Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili na mimi niwe miongoni mwa Wabunge ambao wamechangia kuhusiana na taarifa za Kamati ya PAC na Kamati ya LAAC. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC.
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii pia kumpongeza sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuendelea kuiletea maendeleo nchi yetu ya Tanzania, ama kwa hakika Mama apewe maua yake kwa namna ambavyo ametuheshimisha Watanzania, lakini kubwa zaidi ambavyo ametuheshimisha wanawake wa Tanzania wote, tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze nina mambo mawili tu leo sina mambo mengi, nina suala linalohusiana na miradi ya barabara lakini pia nina suala linalohusu force account, sasa naomba nianze na miradi ya barabara. Nichukue nafasi hii pia kumpongeza CAG ambaye pia ni jicho letu katika Kamati zetu hizi anafanya kazi nzuri sana ya kufukua fukua maovu na upigaji ambao unafanyika katika nchi yetu ya Tanzania. Hongera nyingi sana kwa Kaka yangu Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali Ndugu Charles Kichere, nakupongeza pamoja na delegation yako yote kwa namna unavyofanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo tarehe 15 Februari, 2024 naenda kuchangia kama ifuatavyo. Kumekuwa na ujenzi wa barabara pesa nyingi za Serikali zinapelekwa katika miundombinu ya ujenzi wa barabara huko, lakini Wabunge wengi wamezungumza uzalendo ndiyo tatizo, Mzalendo namba moja ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wanaofuata baadhi yetu wamekuwa si Wazalendo katika nchi hii.
Mheshimiwa Spika, pesa zinapelekwa lakini ukiangalia zipo barabara ambazo tayari zimeharibiwa sana ni barabara ambazo zinatakiwa kujengwa upya zenye zaidi ya kilometa 519 katika nchi yetu. Naomba nitaje hizo barabara na namna urefu wa kilometa zake zilivyo na namna ambavyo zimeharibiwa, kuna barabara ya Bagamoyo – Msata, yenye urefu wa kilometa 49, barabara hii utafikiri imejengwa wakati wa Uhuru, barabara ina mashimo, barabara imeharibika vibaya, sielewi aliyekuwa anajenga hii barabara alikuwa anatumia nini! Nataka niseme kwamba ujenzi huu wa hii barabara unatakiwa uanze upya maana yake ni kupelekea Serikali mzigo mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia ipo Barabara ya Dodoma – Iringa, ina urefu wa kilometa 260, barabara hii ina viraka na barabara hii ni ya muda mfupi tu mpaka sasa hivi imeshaharibika vibaya. Barabara imemomonyoka, pia kwenye hii barabara ni barabara ambayo inaundwa na udongo ambao unakuwa na maji yaani chepechepe lakini kana kwamba haitoshi iliwekwa tabaka moja tu la lami, nataka niseme ni namna gani ambavyo pesa nyingi zimetumika lakini barabara haina ubora. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Barabara ya Ruangwa - Nanganga - kilometa 69 barabara hii haifai. Nzega – Tabora - kilometa 50.3 barabara hii haifai. Masho – Mwigumbi - kilometa 50 haifai. Loliondo – Mto wa Mbu - kilometa 49 haifai. Tanga – Pangani - kilometa 50, haifai. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niseme barabara hizi zina urefu wa kilometa zaidi ya 519, zimetumia pesa nyingi mabilioni ya pesa na sasa hivi hazifai tena zinatakiwa zikwanguliwe, zianze kujengwa tena kwa kiwango cha lami.
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, taarifa.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, tazama namna gani ambavyo pesa hii inapotea.
SPIKA: Mheshimiwa Jacqueline Msongozi Ngonyani, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Innocent Bashungwa.
