Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie kwenye Wizara hii muhimu na Kaimu Waziri Mkuu anisikilize vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunajua adha ambayo wanapata wastaafu wetu, sote tunajua kikokotoo bado ni janga na hii haijaisha, mpaka iishe. Ilianza kulalamikiwa tangu sheria inatungwa. Hitaji lao ilikuwa wachukue mafao kwa mkupuo asilimia 50, mkaleta asilimia 33. Bado kuna manung’uniko kwa watumishi. Nikiwaonesha meseji zangu za askari, walimu, manesi na madaktari, ni shida. Mtu anastaafu anapewa shilingi milioni 17, na hajajenga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua mtumishi wa umma anafanya kazi kwenye mazingira gani? Kuteleza si kuanguka, turudi tukae tuwasikilize. Hizi ni fedha zao Serikali inaweka, wapeni mafao kwa mkupuo kwa 50% na hiyo nyingine mwape kidogo kidogo. Yale mafao ya mkupuo ndiyo yanayowasaidia, siyo hiki ambacho mnawapa kila mwezi. Wakiweka misingi, hayo maisha mengine yatakuwa ya kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulisema hapa tangu mnabadilisha sheria, mnasema mnabadilisha sheria ili kuwe na manufaa, lakini tulikuwa tunajua mlikuwa mnajua mifuko inakufa na hamkufanya tathmini, mkaenda mkaunga tu huko huko. Madhara yake ndiyo haya. Sasa leo mifuko yetu ina shida.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia mfuko mmoja tu hapa unaohusu watumishi wa Serikali wa PSSSF. Kwa mujibu wa Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ukwasi unatakiwa uwe 40%, lakini ripoti ya CAG ya kila mwaka inaonesha ukwasi ni 20%. Kwa sababu gani? Serikali mnachukua fedha kwenye mifuko, mnaenda kuwekeza lakini hamlipi. Wakati tunapitisha bajeti hapa mwaka 2020/2021mlilipa kwa non cash bond shilingi trilioni 2.1, mkasema mwaka ujao wa fedha mnalipa shilingi trilioni 2.4, mpaka leo hamjalipa. Sasa hii mifuko itawezaje kuwa stable? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakupa tu mfano, nianze na takwimu za mwezi Juni, 2020 ambapo michango ya wanachama kwenye mfuko ilikuwa shilingi 1,364,000,000/= huku mahitaji ya mafao ilikuwa shilingi 1,554,000,000/=. Nyongeza waliyokwenda kuchukua kwenye vyanzo vingine ni shilingi 190,000,000/=. Sasa kwenye hiyo nyongeza umeenda kuchukua kwenye investment income yao ambayo kwa mwaka huo ilikuwa shilingi 400,000,000/=, can you imagine! Wakipunguza hapo wanabaki na nini? Yaani hapo wamejikusanya kwenye investment zao kwa mwaka, PSSSF shilingi milioni 400. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya, nakuja mwaka ulioishia Juni, 2022 ambapo michango ya wanachama ni shilingi bilioni 1,526 huku mahitaji ya mafao ni shilingi bilioni 1,697. Pungufu waliyokwenda kuongeza ni shilingi milioni 171. Ukiangalia investment return yao kwa mwaka huo ni shilingi milioni 587. Sasa wakitoa hapo, wanabaki na nini? Yaani kwa mwaka wameangalia waliko-invest kule ni shilingi milioni 500, halafu sasa wapunguze shilingi milioni 177, mfuko ambao Serikali inaenda kukopa haiwalipi, inaenda ku-invest maeneo mbalimbali hairudishi fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naangalia ukurasa wa 28 wa Hotuba ya Waziri Mkuu, ameongelea vizuri tu, ndiyo hatukatai ku-invest PSSSF huko Mkulazi ambako anasema mmezalisha sijui tani 50 za sukari, wamewekeza asilimia 96, lakini kwa miaka minne wamepata hasara ya shilingi bilioni 11. Hawa watu ambao investment income yao kwa mwaka ni shilingi milioni 500, ukienda Kiwanda cha Mbozi wame-invest mtaji wa 86%, wamepata hasara kwa miaka minne mfululizo shilingi bilioni 4.5. