea hiyo taarifa. Katika kuipokea taarifa kwa majengo hayo tunayosema ni mabovu yaani ukilinganisha tu 175 ripoti ya CAG majengo 24 ndiyo salama tunakwenda wapi, baada ya miaka 10 ijayo majengo yatabaki magofu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia ninaunga mkono hoja, ila naomba Serikali ilichukulie kwa uzito sana kwamba force account isiendelee, ama sivyo kwa bajeti isiyozidi shilingi milioni 100, ahsante. (Makofi)