TAARIFA
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Msongozi, anachangia vizuri lakini kwenye orodha anazozitaja baadhi ya barabara ndiyo kwanza zinajengwa sasa hivi. Kwa mfano, Barabara ya Tanga – Pangani, Mkandarasi yupo site anajenga hajaweka hata ile sub base, sasa kwenye mchango wake angebainisha na kujikita kwenye barabara ambazo anataka kujenga hoja, lakini si kuchanganya kwamba barabara zote zimeharibika wakati kuna barabara ambazo mpaka sasa hivi hata level ya kuweka lami bado, lakini anahesabu kwamba barabara tayari imeharibika. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Jacqueline Msongozi, unaipokea taarifa hiyo.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba unilindie muda huo, lakini jambo la pili, Mheshimiwa Waziri ana muda wake wa kuchangia na yeye kwa hiyo achaukue hizo details zote aziweke pembeni atapata muda muafaka.
Mheshimiwa Spika, hiki ninachokisema mimi sijakitoa kichwani kwangu ni jicho la CAG limeona. Kwa hiyo, mimi sijatoa kichwani kwangu. Naendelea kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, haya yote yanatokana na usanifu mbovu ambao unafanyika na Washauri Elekezi hawasimamii vizuri miradi hii, kungekuwa kuna Washauri Elekezi wazuri maana yake haya yasingejitokeza.
Mheshimiwa Spika, pia kumekuwa na ucheleweshaji wa malipo ya pesa kwenye miradi hiyo, jambo ambalo linapelekea kuweka hasara kubwa sana kwenye miradi hiyo, mpaka kufikia Juni, 2023 pesa za Kitanzania yaani riba ambayo inatakiwa Serikali ilipe ni zaidi ya bilioni 701. Nilikuwa najiuliza tu, hivi kwa nini sasa Serikali inampa Mkandarasi kazi ili hali inajua kwamba hakuna pesa na hatimae kwenda kutengeneza riba hii hapa ambayo ni hasara kubwa. Pesa hii shilingi bilioni 701, nilikuwa nafikiria tu hivi fedha hii isingeweza kwenda kujenga barabara ya Likuyufusi – Mkenda yenye urefu ya kilometa 124, inayotoka Songea Mjini mpaka kwenda kuunganisha Nchi ya Mozambique na Tanzania, ikaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
Mheshimiwa Spika, pia nikawa najiuliza tu hivi pesa hii shilingi bilioni 700 inayoenda kupotea kwa maana ya Serikali kwenda kulipa riba hivi ingepelekwa pale kwenye barabara ambayo ni ya Mtwara, Pachani - Lingusenguse – Nalasi – Mbesa na hata kutokeza Tunduru yenye urefu wa kilometa 305, pesa hii ingetosha kabisa kujenga na ingebaki ikaenda kujenga barabara ambayo inatoka Lumecha – Londo kwa Mpepo - Morogoro, inaunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Ruvuma, pesa hii ingetosha kabisa kujenga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pesa hii sasa inaenda kuchukuliwa na inaenda kulipwa huko kwa sababu tu ya kwamba wale Wasanifu wameshindwa kufanya kazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naenda sasa kwenye force account. Kwa masikitiko makubwa sana, masikitiko makubwa sana, kwamba force account imekuwa ni sehemu, ni kichaka cha kujificha watendaji wetu. Nia ya force account ilipokuwa inawekwa ilikuwa ni kusaidia ujenzi kwa haraka lakini pia kupunguza gharama, lakini kilichotokea sivyo. Nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mkurugenzi wa OSHA, Ndugu Khadija Mwenda, ambaye amefanya kazi nzuri sana kwenye Jengo la OSHA, pale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, amejenga jengo lile, ametumia force account, amemaliza lile jengo na pesa imebaki, lakini wale wote ambao wameweza kufanya vizuri, wamepelekewa pesa na wametumia hiyohiyo mpaka wamemaliza hiyo miradi kwa kweli waandikiwe barua za pongezi. Hawa ambao wanafanya …
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, wanafanya mishemishe za kutengeneza mazingira …
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Bashungwa mbona unanifanyia hivyo. (Kicheko)
SPIKA: Mheshimiwa Bashungwa, taarifa mbili kwa Mbunge mmoja? Haya karibu.