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wanachukuaje fedha za wanachama waende kupeleka sehemu ambayo inapata hasara? Inaonekana walikuwa hawajafanya tathmini ya kina kuhusiana na investment kwenye eneo hilo. Hizi fedha ni za wastaafu. Hatukatai kuchukua fedha hizi ili kuwekeza, lipeni madeni basi, tuone hata huko kwenye mshiko wao kwa mwaka unaeleweka. Sasa mnakomba mabilioni halafu wenyewe wanabaki na shilingi milioni 500! Jamani, kweli! Hata wakitaka kulipa wastaafu ni shida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la dawa za kulevya. Nasema kila siku, nina mdogo wangu ameathirika na yuko sober house ya Bagamoyo. Lazima Serikali mwekeze kwenye kutibu. Lengo la kuanzisha Tume lilikuwa ni kuzuia, kukamata na kutibu waraibu wa dawa za kulevya. Mmejikita kwenye kukamata, na sasa hivi mnakamata sana. Mnajua ni kwa sababu gani? Kwa taarifa ya Umoja wa Mataifa huko duniani, wazalishaji wa dawa za kulevya wameongezeka kwa 25%. Hizo mnazozikamata ni ndogo, bado watu wanaingiza kimya kimya huku vijana wetu wanaathirika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakati mnaendelea kupambana, hakikisheni wale walioathirika mnawatibu, na mkishawatibu mtapunguza magonjwa ambayo yanatokana na kutumia dawa za kulevya. Watu wanaharibika ini, figo, mwisho wa siku mnakuwa na mzigo mzito wa kuhudumia magonjwa ambayo yanatokana na dawa za kulevya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kwa sasa hivi multiclinics ziko 11 tu. Tathmini ambayo mnaitumia sasa hivi ya wagonjwa mlionao 530,000 ni ya tangu mwaka 2014. Kweli! Hamjafanya tathmini, mnawezaje kuhakikisha mnapambana na hili janga? Multiclinics 11! Haya, ukienda tu pale kwa mfano multiclinic ya Mwananyamala, watu wanaokunywa dawa pale ni msongamano, watu 1,500; nenda Muhimbili, watu 1,200; nenda multiclinic ya Tanga, ni zaidi ya watu 1,000, lakini walioathirika kwa takwimu zilizopitwa na wakati ni 530,000. Idadi ya watu 30,000 ni ambao wanajidunga, 500,000 ni wale ambao wanavuta na/au wanalamba. Sasa, mnawezaje kupambana bila takwimu ambazo ni latest? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yenyewe mna rehab moja na haijaisha. Seriously, kwa tatizo kubwa namna hii, kweli! Halafu huku mnatupatia taarifa sijui mmekamata bangi mmechoma, sijui nini. Bado kuna tatizo la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiwa na mtu ambaye unamhudumia, mosi, future yake imeharibika; lingine amekuwa ni mzigo wako wa milele. Leo kuna Sober Houses 40, lakini mnazisaidiaje? Hizo ni za watu binafsi, ninyi Serikali hamna, ilhali tatizo ni kubwa sana. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Taarifa.
TAARIFA
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwa mujibu wa mikataba ambayo nchi yetu imeridhia na kukubaliana Kimataifa katika mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya, ni pamoja na kushirikisha wadau mbalimbali na siyo kazi inayoweza kufanywa na Serikali tu. Kwa hiyo, tunachokifanya, Sober Houses zinazoanzishwa na wadau, kila mwaka Serikali ndani ya Bunge lako Tukufu imekuwa ikitenga bajeti ya kuzisaidia hizo Sober Houses ili ziweze kufanya kazi nzuri ya kuendelea kuwahudumia warahibu hao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni lazima Waheshimiwa Wabunge tujue kwamba kazi inayofanywa na Serikali ni nzuri sana kwa kushirikiana na wadau hao ambao wamekuwa wakianzisha hizo Sober Houses, ikiwa ni pamoja na kuyafanyia kazi maeneo hayo yote matatu. Kwa hiyo, Serikali inawajibika ipasavyo na ndiyo maana mmeona mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanafanikiwa na Mheshimiwa Ester utakubaliana na sisi kwamba kazi nzuri inafanyika. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bulaya, taarifa hiyo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei kwa sababu kutenga ni jambo moja, na kupeleka ni jambo lingine. Sisimami hapa kuongea bila kufanya utafiti. Ungezitaja hapo data, mimi ndiyo maana nimekutajia hapa. Zamani Tume ilikuwa inaweza kuwasaidia hata kuwalipia kodi miezi sita, sasa hivi hakuna na wana-suffer. Ni jambo la kupokea tu dada yangu, kwa sababu hili ni janga letu sote. Kizazi kinaharibika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wastaafu wanung’unike, vijana tusiwawekee misingi bora. Tutafika wapi?
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Kengele ya pili hiyo. Ahsante.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)