TAARIFA
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Msongozi ili aweze kuchangia vizuri. Bilioni 701 anazozitaja ni madeni ya Wakandarasi siyo riba, kwa hiyo kama anataka kujenga hoja ya riba ajenge kama hoja ya riba lakini hizi bilioni 701 ni madeni ya Wakandarasi, ambayo wanadai ya malimbikizo. (Makofi)
SPIKA: Aah! sasa hayo madeni ya Wakandarasi yana uwezo wa kuzalisha riba kiasi gani, bilioni 700 riba ikitokeza, itatokeza ngapi ili ndiyo aiseme hiyo Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, riba zinakuwa calculated with time. Kwa hiyo, mpaka Disemba mwaka jana ninaweza nikaleta taarifa kwa sababu ni hoja ya kitakwimu tulikuwa kwenye bilioni 68 hivi.
SPIKA: Bilioni 700 inaweza ikazalisha bilioni 68.
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ndiyo.
SPIKA: Haya. Mheshimiwa Msongozi
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, zinakuwa generated with time lakini kwa takwimu za mpaka Disemba, 2023 ilikuwa around hiyo bilioni 68.
SPIKA: Sawa. Mheshimiwa Jacqueline Msongozi, kuna taarifa hapa inayohusu takwimu kwamba umesema bilioni 701. Bilioni 701 ni madeni kwa mujibu Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, anasema hayo ni madeni ambayo wanadai Wakandarasi, ambayo hayo madeni yana uwezo wa kuzalisha takribani bilioni 68 kwa mujibu wa Mheshimiwa Waziri, unaipokea taarifa hiyo.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, yaani mimi namshauri tu Mheshimiwa Waziri awe anasoma. Kwa kweli, namheshimu sana lakini mimi haya mambo sijayatoa kichwani kwangu taarifa ya CAG hii hapa! Sijayatoa kichwani kwangu, taarifa hii hapa imesomwa na Mheshimiwa Kaboyoka, Mwenyekiti wa Kamati pele amewasilisha sijaitoa kichwani kwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naendelea lakini pia naomba unilindie muda wangu.
SPIKA: Subiri kwanza Mheshimiwa, muda wako ulikuwa umeshaisha dakika moja malizia hoja yako.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nilikuwa nataka tu nifafanue namna ambavyo force account inafanyika. Ni kwamba pesa inatoka TAMISEMI, inapelekwa moja kwa moja kwenye account ya shule, Mwalimu Mkuu anaiona ile pesa anaitwa na Mkurugenzi Halmashauri. Akishafika kwa Mkurugenzi Halmashauri, Mkurugenzi ndiyo anaanza kumpangia sasa na kumpa maelekezo ya matumizi ya zile pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mkandarasi anayeenda kujenga kule shuleni ni Mkandarasi ambaye anapewa maelekezo na anakabidhiwa na Mkurugenzi. Kwa hiyo, mwisho wa siku ikitokea kuna changamoto wale Wajumbe wa ile Kamati wakiuliza jambo yaani kama ni Mjumbe akiuliza jambo anaonekana huyo ni tatizo anapigwa chini, lakini mwisho wa siku Mkurugenzi yule anapoona kwamba mradi ule haujatosha, maana yake ni nini, anaanza kulaumiwa msimamizi lakini anasahau kwamba ile ten percent ameshaipiga kule na Walimu wamebaki tu ni kusimamia, kuangalia mbao zinafanyaje, kuangalia misumari inagongwaje na kila kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka kusema kwamba hii force account iangaliwe upya. Kama ingekuwa amri yangu pekee yangu ningesema futilia mbali turudi kwenye suala la Wakandarasi ili Mkandarasi akipewa ule mradi asipokamilisha atachukua na hela zake za mfukoni ataenda kuweka pale. Kama amefanya tofauti atachukuliwa atawekwa ndani, hapo nadhani umenielewa. (Makofi)
SPIKA: Haya, ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, kwa maana ya hiyo dakika moja nakushukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko)